MAOMBOLEZO: Wananchi wamsaidia Nape ujumbe kwa Nyerere
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye (wa pili kulia) akishirikiana na wanamuziki wa nyimbo za dansi kuimba wimbo maalumu wa kumuaga marehemu John Komba katika Viwanja vya Karimjee juzi. Picha na Venance Nestory
Dar/Mikoani. Wakati wa kumuaga John Komba,
ambaye alikuwa mpiga kampeni mashuhuri wa CCM, kada wa chama hicho, Nape
Nnauye aliimba “Neenda baba… msalimie Mwalimu (Julius Nyerere), mweleze
hali ya Watanzania ilivyo hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo
wakati huu,” bila ya kutaja ikoje, lakini wananchi walioongea na gazeti
hili wamemalizia wimbo huo; wanaona hali ya nchi ni mbaya.
Nape,
katibu wa itikadi na uenezi na mtoto wa kada maarufu wa CCM, Marehemu
Moses Nnauye aliyetunga nyimbo nyingi za uhamasishaji, aliungana na
wasanii wa muziki wa dansi kuimba wimbo huo uliotungwa na Komba wakati
wa kifo cha Julius Nyerere, ambaye ni mwasisi wa Taifa la Tanzania
kwenye Viwanja vya Karimjee juzi.
Katibu huyo wa
Itikadi na Uenezi wa CCM aliongoza kuimba sehemu ya wimbo huo yenye
maishairi yasemayo “Kapteni Komba, familia yako umeiacha na nani, chama
chako umekiacha na nani. Nenda baba, msalimie Mwalimu, mweleze hali ya
Watanzania ilivyo hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo hivi sasa
hasa wakati huu, msalimie Mzee Kawawa Simba wa Vita”.
Baada
ya kuimba sehemu hiyo ya wimbo huo uliotungwa na Komba mwaka 1999
wakati kifo cha Mwalimu Nyerere na ambao umebadilishwa maneno na kupewa
jina la “Nani Yule”, waombolezaji mbalimbali walionekana kuguswa hisia
zao.
Wakati Nape akiwa amerudi nyuma na kuinamisha
kichwa chini, Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili,
Ali Hassan Mwinyi, Spika Anne Makinda, wabunge na viongozi wengine
walionekana kububujikwa na machozi.
Wengi waliohojiwa
walielezea kuwa nchi imejaa maovu yanayofanywa na watu wenye dhamana,
mamlaka na nyadhifa katika taifa, wakitaja ufisadi, rushwa, ubinafsi,
ubadhirifu na hata hali ya kisiasa kuwa mbaya na hivyo hayo ndiyo
angeelezwa Mwalimu Nyerere, ambaye aliongoza harakati za uhuru wa
Tanganyika na anasifika kwa kupinga maovu hayo kwenye jamii.
“Kwa
mtazamo wangu, kama Komba akikutana na Nyerere ningependa amwambie
kwamba, Tanzania ya leo inanuka rushwa viongozi wa Serikali hawana
maadili, bora angekuwepo yeye,” alisema Gervas Mbaya, mkazi wa Nyegezi
wilayani Nyamagana, Mwanza.
Imani Hezron, Mkazi wa
Nyakato alisema: “Amwambie Mzee Nyerere kwamba alipoondoka aliacha
kilimo kama uti wa mgongo wa taifa, leo si hivyo tena, na taifa
halipigani vita kuondoa umasikini ujinga wala maradhi.”
Mkazi
mwingine anayeishi Chuo Kikuu cha St Augustine cha Mwanza, Sarah
Onesimo, alisema: “Ningependa amwambie Mwalimu Nyerere kuwa Tanzania
imechafuka kwa mauaji ya albino... mauaji yanazidi kuongezeka, huku
jitihada ya kudhibiti hazionekani na kama angejaliwa kuwepo, pengine
yote haya yasingetokea.