UTAFITI: UFASIHI SIMULIZI KATIKA RIWAYA ZA SHAABAN ROBERT: Mifano kutoka Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad


SURA YA NNE 

UWASILISHAJI NA UCHAMBUZI WA DATA 

4.0 Utangulizi 

Sura hii inawasilisha na kuchambua data zilizopatikana katika utafiti huu kuhusiana na mada iliyofanyiwa uchunguzi. Utafiti huu ulilenga kuchunguza ufasihi simulizi katika riwaya za Kiswahili kwa kutumia mifano ya riwaya za Shaaban Robert za Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti bint Saad. Lengo lilikuwa ni kuchunguza matumizi ya vipengele vya fasihi simulizi na kuonesha jinsi vipengele hivyo vinavyotumika katika kuibua dhamira za kazi hizo. Utafiti huu umebaini kuwa, riwaya zote mbili zimeandikwa na msanii anayeitwa Shaaban Robert, ambapo msanii huyu anatoka katika mwambao wa Afrika Mashariki katika maeneo ya Tanzania (taz. Chuachua, 2009 na Ponera 2010). Kwa ujumla wa sura hii inajibu maswali mawili ambayo yaliongoza utafiti huu. Kwa hiyo, uwasilishaji na mjadala wa data za utafiti huu umejikita katika maswali hayo. Sura hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza inahusu vipengele vya fasihi simulizi, sehemu ya pili ni dhamira zilizoibuliwa na matumizi ya vipengele vya fasihi simulizi na tatu ni hitimisho. 4.1 Vipengele vya Fasihi Simulizi katika Riwaya Teule Moja ya malengo mahususi ya utafiti huu ilikuwa ni kubainisha vipengele vya fasihi simulizi katika riwaya ya Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Ili kufikia lengo hilo, utafiti huu ulitumia mbinu ya usomaji wa machapisho kwa kusoma, kuchambua na kuchunguza vipengele vya fasihi simulizi katika riwaya zote mbili. Matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kuwa, msanii anatumia vipengele vya fasihi simulizi katika utunzi wake. Aidha, mbinu ya dodoso, usaili na majadiliaano ya vikundi 49 zilitumika kuthibitisha, kujaliza na kukamilisha data za utafiti zilizopatikana kupitia mbinu ya usomaji wa machapisho. Kwa ujumla data zilizopatikana kwa kutumia mbinu hizo, zilithibitisha matokeo ya awali hii ina maana kuwa, matokeo haya hayakutofautiana na matokeo yaliyopatikana wakati wa usomaji wa machapisho. Hivyo basi, matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kuwa riwaya ya Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad zimejengwa kwa kutumia vipengele vya fasihi simulizi. Jedwali lifuatalo linaonesha vipengele vya fasihi simulizi vilivyobainishwa katika riwaya ya Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Jadweli na 3 – Vipengele vya Fasihi Simulizi katika Riwaya Teule Na. Kipengele cha Fasihi Simulizi Adili na Nduguze Wasifu wa Siti binti Saad 1. Mandhari √ 1 - 2 2. Wahusika √ - 3. Masimulizi √ √ 4. Ushairi √ √ 5. Utani √ √ 6. Semi √ √ Chanzo : Data kutoka Riwaya Teule (Novemba 2014) Jadweli Na. 3 hapo juu, linadhihirisha kuwa Riwaya ya Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad, zimejengwa kwa kutumia malighafi ya fasihi simulizi. Data hiyo inaonesha kuwa, msanii katika Adili na Nduguze ametumia vipengele vya mandhari, wahusika, masimulizi, ushairi, utani na semi. Kwa upande wa Wasifu wa Siti Binti Saad msanii ametumia vipengele vyote isipokuwa mandhari na wahusika. Hii ina maana kuwa wahusika waliotumika katika riwaya hii si wahusika wa fasihi simulizi na hata mandhari yake ni ya uhalisia ambayo haina sifa za fasihi simulizi. Kwa ujumla utafiti huu umebaini kuwa, vipengele vya Fasihi Simulizi vimetumika kama mbinu ya kisanii 1 Alama hii inaashiria kuwa kipengele fulani kimetumika 2 Alama hii inaashiria kuwa kipengele hakijatumika 50 katika kujenga Riwaya za Kiswahili. Wakati wa majadiliano ya vikundi wahojiwa walieleza kuwa, matumizi ya mbinu za fasihi simulizi ndani ya fasihi andishi ni kuonesha uasilia wa jamii za Kiafrika na fasihi ya Kiafrika katika fasihi andishi. Vipengele hivi vinaonesha kuwa, kuna kuingiliana na kuathiriana kwa mbinu za utunzi wa kazi za fasihi hoja ambayo inasisitizwa na wana nadharia ya muingilianomatini. Utafiti huu umebaini kuwa, vipengele vya fasihi simulizi vinatumika kama malighafi ya utunzi wa riwaya. 