Ufisadi wa kutisha waibuliwa
Waziri wa Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli akikagua ujenzi wa kituo cha Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (BRT) Morocco jijini Dar es Salaam siku za hivi karibuni. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Machungu ya Watanzania yakiwa hayajapoa
kutokana na kashfa ya Sh306 bilioni kutoka katika Akaunti ya Tegeta
Escrow, ufisadi mwingine wa zaidi ya Sh252 bilioni umeibuliwa na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa
Assad ndani ya wizara ya ujenzi.
Ukaguzi maalumu
uliofanywa na ofisi ya CAG katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 na
2011/12 umebaini kuwa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi, Dk John
Magufuli, bungeni Novemba 2013 kuwa fedha hizo zilitumika kwa miradi ya
ujenzi wa barabara, haikuwa sahihi.
Kutokana na ufisadi
huo, habari zilizolifikia Mwananchi zinasema CAG amependekeza hatua
stahiki zichukuliwe kwa wahusika wa wizara ya ujenzi na wakala wa
barabara ili kuleta imani na uwazi katika bajeti kwa jamii na wahisani.
“Wizara
(ya ujenzi) ililidanganya Bunge kuwa kuna ujenzi wa barabara hizo
wakati wakijua kwamba walikusudia kulipa madeni ya wakandarasi na
washauri wa ujenzi wa barabara...mpango mkakati wa wakala wa barabara wa
mwaka wa fedha 2011/12 pamoja na manunuzi ulioidhinishwa havikuonyesha
utekelezaji wa mradi huo,” chanzo cha habari kilikariri ripoti ya CAG.
Matumizi
hayo yasiyo sahihi yaliibuliwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
Novemba 22, 2013 baada ya kutilia shaka kiasi hicho cha fedha na ofisi
ya CAG kuagizwa kufanya ukaguzi.
Katika kikao hicho
ambacho wizara ya ujenzi iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake wa wakati
huo, Balozi Herbert Mrango alihojiwa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe
kuhusu hati ya mashaka waliyoipata kutoka kwa CAG mwaka 2011/12.
Kamati
hiyo ilieleza kuwa kwenye Bajeti ya mwaka huo Sh348.1 bilioni
zilizokuwa zimetengwa chini ya fungu lililokuwa limetajwa kuwa ni la
mradi maalumu hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa bungeni.
“Ni
vizuri leo (ilikuwa Novemba 22 mwaka 2013) uiambie kamati fedha hizi
ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika kwa jambo gani. Tunajua kwamba
fedha hizi zilipunguzwa Sh95 bilioni na kupelekwa Wizara ya Uchukuzi,
zilibakia Sh252.975 bilioni katika kifungu hicho lakini kuna bilioni 100
zimetumika visivyo,” alisema Zitto.
Alisema katika
majumuisho ya bajeti wizara hiyo, Dk Magufuli na Dk Harrison Makyembe
aliyekuwa Naibu waziri wa wakati huo aliyekuwa Waziri wa Sera, Uratibu
na Bunge, William Lukuvi walitoa maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu
fedha hizo.
Zitto alikariri maneno yaliyorekodiwa kwenye Hansard ya Bunge yaliyosemwa na viongozi hao watatu.
“Tunaomba fedha Sh252 bilioni kwa ajili ya kuanzia kazi za ujenzi wa barabara.”
“Fedha
hizi zitachangia miradi ya wafadhili,” haya yalikuwa maneno ya Dk
Makyembe ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati
akifafanua majumuisho.
“Hizi ni fedha kwa ajili ya
Counterpart fund,” alimkariri Lukuvi ambaye sasa ni Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati akichangia hotuba ya wizara hiyo.
Chanzo
cha habari kimeeleza kuwa ripoti ya CAG imeeleza kuwa, “Katika kikao
cha kuanza ukaguzi huo Aprili 3, mwaka jana uongozi wa wizara
ulithibitisha kwamba hakukuwa na barabara mpya bali walifanya hivyo
baada ya kuona madeni yamekuwa makubwa kiasi cha Sh420 bilioni kama
yalivyokuwa kwenye hesabu za wakala wa barabara za mwaka wa fedha
2010/11.”
Katika ukaguzi huo imebainishwa kuwa Sh3 bilioni hazikujulikana matumizi yake.
Taarifa
zaidi zinasema baada ya wizara kupeleka fedha kwa wakala wa barabara,
fedha hizo zilifanyiwa mchakato wa kuzigawa upya lakini nyaraka halisi
zilizotumika kugawa fedha hizo hazikuwasilishwa kwa ukaguzi.
“Hata
hivyo, kati ya Sh175.3 bilioni zilizopitia kwenye akaunti ya maendeleo
ya wakala wa barabara, kiasi cha Sh3,048,365,229 hakikuweza kupatiwa
maelezo jinsi kilivyotumika.
