Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu Katiba inayopendekezwa
Sisi
Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania linaloundwa na Taasisi za
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) tuliokutana
leo tarehe 10.03.2015, tumepata nafasi ya kujadili kwa kina kuhusu hali
ya usalama wa nchi ilivyo sasa na mustakabali wake, Katiba
inayopendekezwa na uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi.
Baada ya kutafakari yote hayo, Jukwaa limefikia maazimio yafuatayo:
Kuhusu uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi: Suala
la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini kama tulivyotoa maoni yetu
kwa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria (Januari 16, 2015); barua yetu
kwa Waziri Mkuu na matamko mbalimbali yaliyokwisha kutolewa kuhusu jambo
hili; Mahakama ya Kadhi inakiuka misingi ya Taifa hili kuwa na Serikali
isiyokuwa na dini wala mfumo wa sheria unaobagua raia wake kwa misingi
ya dini. Pia mjadala unaoendelea unavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ya 1977 Ibara ya 19.
Kwa
kuendelea kujadili suala hili katika Ilani za Vyama vya Siasa, Majukwaa
ya Kisiasa na Bungeni, limeligawa Taifa letu, Serikali, Bunge, Mahakama
na wananchi. Mahakama ya Kadhi imekuwa likiendelea kutumiwa na
wanasiasa kama mtaji wao wa kujipatia madaraka kwa gharama za kuleta
chuki za kidini.
Kwa
dhamiri safi, Jukwaa linatamka wazi kuwa mjadala unaoendelea kati ya
Serikali na vikundi vya kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi
kikatiba na kisheria ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za
kidini kuamua juu ya masuala hayo bila kuih usisha serikali wala waumini
wa dini nyingine.
Kuhusu Katiba inayopendekezwa:
Katiba Inayopendekezwa imeleta mgawanyiko mkubwa katika Taifa kwani
imepatikana kwa njia zisizo za kiadilifu; na mchakato wake umeendeshwa
kwa hila na ubabe.
Aidha,
Katiba Inayopendekezwa haijajibu bado matakwa na malalamiko ya wananchi
kwenye masuala mbalimbali (Muundo wa serikali, miiko na maadili ya
viongozi wa umma, haki za binadamu, madaraka ya Rais, uwiano wa mihimili
ya dola n.k). Ikumbukwe Katiba Inayopendekezwa ilipitishwa kwenye Bunge
Maalum la Katiba kwa ahadi ya Serikali kuipa dini ya Kiislam Mahakama
ya Kadhi.
Inashangaza
kuwa hata Serikali inatoa rushwa ili kufikia malengo yake!!! Kwa hali
kama hii, Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa Katiba
Inayopendekezwa.
Hivyo
basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba
Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba
Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya HAPANA kwa Katiba Inayopendekezwa kwa sababu zilizotajwa hapo juu.
Hali ya usalama wa nchi ulivyo sasa: Jukwaa linasikitishwa na viashiria pevu vya ugaidi vilivyoanza kujitokeza nchini kwa takribani miaka mitano iliyopita.
Kumekuwa
na vitendo vinavyoashiria kuchipuka kwa ugaidi kama vile uvamizi wa
vituo vya polisi, kuporwa silaha na mauaji ya polisi, mafunzo ya kareti
katika nyumba za Ibada, mafunzo ya itikadi kali za kidini kwa watoto
(Kilimanjaro), tukio la Amboni Tanga, mauaji ya viongozi wa dini
(Buselesele, Zanzibar, Arusha), uchomaji wa nyumba za Ibada na kumwagiwa
tindikali kwa viongozi wa dini.
Mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (maalbino): Jukwaa
linasikitishwa na mwendelezo wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi
(maalbino) na ukatili unaosababisha ulemavu wa kudumu wa maalbino katika
nchi yetu.
Hali
hii inatishia utulivu, amani na umoja wa kitaifa tuliokuwa nao kama
taifa la mfano barani Afrika. Jukwaa linawaasa wananchi kuacha tabia hii
ya kuua albino.
Jukwaa
linaa mini kuwa kukosekana kwa uwajibikaji wa viongozi wa serikali na
kuongezeka kwa wigo wa kipato kati ya walionacho na wasionacho
kunachangia ongezeko la vitendo hivyo viovu.
Jukwaa
linajiuliza: mbona tembo na ng’ombe wakiuawa operesheni maalum
zinafanyika na viongozi wanawajibika, kwa nini maalbino wakiuawa
viongozi hawawajibiki?
Kutokana
na hayo yote, Jukwaa linatilia shaka dhamira thabiti ya uongozi wa
Chama Tawala na Serikali yake katika kuvitokomeza vitendo vya kigaidi,
mauaji ya albino na uvunjifu wa amani unaoendelea hasa kutokana na
mikakati hafifu na udhaifu mkubwa uliojitokeza wakati wa kuyashughulikia
masuala hayo.
Kwa
kuwa Chama Tawala na Serikali wameshindwa kusimamia misingi iliyolea
taifa kama serikali isiyo ya kidini na taifa lenye amani; umoja na
utulivu; Jukwaa linawaelekeza waumini wote na wenye mapenzi mema wakati
wa Uchaguzi Mkuu ujao kufanya maamuzi yanayolitanguliza Taifa badala ya
kutanguliza mazoea, mapokeo, itikadi na ushabiki wa chama fulani cha
Siasa.
YATOSHA KWA SIKU MAOVU YAKE: MATHA YO 6:34
Imetolewa na: