Tumia vipaji ulivyopewa na Mungu ufanikiwe maishani
Miongoni mwa tunu muhimu za mafanikio ambazo Mungu amewekeza ndani ya kila mtu ni vipawa.
Kwa bahati mbaya na pengine kwa kutojua umuhimu wa vipawa, watu wengi hawatilii maanani vipaji walivyonavyo.
Wengi
wanaishi kwa kuiga maisha ya watu wengine kana kwamba wao ni nakala ya
wengine. Kipaji chako ni utajiri mkubwa kama utaamua kukitumia ipasavyo.
Kipaji
ni umahiri wa kipekee alioweka Mungu ndani ya akili ya mtu unaoongoza
usadifu wa viungo na fikra zake kufanya jambo fulani kwa upekee kabisa.
Ni
talanta ambazo mtu anazo siyo kwa sababu kasomea bali ni ujuzi wa
kuzaliwa nao, elimu inasaidia tu katika kumfanya atumie kipaji chake kwa
ufanisi na kwa manufaa zaidi.
Kwa mfano, michezo
mbalimbali, sanaa kama muziki, kuchora, kucheza mpira, kuimba, kusanifu,
kubuni programu za kompyuta, mitandao, kuchonga ni vipaji.
Wanachotakiwa kufanya ni kufanyia kazi vipaji vyao.
Watu
mashuhuri na waliofanikiwa ni wale waliotumia vipaji vyao vizuri. Kuna
mifano hai kama Filbert Bayi wa Tanzania alitumia talanta yake ya
kukimbia mbio.
Wanamuziki kama vile, Rose Muhando
wanatumia sauti yao kufanikiwa. Na hata wachezaji maarufu duniani
wanatumia vipaji vyao kucheza mipira wanafanikiwa kuliko hata wasomi
wenye shahada lukuki.
Wasanii na wana michezo wengi ni
miongoni mwa watu maarufu na matajiri duniani, japokuwa wengi hawana
elimu kubwa kiasi cha kushangaza, walichofanya ni kutumia vipawa vyao
kama ipasavyo.
Mungu alituumba na vipaji na talanta
nyingi tofauti ili tuvitumie kufanikiwa maishani. Kila mtu ana talanta
yake imejificha ndani ya umaizi wa akili yake.
Tunahitaji kuziibua ziliko talanta hizo na kuzitumia huku tukibadili mitazamo na kasumba.
Huwa nasikitika kumsikia Mtanzania anasimama kwenye chombo cha habari akidai yeye ni masikini na anahitaji msaada.
Wakati
huo kafunika talanta zake kibindoni, na nyumbani kaacha ardhi kubwa,
misitu mingi na hata watoto wengi ambao ni nguvu kazi muhimu katika
kuchangia maendeleo.
Wapo Watanzania wanaodiriki kusema
“sisi tutabaki kuwa maskini hivi hivi” na wengine wanadai umaskini wao
ni mpango wa Mungu. Huu ni uongo! Na ni dhambi.
Mungu
angetaka sisi tuwe maskini asingetupa ardhi kubwa, asingetupa mvua
nyingi na maji mengi, asingetupa samaki wengi, asingetupa madini,
asingetupa ndege na wanyama wengi wa mwituni.
Mungu
alitupatia hivi vyote ili tuwe matajiri tuwasaidie na wale wanaoishi
nchi zenye mawe tu, nchi zisizo na bahari, msitu, mto wala bwawa. Sisi
siyo maskini kamwe!
Pia kiongozi au mwanasiasa
anayetamka kuwa Tanzania ni masikini (wakati yeye ni tajiri) huyo ni
mpotoshaji. Tusiwafundishe watoto wetu mtazamo hasi hata kama tuna
changamoto.
Kuwa na matatizo ni sehemu ya changamoto za maisha, tunapaswa kuzikabili. Maana hakuna mtu au nchi inayejitosheleza.
Ndio maana hata hao walioendelea huko Ulaya bado wanakuja kwetu kununua malighafi ili wakatumie kwao.
Tena
nadhani hata walioita Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini
(Mkukuta) walikosea sana. Ingefaa ukaitwa “Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Ustawi wa Maisha ya Watu”.
Kuutaja umaskini wakati tumo ndani ya utajiri mkubwa na neema nyingi ni kujitafutia laana ya kudumu.
Maana kama tunakubali sisi ni maskini kamwe hatuwezi kuweka mikakati ya maendeleo. Tutabaki na mikakati ya kimaskini.
Nafadhaishwa
pia na mtazamo unaotaka kuzoeleka hapa Tanzania miongoni mwa vijana
kuwa mtu yeyote akifanikiwa kumiliki nyumba nzuri, shamba zuri lenye
mavuno mengi, gari zuri, kiwanda na hata kuwa na elimu nzuri anaitwa
fisadi; yaani mwizi.
Unakuta vijana wenye nguvu wanapita makazi ya watu wenye nyumba nzuri wanasema “umeyaona mahekalu ya mafisadi?”
Wanasema
hivyo wakimaanisha kuwa kila nyumba nzuri, kiwanda kikubwa, shamba
kubwa ni la fisadi au mwizi. Kwao; maendeleo ni wizi siyo jitihada za
kazi.
Hawa wamepotoka, umasikini siyo mpango wa Mungu wala siyo ngozi ya kuzaliwa nayo isiyobadilika.
Hata vitabu vitakatifu kama vile Biblia na Quran vimesema wazi kwamba umaskini siyo mpango wa Mungu.
Mungu
anataka kila mtu aishi maisha mazuri yenye ustawi, huku akimpenda na
kutii mwongozo wake. Kila binadamu anahitaji maisha bora.
Kila
binadamu anahitaji kulala pazuri, kula vizuri, kusafiri vizuri, afya
bora, kupata elimu bora, mazingira safi, kucheza pazuri na kufurahia
maisha kwa jumla. itaendelea
Watu wanakuwa kwenye shida
kama vile kuishi katika nyumba mbovu na kula chakula kibaya au
kisichotosheleza siyo kwa sababu wao wanapenda, au kudhani kuwa masikini
ndiyo sifa ya uadilifu. La hasha! Ni kwa sababu hawana.
Fikra
za kuyaona maendeleo ya mtu au kikundi cha watu ni ufisadi , ni dalili
ya kupoteza dira na kukosa matumaini kuelekea ufukara wa kudumu na dhiki
kuu. Itaendelea