Daktari bingwa KCMC asotea mafao kwa miaka 10
Daktari bingwa wa zamani wa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk Fulgence Mosha
Moshi. Daktari bingwa wa zamani wa upasuaji katika Hospitali
ya Rufaa ya KCMC, Dk Fulgence Mosha anasotea mafao yake ya kiinua
mgongo na pensheni kwa miaka 10 mfululizo bila mafanikio.
Akizungumza
juzi, Dk Mosha alisema licha ya kulifikisha suala hilo kwenye vyombo
husika, ikiwamo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, bado mafao
yake ni kitendawili.
Dk Mosha aliajiriwa na Serikali
mwaka 1983 kabla ya Januari 1,1995 kupelekwa KCMC kwa barua ya Desemba
29, 1994 yenye kumb HE/MP ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii.
Desemba 11, 2004, Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii ikauandikia barua uongozi wa KCMC kutoa kibali cha Dk Mosha
kustaafu rasmi baada ya kufikisha umri wa miaka 60 wa kustaafu kisheria.
Alisema
baada ya kustaafu, alilipwa Sh10 milioni na Shirika la Hifadhi za Jamii
(NSSF), ikiwa ni michango yake na ya mwajiri ambaye ni Shirika la
Msamaria Mwema (GSF) linalomiliki KCMC.
“Katika
utumishi wangu nimefanya operesheni kubwa zaidi ya 7,000 zikiwamo za
viongozi wakuu wa nchi hii lakini leo baada ya kustaafu napigwa danadana
sina thamani tena kwa Serikali,” alisema.
Kwa mujibu
wa Dk Mosha, utata wa mafao yake ikiwamo kulipwa pensheni kila mwezi,
unatokana na Hazina kutopeleka mchango wowote katika Mfuko wa Pensheni
kwa Watumishi wa Umma (PSPF).
Dk Mosha alisema baada ya
kustaafu, alichukua malipo yake ya NSSF na kuyapeleka PSPF ili
yajumlishwe na michango ya Serikali katika kipindi alichokuwa mtumishi
wa Umma (1983-1994).
“Zile fedha zilikaa kule, PSPF
wakaamua kunirudishia maana Serikali haikupeleka ile michango yake
ambayo walitakiwa wailipe kati ya 1983 na 1994 nilipokuwa serikalini,”
alisema.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka,
alipoulizwa na gazeti hili kuhusu malalamiko ya Dk Mosha alionyesha
kushtushwa na kusema, huenda daktari huyo hakutumia njia sahihi kudai
haki yake.
“Simfahamu huyo daktari lakini ni jambo
linaloshtua. Naomba mwelekeze aje ofisini na nyaraka zake zote nimpeleke
SSRA (Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii),” alisema
Kabaka.
Kwa mujibu wa Kabaka, kwa sasa zipo kanuni
zinazounganisha mafao kama mfanyakazi alifanya kazi katika maeneo mawili
yanayohudumiwa na mifuko miwili tofauti ya hifadhi ya jamii.
“Kwa
jinsi ulivyonieleza isingewezekana kulipwa pensheni. Ni lazima mifuko
hii miwili (PSPF na NSSF) ilitakiwa ikae na kuoanisha michango na
mamlaka inayowakutanisha ni SSRA,” alisema.
Dk Mosha
alipoelezwa kwamba Waziri amemuomba aende Dar es Salaam kumuona, alisema
kwa sasa hana hata nauli kwa vile kwa miaka yote 10 tangu amestaafu
amekuwa akiishi maisha ya shida.
“Nitapata wapi nauli?
Dar nimekanyagia mpaka nimechoka sasa hivi nina miaka 70 hiyo nguvu iko
wapi? Miaka 10 nimeishi bila pensheni na kumbukumbu zangu zipo. Kabaka
naomba nisaidie,”alisema.