4.2 Vipengele vya Fasihi Simulizi na Uibuaji wa Dhamira Moja ya lengo mahsusi ya utafiti huu ilikuwa ni kubainisha dhamira zinaziowasilishwa na matumizi ya vipengele vya fasihi simulizi. Kwa kutumia mbinu ya majadiliano ya vikundi utafiti ulibaini kuwa, vipengele vya fasihi simulizi si kwamba vinatumika kama malighafi ya utunzi katika riwaya za Kiswahili hususani za Shaaban Robert bali matumizi ya vipengele vya fasihi simulizi huwa na dhima maalumu kisanii. Vipengele hivyo hutumika kama mbinu za kisanii zinazobeba dhamira za riwaya hizo. Sehemu ifuatayo inajadili vipengele vya Fasihi Simulizi na dhamira zilizoibuliwa kutokana na matumizi ya vipengele hivyo. 4.2.5 Matumizi ya Dhamira katika Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad Kipengele cha dhamira pia kimetumika katika kukamilisha kazi ya Adili Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Utafiti umebaini kuwa dhamira zilizotumika ni zile zile za fasihi simulizi. Kwa upande wa Adili na Nduguze ni kama ifuatavyo : mandari ya baharini, maweni na majabalini (yameibua dhamira za ubinafsi, uvivu, umasikini), wahusika kama vile Ikibali, Adili na Faraja, Hasidi, na Mwivu (uadilifu, uwajibikaji, 51 elimu, huruma, upendo, uadui, choyo na wivu), mhusika dhahania/jini/Huria ( Dhamira ya uadilifu na uhuru katika maamuzi), masimulizi (wivu, choyo, na chuki, uongozi mbaya, uongozi bora, ubinafsi, usaliti, elimu na uwajibikaji, ujasiri, na nguvu), ushairi (kuepuka maovu, semi kama vile methali, tamathali ya semi ya takriri (ustahamilivu, mapenzi, majisifu,uadilifu). Katika riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad vipengele husika na dhamira zake ni (utubora, kujiamini na kutokata tamaa), ushairi (wivu, chuki, dini, heshima, kutenda mema), utani (ukweli, pongezi), na semi kama vileta ta ta methali, takriri (ukweli wa maisha, mafanikio). Uchambuzi wa data umerejelea data za uwandani na mifano kutoka kitabu cha Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. 4.2.1 Vipengele vya Fasihi Simulizi na Dhamira katika Adili na Nduguze Kama tulivyoeleza hapo awali, utafiti huu ulibaini kuwa, vipengele vya fasihi simulizi hutumiwa na msanii katika kuibua dhamira za kazi yake ya fasihi. Sehemu ifuatayo inajadili vipengele vya fasihi simulizi vinavyojitokeza katika riwaya ya Adili na Nduguze na dhamira zinazoibuliwa kutokana na mbinu ya matumizi ya vipengele vya fasihi simulizi. 4.2.1. 1 Matumizi ya Mandhari katika Adili na Nduguze Utafiti huu ulibaini kuwa, mtunzi katika Adili na Nduguze, ametumia mandhari ya fasihi simulizi kama vile mandhari ya baharini na kuibua dhamira ya ubinafsi. Tazama dondoo ifuatayo; (1) Usiku Adili alipokuwa amelala na jahazi inakwenda mbio kwa pepo za omo, ndugu zake walikuwa macho. Mawazo mabaya hurusha usingizini. Kuzinduka kwake usingizini Adili alijiona amechukuliwa 52 hangahanga. Mmoja alimshika kichwani na mwengine miguuni. Koo yake ilisongwa sana”. (Adili na Nduguze Uk. 33) Mfano namba 1 hapo juu unaonesha kuwa msanii ametumia mandhari ya bahari ambayo yanaibua dhamira ubinafsi. Mandhari ya aina hii ni mandhari ambayo hutumiwa katika masimulizi ya hadithi, visakale na ngano za Kiafrika. Wakati wa majadiliano ya vikundi