Tumia vipaji vyako ufanikiwe maishani-2
Hoja yangu tangu wiki iliyopita ni umuhimu wa kubaini vipaji tulivyojaliwa na Mungu na kuvitumia kufanikiwa maishani.
Kipaji
ni umahiri wa kipekee alioweka Mungu ndani ya akili ya mtu unaoongoza
usadifu wa viungo na fikra zake kufanya jambo fulani kwa upekee kabisa.
Ni
talanta ambazo mtu anazo siyo kwa sababu kasomea bali ni ujuzi wa
kuzaliwa nao, elimu inasaidia tu katika kumfanya atumie kipaji chake kwa
ufanisi na kwa manufaa zaidi.
Ni tunu muhimu za
mafanikio ambazo Mungu amewekeza ndani ya kila mtu mfano michezo
mbalimbali, sanaa kama muziki, kuchora, kucheza mpira, kuimba, kusanifu,
kubuni, kuvumbua, mitandao, kuchonga.
Ni kosa kubwa
kuishi kwa kuiga maisha ya watu wengine kana kwamba wewe ni nakala ya
wengine. Nilisema wiki iliyopita kuwa watu mashuhuri na waliofanikiwa ni
wale waliotumia vipaji vyao vizuri.
Wasanii na
wanamichezo wengi ni miongoni mwa watu maarufu na matajiri duniani,
japokuwa walio wengi hawana elimu kubwa. Walichofanya ni kutumia vipaji
na vipawa vyao kikamilifu.
Kumbuka pia kuwa ili
ufanikiwe ni lazima uamue kufanikiwa. Pamoja na mambo yote muhimu ambayo
nimetangulia kuyasema, bado unahitaji kufanya uamuzi thabiti ili
ufanikiwe.
Uamuzi unaochochewa na utashi mkubwa wa kutaka kufanikiwa ndiyo utakaokufunulia hazina ya utajiri ulionao.
Watu
wengi hawana utashi wa kufanikiwa, najua hata baada ya kupata elimu
nzuri au kusoma vitabu na kupokea ushauri mbalimbali bado wanaendelea
kuishi na kufanya kama walivyozoea kufanya kwa sababu hawana uamuzi wa
kutaka kubadilika kutoka kwenye hali duni ya maisha kwenda kwenye hali
nzuri.
Ili ufanikiwe lazima uamue kwa vitendo kwamba
sasa umechoshwa na umasikini na ufanye kila kitu ulichoshauriwa kufanya
mpaka ufanikiwe.
Haitoshi kuwa na malengo makubwa kama hutaamua kuyatimiza kwa vitendo. Mafanikio ni wewe na uamuzi wako.
Ukiwaza
umasikini utakuwa na vitendo vya kimaskini, utajenga mitazamo na tabia
za kimasikini na utaishi kwenye umasikini. Mawazo yaujazayo moyo wako
huamua hatima yako.
Pamoja na yote, usikate tamaa. Mtu aliyeamua kufanikiwa huwa hakati tamaa hata kama atashindwa mara kadhaa hakati tamaa.
Ukishafanya
uamuzi hakikisha unabaki katika lengo lako iwe masika au kiangazi,
wakati wa joto au baridi wewe songa mbele mpaka kieleweke, usikate
tamaa.
Mafanikio ni safari ndefu, siyo kitu cha mara
moja kama muujiza au bahati nasibu kama wengi wanavyodanganywa na kuliwa
pesa zao katika michezo ya bahati nasibu na kubaki wanalalamika pasipo
kufanikiwa.
Wengi wameua akili zao na jitihada zao kwa kutegemea
michezo ya bahati nasibu kwenye kumbi za starehe, kwenye simu za mkononi
na pia bahati nasibu za wajanja wanaotumia miujiza kwenye nyumba za
ibada. Kamwe hutafanikiwa!
Hakuna ushahidi wa mtu au
taifa fulani lililoendelea kwa kupitia bahati nasibu au miujiza. Hakuna!
