Mama Aliyemsaidia Mwanae Kubaka Atupwa Jela Miaka 30 Sawa Na Mwanae
Mama aliyemsaidia mwanawe kubaka , Regina Kigelulye, ametupwa jela miaka 30 sawa na mtoto wake ambaye alikuwa anakabiliwa na kosa la kubaka, Sagimembe Mroso.
Mtoto huyo pamoja na kwenda jela miaka 30 amepewa adhabu ya kuchapwa viboko 12, sita akiingia jela na sita akitoka.
Mbele
ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpwapwa, Paskal Mayumba
mwendesha mashitaka wa Polisi Godwin Ikema alisema watuhumiwa hao
Sagimembe Mroso na mama yake Regina Kigelulye, wakazi wa mtaa wa Hazina
mjini Mpwapwa, Machi 6, 2014 walikula njama ya kumbaka Belita Ndahani.
Ilidaiwa
kuwa mtuhumiwa namba moja Sagimembe Mroso alifanya kosa hilo kinyume na
kifungu namba 130(A) na kifungu kidogo 2 na kifungu 131(1) na sheria
namba 16 ya kanuni ya adhabu.
Aidha
ilidaiwa kwamba mshitakiwa wa pili Regina Abdalah Kigelulye alimsaidia
mwanawe huyo kufanikisha tukio hilo kwa kufunga mlango kwa nje ili
mwanamke huyo ashindwe kutoka nje.
Kitendo hicho kilielezwa kuwa kinyume na kifungu namba 22 kifungu kidogo cha 1 na sheria ya kanuni ya adhabu namba 16.
Mayumba
aliiambia Mahakama kuwa siku ya tukio Regina akiwa muuguzi katika
hospitali ya Benjamin Mkapa alimchukua Belita Ndahani aliyekuwa
akimuuguza baba yake katika hospitali hiyo na kwenda kulala nyumbani
kwake na ndipo alipomfungia mlango kwa nje na mwanawe huyo wa kiume huku
akimsihi yeye ni mtu mzima hivyo asipige kelele ndipo alipomwingilia
kinyume na ridhaa yake.
Aidha
ilidaiwa mahakamani hapo kwamba mama huyo hakuridhika na kitendo hicho
akawa anapiga makelele na majirani walipoulizia kelele hizo waliambiwa
kwamba mama huyo alitoka kijijini hivyo alikuwa anaogopa watu aliokuwa
anawaona ndani ya luninga.
Hata
hivyo maswali yalipoongezeka alimfungulia mlango na kumuamuru mwanawe
amsindikize hospitalini kwamba alipofika korongoni alimbaka tena.
Pia
aliiambia Mahakama kuwa kutokana na kumbukumbu zilizopo zinaonesha kuwa
mtuhumiwa anaishi na virusi vya Ukimwi hivyo alimbaka mama huyo bila
kutumia kinga na kumhatarishia kupata maambukizi na yeye.
Aliongeza
kuwa hospitali ilimwanzishia na kwamba mama huyo amepima mara kadhaa
lakini imeonesha kuwa hana virusi vya Ukimwi. Hata hivyo alisema kuwa
baada ya kufanyiwa kitendo hicho mumewe alimfukuza nyumbani na mgonjwa
wake ambaye alikuwa ni baba yake alifariki dunia sasa ameathirika
kisaikolojia.
Akitoa
hukumu Hakimu Mayumba alisema kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 22
kidogo 1 (C) kinachosema atakayesaidia kufanikisha uharibifu kutendeka
au kwa kutazama kuwa mazingira yako salama adhabu yake ni sawa na
aliyetenda kosa hilo, alimtupa jela miaka 30.
Wakijitetea
kabla ya hukumu mshitakiwa wa kwanza (mtoto) aliomba Mahakama
impunguzie adhabu kutokana na kuwa yeye ana watoto watatu na anaishi na
virusi vya Ukimwi.
Mtuhumiwa
wa pili aliiambia Mahakama kuwa yeye ni mzee ana miaka 60, pili ana
watoto 10 wakiwemo watoto yatima ambao anawalea yeye, pia ana ugonjwa wa
shinikizo la damu hivyo aliiambia Mahakama impunguzie adhabu.
Hata
hivyo Hakimu Mayumba akitoa maelezo alisema mashahidi na vielelezo
vilivyofika mahakamani vimewatia hatiani watuhumiwa hao na kwa
kuzingatia sheria kifungu na 130 (1) sura ya 16 ya kanuni ya adhabu,
mtuhumiwa namba 1, Sagimembe Mroso alihukumiwa kutumikia kifungo cha
miaka 30 jela na kuchapwa viboko 12.
Aidha
mtuhumiwa namba 2, Regina Kigelulye kwa kuzingatia kifungu 22 kifungu
kidogo (1)C na sheria namba 16 ya kanuni ya adhabu Mahakama ilimtupwa
jela miaka 30 .
Pamoja
na dhabu hiyo Mahakama iliagiza mali zao kupigwa mnada kulipa fidia ya
Sh milioni 5 kama sehemu ya fidia ya kudhalilishwa, kumpoteza baba yake,
na kupoteza ndoa yake kwa Belita Ndahani.