Mtoto Albino Anusurika Kuuawa na 'Wawindaji' wa Albino Alipokuwa Mpirani Akicheza ..Wenzake Wamuokoa
Mtoto wa umri wa miaka sita, mwenye ulemavu wa ngozi
(albino), anayeishi Kijiji cha Ndoleleji, amekoswakoswa na watu
waliokuwa wakimvizia akiwa katika michezo, baada ya watoto wenzake
kuchukua uamuzi wa kumlinda.
Taarifa zilizomfikia mwandishi, zilieleza kuwa ‘wawindaji’
hao waliokuwa na gari lililokuwa na vioo vya giza, walionekana
wakimfuatilia mtoto huyo Jumamosi ya wiki iliyopita alipokuwa akiogelea
mtoni na baada ya kumkosa, wakamfuatilia katika uwanja wa mpira
Jumatatu, ambako nako walimkosa.
Akizungumza na mwandishi, diwani wa Kata ya Shagihilu
wilayani Kishapu mkoani hapa, Mohamed Amani alisema kumefanyika
majaribio mawili ya kutaka kumteka mtoto huyo (jina limehifadhiwa),
lakini kwa msaada wa watoto wenzake hayakufanikiwa.
Kwa mujibu wa Diwani Amani, Jumamosi iliyopita watu watatu
wakiwa kwenye gari hilo, walifika kijijini hapo na kwenda mpaka mtoni,
ambako mto huyo mwenye ulemavu wa ngozi alikuwa akicheza na wenzake.
Baada ya kufika mtoni, watu hao wote watatu waliteremka
kwenye gari na kusogea katika eneo la mto, hatua iliyowashitua watoto
wenzake waliokuwa wakicheza wote mtoni.
Kwa mujibu wa Amani, watoto hao wenye umri mkubwa zaidi ya
mtoto huyo, walitambua hatari iliyokuwa ikimkabili mwenzao mwenye
ulemavu wa ngozi na dalili za watu hao waliokuwa hawawafahamu, waliokuwa
wakizidi kuwasogelea.
Baada ya kuona watu hao wakizidi kusogelea eneo lao la
michezo, watoto hao walimshauri mwenzao mwenye ulemavu wa ngozi,
akimbilie nyumbani kwao na mtoto huyo akasikia ushauri huo na kurudi
nyumbani.
“Baada ya mtoto (albino) kukimbilia nyumbani kwao, wale watu waliingia kwenye lile gari na kuondoka,” alisema Amani na kuongeza kuwa hatua ya watu hao kutosema lolote kwa watoto hao lilizidi kuwapa mashaka.
Jumatatu ya wiki hii jioni wakati mtoto huyo alipokuwa na
wenzake, wakiwemo wale aliokuwa nao mtoni, wakicheza mpira wa miguu
katika kiwanja cha kijijini hapo, gari hilo lililoonekana mtoni,
lilifika uwanjani hapo na kusimama.
Inaelezwa kuwa baada ya kusimama, watu wale watatu
walioonekana mtoni walishuka katika gari hilo, wakaegemea gari na
kuangalia watoto hao wakicheza mpira, akiwemo mwenzao mwenye ulemavu wa
ngozi.
“Safari hii haikuwa mtoni, bali katika eneo jingine tena
la wazi ambalo mtoto huyo alikuwa akicheza mpira na wenzake… walipofika
walisimama nje ya gari lao,”alisema Diwani Amani.
Kutokana na hali hiyo, watoto hao walihisi kuna hali ya
hatari kwa mwenzao, baada ya watoto hao kuona gari hilo kwa mara
nyingine, na watu hao wakiwa wamewasimamia na hawakuwa wakizungumza
chochote.
Diwani huyo alisema watoto hao walisitisha mchezo wao, na
kumtaka mwenzao kwa mara nyingine akimbilie nyumbani kwao, ili
kusalimisha maisha yake kutokana na utata wa usalama ulioanza kujitokeza
hapo.
Akizungumza na mwandishi, mama mzazi wa mtoto huyo, Regina
Malando, alithibitisha kurejea nyumbani mara mbili kwa mtoto wake huku
akikimbia.