Cheyo akaribisha ‘wageni’ kuwania urasi kupitia UDP


Mwenyekiti wa UDp, John Cheyo.
Dar es salaam. Mbunge wa Bariadi  Mashariki na Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo  amesema wanakaribisha wanachama wa chama chochote cha siasa nchini kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho.
Akizungumza leo jijini Dar es salaam, kiongozi huyo alisema chama hicho bado hakijateua mgombea  urais hivyo milango iko wazi kwa wanasiasa ambao wako tayari kujiunga na chama hicho kwa lengo la kuwania urais.
“Hiki chama ni cha watanzania wote hivyo tunatoa rai kwa mtu yeyote  aliye tayari kuwa mwanachama wetu milango ya kuwania urais kupitia chama hiki ipo wazi’’ alisema Cheyo
Alisema  yeye bado hajaamua kuwania nafasi hiyo kwa sasa muda ukifika atasema lakini kwa sasa ni mapema kutoa tamko kwamba atawania wadhifa huo.
Aliongeza kwamba  anasikitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwahamasisha watu wasipigie kura Katiba inayopendekezwa, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwanyima haki wananchi.
‘’Raia wote wana haki ya kupiga kura sasa ikiwa Ukawa wanatembea kila kona ya nchi kuwahamasisha wananchi kuacha kuipigia kura katiba hiyo ni kosa,’’ alisema Cheyo
Pia Kiongozi huyo wa UDP alisema tume ya uchaguzi ndio yenye majibu ya mashine zinazotumika kuandikisha wapiga kura  kwenye daftari la kudumu, (BVR) kwamba zinafaa au hazifai.
Alisema anashangazwa sana na baadhi ya watu hususan wanasiasa na wasomi wanaojitokeza na kusema mchakato wa kuandikisha wapiga kura usimamishwe kwa sababu zao mbalimbali
Powered by Blogger.