FORBES: Dewji sasa bilionea kijana Afrika
Dar es Salaam. Mfanyabiashara maarufu
nchini na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohammed Dewji (pichani) kwa
mara ya kwanza ameingia kwenye orodha ya mabilionea 29, akiwa tajiri
kijana kuliko wote barani Afrika.
Jarida la Forbes la
Marekani limemtaja Dewji (39), katika nafasi ya 24 ya matajiri wa Afrika
akiwa na utajiri wa Dola 1.3 bilioni za Marekani (Sh2.34 trilioni)
unaotokana na biashara mbalimbali anazozifanya kupitia kampuni yake ya
Mohammed Enterprises (Metl Group).
“Dewji alibadilisha
biashara aliyoanzisha baba yake kutoka uuzaji bidhaa na kuwa na
viwanda vya Metl,” inasema sehemu ya habari inayomuhusu bilionea huyo
Mtanzania iliyochapishwa juzi jioni.
“Alinunua viwanda
vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei ndogo na
kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa
menejimenti,” inaongeza ripoti hiyo.
Metl ina viwanda
vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo
vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni
za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.
Katika kampuni
hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama
Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.
Kwa
mujibu wa tovuti yake, Metl inaendesha shughuli za uagizaji na
usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo,
vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji
baiskeli.
Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Dewji anashika nafasi mbili juu zaidi ya kada maarufu wa
CCM na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, Aziz Rostam (50) aliyewekwa
nafasi ya mwisho.
Rostam amefungana nafasi ya 26 na
mabilionea wa Nigeria, Abdulsamad Rabiu na Femi Otedola wenye utajiri wa
Sh1.8 trilioni kila mmoja.
Orodha hiyo ya 29 bora
inaoongozwa na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote akiwa na utajiri wa
Dola 15.7 bilioni za Marekani (Sh28.2 trilioni), kiwango ambacho ni mara
moja na nusu ya bajeti ya Serikali ya Tanzania ya mwaka 2014/15.
Forbes
linamtaja Rostam kuwa na utajiri wenye thamani ya Dola 1 bilioni za
Marekani (Sh1.8 trilioni), kiwango ambacho kimebaki pasi na mabadiliko
kutoka orodha ya mwaka jana. Rostam anamiliki asilimia 35 ya hisa
katika kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Vodacom.
“Anamiliki
pia Kampuni ya Ukandarasi ya Madini ya Caspian ambayo hutoa huduma kwa
kampuni kubwa za madini kama BHP Billiton na Barrick Gold (Accasia
Gold),” ilibainisha habari hiyo. “Caspian inamiliki pia kampuni nyingine
za dhahabu, shaba na chuma, Tanzania,” iliongeza.
Jarida
hilo lilibanisha kuwa, Rostam ana miliki nyingine katika Bandari ya Dar
es Salaam ambaye yeye ni mbia na Kampuni ya Hutchison Whampoa.
Pia, utajiri wake unatokana na uwekezaji katika tasnia ya maendeleo ya makazi Tanzania, Dubai, Oman na Lebanon.
Ripoti
ya Forbes inaenda sanjari na ile ya Jarida ya Ventures Afrika
iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana, ambayo iliwataja Dewji na Rostam
kuwa ndiyo mabilionea pekee walioingia kwenye orodha ya ‘mabepari’ 55
barani Afrika. Katika orodha ya ripoti ya jarida hilo, Dewji alikuwa
nafasi ya 24, sawa kabisa na anayoshikiria sasa kwenye orodha ya Forbes,
akiwa na utajiri wa Dola za Marekani 2 bilioni (Sh3.6 trilioni).