wahojiwa walibainisha kuwa, msanii ametumia mandhari hii kuonesha ubinafsi hali ambayo inasababisha usaliti wa ndugu za Adili kuamua kumtosa baharini ndugu yao ambaye ni mhusika Adili. Mwandishi anaonyesha kuwa Adili, alitoswa baharini kutokana na mali yake mwenyewe. Hii inadhihirisha usemi wa Kiswahili usemao „Nyuki hutiwa moto sababu asali yake‟. Aidha, mandhari ya mji wa mawe ni mandhari ya fasihi simulizi inaibua dhamira ya uvivu. Tazama mfano ufuatao (2) “Kila barabara aliyopita ilikuwa na watu, Ng’ombe, farasi, Nyumbu, punda na mbwa lakini wote walikuwa mawe matupu. Hofu kubwa ilitamba moyoni mwake kuwa naye asije geuzwa jiwe. Lakini alifarijika kuwa labda ilikuwako katika mji ule, wanyama na vitu vyake kuwa mawe, na kuwa lilikuwa fundisho kwake”. (Adili na Nduguze uk 28) Mfano namba 2 hapo juu unaonesha matumizi ya mandhari ambayo yanaibua na kujenga dhamira ya uvivu. Msanii anaonesha kuwa katika sehemu hiyo kuna rasilimali nyingi lakini watu wote walikuwa mawe matupu. Mawe matupu hapa imetumika kama sitiari inayowakilisha watu wasiofanya kazi wavivu. Kwa kawaida jiwe haliwezi 53 kufanya kazi na haliwezi kuhama sehemu lilipo. Dhana hii inajenga dhamira ya uvivu pamoja na kuwepo kwa utafjiri mkubwa watu walikuwa hawautumii. Vile vile utafiti huu ulibaini kuwa msanii ametumia mandhari ya jabali kuibua dhamira ya umaskini. Tazama dondoo ifuatayo; (3) “Baada ya safari ya siku moja walifika jabalini. Nahodha aliamuru kutua tanga na kutia nanga. Kisha mabaharia walitakiwa washuke jabalini kutafuta maji kwa sababu jahazini mlikuwa hamna maji hata tone moja”. (Adili na Nduguze uk. 22,) Mfano namba 3 hapo juu unaonesha kuwa, msanii anatumia mandhari ya jabali kuibua dhamira ya umaskini. Hii inadhihirishwa na pale msanii anaposema jahazini mlikuwa hamna maji hata tone. Maneno hayo yanaonesha kuwa, wafasiri hao walikuwa na njaa na kiu kutokana na umaskini uliokithiri katika nchi yao. 4.2.1.2. Matumizi ya Wahusika katika Adili na Nduguze Wahusika kama inavyojulikana ni wawakilishi katika kazi ya fasihi ambao huwakilisha tabia, matendo, hulka na silka kulingana na muktadha halisi wa jamii ambao huambatana na mila na desturi za jamii husika. Wahusika hawa ni wahusika wa kiishara ambao pia huwasilishwa kitabia kulingana na majina yao, ambao vile vile hupatikana katika fasihi simulizi, mfano katika hadithi kama vile Visakale, Visajanja na Vigano. Mwandishi wa kitabu cha Adili na Ndguze ametumia wahusika na wameibua dhamira ya uadilifu na uwajibikaji Mwandishi anasema kuwa; 54 (4) “Jioni Ikibali na Adili walipokuwa peke yao mazungumzo juu ya kodi yalianza. Hapakuonekana na upungufu wowote. Hesabu haikuwa kamili tu, lakini ilionyesha ziada vile vile”. (Adili na Nduguze uk. 06,) Mfano namba 4 hapo juu unaonesha kuwa msanii anawapa majina wahusika kulingana na sifa zao, kulingana majina yao, mfano Ikibali kwa maana ya kuwa mtu anayeelekeza mambo fulani na pia ni ujio wa mtu mwenye kazi maalumu inayotakiwa kuchunguzwa. Kwa kutumia majina ya wahusika msani anaibua dhamira ya uwajibikaji kwa kuonesha umuhimu wa kufanya kazi. Dhamira hii inonyesha kuwa kila mtu afanye kazi kulingana na ujuzi ilioupata, na pia ni muhimu kufanya kazi, kwasababu kazi ndio msingi wa maendeleo. Vile vile jina la Adili linaibua dhamira ya uadilifu. Kwa kutumia jina la mhusika Adili msanii anaibua dhamira ya uadilifu katika maisha na jamii. Hapa anaonesha kuwa, kiongozi lazima awe mwadilifu, mnyenyekevu na mwaminifu. Apende kutimiza wajibu wake katika jamii kulingana na kazi yake aliyopewa na wajibu wake katika jamii. Dhamira hii inadhdihirisha kuwa, kazi ndio msingi wa kila kitu katika jamii