Rais Kikwete: Uvamia wa polisi una dalili za ugaidi
Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete
Dar es Salaam. Hatimaye Rais Jakaya Kikwete amedokeza kuwa
matukio ya watu wasiojulikana kuvamia vituo vya polisi, kupora silaha na
kuwashambulia askari kuwa, “yana sifa za ujambazi na mwelekeo wa
kigaidi.”
Akizungumza katika hotuba yake ya mwisho wa
mwezi jana, Rais Kikwete alisema hali ya usalama nchini ni nzuri
kutokana na matukio hayo pamoja na mengine ya mauaji ya albino.
“Matukio
haya yana sura mbili. Yana sura ya ujambazi, lakini pia baadhi yake
yana dalili za ugaidi. Vyombo vyetu vya usalama vinaendelea kufanya kazi
yake ya uchambuzi wa kila tukio na kulipa nafasi yake stahiki,” alisema
Rais Kikwete.
Matukio yenyewe
Katika
hotuba hiyo ya maneno 3,362, Rais Kikwete alitoa orodha ya matukio ya
kuvamiwa vituo vya polisi kuwa katika kipindi cha miezi 12 jumla ya
bunduki 38 ziliporwa na askari polisi saba kuuawa.
Alivitaja
vituo vya polisi vilivyovamiwa kuwa ni Newala mkoani Mtwara ambako
bunduki tatu ziliporwa, Ikwiriri katika Wilaya ya Rufiji (bunduki saba),
Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga (bunduki tano), mbili zikiwa za polisi
na tatu za raia zilizokuwa zimezihifadhiwa hapo.
Alisema katika Kituo cha Ushirombo Wilaya ya Bukombe bunduki 18 ziliporwa, ingawa baadaye zilipatikana zote.
Kadhalika,
alisema katika maeneo ya Pugu Machinjioni na Tanga, askari waliokuwa
katika shughuli za ulinzi na doria walishambuliwa na kuporwa silaha
tatu.
Askari waliouawa
Katika
matukio hayo, Rais Kikwete alitaja idadi ya askari saba waliopoteza
maisha mmoja akitoka katika kituo cha Newala, Kimanzichana mmoja,
Ikwiriri wawili na Ushirombo watatu.
Hata hivyo,
Kikwete alitumia nafasi hiyo pia kutoa pongezi kwa polisi na Jeshi la
Ulinzi la Wananchi (JWTZ) kwa kazi nzuri ya kupambana na uhalifu nchini.
“Silaha
zote 18 zilizoporwa Ushirombo zimepatikana na watu 10 wanaotuhumiwa
kuhusika na uhalifu huo wamekamatwa. Katika tukio la Tanga silaha moja
kati ya mbili zilizoporwa imepatikana,”alisema Rais Kikwete.
Kadhalika
katika operesheni hiyo, Rais Kikwete alisema watuhumiwa saba walitiwa
mbaroni, wanne kati yao wakiwa ni wale waliokuwa wamejificha katika
mapango ya Kiomoni katika Kitongoji cha Karasha-Mikocheni, kilichoko
kijiji cha Mzizima wilayani Tanga.
Wito kwa wananchi
Kuhusu
uhalifu, Rais Kikwete aliwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya
usalama hasa Jeshi la Polisi ili kukomesha uhalifu huo na mwingine.
“Nawaomba
mfanye mambo mawili: Kwanza, toeni taarifa polisi mnapozipata habari za
vitendo viovu au nyendo za watu waovu wanavyokusudia kufanya wahalifu
au taarifa za wale waliokwishafanya uhalifu,” alisema.
Kadhalika
Rais Kikwete aliwataka Watanzania kuacha kushabikia uhalifu na kueneza
taarifa potofu katika mitandao ya kijamii badala yake watumie mitandao
hiyo kupinga fikra potofu na kuwafichua wahalifu.
Mauaji ya albino
Katika
hatua nyingine, Rais Kikwete aliagiza watu wanaojihusisha na mauaji ya
albino wasakwe, kufikishwa mahakamani na kuadhibiwa vikali pindi
watakapopatikana na hatia.
