Ngeleja awatumia Zitto, Mengi, Manji kujitetea
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja akiapa kabla ya kuanza kuhojiwa na Baraza la Sekretarieti ya Viongozi wa Umma, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame
Dar es Salaam. Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja jana alimtaja Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe na baadhi ya matajiri wanaowafadhili wabunge
nchini, kama sehemu ya utetezi wake mbele ya Baraza la Maadili ya
Viongozi wa Umma.
Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa
Nishati na Madini alikuwa anajitetea mbele ya baraza hilo kuhusiana
mgawo wa Sh40.4 milioni, aliopata kutoka kwa mfanyabiashara na mmiliki
wa Kampuni ya VIP Engeneering & Marketing Limited, James Rugemalira.
Pamoja
na kudai kuwa mgawo huo haukuwa na mgongano wa masilahi, Ngeleja
aliibua tuhuma mpya akihoji ni kwa nini Zitto hakuhojiwa na baraza kwa
kutuhumiwa kupokea fedha kutoka katika Kampuni ya Pan African Power
Solution (PAP), ambayo pia inahusishwa katika kashfa ya Akaunti ya
Tegeta Escrow iliyokuwa ndani ya Benki Kuu ( BoT) wala tuhuma za
kufadhiliwa na Mfuko la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mashtaka dhidi ya Ngeleja
Akimsomea
mashtaka, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,
Mwanaarabu Talle alidai kuwa Ngeleja akiwa kiongozi wa umma alipokea
fedha hizo kwenye akaunti yake namba 0011010265260 katika Benki ya
Mkombozi na hivyo kusababisha mgongano wa kimaslahi.
Wakili
Talle alidai kuwa kwa kupokea fedha hizo kutoka kwa kampuni hiyo,
Ngeleja alikiuka kifungu cha 6(e) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma, kinachozuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa
masilahi.
Pia wakili Talle alidai kuwa Ngeleja alijipatia manufaa ya kifedha kinyume cha kifungu cha 12 (1) (e) cha sheria hiyo.
Ushahidi wa sekretarieti
Baada
ya kumsomea mashtaka hayo, Ngeleja alikana na shahidi wa Sekretarieti,
Waziri Yahya akiongozwa na Wakili Talle alidai kuwa baada ya kuchunguza
walibaini kuwa Ngeleja alipewa Sh40,425,000 kutoka VIP Engeneering &
Marketing Februari 12, 2014.
Alidai kitendo cha
Ngeleja cha kupokea pesa hizo kumekiuka sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma ambayo hairuhusu kuomba, kupata au kupokea fedha.
Kwa
mujibu wa shahidi huyo, walibaini kuwa mwaka 2007 Ngeleja alikuwa Naibu
Waziri wa Nishati na Madini na kwamba kuanzia 2008 hadi 2012 alikuwa
Waziri wa Nishati na Madini ambapo aliendelea na majukumu ya kusimamia
utekelezaji wa mkataba kati ya Tanesco na IPTL ambayo VIP ilikuwa na
hisa.
Alidai kitendo cha Ngeleja baadaye kupokea fedha
kutoka kwa kampuni hiyo ni kujiingiza katika mgongano wa masilahi na
kwamba ni muhimu viongozi wa Serikali wakasimamia misingi ya maadili ya
viongozi, vinginevyo itasababisha wananchi wasiwe na imani na Serikali.
Akijibu
moja ya maswali kutoka kwa Ngeleja, shahidi huyo alidai kuwa ni si
vibaya wabunge kuomba misaada lakini akasema kuwa ni vema iwe katika
misingi ya sheria.
Pia alidai kuwa kwa uchunguzi wao msaada kutoka VIP ulikuwa ukichagua baadhi ya viongozi na si wabunge wote waliopewa.
Utetezi wa Ngeleja
Baada
ya kusikiliza ushahidi huo, Ngeleja ambaye hakuwa na mwanasheria,
alikiri kupokea fedha hizo kutoka kwa Rugemalira, akisema zilikuwa ni
msaada wa kawaida kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ndani na nje ya
jimbo lake.