na ni msingi wa maendeleo kwa jamii yoyote. Vile vile msanii anatumia jina la Ikibali, kuibua dhamira ya elimu na umuhimu wake katika jamii. Wakati wa majadiliano ya vikundi wahojiwa walieleza kuwa, majina ya wahusika yametumika kuibua na kubeba dhamira mbalimbali. Wakitolea mfano wa Adili na Ikibali wahojiwa walisema kuwa, wahusika hawa kwa pamoja wamebeba dhamira ya umuhimu wa kutafuta elimu kwa njia yoyote ile, mpaka mtu afanikiwe na kile anachokitafuta kwa kujua jema na lililo baya. Aidha, anatumia mbinu ya safari kuonesha umuhimu wa elimu na sababu ya kuitafuta elimu kwa gharama yoyote ile. Hapa msanii anawatumia wahusika hao na safari yao ya kuitafuta elimu katika maeneo mengine. 55 Utafiti huu ulibaini kuwa, mwandishi anatumia majina ya wahusika na wahusika wenyewe kuwabebesha dhamira ndani yao. Katika matendo yao, tabia zao na majina yao. Tazama mfano katika dondoo lifuatalo; (5) “Adili alisema manyani manyani walikuwa ni ndugu zake. Baba yao aliitwa Faraja. Faraja alikuwa mtoto wa pacha. Wakati wa kuzaliwa pacha hiyo mtoto mmoja alikufa. Huyu aliyebakia aliitwa Faraja kwa sababu aliwafariji wazazi wake katika msiba wa ndugu yake. Alipokuwa wazazi wake walimwoza mke, yaani mama yao. Mama yao ilichukuwa mimba ya kwanza akazaa mwana aliyeitwa Hasidi. Alichukuwa mimba ya pili akazaa mtoto aitwae Mwivu na kuchukuwa mimba ya tatu akazaa mwana tena aliyeitwa Adili”. (Adili na Nduguze uk. 14,) Katika mfano namba 5 hapo juu unaonesha kuwa mhusika mwenye jina la Faraja anaibua dhamira ya faraja na kufarijiana katika kila jambo. Katika matatizo na shida zote ndani ya jamii. Dhamira hii pia inaenda sambamba na dhamira ya huruma na upendo. Kwamba mtu anayetoa faraja kwa mwingine ni mwingi wa huruma na upendo. Kwa upande wa mhusika Hasidi mtunzi anatumia jina la mhusika huyu kuibua dhamira ya uadui na choyo. Uchoyo ni hali ambayo inaonyesha ukosefu wa usawa na haki katika uongozi wa aina yoyote. Aidha, kwa kutumia muhusika Mwivu msanii anaibua dhamira ya wivu. Kwa kutumia mhusika huyu, msanii anaonesha kuwa wivu na uhasidi ni adui wa maendeleo katika jamii. Vile vile ni hali inayonyesha kuwa wivu ukizidi sana kwa kwa kitu chochote huleta madhara katika jamii. Msanii anaonesha kuwa wivu ndio uliowafanya nduguze Adili kumwonea wivu na kumtupa baharini kwa kusudia kumuuwa. 56 Utafiti huu ulibaini kuwa, msanii katumia wahusika dhahania kwa mfano, mhusika Huria ambaye amechorwa kama jini lakini anawakilisha muhusika ambaye ni hakimu muadilifu katika kuamua kesi kwa kumsikiliza muathirika na aliyesababisha tukio linalojadiliwa. Huria kulingana na mwandishi anatupatia dhamira ya uadilifu na uhuru katika maamuzi. Uadilifu huu unaonekana pale ambapo wahusika wawili, Hasidi na Mwivu walipotenda mabaya na kisha kuhukumiwa na kulingana na makosa yao, walihukumiwa kupigwa pamoja na kufungwa, ndio hukumu waliyopewa walipotaka kumuua ndugu yao Adili. Vile vile kulingana na mwandishi maelezo yanaonyesha kuwa unapoaminiwa na wewe unatakiwa kujiamini, kwasabubu Adili aliwaamini ndugu zake Wivu na Hasdi lakini wao walishindwa kujiaminisha kwa ndugu yao Adili. 