Maendeleo ni fikra, ni sayansi, ni kazi ni kujituma na kuchangamkia
fursa.
Unahitaji kulenga mbali na kuwa na bidii ili
ufanikiwe. Unapokutana na ugumu katika safari yako ya mafanikio
usichoke, watu wengi waliofanikiwa ni wale walioshindwa mara nyingi
lakini hawakukata tamaa, kila waliposhindwa, walijifunza kitu,
wakaboresha mbinu za kufanyakazi, wakazidi kurudiarudia mpaka
wakafanikiwa.
Abraham Lincoln ni miongoni mwa marais
ambao hawatasahaulika Marekani. Lakini historia yake inaonyesha alianza
kushindwa akiwa na umri wa miaka 22.
Alifanya biashara
akashindwa kwa kupata hasara kiasi cha kufilisika, baada ya hapo akaamua
kuingia kwenye siasa ambako pia alishindwa katika chaguzi kwa awamu
tano tofauti huku akijaribu kuendeleza biashara yake lakini hata hivyo
bado alifilisika mara ya pili. Kibaya zaidi, mke wake akafariki miaka
hiyohiyo.
Alipohojiwa nini anatarajia kufanya baada ya
shida na kushindwa karibu katika kila alichofanya alijibu “Nitagombea
umakamu wa Rais”. Ni kweli aligombea lakini hakupata ushindi bali
aliongeza aibu nyingine kwa kushindwa mara ya sita. Alipohojiwa tena
kwamba anajisikiaje kwa kushindwa kote huko, alisema yeye hajashindwa
hata mara moja bali alikuwa anapata uzoefu.
Uchaguzi
uliofuata aligombea nafasi ya urais na kupata ushindi mkubwa, alikuwa
Rais wa Marekani akiwa na umri wa miaka 51. Je, angekata tamaa
ingekuwaje?
Ni wale wanaoshindwa kwa kiwango kikubwa
ndiyo wanaofanikiwa kwa kiwango kikubwa, ikiwa hawatakata tamaa. Kila
historia ya mafanikio inatokana na historia ya kushindwa, usiogope
kuchekwa.
Jambo la msingi pia la kukumbuka, huu ni
ulimwengu wa ujuzi na maarifa ya sayansi hivyo ukitaka kufanikiwa ongeza
ujuzi na maarifa bila kuchoka. Katika mafanikio kinachowafanya wengi
washindwe ni kukosa ujuzi wa kutosha.
Tunaposema ujuzi
hatumaanishi kwenda shule na kupata vyeti pekee japokuwa nayo ni hatua
ya kupata ujuzi. Lakini ujuzi ni zaidi ya mtu kuwa na vyeti, ujuzi ni
zaidi ya maarifa, ujuzi ni uwezo wa kutenda na kuleta matokeo chanya
kama ilivyokusudiwa au zaidi ya kilichotarajiwa.
Katika
mbio za mafanikio kinachouzika ni ujuzi siyo maarifa ya nadharia.
Utakubaliana nami kwamba wapo watu wengi ambao wamesoma na wana vyeti
vizuri lakini mambo yao kwa ujumla ni ovyo, hakuna uwiano kati ya elimu
yake na maisha yake kwa jumla. Mafanikio ni matokeo ya matumizi ya
maarifa na ujuzi wa mtu katika shughuli zake.
Kama una
fursa ya kwenda shule nenda kasome lakini lengo lako isiwe kupata vyeti
tu, maana wengi hulenga kupata vyeti hata kwa udanganyifu. Bali wewe
lenga kupata ujuzi.
Lakini pia ujuzi haupatikani shuleni pekee, unapatikana kwenye kazi na kutenda.
Kutamani kufanya vitu kwa upekee na kujifunza kwa wengine.
Tukifanya bidii na kuheshimu kanuni za maendeleo tutaivusha nchi yetu kutoka kwenye lindi la umaskini uliopo.