Kamati ya Zitto yataka ATCL mpya kuundwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Zitto Kabwe akizungumza jambo wakati wa kikao cha kamati hiyo na wadau wa Sekta ya Utalii na Usafiri Dar es Salaam jana. Kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), imetoa
siku 113 kwa Msajili wa Hazina (TR), Lawrence Mafuru kukamilisha mpango
mkakati wa kuanzisha upya Shirika la Ndege Tanzania kwa kushirikiana na
Mamlaka za Hifadhi za Ngorongoro na Tanapa.
Kauli hiyo
ilitolewa kwenye ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam wakati wa kikao cha
mashauriano baina ya TR, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) na Kamati hiyo kilichofanyika jana na kukubaliana kuwa TR asimamie
mchakato huo.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema:
“Baada ya majadiliano kamati inamuagiza TR asimamie mchakato huu ambao
umekwisha anza miaka miwili iliyopita kuhakikisha ifikapo Juni 30, iwe
imewasilisha ripoti yake kabla ya Bajeti ya Serikali kuleta mpango
mkakati huo.”
Zitto aliongeza kuwa, “Tunataka kuwa na
shirika jipya linaloweza kujiongoza na TR ndiye ana wajibu wa hilo,
mchakato huu ulipoanza haukuwa umesimamiwa vizuri kwani hata TR mwenyewe
hakuwa anaufahamu lakini sasa tunamkabidhi jukumu hilo yeye mwenyewe.”
Alisema mapato wanayopata Tanapa na Ngorongoro yanaweza kununua ndege na wala si kuchangia mapato kama ilivyokuwa awali.
Kwa
upande wake, Mafuru alisema: “Mimi nitakwenda kutumia taarifa za kamati
ambazo zilikwisha undwa na kuangalia jinsi gani shirika litafufuliwa
pamoja na maoni ya kamati kisha nitakuja na kile ambacho kamati
imekipendekeza.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL), Salim Msoma alisema, suala la wawekezaji hususani wa
nje halitakiwi kutegemewa kwani linapokuja katika utekelezaji wake,
miradi yake inakuwa na changamoto nyingi.