4.2.1.3 Matumizi ya Masimulizi katika Adili na Nduguze Utafiti huu ulibaini kuwa, msanii anatumia masimulizi ya kifasihi simulizi katika kuibua dhamira za kazi yake. Masimulizi katika riwaya ya Adili na Nduguze yanaibua dhamira mbalimbali kama vile wivu, choyo na chuki, uongozi mbaya, ubinfasi, usaliti, umuhimu wa elimu na uadilifu na uwajibikaji. Tazama mfano ufuatao; (6) “Rai, mfalme wa Ughaibuni, alikuwa mfalme wa namna ya peke yake Duniani, alikuwa na tabia iliyohitilafiana kabisa na tabia ya watu wengine wa zama zake. Tabia yake ilijigawa katika thuluthi tatu mbalimbali kama ngozi ya punda milia. Kwa thuluthi ya kwanza alikuwa msuluhifu, akapendwa na watu, kwa thuluthi ya pili alikuwa kama Daud akaheshimiwa kama mtunzaji mkuu wa wanyama, na 57 kwa thuluthi ya tatu alikuwa kama Suleiman akatiiwa na majini”. (Adili na Nduguze uk. 01) Katika mfano namba 6 hapo juu msanii anatumia masimulizi ya hadithi kuibua dhamira ya kiongozi bora na uongozi bora. Hapa msanii anatuonesha jinsi kiongozi bora anavyoweza kuheshimiwa na kupendwa na watu. Msanii anatumia masimulizi kuibua sifa za kiongozi bora ni yule anayesikiliza mawazo ya wale anaowaongoza. Katika mfano namba 6 pia tunaona mwandishi akiibua dhamira ya utamaduni. Jamii za pwani ya Afrika Mashariki huamini kwatika viumbe visivyoonekana ambavyo ni majini. Viumbe hawa wamepewa nguvu na uwezo wa ajabu na jamii huamini katika uwepo wa viumbe hao. Kwa hiyo, msanii anatumia wahusika hawa dhahania kuonesha nguvu na uwezo wa kiongozi ambaye pia anapewa heshima na utii wa viumbe hivi dhahania. Vile vile mwandishi anasema (7) “Kila mahali Huria alipopita, Hunde alifuata Nyayo zake mpaka aligundua alikokuwa, iliendelea hivyo hata kiasi akapigana naye. Alishindwa akakimbia, huria. Huria alipotaka kutembea alijigeuza umbo la mnyama, kila alipojigeuza na yeye alijigeuza vile vile, akanusa harufu yake kama mbwa. Alipojigeuza panya, yeye alikuwa paka, alipojifanya paka, yeye alijigeuza chui, na alipokuwa chui, yeye akawa simba”. (Adili na Nduguze uk. 45). 58 Masimulizi haya yanaibua dhamira ya ujasiri na nguvu. Hapa msanii anatumia masimulizi haya kuonesha ujasiri, ushujaa na nguvu za mhusika. Wakati wa majadiliano ya vikundi wahojiwa walisema kuwa, masimulizi haya yanaibua dhamira ya ujasiri na ushujaa ambao unaonesha uwezo waliokuwa nao wahusika katika kuyakabili mazingira yao. Masimulizi pia yametumika kuibua dhamira ya elimu kwa mfano Adili aliposema; (8) “Alipogeuka kwa ndugu zake Adili, Rai alionya kama wavivu walijitahidi kuwa hodari, ilikuwa kinyume hodari kuwa mvivu; kama waovu walitaka kuwa wema, ilichukiza wema kuwa waovu; kama masikini walitafuta utajiri, ilikuwa ujinga matajiri kufuja walichonacho; kama mbegu kidogo iliyogeuzwa mchanga ilikuwa uharabu mtu kuuwa ndugu yake; pia ilikuwa aibu kubwa sana kwa wazuri kutenda maovu”. (Adili na Nduguze uk. 48) Katika mfano namba 8 hapo juu, tunaona kuwa, msanii anaibua dhamira ya elimu kwa kutumia mbinu ya masimulizi. Funzo analolitoa Adili katika masimulizi hayo ni kila moja ajitahidi kuwajibika kulingana na elimu aliyonayo na kuitumia elimu hiyo katika kufanya kazi na kuwajibika. 4.2.1.4 Matumizi ya Ushairi katika Adili na Nduguze Utafiti umebaini kuwa msanii ametumia utanzu wa ushairi katika kuibua dhamira za kazi yake. Tazama mfano namba 9 hapa chini; (9) Mawe huwa dhahabu Au johari na chuma, 59 Na mtu anapotubu Dhambi yake kukoma, Nishani zake dhahabu Na heshima ya daima. (Adili na Nduguze uk. 48). Mfano namba 9 hapo juu unaonesha matumizi ya ushairi katika riwaya. Kwa kutumia mbinu ya ushairi mtunzi anaibua dhamira ya kuepuka uovu. Hapa msanii anaonesha kuwa mtu anapoacha kutenda dhambi hubadilika na kuwa mwema na kuheshimiwa na jamiii. Dhamira hii inajenga umuhimu wa kupatikana kwa amani, upendo na kutokea kwa utulivu katika jamii, na pia huwa ni heshima kwa wale walioomba msamaha baada ya kufanya kosa na kuwa watu bora kulingana na jamii. 