Wimbo wa Komba wamliza Kikwete
Rais
Jakaya Kikwete akiwa katika hali ya majonzi wakati wasanii walipokuwa
wakiimba wimbo maalumu wa kumuaga Mbunge wa Mbinga Magharibi na Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya CCM, Marehemu John Komba katika Viwanja vya
Karimjee, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Spika wa Bunge, Anne
Makinda. Picha ndogo ni jeneza lililobeba mwili wa Komba. Picha na
Anthony Siame
Dar es Salaam. Wimbo wa John Komba aliouimba katika msiba wa
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999, jana uliibua majonzi
na kusababisha viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, kutoa
machozi ulipoimbwa kumuaga mbunge huyo.
Wimbo huo
uliobadilishwa maneno yanayohusu Mwalimu Nyerere na kuingizwa
yanayomtaja mbunge huyo wa Mbinga Magharibi, mbali na Rais Kikwete
ulimliza pia Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Bunge, Anne
Makinda, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Katibu Mkuu
mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba na waombolezaji wengine.
Sehemu
ya mashairi ya wimbo huo uliokwenda kwa jina la “Nani Yule” ulioimbwa
na wanamuziki mbalimbali wa bendi nchini, na kuwatoa watu machozi
iliimbwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
“Kapteni
Komba familia yako umeiacha na nani, chama chako umekiacha na nani,
nenda baba msalimie Mwalimu, mweleze hali ya Watanzania ilivyo hivi
sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo hivi sasa hasa wakati huu,
msalimie Mzee Kawawa Simba wa Vita”
Baadhi ya
wanamuziki walioshiriki kuimba wimbo huo ni King Kiki, Mbunge wa Viti
Maalumu, Martha Mlata, Jose Mara ambaye ni mwanamuziki wa bendi ya
Mapacha Watatu na Luiza Mbutu wa African Stars.
Wakati
wanamuziki hao wakiendelea kuimba wimbo huo, idadi ya watu wanaolia
ilizidi kuongezeka, hasa wanafamilia ndugu na jamaa wa marehemu.
Waombolezaji
walisikika wakilia huku wakisema, “Jamani alikuwa akitunga nyimbo
kuwaimbia wenzake waliofariki dunia, sasa leo anaimbiwa yeye.”
Alipofariki
Mwalimu Nyerere Oktoba 14, mwaka 1999, aliyekuwa Mbunge wa Mbinga
Magharibi, Komba akiwa na bendi ya TOT alitunga nyimbo za maombolezo
ukiwamo wa “Nani Yule’, ‘Kwaheri Mwalimu’, ambazo jana zilitumiwa na
wanamuziki kumuimbia yeye, wakibadilisha baadhi ya maneno.
Mwili
wa mbunge huyo (61) aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita kwa ugonjwa wa
kisukari na shinikizo la damu, uliagwa katika viwanja vya Karimjee
ambapo salamu mbalimbali za rambirambi zilitolewa kabla ya mwili huo
kusafirishwa kwenda Songea mkoani Ruvuma.
Hata wakati
wa kuagwa mwili huo, idadi kubwa ya wabunge wenzake waliohudhuria
walishindwa kujizuia kulia huku wakikumbushana ucheshi aliokuwa nao
Komba enzi za uhai wake.
Pengine msiba huo utakuwa
umewagusa wengi wanaomfahamu kwa mambo mengi, na kwa kuwa kipindi hiki
nchi inajiandaa kupata rais mpya, kwa kuwa kazi yake kubwa ilikuwa ni
kuipigia debe CCM kupitia uimbaji wake.
Kulingana na
maelezo ya waombolezaji, Mwanajeshi huyo aliyestaafu akiwa na cheo cha
kapteni alikuwa ni mtu ambaye hakusita kueleza kile alichokiamini,
jasiri asiyekubali kushindwa, mcheshi wakati fulani na mtu wa kutoa
misaada.
Kijana mmoja ambaye alishindwa hata kutaja
jina lake kutokana na kulia kwa uchungu, alilazimika kuondolewa katika
viwanja hivyo baada ya kutaka kwenda kuaga tena mwili wa mbunge huyo,
huku akisisitiza kuwa ndiyo aliyekuwa akimsomesha.
“Kapteni
jamani umeondoka, hivi nani atanisomesha mimi. Niacheni nikamuage kwa
mara nyingine huyu ni kama baba yangu mzazi, nitakuwa mgeni wa nani,”
alisema kijana huyo na kuzidisha vilio, hasa kwa watoto wa marehemu.
Watu
kutoka maeneo mbalimbali walifika katika viwanja vya Karimjee kumuaga
mbunge huyo kuanzia saa tatu asubuhi, akiwamo mama mmoja aliyedai kuwa
ametoka mkoani Mwanza kuja kuuaga mwili wa mbunge huyo.
Huku
akilia mama huyo alisema, “Komba baba nimetoka Mwanza kwa ajili yako
jamani, nenda ndugu yangu, nenda tu ipo siku tutaonana.”
Shughuli
hiyo ilianza saa 3 asubuhi kwa wanamuziki mbalimbali wa bendi, muziki
wa kizazi kipya na waigizaji wa filamu kuimba nyimbo za kumkumbuka
mbunge huyo.
Wakazi wa Dar es Salaam walimiminika
katika viwanja hivyo na tofauti na shughuli nyingine kama hizo, hakukuwa
na ulinzi mkali wala watu kukaguliwa na vifaa maalumu.
