Komba azikwa kwa tingatinga
Ndugu na jamaa wakisaidiwa na kijiko cha tingatinga kushusha mfuniko wa zege kwenye kaburi la Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba aliyezikwa katika Kijiji cha LItuhi, wilayani Nyasa, Ruvuma jana. Picha na Emmanuel Herman
Nyasa. Safari ya mwisho ya mbunge wa Mbinga
Magharibi jana ilihitimishwa saa 9.25 alasiri wakati mwili wake
ulipofunikwa na mfuniko mkubwa wa zege uliobebwa na gari maarufu kwa
jina la “kijiko”.
Haikuwa kitu cha kawaida wakati gari
hilo kubwa likishusha mfuniko huo wa zege kwenye kaburi la mwimbaji huyo
maarufu wa nyimbo za uhamasishaji za CCM na kiongozi wa kundi la
Tanzania One Theatre (TOT), lakini majonzi yaliwafanya waombolezaji
kulichukulia tukio hilo kuwa la kawaida.
Safari ya
Komba, iliyoanza miaka 61 iliyopita kwenye kijiji cha Lituhi ambako
aliazikwa jana, ilikamilishwa kwa salamu mbalimbali ambazo zilielezea
ushupavu wa kapteni huyo mstaafu wa jeshi.
Mazishi hayo
yaliyohudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi
mbalimbaliwakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete na mkewe Salma, yalifanyika
katika makaburi ya Misheni,katika Kijiji cha Lituhi (Bundi) wilayani
Nyasa mkoani Ruvuma.
Nyuso za majonzi zilitawala kwa
waombolezaji waliojitokeza nyumbani kwa marehemu, takriban mita 500
kutoka katika makaburi hayo na baadaye katika misa iliyofanyika kwenye
uwanja wa Shule ya Msingi ya Lituhi, ikiongozwa na Askofu John Ndimbo wa
Jimbo Katoliki la Mbinga.
Kaimu katibu wa Bunge, John
Joel, akisoma wasifu wa marehemu, alisema Kapteni Komba aliyefariki
dunia Februari 28, mwaka huu akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ
jijini Dar es Salaam, alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la
damu na mara kadhaa Ofisi ya Bunge ilimpeleka India kwa matibabu. Pia
alikuwa na tatizo la kisukari ambalo ndilo lililochukua maisha yake.
Mazishi
hayo yalishuhudiwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Edward Lowassa,
ambaye alikuwa Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Steven Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na
Bunge), Jenister Mhagama na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine
ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Naibu Spika wa Baraza la
Wawakilishi, Ali Abdallah Ali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Uwanja wa ndege
Kwenye
Uwanja wa Ndege wa Songea, viongozi mbalimbali waliwasili kwa ndege za
kukodi na Lowassa ndiye aliyefungua mlango kwa ndege iliyotua saa 2:33
asubuhi akiambatana na mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani.
Haikupita
muda mrefu, ndege nyingine ilitua saa 2:50 ikiwa na Spika Makinda na
msafara wake uliomjumuisha mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe.
Saa
3:22 ilitua ndege iliyobeba ujumbe wa CCM ukiongozwa na Kinana. Wengine
waliokuwamo ni naibu katibu mkuu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba, katibu wa itikadi na uenezi, Nape Nnauye na mwimbaji wa
kikundi cha TOT, Khadija Kopa. Pia baadaye Rais Kikwete alitua na ndege
ya Serikali.
Mwili wa marehemu uliwasili ukiwa katika moja ya ndege mbili zilizobeba familia yake, ndugu na watu mbalimbali wa karibu.
Fulana za Lowassa
Wakati
ibada ya misa ikiendelea, walionekana vijana wakiwa wamevaa fulana
nyeupe na nyeusi zenye ujumbe wa “Marafiki wa Lowassa”, zilizokuwa
zimeandikwa mbele “4 U Movement Lowassa” huku mgongoni zikiandikwa
“Kapteni John Damiano Komba 1954-2015 Friends of Lowasa”.
Baada
ya vijana hao kuonekana, mmoja wa viongozi wa Bunge alimwamuru mmoja
wao aliyekuwa anapiga picha kwenda kuivua, lakini aligoma na hakuna kati
yao aliyekubali kuivua hadi mazishi yalipomalizika. Mmoja wa vijana hao
ambaye aligoma kutaja jina lake aliiambia Mwnanchi akisema: “Kwa sasa
fulana zimeisha kwa kuwa zilizokuwa zinagawiwa. Lakini kama unazitaka
unaweza kuacha namba yako na utaletewa sehemu yoyote utakapokuwa.
“Tumeamua
kutoa fulani hizi kama zawadi ya kumbukumbu kwa mchango alioutoa Komba
wakati wa urafiki wao (na Lowassa) na ndiyo maana unaona tumezivaa.”
Salamu za rambirambi
Katika
salamu zake, Gasper Tumaini, katibu wa kikundi cha Sanaa cha TOT
kilichokuwa kikiongoza Kapteni Komba, alisema Komba alipenda jimbo lake
na chama chake na kuwa siku moja kabla kifo walikwenda kurekodi nyimbo
za uchaguzi. Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, mbunge wa Lindi Mjini
(CUF), Salum Barwany alisema: “Tunatoa pole kwa wananchi na familia kwa
kuondokewa na mbunge mahiri na shupavu, tumefika kuonyesha namna Komba
alivyoishi vizuri nasi.
“Kila mmoja amejifunza namna
Komba alivyoishi na watu vizuri , alikuwa akinipa faraja wakati matukio
ya mauaji ya albino yalipotokea na wakati wote alikuwa akinihakikishia
usalama wangu, hivyo tumepata pigo kubwa kwa kuondoka kwake.”
Katibu
Mkuu CCM, Abdulahman Kinana, alisema: “Tuna huzuni kubwa kutokana na
msiba mkubwa uliotokea. Komba alifanya kazi nzuri ya kuwahudumia na
kuwajali na kuangalia maslahi ya wananchi aliowaongoza. Alhamisi
iliyopita alikuja ofisini kwangu na kuniambia anakwenda kiwandani
kutafuta mabati 900 kupeleka jimboni kwake.”
Waziri
Mhagama kwa niaba ya Serikali alisema: “Komba alikuwa kiungo muhimu kwa
serikali. Wengi wamemzoea katika masuala ya siasa na chama, wote
wanamkumbuka kwa tukio la kuimba nyimbo za maombolezi wakati wa msiba wa
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.”
Spika Makinda
alitumia fursa hiyo kuzungumzia muswada wa mabadiliko katika sheria za
Kiislamu ya mwaka 1963 kuhusu Mahakama ya Kadhi akisema inatakiwa
kubadilishwa kushughulikia mirathi, talaka hivyo Wakristo wawe
wavumilivu, wasikubali kuzungumzia vitu ambavyo hawana uhakika navyo.