4.2.1.5 Matumizi ya Semi Adili na Nduguze Utafiti umebaini kuwa katika kitabu cha Adili na Nduguze misemo imetumika kuibua dhamira. Dhamira ambazo zinathibitishwa na maelezo yafutayo; (10) “Ulimi wake mwenyewe ulimponza” (Adili na Nduguze uk. 11) (12) “Adili ilitamka kuwa maisha ni safari na Dunia ni matembezi kwa wanadamu” (Adili na Nduguze uk. 15) (13) “Hakika mtu mwenye kuhesabu mapato yake hafi maskini” (Adili na Nduguze uk. 16) Misemo yote hiyo inaonyesha jinsi ya maisha baada ya kufa au kitu chochote kina faida na hasara. Hivyo utafiti umebaini kila kiti kina mafanikio na pia kina matatizo. Ustahamilivu juu ya mafanikio ya kitu katika maisha huwa kunastahili ustahamilivu. Dhamira ya ustahamilivu inaonekana ni sawa ma kusema mstahamilivu hula mbovu. 60 Hali aliyomfanya Adili kusubiri ukweli utokee juu yake na kukosa kufa lakini ni sawa na kusema mwenye kusubiri hajuti hata kidago. Vile vile dhamira ya ustahamilivu inapatikana pale ambapo mtu anapotafuta kitu kwa muda mrefu bila ya mafanikio na baada ya muda kaweza kufanikiwa, hii ina maana kwamba hakuna kitu rahisi kupatikana. Kila kitu hupatikana kwa shida na huwa kina masharti katika kukitafuta, hakuna kupata kwa urahisi isipokuwa ni lazima kuhangaika. Pia utafiti umebaini kuwa mtu anavyoishi ajuwe kuna siku ataondoka katika jamii anayoishi. Hivyo muhusika yoyote anatakiwa kutenda yalo mema ili yamfae baada ya kuondoka katika ulimwengu kwa kufuata mila na desturi za jamii. Pia misemo mengine katika kitabu cha Adili na Nduguze ni ile isemayo; (14) “Mwanaume hakukusudiwa kuwa fahali wa kila mtamba wa kila jogoo, wala mwanamke kuwa tembe wa kila jogoo” (Adili na Nduguze uk. 32) Kutokana na misemo hiyo, utafiti umeibuwa dhamira ya mapenzi ya kweli. Mwandishi anaonyesha kuwa mapenzi ya kweli ni chanzo cha mafaniko ya kuwepo ukweli na uwazi katika jamii. Mapenzi siku zote ndio muonekano wa mtu uzuri wake na hata awe kiongozi wa ngazi yoyote katika jamii hata ile ya familia, na pia utafiti uliona kuwa, swali la ndoa kuwa ndio taasisi kubwa ya kukuza na kuendeleza utamaduni unaopinga mila na desuri mbaya, kwa mfano kuepusha na maradhi mbali mbali yanayosumbua jamii na hata ulimwengu mzima. Utafiti ulibaini ya kuwa dhamira ya kujisifu. Kujisifu ni hali ya mtu kufanya jambo ambalo haliwezi kulifanya, anafanya kwasababu aonekane tu. Hivyo kujisifu kwa kujua 61 kitu sio sababu ya kuweza kutatau jambo lililoikabili jamii. Mfano wa maelezo yafuatayo yanathibitisha hilo; (15) “Aliudhika akataka kumuonyesha Huria uwezo wake. Na tangu alipotishia hivyo hakumpa nafasi hata ya uzi kupenya tundu la Sindano”. (Adili na Nduguze uk. 45,) Vile vile kutokana na lengo la utafiti kwa kutokana na msemo uliotangulia, utafiti umegundua dhamira kujitambua. Kujitambua na hali ya kuwepo kwa tabia ya baadhi ya wale wanaojifanya wanajua baadhi ya vitu, kumbe ni kujionyesha tu kuwa wanajua na kumbe hawajui kama hawajui. Hali inayothibitisha kuwa ajuwaye ni yule asiyetaka kusifiwa na ajuae ni yule anayefanya mambo bila kujisifu. Pia misemo imetumika kuibua dhamira iliyokusudiwa kufikishwa kwa wahusika, waliokusudiwa kupewa kufikishiwa dhamira hiyo. Dhamira inayopatikana kutokana na utafiti ni yale yanayobainishwa na maneno yafuatayo; (16) Alimwambia mama yake kuwa deni alilowiwa na Adili lilikuwa kubwa sana. Hakudai lilipwe lote lakini alitaka lipunguzwe kama lilivyowezekana. Mjeledi ulimwambia Adili wema wake haukuoza”. (Adili na Nduguze uk. 46) Maelezo hayo yanaonyesha jinsi ya dhamira ya uadilifu. Uadilifu ni hali kufanya jambo kufuata misingi na sheria ya jamii. Hivyo kila mtenda wema huitendea nafsi yake na pia mtenda mabaya vile vile huitendea nasfi yake. Dhamira inaonyesha kuwa “kila mchuma janga hula na wa kwao”, hii inamaanisha kuwa yoyote anayefanya kosa huwa haathiriki peke yake bali na jamii yake na pia wema hauozi milele. Hivyo utafiti umebaini kuwa