Kinana: Lowassa safi, Nyalandu anazurura
“
Mfano ni Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye anafanya kazi ya kuzunguka nchi nzima na maeneo mengine wakati mizunguko yake haisaidii kuondoa matatizo ya wananchi.” Kinana
Mfano ni Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye anafanya kazi ya kuzunguka nchi nzima na maeneo mengine wakati mizunguko yake haisaidii kuondoa matatizo ya wananchi.” Kinana
Kondoa/Monduli. Jana ilikuwa siku ya hisia
tofauti kwa watu wawili wanaotajwa kwenye kinyang’anyiro cha urais,
Edward Lowassa na Lazaro Nyalandu baada ya Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana kumsifu mmojawao na kumponda mwingine.
Akiwa
Kondoa, Kinana alitumia muda mwingi kujibu kilio cha wananchi
wanaosumbuliwa na askari wa wanyamapori kwa kumponda Waziri Nyalandu
kuwa anazurura bila kushughulikia matatizo ya wananchi, lakini saa
chache baada ya kuwasili Monduli alimsifu Lowassa kuwa ni kiongozi
shupavu.
Tayari Nyalandu ameshatangaza nia ya kugombea
urais, wakati Lowassa, mmoja wa wanachama wa CCM wanaotajwa sana kwenye
kinyang’anyiro hicho, hajatangaza uamuzi wake lakini anatumikia adhabu
ya chama chake kilichomfungia kujihusisha na harakati za uongozi pamoja
na makada wengine watano.
Baada ya msafara wa Kinana
kuwasili Monduli na kupokewa na viongozi wa chama hicho wa eneo, katibu
huyo wa CCM, Kinana alipata nafasi ya kuzungumza machache kabla ya
kuanza safari ya kukagua shughuli mbalimbali.
“Hatuna
shaka na Monduli kwa kuwa yupo kiongozi shupavu, ndugu yetu Waziri Mkuu
mstaafu na mjumbe wa (Halmashauri Kuu ya CCM) Nec,” alisema Kinana
akiwaelezea wananchi waliokuwapo eneo hilo.
“Wa Monduli mna kiongozi shupavu na mchapakazi. Hongera Bwana Lowassa.”
Baadaye, Lowassa aliwakaribisha akisema: “Mmefanya kazi kubwa sana ya kukijenga chama chetu. Nawashukuru sana, karibuni.”
Naye
katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Nafurahi kuwa
katika jimbo la mzee wangu, rafiki yangu Edward Lowassa. Mapokezi
mazuri, bila shaka Arusha mmeamka.”
Kinana amekuwa
akitumia sehemu kubwa ya ziara yake kushuhutumu viongozi wa Serikali na
hasa mawaziri kwa kushindwa kuwatatulia wananchi matatizo yao na
ilifikia wakati aliwataja mawaziri wanne aliowaita kuwa ni mizigo,
tofauti na alivyofanya kwa waziri mkuu huyo wa zamani.
Lowassa
alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne na
anajulikana kama mtu aliye tayari kufanya uamuzi mgumu. Alilazimika
kujiuzulu wadhifa huo mwaka 2008 baada ya kuibuka kwa kashfa ya
Richmond.
Kinana alikuwa mtu tofauti wakati akijibu
kero za wananchi mkoani Singida, ambako alimtaja moja kwa moja Waziri
Nyalandu kuwa hashughulikii matatizo ya wananchi na badala yake amekuwa
akizunguka bila msaada wowote.
Kinana alisema hayo juzi
katika Kijiji cha Ikengwa, Kata ya Kinyasi wilayani Kondoa baada ya
wananchi wa kijiji hicho kumchongea Nyalandu kwa Kinana kwamba wizara
yake inawaua na kuwaumiza bila ya hatia, hivyo wamechoka.
Wananchi
hao walisema mateso wanayoyapata kutoka kwa askari wa wanyamapori
katika Pori la Mkungunero ni makubwa ambayo yanalenga kuondoa uhai wa
watu.
Katibu wa CCM wa Kata ya Inyasi, Jusberi Jumanne
aliyesoma risala ya malalamiko hayo, alisema wanaishi ndani ya kijiji
chao na kufanya shughuli zao za kilimo, lakini kila wakati wanachomewa
nyumba, mazao yao kufyekwa na hata kuwasababishia ulemavu na vifo.
“Mheshimiwa
katibu mkuu, hapa ni kijiji halali kilichosajiliwa 1974 na kupewa hati
398, lakini hifadhi hiyo ilikuja kuweka mipaka yao mwaka 2006, jambo
hili sisi tunaona ni uonevu ambao tunafanyiwa bila ya kushirikishwa na
kuambiwa tuhame kwa nguvu na hatujui mahali pa kwenda,” alisema.
Akijibu
hoja hiyo Kinana alionekana kukerwa na namna maisha ya watu wa maeneo
hayo yasivyoshughulikiwa ili nao waishi kama Watanzania wengine.
“Ni jambo la aibu kwa Waziri wa Maliasili na Utalii kusikia migogoro lakini yeye akawa kimya,”alisema Kinana.
“Nyalandu
awaeleza Watanzania kama kuna mahali amefanikiwa kumaliza kabisa
migogoro walau 10 kwani amekuwa ni bingwa wa maneno na matembezi.”
Kinana
alisema ni lazima Nyalandu abebe msalaba huo kwani roho za binadamu
zina thamani… ni heri roho ya binadamu kuliko mnyama ingawa alizuia
wanyama wasiuawe.
“Hawa mawaziri lazima waje, na nina
wasihi waje haraka, yaani Waziri wa Maliasili na Utalii na mwenzake wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,” alisema.
“Mfano
ni Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye anafanya kazi ya kuzunguka nchi
nzima na maeneo mengine wakati mizunguko yake haisaidii kuondoa matatizo
ya wananchi.”
Kinana alitaka kamatakamata ya wananchi
isimamishwe kwanza hadi ufumbuzi kuhusu mipaka ya pori hilo
itakapoangaliwa upya. Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, Waziri Nyalandu
alisema anakubaliana na alichosema Kinana, lakini akataka watu wajjue
kuwa mgogoro huo ni wa muda mrefu.
“Mgogoro huo ni wa
siku nyingi, hivyo busara inahitajika sana kulinda watu, mali zao na
maliasili. Niliunda kamati ambayo yumo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na
Manyara, Ma-RAS (maofisa utawala wa mikoa) wao na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii ambayo imefanya uchunguzi pamoja na kuongea na
wananchi,” alisema.
“Kamati inatarajiwa kumaliza kazi
wiki hii na itanikabidhi kwa kuwa mimi ndiye niliyeiunda. Nimepanga
kwamba ndani ya hizi wiki mbili za Bunge, mimi na Waziri wa Ardhi
tutatangaza suluhisho la tatizo hili. Tutaenda pamoja Mkungunero
kuongea na wananchi.”
Katika mkutano huo, Mbunge wa
Kondoa Kaskazini, Zabein Mhita alisema kuwa katika kata hiyo na maeneo
mengine kumekuwa na kelele zinazotishia amani na tayari kwa baadhi ya
watu wameshapoteza maisha.
Walimkabidhi Kinana maganda ya risasi pamoja na rundo la mabaki ya nguo zilizochomwa moto na askari wa wanyamapori.