Alidai kuwa msaada huo hautofautiani na
misaada ambayo wabunge wengine wamekuwa wakipewa na marafiki na
wafadhili mbalimbali na kwamba jambo hilo si geni na ndiyo maana hata
Bunge halijawahi kuona ni tatizo.
Ngeleja aliwataja
baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitoa misaada ya fedha kwa
wabunge kuwa ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, mwanzilishi
na Mwenyekiti wa Kampuni ya Bakhresa Group, Said Salim Bakhresa.
Aliwataja
wafanyabiashara wengine ambao wamekuwa wakiwapa misaada wabunge kuwa ni
mwenyekiti wa Quality Group, Yusufu Manji na mfanyabiashara Subhash
Patel.
Mbali na matajiri hao pia Ngeleja alidai kuwa
wabunge pia wamekuwa wakinufaika na ufadhili kama huo kutoka kwa taasisi
za umma na kampuni binafsi.
Alizitaja kuwa ni pamoja
na mifuko ya Hifadhi ya Jamii na taasisi za kifedha kama vile NSSF, PPF,
LAPF PSPF, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), benki za CRDB, NMB na
Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).
Ngeleja alizitaja
kampuni binafsi ambazo zimekuwa zikiwafadhili wabunge kama vile VIP
Engeneering & Marketing, Songas na IPTL, huku akidai kuwa hizo kwa
uchache tu kati ya orodha ndefu aliyo nayo.
Tuhuma kwa Zitto
Katika
namna ya kujinasua katika tuhuma hizo, Ngeleja alirejea tuhuma dhidi ya
Zitto zilizowahi kutolewa bungeni kwa nyakati tofauti za kujipatia
msaada kutoka katika taasisi za umma na kampuni binafsi.
Alinukuu
taarifa ya Kambi ya Upinzani bungeni wakati wa Bajeti ya Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo mwaka jana kuhusu uhalali wa Zitto
kupata msaada wa jumla ya Sh119 milioni kutoka NSSF na Shirika la
Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Alidai kuwa licha ya tuhuma hizo kuwasilishwa bungeni, mbunge huyo ni mwenyekiti wa PAC, na Bunge halikumwajibisha.
Tuhuma
nyingine dhidi ya Zitto ambazo Ngeleja alizirejea ni zile zilizotolewa
bungeni na Mbunge wa Mtela, Livingstone Lusinde kuwa alipewa zaidi ya
Sh30 milioni kutoka kwa kampuni ya PAP, inayohusishwa na escrow kwa
nyakati tofauti.
Huku akibainisha tarehe tofauti tofauti na kiasi
alichokuwa akipokea Zitto kutoka PAP, Ngeleja alidai kuwa licha ya
tuhuma hizo kuwasilishwa mezani kwa Spika, Bunge halikuchukua hatua.
Ngeleja
alidai kuwa licha ya Zitto kusema kuwa yuko tayari tuhuma hizo
zipelekwe kwenye Kamati ya Bunge ya Maadili, zichunguzwe bado Bunge
halikuchukua hatua.
Akizungumzia tuhuma hizo, Zitto
alisema alishajibu hilo bungeni na kuitaka tume ifanye uchunguzi wake na
ikigundulika amehusika kwenye lolote basi ahojiwe.
“Mheshimiwa
Ngeleja yeye alipaswa kujibu hoja zake na kama anadhani kuna tuhuma
azipeleke tume. Mimi naunga mkono kwa asilimia 100 kazi inayofanywa na
tume na kazi hiyo walipaswa wafanye siku nyingi,” alisema Zitto na
kuongeza:
“Analosema Ngeleja ni la juu juu tu, hivyo sekretarieti ifanye uchunguzi na kujiridhisha halafu ihoji.”
Ngeleja alikanusha
Hata
hivyo, Ngeleja ambaye alianza kuhojiwa saa 4.00 asubuhi hadi saa 7.30,
mchana alisema hakuomba wala kupokea fedha kutoka katika Kampuni ya VIP
Engineering & Marketing Ltd ya James Rugemalira kama ilivyodaiwa
kwenye mashtaka dhidi yake bali alimwomba Rugemalira fedha hizo kama mtu
binafsi ambaye alimpa Sh40 milioni kupitia akaunti ya VIP TZS Trust.