“Pia, kati ya malipo ya
Sh77.7 bilioni yaliyofanyika kwa wakandarasi au washauri wa barabara
moja kwa moja kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Novemba 30, mwaka
2011 kupitia barua ya kumbukumbu namba GA.65/263/01/VOL.XI Gavana Mkuu
wa BoT, alikanusha kulipa asilimia 30 ya fedha hizo Sh30.6 bilioni.
“Gavana
wa BoT amekanusha kulipa Sh30.6 bilioni kwa kampuni ya M/S Strabag
Internationl Gmbn na M/S China-Engineering Corporation Co, kati ya
Sh77.7 ambacho kilipelekwa BoT kwa ajili ya malipo kwa wakandarasi au
washauri mbalimbali,” alifafanua zaidi mtoa habari hizi na kuongeza:
“Ukaguzi
maalumu umeshindwa kuthibitisha malipo yenye jumla ya Sh47.1 bilioni
sawa na asilimia 61 kama yalilipwa kwa walengwa waliokusudiwa kwa sababu
Gavana wa BoT amesema kuwa kisheria hatakiwi kutoa taarifa za wateja.”
Pia,
habari za ndani kutoka ofisi ya CAG zinadai kuwa, Sh13.4 bilioni za
ujenzi wa barabara za mikoa zilitumika kulipia barabara binafsi na za
halmashauri za wilaya ambazo hutengewa fedha kupitia mfuko wa barabara
kinyume na makusudio yaliyopitishwa na Bunge.
“Pia,
nimebaini kwamba baadhi ya miradi haikuwamo kwenye kasma zilizopitishwa
na Bunge kwenye makisio ya mwaka wa fedha 2010/11 na miradi mingine
ilitengewa fedha kidogo lakini wakala wa barabara alitumia fedha nyingi
kulipia miradi hiyo bila kuonyesha jinsi alivyozipata,” chanzo cha
habari kimekariri ripoti ya CAG.
Katika ukaguzi huo,
ufisadi mwingine wa Sh36.6 bilioni ambazo ni malipo ambayo hayakutolewa
taarifa kwenye ripoti za washauri au wakandarasi, jambo linaweza kuwapo
kwa uwezekano mkubwa wa wakandarasi kuidai Serikali zaidi ya mara moja
na kuitia Serikali hasara.
Mtoa habari wetu alisema
kuwa Sh6.2 bilioni zilitumika kuwalipa wakandarasi ambao hawakuonyeshwa
katika orodha ya madeni yaliyowasilishwa bungeni pamoja na malipo ya
Sh6.6 bilioni yaliyokwishalipwa yaliombewa tena.
“Madeni
hayo yalikuwa yamelipwa na wakala wa barabara katika mikoa husika. Hali
hii inaashiria kwamba kwa hati ya madai moja kuna uwezekano wa
mkandarasi kulipwa mara mbili au zaidi.
Katika
mapendekezo ya jumla, chanzo chetu kimesema ofisi ya CAG imeishauri
Serikali kusimamisha kuingia mikataba mipya ya ujenzi wa barabara na
ilipe madeni ya wakandarasi yaliyopo kwa sasa ili kuepuka ukuaji wa deni
hilo kwa siku za baadaye na kuwa mzigo kwa Taifa na wananchi.
“Serikali
ihakikishe inaheshimu mikataba iliyowekwa kati yake na wakandarasi ili
kuepuka malipo yenye riba na kushtakiwa na wakandarasi kutokana na
kuvunja masharti yaliyowekwa kwenye mikataba,” kilifafanua chanzo chetu
na kuongeza:
“Zabuni za ujenzi wa barabara mpya
ziendane na fedha zilizotengwa katika mwaka wa fedha husika kama
itakavyokuwa imeainishwa katika mpango wa manunuzi wa mwaka huo.”
Ukaguzi
huo maalumu uliohusisha miradi 46 ya ujenzi wa barabara kuu na barabara
za mikoa ambazo wakandarasi na washauri wa ujenzi wa barabara walitoa
huduma kwa wakala wa barabara.
“Mbali na miradi hii 46,
miradi yote ya wakala wa barabara ilikuwa imezalisha madeni ya jumla ya
Sh420 bilioni kama yalivyo kwenye hesabu za wizara kufikia mwaka wa
fedha 2010/11,” kilieleza chanzo chetu.
Sakata hili
limeibuka wakati lile la uchotwaji wa fedha za Akautni ya Tegeta Escrow
halijapoa na hadi sasa limesababisha Rais Jakaya Kikwete kufanya
mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kufuatia kumfukuza kazi,
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
huku Profesa Sospeter Muhongo alitangaza kuachia wadhifa wa Waziri wa
Nishati na Madini.
Mbali na hao, pia Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Jaji Frederick Werema alitangaza kujiuzuru huku Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akimsimamisha kazi, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi kupisha uchunguzi wa sakata hilo.
Katika
mlolongo wa hatua za kinidhamu kuchukuliwa, baadhi ya watumishi wa umma
wamefikishwa mahakamani na wengine mbele ya Baraza la Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma.