Aliyejifanya katibu wa JK atiwa mbaroni
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, limemtia nguvuni mkazi mmoja wa jijini hapa
kwa tuhuma za kutumia wadhifa wa Katibu wa Rais Jakaya Kikwete kujipatia
fedha kutoka taasisi na watu binafsi.
Kamishna wa
Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova akizungumza na waandishi wa habari
jana alisema, mtu huyo alikuwa akijiita Prosper Mbena ambaye ndiye
Katibu wa Rais Kikwete.
“Mkazi huyo wa Mbagala Rangi
Tatu jijini Dar es Salaam tulimkamata jana (juzi) ambaye amekuwa
akijiita Prosper Mbena na ameshatapeli Wizara ya Ardhi, Maji, taasisi na
watu mbalimbali na mara ya mwisho alikamatwa akichukua Sh300,000,”
alisema Kamishna Kova.
Aliongeza: “Tunawaomba wananchi
kuwa makini na watu wa aina hii lakini taasisi zihakikishe wanaweka
ulinzi katika milango yao ya kuingilia pindi wanapomwona mtu anapita
pita mara kwa mara wamchukulie hatua na kujua anachokifanya hapo.”
Kamishana
huyo alisema, vitendo vya watu kutumia majina ya watu kujipatia manufaa
hususan ya kifedha, yamekuwapo na ili kuyaondosha kabisa ni lazima
ushiriki wa wananchi na Jeshi la Polisi uwapo kwa kubadilishana taarifa.
“Tulipata
taarifa kutoka kwa mmoja wa waliotaka kutapeliwa na mtego aliowekewa ni
kuambiwa kuwa kati ya zile fedha Sh300,000 kuna fedha zilibaki hivyo
aje kumalizia na hapo hapo tukamweka chini ya ulinzi,” alisema Kova.
“Vitu
vya mwisho au vya kumalizia siyo vizuri, ukichukua umechukua ukirudi
matokeo yake ndiyo hayo yaliyomfika huyu bwana ambaye hana kazi wala
biashara yeyote.”
Tukio hilo siyo la kwanza kutokea kwani yamekuwapo matukio kama haya ya watu kutumia majina ya viongozi kujinufaisha.