Njemba anaswa wizi wa fedha mtandaoni...

Jamaa aliyetambulika kwa jina moja la Jacob, mkazi wa Majengo wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza, amejikuta yuko mikononi mwa polisi wakati akifanya jaribio la wizi wa fedha sh. 70, 000 kupitia huduma za fedha za mtandao wa simu.


  Kijana Jacob anayedaiwa kuiba kwa kutumia mtandao.
 
Jamaa huyo amefanya tukio hilo hivi karibuni maeneo ya Misungwi Stand ambapo aliingia dukani kwa wakala Robert Bukoli na kuomba awekewe fedha hizo, wakala alichukua namba yake ya simu ili amuwekee fedha hizo.
Chanzo makini kilichokuwepo dukani hapo kilidai kuwa, wakati Bukoli akiendelea kuingiza namba za simu za mteja huyo kwenye simu yake, alimuomba mteja huyo aweke fedha hizo taslim mezani ili itakapoingia kwake (mteja) naye wakala awe na chake mkononi ndipo mteja huyo alianza kuhaha.

Wakala aliendelea kumsisitiza mteja huyo aweke pesa mezani lakini mteja huyo alianza kuonesha dalili za kukimbia ndipo aliamua kumshikilia na kupiga simu polisi ambapo alikamatwa na kupelekwa kituoni. “Inaonekana mpango wake alikuwa anataka awekewe fedha kisha azuge kama anaongea na simu, atimke  bahati nzuri wakala naye alishamshtukia,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumzia sakata hilo, wakala huyo alisema alianza kumtilia shaka jamaa huyo baada tu ya kufika dukani kwake.“Jamaa nilimtilia shaka mapema alipofika dukani maana alianza kuongea na mtu mwingine kwenye simu kwa muda mrefu kabla hajaniambia nimuwekee pesa baadae ndio akasogea na kuniambia ana haraka nimuwekee pesa upesi.
“Nikachukua namba yake ya simu, nikiwa naijaza kwenye simu yangu nikamwambia naye aweke pesa mezani lakini hakufanya hivyo, nilipo msisitiza zaidi jamaa nikamwona anaingiwa na hofu na akataka kukimbia ndipo nikamshika na kupiga simu polisi akakamatwa, nilipofuatilia kituoni nikakuta ana kesi nyingine ya kuuza kiwanja mara mbili hivyo inasemekana alitaka kunitapeli hizo pesa ili akalipe deni lake la kesi ya nyuma,” alisema wakala huyo ambapo alimuacha mtuhumiwa kituoni kwa ajili ya taratibu za kisheria.
Powered by Blogger.