Viongozi wa Chadema kizimbani
Dar es Salaam. Viongozi watatu wa Chadema,
akiwamo diwani wa Ubungo, wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
wa Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kuteka na kujeruhi.
Diwani
huyo, Boniface Jacob (32), mkuu wa walinzi wa Chadema, Hemed Sabula
(48) na ofisa utawala wa chama hicho, Benson Mramba (30) walipandishwa
kizimbani jana wakituhumiwa kumteka aliyekuwa mlinzi wa katibu mkuu wa
chama hicho, Khalid Kagenzi.
Akiwasomea mashtaka hayo,
Wakili wa Serikali Janeth Kitali alidai kuwa Machi 7, 2015 walimjeruhi
na kumteka nyara Kagenzi kwa nia ya kuzuia uhuru wake.
Kitali
alidai kuwa washtakiwa hao walifanya makosa hayo kinyume na kifungu cha
225 na 249 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Akisoma hati hiyo ya mashtaka
Kitali alidai kuwa Machi 7,2015 washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa katika
ofisi za makao makuu ya Chadema ziliyopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni
walimjeruhi Kangezi katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Kitali
alidai kuwa siku hiyo ya tukio washtakiwa hao kwa pamoja, wakiwa katika
ofisi hizo za Chadema, walimteka Kagenzi na kumpeleka Hoteli ya River
View iliyopo Sinza.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Wakili
wa washtakiwa hao, Peter Kibatala akishirikiana na wakili John Mallya
waliiomba mahakama kuwapa dhamana wateja wao kwa kuzingatia kifungu cha
148 cha Sheria ya Makosa ya Jinai Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho
2002.
Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema alimtaka kila
mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja asaini hati ya dhamana
ya maneno ya Sh10 milioni na kwamba wadhamini hao wasiwe walimu.
Wadhamini
wa washtakiwa hao waliwasilisha nyaraka zao, lakini Kitali aliomba
kupewa nafasi kuzihakiki, lakini hazikukidhi masharti na hivyo
washtakiwa kutakiwa kupelekwa mahabusi.
Hakimu Lema aliiahirisha kesi hadi Machi 26,2015 kwa ajili ya kutaja kuangalia upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Chanzo
cha washtakiwa hao watatu kufikishwa mahakamani ni tuhuma zilizotolewa
kuwa Kagenzi alihojiwa na maofisa wa Chadema waliomtuhumu kumwekea sumu
Dk Slaa.
Tuhuma hizo zilitolewa hadharani na mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, ambaye alisema Kagenzi alikuwa
akishirikiana na maofisa wa usalama wa taifa kutekeleza tukio hilo.
Kagenzi
alichukuliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano na baada ya siku kadhaa,
aliachiwa huru na kuzungumza na vyombo vya habari yale yaliyomtokea na
jinsi alivyoteswa.
Wakati Kagenzi akieleza hayo, washatakiwa hao watatu walikamatwa na polisi kwa mahojiano hadi walipofikishwa mahakamani.