Dk Slaa: Nalindwa na Mungu
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
amesema analindwa na Mungu na ndiyo maana chama hicho kimegundua mpango
wa mlinzi wake kushawishiwa na maofisa usalama wa taifa ili kumwekea
sumu katika chakula au maji.
Mlinzi huyo (jina
tunalihifadhi kwa sasa) ambaye alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha
polisi cha Oysterbay juzi, pia anadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa CCM
kuiba siri za chama hicho.
Tayari polisi imeanza
kuchunguza taarifa hizo na jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni,
Camillius Wambura aliliambia gazeti hili kuwa mtuhumiwa huyo ana haki
kama watuhumiwa wengine wanaofikishwa polisi wakikabiliwa na kesi za
jinai na kusisitiza kuwa; “Tuhuma zinazomkabili ni za kawaida na
tunazichunguza.”
Akieleza alivyopokea taarifa hizo Dk
Slaa alisema, “Ninalindwa na Mungu ndivyo ninavyoweza kusema. Chadema
sisi huwa tunaanza na Mungu na kumaliza na Mungu. Ushahidi umewekwa wazi
na hili ni jambo la kweli na limenigusa kwa kiasi kikubwa.”
Alisema
baadhi ya mambo yaliyofanywa na mlinzi wake ameyaona kwa macho na
kusisitiza kuwa njama zinazofanywa na wanaomtumia haziwezi kukiondoa
chama hicho katika harakati zake za kila siku.
“Tupo
makini ndiyo maana tumebaini yote. Tunawajua waliohusika na tupo makini
katika kuwafuatilia. Kama Mungu yupo upande wetu tumuogope nani zaidi,”
alisema.
Alisema Chadema ina safari ndefu hivyo ni
lazima wana-Chadema kuvaa viatu ili kujikinga na vumbi na uchafu wa kila
aina, akimaanisha kuwa chama hicho kinakumbana na vikwazo vingi.
Tuhuma
dhidi ya mlinzi huyo zilitolewa juzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema, Mabere Marando kuwa wamebaini nyendo za mlinzi huyo na
kuzifuatilia kwa ukaribu hadi kupata taarifa hizo alizosema ni ukweli
mtupu.
Hili ni tukio la tatu kwa Chadema kudai kuna
mipango ya kumfuatilia Dk Slaa, mara ya kwanza ilikuwa Februari 2009
alipobaini kutegewa vinasa sauti hotelini mkoani Dodoma na mkakati
uliotajwa kuwa wa kuwaua yeye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akieleza jinsi walivyombaini mlinzi huyo, Marando
alisema pamoja na ushahidi wa mawasiliano ya simu, lakini pia mlinzi
huyo alikiri kwa kinywa chake kutumiwa na maofisa hao ambao hakuwataja
majina lakini alisema wako 22.
“Mlinzi alitueleza
kwamba alikuwa akipewa fedha kwa ajili ya kutoa siri za vikao vya chama
kupitia simu yake…kwa kuwa anaruhusiwa kuingia kwenye vikao vya chama
hicho kama mlinzi amekuwa akitegesha simu yake ili kuwapa taarifa watu
wa CCM `live’ ili wasikie kila kinachojadiliwa,” alidai Marando.
Marando aliyewahi kuwa ofisa wa usalama wa taifa na kuongeza kuwa wako mbioni kufikisha suala hilo polisi.
Mipango yenyewe
Akifafanua
namna mipango hiyo ilivyofanywa, Marando alidai walibaini mlinzi huyo
kutumiwa muda wa maongezi kwa nyakati tofauti wa jumla ya Sh7 milioni
kwenye simu zake.
Marando alisema, “Kilichokuwa
kinatokea ni kwamba kigogo wa CCM (anamtaja) na wenzake walikuwa
wanasikia kila kinachozungumzwa kutoka kwenye vikao vya ndani vya
Chadema kwa sababu ya mlinzi huyo.”
Kigogo huyo wa CCM
hakupatikana juzi na jana kujibu tuhuma dhidi yake, lakini ofisa mmoja
wa makao makuu alisema taarifa hizo zimewafikia na zitajibiwa kwa njia
rasmi.
Kadhalika, Marando alisema walibaini kuwa mlinzi
huyo amekuwa akizungumza kwa simu kwa saa mbili hadi tatu na maofisa
usalama hao ili kuwapa taarifa mbalimbali za chama.
Marando
alisema kwa miaka miwili mfululizo mlinzi huyo amekuwa na mawasiliano
ya mara kwa mara na ofisa mmoja usalama wilayani Kinondoni ambaye ana
uhusiano wa karibu na kigogo huyo wa CCM.