Mara
baada ya viongozi wa Serikali kumaliza kuaga mwili wa mbunge huyo,
wananchi wengine nao walipewa fursa ya kuaga na kusababisha askari wa
Bunge kutumia nguvu ya ziada kuwazuia kutokana na kutofuata utaratibu
uliowekwa.
Watu hao walionekana kuwa na shauku ya kuaga
mwili wa mbunge huyo, baadhi wakilalamikia kitendo cha kuzuiwa na
askari hao wakisema kuwa Komba alikuwa mtu wa watu na wao wana haki ya
kumuaga.
Hata hivyo, baadaye askari hao waliwahimiza
watu hao kufuata utaratibu uliokuwa umepangwa na wote wakapata fursa ya
kuaga mwili huo hadi shughuli zilipomalizika saa 7:30 mchana.
Salamu za CCM
Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema, “Sauti ya Komba imezimika
lakini imefuatiwa na sauti ya vilio vya watu waliompenda wakiomboleza.
Alikuwa mwalimu, mwanajeshi, kiongozi, mbunge, mwanasiasa na mwanamuziki
mwenye kipaji cha kutunga nyimbo zinazoendana na wakati.”
Kinana alisema nyimbo zilizotungwa na Komba zilitumika
kuwapa hamasa wanajeshi wa Tanzania waliopigana vita vya Tanzania na
Uganda mwaka 1978 hadi 1979 vilivyouondoa utawala wa Iddi Amin nchini
humo.
“Katika msiba wa Mwalimu Nyerere nyimbo
alizozitunga ziliwaliza Watanzania, atabaki kuwa mfano wa kuigwa. Kifo
chake ni pigo wa CCM, bendi yake, wasanii na wana familia yake,” alisema
Kinana na kufafanua kuwa chama hicho kimetoa rambirambi ya Sh5 milioni.
Kambi ya Upinzani
Akitoa
salamu za rambirambi kwa niaba ya Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa
Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alisema kifo cha Komba kimewagusa
wabunge wote bila kujali itikadi zao za vyama.
“Kifo
hiki kinatukumbusha kuwa hapa duniani binadamu tunapita tu. Tunatakiwa
kutenda mema kwa ndugu, rafiki na Taifa letu,” alisema.
Kamati ya Bunge
Mbunge
wa Mchinga na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ambayo Komba
alikuwa makamu wake, Said Matanda alisema kuwa alizungumza na marehemu
saa tano kabla ya kufikwa na mauti.
“Tulikuwa
tukizungumzia safari ya kamati yetu kwenda Ethiopia ambayo ilikuwa
tuifanye kesho yake (Jumapili iliyopita), lakini saa tano baadaye
nikapata ujumbe kuwa amefariki dunia, sikuamini,” alisema.
Alisema
marehemu alikuwa zaidi ya kiongozi kwa kutunga nyimbo zenye ujumbe
mzuri kwa jamii na alikuwa na uzoefu wa miaka tisa katika kamati hiyo na
ndiyo maana wajumbe wa kamati hiyo hawakusita kumchagua kuwa makamu
mwenyekiti wao.
Salamu za Serikali
Akitoa
salamu za Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
wa Bunge), Jenista Mhagama alimwelezea Komba kama kiongozi aliyejitolea
katika kila jambo.
“Juhudi na mipango aliyoifanya
Komba katika jimbo lake Serikali kupitia ilani ya CCM itatekeleza.
Serikali itatoa rambirambi zake kwa familia ya Komba wakati mwafaka,”
alisema.
Ujumbe wa Makinda
Spika Makinda aliwataka Watanzania kuwa na tabia ya kusamehe hata kama wametendewa mambo yanayowakwaza.
“Hapa
duniani tunapita tu, hatutakiwi kuwatendea watu mambo ambayo sisi
hatupendi kutendewa. Tusidhani kuwa kila tunachokitaka na kukiamini
kitadumu, si hivyo. Komba ameondoka kama moto wa kibatali unavyozimika,”
alisema.
Makinda alisema kama Komba angepewa dakika 15
za mwisho kabla ya kufariki ili aseme jambo lolote, ni wazi kuwa
angesema kama kuna aliowakosea wamsamehe.
Alisema
binadamu wote ni ndugu na hata wakifa inaelezwa na viongozi wa dini kuwa
wanakwenda kukutana na raha au shida ambazo zinategemea na matendo yao
waliyokuwa wakiyafanya duniani.
“Wanachama wa CCM tunamwombea marehemu na tunaamini kuwa Mungu atatupa Komba mwingine,” alisema.
Salamu za familia
Msemaji
wa familia ya Komba, Dominick Mwakangale alisema mwili wa mbunge huyo
ambao baadaye jana jioni uliagwa na wakazi wa Songea, utazikwa leo
kijijini kwake Lituhi wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Baadhi
ya viongozi waliohudhuria ni Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu
wa zamani Edward Lowassa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue,
Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa.
Wengine ni Mwenyekiti wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (Nec) Jaji Damian Lubuva, Msajili wa Vyama vya Siasa,
Jaji Francis Mutungi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga, Katibu
wa Shughuli za Bunge John Joel, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Masaju, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Meya wa Jiji
la Dar es Salaam, Didas Masaburi na Mbunge wa Bunge la Afrika
Mashariki, Adam Kimbisa.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Raymond Kaminyoge na Susan Mwillo.