UDHAIFU: Dakika 45 za mwisho zaiua Yanga SC
Dar es Salaam. Ni nguvu ya soda. Hivyo,
ndivyo unavyoweza kuzungumzia Yanga ambayo imekuwa ikisifika nchini kuwa
na beki imara iliyotengeneza ukuta mgumu, usiopitika kwenye mechi za
Ligi Kuu msimu huu, lakini ndiyo imeonekana nyepesi zaidi kwa mabao
kipindi cha pili.
Ukuta wa Yanga, msimu huu umeruhusu
mabao tisa kwenye Ligi Kuu, lakini ndio uliogeuka dhaifu, unaopwaya,
hasa kipindi cha pili na hivyo kuruhusu mabao kirahisi.
Upungufu
huo unawatia homa makocha Hans Pluijm na msaidizi wake, Charles
Mkwassa, ambao timu yao inawakilisha nchi kwenye mashindano ya Afrika,
dhidi ya Platinum ya Zimbabwe, kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Uchunguzi wa gazeti hili pamoja na takwimu
mbalimbali zinaonyesha kuwa timu hiyo imeruhusu mabao mengi ya kipindi
cha pili, ingawa inaonekana kuwa vizuri kwenye upachikaji wa mabao,
vipindi vyote viwili vya mchezo.
Takwimu hizo
zinaonyesha kuwa Yanga imecheza michezo 16 ya ligi mpaka sasa na miwili
ya kimataifa, lakini katika michezo hiyo imeshinda bila kuruhusu bao
katika michezo saba, imeruhusu mabao ya kipindi cha pili katika michezo
minane na imetoka sare ya 0-0 kwenye michezo mitatu.
Hadi
sasa, timu hiyo imeruhusu mabao ya kipindi cha pili katika mchezo wa
ufunguzi wa msimu dhidi ya Mtibwa Sugar ilipofungwa mabao 2-0.
Mabao
ya Mtibwa yalifungwa dakika ya 56 na 59, pia katika ushindi wa mabao
2- 1 ilioupata Yanga dhidi ya Prisons kwenye mzunguko wa kwanza, timu
hiyo iliongoza kwa mabao ya dakika ya 32 na 73 na Prisons kufunga bao
lao la kufutia machozi, dakika ya 65. Pia, timu hiyo iliruhusu bao la
kipindi cha pili katika ushindi wa mabao 2- 1 dhidi ya Ruvu Shooting ,
bao la wapinzani likifungwa dakika ya 88.
Katika mechi dhidi ya Kagera Sugar ambao Yanga ilichapwa bao 1- 0, bao hilo lilifungwa dakika ya 53.
Yanga
ilitoka sare ya mabao 2 - 2 dhidi ya Azam, timu ambayo licha ya
kuongoza na Yanga kusawazisha, iliongeza bao la pili, Azam
ikasawazisha dakika ya 65 na kuifanya mechi hiyo kumalizika kwa mabao
2-2 na timu hizo kugawana pointi.
Udhaifu wa Yanga wa kuruhusu mabao ya kipindi cha pili
uliendelea katika mchezo dhidi ya Mbeya City, ambako timu hiyo iliongoza
kwa mabao 3- 1, lakini bao la wapinzani wao likafungwa dakika ya 61.
Pia,
beki hiyo ya klabu ya mitaa ya Twiga na Jangwani iliruhusu bao la
Emmanuel Okwi wa Simba, dakika ya 51 katika kipigo cha bao 1- 0 wiki
iliyopita.
Kimataifa, timu hiyo licha ya kushinda mabao
2- 0 nyumbani katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho, dhidi ya
BDF XI ya Botswana ilijikuta ikichapwa mabao 2- 1 katika mchezo wa
marudiano mjini Lobatse, yote yakipatikana kipindi cha pili, dakika ya
49 na 85.
Mechi saba ambazo timu hiyo imeshinda bila
nyavu zake kutikiswa ni dhidi ya Polisi Morogoro, Mtibwa Sugar,
Prisons, Stand United, Mgambo Shooting, mechi zote zikiwa za mzunguko
wa pili pia dhidi ya Coastal Union wakati pia ikifunga BDF mabao 2- 0
kwenye mchezo wa awali wa kimataifa.
Mechi ambazo Yanga
imetoka suluhu 0-0 ni dhidi ya Ndanda na Simba katika mechi za mzunguko
wa kwanza na Ruvu Shooting kwenye mzunguko wa pili.
Kocha
mkuu, Mholanzi Hans Pluijm amekuwa akiwaeleza mabeki wake kuwa makini
wawapo mchezoni, la sivyo safari yao itaishia kwa Wazimbabwe.
Pluijm
amekiri kuwapo kwa tatizo katika safu yake ya ulinzi na ndiyo maana
amekuwa akipigia kelele kila mara kuongeza umakini na kuweka akili zao
uwanjani.
“Tunatakiwa kuwa makini wakati wote,
tunatakiwa akili zetu tuzitulize uwanjani, hasa kwa watu wa ulinzi,
hatutakiwa kufanya makosa na kuwapa nafasi wageni kupata bao lolote
nyumbani,” amekuwa akieleza kocha huyo.
“Najua soka ni
mchezo ambao huwezi kucheza kwa uwezo wako bora kila siku, lakini safu
ya ulinzi imefanya makosa mengi katika mechi zilizopita, ila tunatakiwa
kusahau na kuangalia jinsi gani tutashinda mchezo ujao na kupunguza
makosa,” alisema Pluijm.