Vilevile
alisema fedha hizo alizipokea kupitia akaunti namba 00110102652601
iliyopo katika Benki ya Mkombozi tofauti na akaunti namba 00110102652660
inayosomeka kwenye hati ya mashtaka.
“Hakukuwa na
mgongano wa kimaslahi kwa sababu msaada huo niliupata baada ya wadhifa
wangu wa uwaziri kuwa umekoma, hivyo nisingeweza kufanya ushawishi
wowote,” alisema Ngeleja.
Akifafanua, alisema baada ya
kupewa fedha hizo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilimwandikia barua
ikitaka asilimia 30 ya kodi ya kiasi hicho na alilipa Sh13 milioni na
kubakiwa na Sh27 milioni.
“Kwa hiyo naomba ieleweke
kwamba kiasi nilichobakiwa nacho ni Sh27 milioni, ambazo nimezitumia kwa
ajili wa wananchi wa jimbo langu la Sengerema na Watanzania wengine,”
alisema Ngeleja.
Mahojiano
Mwanasheria: Huoni kwamba kuomba ni aibu?
Ngeleja:
Hata Serikali inaomba, haya ni maisha ya kisiasa, tunaomba ili kusaidia
wananchi hasa katika maeneo ambayo hakuna Bajeti ya Serikali.
Mwanasheria: Rugemalira alikueleza fedha hizo ni za nini?
Ngeleja:
Nilimwomba fedha hizo ili zinisaidie kwa ajili ya shughuli mbalimbali
za wananchi wa Jimbo la Sengerema na nje ya jimbo.
Mwanasheria: Ulipeleka fedha hizo kwenye Kamati ya Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kupanga matumizi ya fedha ulizoomba?
Ngeleja:
Hapana, kwa sababu Mfuko wa Jimbo ni fedha ambazo zinatokana na bajeti
ya Serikali. Hivyo siwezi kuchanganya fedha hizo kwa sababu kama mbunge
nimekuwa nikisaidia shughuli mbalimbali za kijamii kama vile ujenzi wa
misikiti na makanisa na fedha za mfuko wa jimbo haziwezi kusaidia katika
maeneo hayo.
Mujunangoma aweka pingamizi
Wakati
huohuo. Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma ameweka pingamizi katika baraza hilo
akisema ana kesi katika Mahakama ya Kisutu inayohusu mgawo wa Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Mashtaka ya Mujunangoma kwa mujibu wa
Talle, ni kwamba mtuhumiwa huyo alitoa ushauri wa kisheria kwa Kampuni
ya VIP Mabibo Wines and Spirit uliompatia Sh423.4 milioni kinyume na
kifungu cha 12 cha Sheria za Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mujunangoma
akiwakilishwa na wakili Jamhuri Johnson, alisema mbali na kesi iliyoko
katika Mahakama ya Kisutu pia kuna pingamizi ya Mahakama Kuu
linazozitaka taasisi mbalimbali zisijadili suala la Akaunti ya Tegeta
Escrow.
Wiki iliyopita Mbunge wa Bariadi Magharibi,
Andrew Chenge alipinga kuhojiwa na baraza hilo akisema Mahakama Kuu
ilizuia suala hilo kujadiliwa na taasisi yoyote.
Hata
pale mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu wa Hamis Msumi aliposema
baraza lina mamlaka ya kulijadili suala hilo, Chenge atakata rufaa
Mahakama Kuu.
Akitetea hoja hiyo, Wakili Johnson
alisema mteja wake ana kesi namba 11 katika Mahakama ya Kisutu inayohusu
masuala hayo ya mgawo wa Akaunti ya Tegeta Escrow.
Alisema mteja wake anapokuwa na kesi ya aina moja katika sehemu mbili tofauti hatapata nafasi ya kujitetea vizuri.
Jaji
Msumi baraza hilo litatoa uamuzi wake leo ili kuangalia kama shauri
hiyo liendelee au lisimame kusibiri kesi iliyoko katika Mahakama ya
Kisutu.