“Lazima tulaani vikali
mauaji ya ndugu zetu albino. Ni vitendo vya kinyama ambavyo havitegemewi
kufanywa au kutokea katika jamii yoyote ya watu waliostaarabika,
wanaomuabudu Mungu,” alisema.
Rais Kikwete alisema
mauaji ya watu wa kundi hilo yanafedhehesha na kuharibu sifa ya Taifa na
kusema kuwa Serikali imelipa uzito mkubwa suala la kudhibiti na
kukomesha mauaji hayo.
Alisema tangu aingie madarakani
Aprili 17, 2006, alianza kupambana na mauaji hayo na yalipungua kutoka
18, mwaka 2008 hadi sifuri mwaka 2011.
“Inawezekana
kuwa matukio ya hivi karibuni yanaashiria kuwa uhalifu huu unataka
kuibuka upya, hatutaacha hali iwe mbaya kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Tutatumia mbinu na maarifa tuliyoyatumia kukabili wimbi kubwa la mauaji
lililokuwapo mwaka 2007 na 2008,”alisema Rais Kikwete.
Vilevile
Rais Kikwete alisema ili kutokomeza kabisa matukio ya mauaji na ukataji
wa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi wananchi hawana budi kuachana
na imani za kishirikina.
“Ni ujinga ulioje kwa mtu
kuamini kuwa mafanikio yake hayatategemea juhudi zake na maarifa yake
bali kuwa na kiungo cha mwanadamu mwenzake mwenye ulemavu wa ngozi,”
alisema.
Alisema kinachochochea uovu huo ni imani
potofu ya kuamini kuwa kiungo cha mtu mwenye ulemavu wa ngozi kinasaidia
katika shughuli za biashara, uvuvi au uchimbaji wa madini.
“Serikali
na jamii haitalazimika kushughulikia mambo haya ambayo siyo tu ni
fedheha hata kumsimulia mtu, bali yanatisha na kusikitisha,” alisema.
Kukuta na chama cha albino
Pamoja
na kulaani mauaji hayo, Rais Kikwete ameahidi kukutana na baadhi ya
viongozi wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi wiki hii ili
kusikiliza maoni yao ya namna ya kumaliza tatizo hilo.
Kura ya maoni
Pamoja
na mambo mengine, Rais Kikwete alizungumzia mchakato wa kura ya maoni
ya Katiba Inayopendekezwa na kuwataka Watanzania wawe na subira huku
wakizingatia sheria ya kura ya maoni na kanuni zake.
Alisema
kinachoendelea sasa ni matayarisho ya kufanyika kwa kura hiyo baada ya
Bunge Maalumu la Katiba kutunga Katiba Inayopendekezwa na Rais
kuichapisha na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni.
Katika
mchakato wa kuelekea kupiga kura hiyo Rais alisema utekelezaji wa
kuandikisha wapiga kura, kuchapisha na kusambaza Katiba Inayopendekezwa
tayari vimeshaanza.
“Tayari Katiba Inayopendekezwa
imetangazwa katika tovuti za Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya
Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo na katika tovuti ya Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Pia imechapichwa magazetini,” alisema.
Uandikishaji wapiga kura
Rais
Kikwete pia alizungumzia zoezi la uandikishaji katika daftari la kudumu
la wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya utambuzi wa alama za
mwili (BVR).
Aliisifu teknolojia ya BVR na kusema kuwa
itasaidia kuondoa kutoaminiana, manung’uniko na madai ya udanganyifu
katika chaguzi nchini.
“Kuanza kutumika kwa teknolojia
hii ni kielelezo cha utashi wa Serikali kuwa nchi yetu iwe na chaguzi
zilizo huru, wazi na haki,” alisema.
Kadhalika
aliwataka wananchi kutumia fursa iliyopo kujiandikisha kabla ya uchaguzi
mkuu kwani hakutakuwapo na fursa nyingine baada ya hapo.
“Kama
ilivyoelezwa na Tume na mimi kusisitiza mara kadhaa, watakaojiandikisha
wakati huu ndio watakaopiga kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa
na ndio watakaopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu,”
alisema.
Kuhusu kazi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
Rais Kikwete alisema hatua iliyofikiwa na tume hiyo inatia moyo na
kuondoa hofu iliyoanza kuingia kuwa huenda zoezi hili lisingefanikiwa.