Waganga 55 Wakamatwa Jijini Mwanza Wakihusishwa Na Mauaji Ya Albino Na Ramli Chonganishi
Jeshi
la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia waganga wa kienyeji 55 wanaopiga
ramli chonganishi na kusababisha madhara makubwa yakiwemo ya mauaji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na vikongwe.
Katika
idadi hiyo, mmoja wa waganga hao anadaiwa kukutwa na nywele
zinazodhaniwa kuwa ni za mlemavu wa ngozi (albino) pamoja na debe tatu
za bangi.
Hayo
yalielezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola,
wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia operesheni za
kuwasaka waganga wakienyeji wanaopiga ramli chonganishi ambazo zimekuwa
zikiathiri walemavu wa ngozi kwa kauli na matendo yao.
Alisema
kati ya hao waliokamatwa 18 ni wanawake na 37 na wanaume ambapo
walipokamatwa walikutwa wakiwa na nyara mbalimbali za serikali
walizokuwa wakizitumia huku wakizimiliki pasipo halali zikiwemo ngozi za
simba.
Alisema
operesheni hiyo ambayo ni endelevu ilianza Machi 6, mwaka huu
watuhumiwa hao walikutwa na nyara mbalimbali za serikali zikiwemo ngozi
za simba, chui,fisi, swala, kiboko, chatu, nyoka aina ya kifutu, yai la
mbuni, nyegere na nungunungu.
Aidha,
alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na vifaa mbalimbali vya
kupigia ramli chonganishi ambavyo ni simbi, vibuyu, visonzo, sarafu za
kale, ungo, ngoma, manyanga, vyungu, mizizi ya miti shamba, mikuki,
mishale, shuka nyeupe, nyekundu na nyeusi.