Flora Mbasha: Nipo tayari kurudiana na mume wangu
Muimbaji wa muziki wa Injili, Flora Mbasha amesema yupo tayari kurudiana
na mume wake Emmanuel Mbasha, ikiwa atakwenda kumuangukia miguuni na
kumuomba msamaha.
Flora alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya
kumaliza kutoa ushahidi wake juu ya kesi ya ubakaji inayomkabili Mbasha
ambayo inasikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
“Mbasha nimemsamehe siku nyingi na nipo tayari kuishi naye iwapo atakuja
kuniangukia miguuni na kuniomba msamaha… lakini hili (ubakaji) ni suala
la mahakama,” alisema.
Alipoulizwa baba halali wa mtoto wake wa kike aliyejifungua hivi karibuni, alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo hivi sasa.
“Siwezi kulizungumzia nikifanya hivyo nitakuwa simtendei haki mwanangu.
Siwezi kubadili mitizamo ya watu jinsi wanavyotafakari kuhusu jambo
hili,” alisema.
Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga alisema awali Flora alitoa ushahidi
wake mbele ya Hakimu Flora Mjaya na kueleza alivyosimuliwa na binti huyo
anayedai kubakwa na Mbasha.
Katuga alikuwa akitoa ufafanuzi huo kwa waandishi kwa vile kesi hiyo
inasikilizwa katika mahakamani ya siri kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo
wa makosa ya jinai ya mwaka 2003 sura ya 20 kifungu cha 186, kifungu
kidogo cha tatu ili kulinda haki ya binti huyo.
Wakili alisema Flora aliieleza Mahakama kuwa Mei 23 mwaka jana, alimkuta
binti huyo akiwa mnyonge huku amelala kitandani na kujifunika shuka.
Alisema alimhoji binti huyo kama alikuwa anaumwa au la lakini hakumjibu chochote.
Flora alisema siku iliyofuata Mei 24, waliondoka na kwenda kanisani yeye
na watoto waliokuwapo nyumbani lakini Mbasha hakuongozana nao.
“Flora alipotoka kanisani na watoto aliwarudisha nyumbani kisha
akaondoka na kwenda hotelini kwa sababu alikuwa na ‘stress’ (mawazo)
lakini akiwa huko alipigiwa simu na mdogo wake Suzan (shahidi wa pili)
akimueleza kile alichoambiwa na binti huyo,” alisema Katuga.
Alisema Flora baada ya kuambiwa jambo hilo kwa simu alimwambia mdogo wake huyo ampeleke binti huyo katika hoteli iliyoko Sinza.
Alisema walipofika binti huyo alimsimulia tukio hilo la kubakwa na ndipo
akawaambia waende wakatoe taarifa hizo kituo cha polisi kabla ya kwenda
hospitalini.
Mahakama hiyo ilisikiliza ushahidi wa Flora kwa takriban saa nne.
Awali wapiga picha walizuiliwa na ndugu zake kumpiga picha huku wakidai kuwa watawashtaki.
“Mnataka kumpiga picha za nini, mmetumwa… mnajua sheria za nchi nyinyi,” alisikika mmoja wa ndugu zake.
Tukio hilo lilizua minong’ono mingi kutoka kwa wananchi waliofika mahakamani hapo kufuatilia kesi mbalimbali.
“Jamani kwani hawa si wapiga picha… waandishi si wanaruhusiwa kuchukua
matukio na kwenda kuyaripoti kulikoni hawa wazuiliwe…jambo hili
linashangaza kweli kweli,” alisema mwanamke mmoja ambaye hakutaka jina
lake liandikwe gazetini.
Tukio hilo lilimshangaza pia Wakili George Mwalali aliyekuwa mahakamani hapo ambaye alisema kitendo hicho ni kosa.
“Haiwezekani mzuiliwe kupiga picha mpo sahihi kwa sababu hapa ni nje ya
Mahakama, nitakwenda kuzungumza na wakili mwenzangu juu ya jambo hili,”
alisema.
Baadaye ndugu hao wa Flora waliwafuata waandishi na kuwauliza kwa nini
walikuwa wakipiga picha hizo na kudai kuwa walikuwa wakiwazuia kwa vile
walipata taarifa kwamba kuna mtu amewapa fedha wapige picha hizo.
“Hapana ndugu yangu, sisi hakuna aliyetupatia fedha… tunachotaka ni habari hii na si vinginevyo,” alisema mmoja wa wapiga picha.
Baada ya ndugu hao kuridhishwa na ufafanuzi waliopewa na wapiga picha
waliokuwa mahakamani hapo waliwaruhusu kuendelea na kazi yao.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi April 16 mwaka huu itakapotajwa tena.