kila mtu analolifanya atalipwa kulingana na kile alichokifanya kwa jamii yake. Vile 62 vile unapotenda wema basi kama yalivyoonyesha maandishi basi iko siku yatakurejea yale yale, ama kama ni mema au ni mabaya lakini yatatokea na kuathiri kwa ubaya au wema. Ni sawa na Adili baada ya ndugu zake kugeuzwa Manyani, yeye mwenyewe Adili kwa mikono yake aliwaadhibu ndugu zake, ni kawaida ya sharia ni sawa na msumeno kukata mbele na nyuma, haichaguwi alipotoka mtu wala anatoka familia fulani katika jamii. Hali iliyoonyesha kuwa hukumu inayofuata linalotakiwa na jamii, ndio kitulizano kwa jamii pale inapofanyiwa uadilifu sheria katika hukumu. Kwa upande wa methali katika kitabu cha Adili na Nduguze, utafaiti umegunduwa kuwa kuna dhamira imeibuliwa kutokana na methali. Methali ndio moja ya njia ya kufikishia mawazo, fikra, shauku pamoja hisia kulingana na matendo ya jamii. Kulingana na maelezo hayo ni kweli kwamba methali ndio kitu rahisi cha kupelekea dhamira kwa jamii kwa urahisi, utafiti umebaini kuwa methali huwa ni daraja baina mtoaji wa methali na jamii. Hivyo dhamira mbali mbali zinapatikana kupitia methali zilizotangulia kwa ajili ya kuvutia na kufikisha dhamira kwa urahisi. Kwasababu methali hutolewa wakati wowote na ni kitu ambacho hutumiwa sana na wazungumzaji. Dhamira mbali mbali zimeonekana kuwa zimetokana na methali hizo. Dhamira kama ile ya ubinafsi, uchoyo na pia ile ya uonevu. Dhamira hizi zimetumika kuweza kuipamba kazi hii ya fasihi andishi. Hali inayonyesha kuwa kumbe fasihi simulizi ni mali ya jamii na pia ndio inayotoa mchango mkubwa katika kazi ya fasihi andishi. (17) “Hasidi na Mwivu hawakujua la kutenda. Atakae makaa ya mgomba hapati kitu ila jivu tupu”. (Ukurasa wa 50, Adili na Nduguze) 63 (18) “Walakini Adili aliwashukuru akisema bahari haiweki amana ya kitu kieleacho. Kwa kuwa alielewa ameokoka”. (Ukurasa wa 50, Adili na Nduguze) (19) “Damu nzito kuliko maji. Hasidi na Mwivu walikuwa damu ya Adili”. (Ukurasa wa 50, Adili na Nduguze) Maelezo yaliokwisha tangulia yanaonyesha kuwa dhamira ya ubinafsi imetawala miongoni mwa wanajamii. Ubinafsi huu unasababisha kuviza maendeleo ya jamii kutoka hatua moja hadi hatua nyingine ya kimaendeleo. Kwa kawaida kila mtu ni mbinafsi wa nafsi yake lakini utafiti umebaini kuwa ubinafsi ukizidi huwa unaleta hasara miongonimwa wanajamii. Hivyo ubinfasi ndio chanzo kimojawapo kinacholeta mfarakano miongoni mwa wanajamii, kulingana na mila, desturi, silka na utmaduni wa jamii. Vile vile methali kutokana na riwaya ya Adili na Nduguze zimeibuwa dhamira tofauti kulingana na maelezo yafuatayo; (20) Kula uhundo kwataka matendo, asiye matendo hula uvundo”. (Ukurasa wa 28, Adili na Nduguze) Dhamira ya kujitolea inaonekana kuwepo katika methali iliyopita. Kujitolea kuna namna nyingi, hapa imekusudiwa iwe ya kufanya kazi kwa bidii, na kujiamulia kufanya kazi kwa njia yoyote lakini iwe ile ya halali katika kufuata mila na desturi na maelekezo jamii kulingana na wahusika na matendo yao. Hivyo tunatakiwa tujitolee katika kufanya kazi tuepekane na ile hali kuomba omba ndio mafanakio, lakini kumbe uvvivu hauzai 64 mwana mwema na pia macho sio kipimo ni kidanganyo cha moyo, maneno ndio yanayoweza kuutengeza moyo au kuharibu moyo, hivyo maneno ni kipimo cha kila kitu kwa mwanadamu. Utafiti umebaini kuwa maneno na matendo mazuri ndio mafanikio katika kila kitu, kwasababu kinachosemwa mdomoni huwa kiko moyoni. Maneno yanatakiwa yasiwe mengi bali yafuatwe na matendo na ndipo tuunapochuma juani na kula kivulini kwa raha. Kwa wale wasiopenda kufanya kazi basi wao watabakiwa na kuomba omba tu ni sawa na uvundo. 