Luku yazua tafrani Mbeya
Wananchi jijini Mbeya wakiwa nje ya ofisi za Shirika la Umeme (Tanesco), kitengo cha huduma kwa wateja baada ya kufunga ofisi hizo kwa madai ya kutopewa majibu sahihi juu ya matatizo ya kulipia umeme kwa njia ya mtandao. Picha na Godfrey Kahongo.
Mbeya/Dar. Wakazi wa jijini hapa jana
walizua tafrani baada ya kufunga ofisi za Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) kwa muda wakidai kupewa majibu kuhusu tatizo la upatikanaji wa
umeme lililodumu kwa zaidi ya siku tano.
Tukio hilo
lilitokea jana saa 4:00 asubuhi baada ya wateja hao kusubiri majibu
kutoka kwa wahusika, ambao awali walitangaziwa kuwa huduma hiyo ingeanza
kupatikana juzi, lakini mpaka jana tatizo hilo lilikuwa likiendelea.
Wakazi
hao waliwafungia wafanyakazi wa Tanesco wa kitengo cha malipo, wakisema
kuwa hawafanyi kazi yoyote na hivyo hawatakiwi kutoka nje. Hali hiyo
ilidumu hadi askari wa walipowasili na kuwashauri waondoke.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti ofisini hapo, wateja hao walisema baada ya
kukosekana kwa huduma ya luku kwa siku tatu, jana kupitia simu zao za
mkononi walipokea ujumbe uliowataarifu kuwa huduma hiyo ingeanza
kutolewa jana kwa mawakala na katika ofisi za Tanesco, hata hivyo hali
haikuwa hivyo.
Mkazi wa Mwanjelwa, Dickson Mwangunga alisema watendaji wa shirika hilo wanatoa taarifa zisizo sahihi na kusababisha usumbufu.
“Ni
vema kama wangetoa taarifa sahihi, watu tumefika hapa kwa ajili ya
kununua umeme, lakini huduma hiyo haipo. Baadhi yao wanatuambia eti hali
bado haijatengemaa, wengine wanasema tusubiri na muda unazidi kwenda,
sasa nani mkweli? ndiyo maana tumeamua kuzifunga ofisi zao watupe jibu
sahihi lini huduma hii itatengemaa,” alisema Mwangunga.
Hata
hivyo, sakata hilo liliokolewa na mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Mbeya,
Kitinkwi Mtatiro ambaye alifika katika ofisi hizo na kuwaomba wateja
hao warejee nyumbani hadi watakapopewa taarifa ya kurejeshwa kwa huduma
na uongozi wa Tanesco.
“Nawaomba mfungue milango ya
ofisi, waacheni wafanye kazi hili ni tatizo limetokea. Hata wao
hawapendi karaha hii itokee ni vema mkawa watulivu msipende kujichukulia
sheria mkononi. Jambo hili linaweza kuvuruga amani,” alisena Mtatiro.
Akizungumzia
hali hiyo, meneja wa Tanesco wa Mbeya, Amos Maganga aliwaomba wananchi
kuwa watulivu kwa kuwa tatizo hilo ni la kitaifa na mara mitambo
itakaporekebishwa watajulishwa kupitia simu zao za mkononi.
Dar es Salaam
Jijini Dar es Salaam, wananchi waliendelea kulia na tatizo hilo lililodumu kwa siku tatu mfululizo.
Baadhi
yao wamelalamikia hasara wanayoipata kwa sababu ya kukosa umeme na
kushindwa kufanya kazi za uzalishaji zinazotegemea uwapo wa umeme.
Februari
28, Mkoa wa Dar es Salaam ulianza kukabiliwa na tatizo la mtandao
ambalo lilikwamisha mawakala wa Luku kuuza umeme, huku Tanesco walikidai
kuwa lilisababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa mtandao.
Mahamudu
Ilihaji, anayetoa huduma ya usagishaji eneo la Tandale, alisema
kukosekana umeme kwa siku mbili kumewasababishia hasara kubwa.
Alisema akifanya kazi siku nzima huwa anakusanya zaidi ya Sh150,000, lakini amesikosa kutokana na ukosefu wa umeme.
Mkazi
mwingine wa Mbagala Majimatitu, Zuwena Shomari alisema: “Tanesco
wenyewe wala hawasemi ukweli, ukihoji kupitia huduma kwa wateja wanajibu
kwa kifupi tu eti sababu ni mtandao.”
Ofisa uhusiano
wa Tanesco, Adrian Severin alisema shirika hilo haliwezi kuwalipa fidia
wateja wake kutokana na hasara wanayoipata kutokana na tatizo la
kukosekana kwa umeme wa Luku.
Severin alisisitiza kuwa
utoaji wa umeme ni huduma kama nyingine na linapotokea tatizo, uongozi
hutoa taarifa na kuwaomba radhi wananchi wakati wakiendelea kuchukua
hatua za haraka kutatua tatizo linalojitokeza.
Hata hivyo, Severin alisema tatizo hilo tayari limeshapatiwa ufumbuzi katika maeneo mengi toka jana mchana.