Nchi kukumbwa na ukame
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za masika katika
kipindi cha Machi mpaka Mei na kusema kuwa hali ya mvua haitarajiwi kuwa
ya kuridhisha katika maeneo mengi ya nchi.
TMA imesema kuwa kutokana na kuwapo kwa kiwango hicho cha mvua, maeneo mengi yatakumbwa na ukame.
Hayo
yalisemwa jana na mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alipokuwa
akitoa mwelekeo wa hali ya hewa katika maeneo mengi ya nchi ambayo
hayajapata mvua za masika za kutosha.
Aliitaja mikoa
inayotarajiwa kupata mvua za wastani mpaka chini ya wastani kuwa ni
Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Unguja na Pemba, Morogoro, Kilimanjaro,
Arusha na Simiyu.
Mikoa mingine ni Singida, Dodoma,
Tabora, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Kigoma, Shinyanga na
Manyara ambayo pia inatarajiwa kupata kiasi kidogo cha mvua.
Dk Kijazi alisema Kanda ya Ziwa inayohusisha mikoa ya
Mwanza, Geita, Mara na Kagera inatarajiwa kupata mvua za wastani mpaka
juu ya wastani.
Akizungumzia utabiri huo katika sekta
ya kilimo, Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Karim Mtambo aliwataka
wakulima wanaoishi katika maeneo yatakayopata mvua chini ya wastani
kulima mazao yanayokomaa haraka na kustahamili ukame.
“Mikoa
ya kanda ya Ziwa Victoria inaweza kupata mvua za wastani mpaka juu ya
wastani, hivyo mamlaka husika zinapaswa kujiandaa kwa hali yoyote
inayoweza kujitokeza,” alisema Dk Kijazi.
“Wasimamizi
wa maeneo ya utalii wachukue hatua ya kuzuia uharibifu wa miundombinu ya
barabara na madaraja katika mbuga zilizo karibu na maeneo ya Ziwa
Victoria.”
Mtaalam wa Afya ya Jamii kutoka Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii, Jubilate Benard alisema kuna hatari ya kutokea
kwa magonjwa ya mlipuko kwenye maeneo yatakayopata mvua nyingi.