MISEMO YA KISWAHILI
Maji ya kifuu bahari ya chungu
Msemo huu una maana kuwa jambo dogo unalolidharau wewe, wenzako linawatoa jasho. (maji ya nazi mdudu chungu/sisimizi kwake sawa na bahari).
Mgala mwue na haki yake umpe
Maana ya musemo huu ni kuwa, Hata kama umeamua kumkandamiza mtu kwa kumfanyisha kazi ngumu ama malipo duni, mtimizie ulichomwahidi ama iliyo haki yake.
Kutoa ni moyo usambe ni utajiri
Msemo huu unatufunza kwamba kuwasaidia wengine si kuonyesha utajiri mtu alionao bali ni ishara ya upendo na kujali maslahi ya wengine.
Bure huchosha
Msemo huu unadhamiria kutufunza kuwa si vizuri kuzoea kupenda kupokea vitu bila kufanya kazi. Tabia hii ya kupokea tu hukwaza wanaotupa, ama labda wao wakatusema vibaya na kutukera.
Ampaye shetani maana,hujipatisha ghadhabu za Rahamani
Msemo huu unamaanisha kuwa anayemsifu shetani au mtu mwovu humchukiza Muumba na kujiletea adhabu. Msemo huu unatuonya kama wanajimii dhidi ya kuwapa watu waovu sifa nzuri.
Bahati yenda kwa wawi wema wakalia ngoa
Maana ya msemo huu ni kuwa bahati ikiwaendea watu waovu, wema huwewaonea wivu iweje wamebahatika? Husistaajabishwe na hayo kwani bahati haibagui.
Akuchukiaye hakosi hila ya kukutia
Maana ya msemo huu ni kuwa, mtu asiyekupenda anaweza kukuzushia mabaya ilimradi tu, akuchafue, akuharibie sifa zako, au mambo yako.
Waja kufa na laiti na vyanda kinywani
Msemo huu unatufunza kuwa tusipozingatia ushauri ama makanyo tutaishia tukifikwa na mabaya na tujutie kutoyazingatia.
Afichaye ugonjwa hufichuliwa na kilio
Funzo kuu katika msemo huu ni kuwa anayefanya siri matatizo yake huumbuka pale yanapomzidi ama kumgharimu hadi kuonekana.
Utatumiaje mchuzi nyama usile
Msemo huu unawalenga watu ambao wnapenda kujinufaisha na mali ya watu wengine ilhali hawataki kuhusishwa na wao. Maana ya msemo huu ni iweje wamkataa mtu ilhali unajinufaisha na vilivyo vyake?
Hutendwaje ikafana shubiri ikawa tamu?
Msemo huu unatufunza kuwa haiwezekani mtu kubadili jambo hata likawa kinyume na lillivyoumbwa au linavyofahamika.