4.2.2 Vipengele vya Fasihi Simulizi na Dhamira katika Wasifu wa Siti Binti Saad Kama tulivyoeleza hapo awali, utafiti huu ulibaini kuwa, vipengele vya fasihi simulizi hutumiwa na msanii katika kuibua dhamira za kazi yake ya fasihi. Sehemu ifuatayo itajadili vipengele vya fasihi simulizi vinavyojitokeza katika riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad na dhamira zinazoibuliwa kutokana na mbinu ya matumizi ya vipengele vya fasihi simulizi. 4.2.2.1 Matumizi ya Masimulizi katika Wasifu wa Siti Binti Saad Katika kuchunguza matumizi ya vipengele vya fasihi simulizi katika riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad utafiti huu ulibaini kuwa, msanii ametumia masimulizi kama mbinu ya kisanii kuibua dhamira za kazi yake. Utafiti umegundua kuwa mtindo wa riwaya ya Siti Binti Saad, ni masimulizi ya hadithi ya wasifu mwanamke shujaa, ambaye aliishi zamani. Msanii anatumia mbinu ya masimulizi kusimulia habari za sifa, wasifu, na tabia za mwanamke huyo mwenye kipaji ambacho alikitumia katika kuitangaza nchi yake pembe zote za Dunia na kujipatia umaarufu. Tazama mfano ufuatao hapa chini. 65 (21) “Nchi hazikuhesabu ubora wa watoto wake, mpaka watoto wake walipokuwa wamepita maisha ya mwili, roho zao zilipokuwa zimevuka Ng’ambo ya pili ambako upeo wa macho haukuweza kufika wala mweto wa mwanadamu haukuweza kusikika, tena baada ya miili yao ilipokuwa imekwisha changanyika na vumbi la ardhi, na thamani yao yote kama viumbe bora ilipokuwa imepotea”. (Ukurasa wa 01, Wasifu wa Siti Binti Saad.) Mfano namba 21 hapo juu unaonesha masimulizi ambayo yaibua dhamira ya utubora na umuhimu wa kutambua utu wa mtu akingali hai. Hapa msanii anaibua tabia ya binadamu ambao hawathamini mchango wa mtu mpaka pale anapokufa ndipo huelewa thamani yake. Wakati wa majadiliano ya vikundi wahojiwa walieleza kuwa mara nyingi watu wenye mchango mkubwa kwa taifa sifa zao huoneka wakati wakiwa wamefariki dunia. Utafiti umebaini kuwa matendo mema ni hesabu baada kuondoka katika jamii, na vile vile, matendo mabaya ni sifa baada ya kuondoka katika jamii aliyoishi mwanajamii katika uhai wake, kulingana na utamaduni wa jamii husika. Mwandishi anaonyesha ubora wa Siti ulijulikana katika Afrika Mashariki baada ya kuaga Dunia, hii inadhihirisha kuwa mtu husifiwa baada ya kuondoka Duniani, ndipo huonekana thamani yake. Vile vile utafiti umebaini kuwa masimulizi yametumika kuibua dhamira ya kujiamini na kutokata tamaa. Tazama mfano ufuatao; (22) “Siti alipotokea katika taarabu katika mara ya pili na baadaye, alionekana na mabadiliko kabisa. Zaidi ya kuweza kuimba 66 alionyesha vile vile madaha na mtindo mpya uliochukuwa watu kwa ghafla ukawatia katika mshangao mkubwa”. (Ukurasa wa 03, Wasifu wa Siti Binti Saad). Kutokana na maelezo hayo utafiti umebaini kuwepo kwa dhamira ya kujiamini. Wakati wa mahojiano ya vikundi, wahojiwa walibainisha kuwa, ujasiri na kujiamini ndiyo silaha aliyoitumia Siti katika uimbaji wake na kujitangaza duniani kote. Hili linathibitishwa na masimulizi ya mwandishi kuwa Siti alipata mafanikio pale alipoondoa hofu na hii ilimpa umaarufu na kutangaza jina lake duniani kote. 4.2.2.2 Matumizi ya Ushairi katika Wasifu wa Siti Binti Saad Katika riwaya ya Wasifu wa Siti binti Saad, utafiti huu ulibaini kuwa, mtunzi ametumia mbinu ya ushairi kuibua dhamira ya kazi yake. Tazama mfano ufutao; (23) Siti binti Saad Ulikuwa mtu lini? Ulitoka shamba, Na kaniki mbili chini, Kama si sauti, Ungekula nini? (Ukurasa wa 22, Wasifu wa siti Binti Saad). Katika mfano namba 12 hapo juu, msanii anatumia ushairi kuibua dhamira ya wivu na chuki. Hapa msanii anaonesha jinsi Saad alivyopigwa vita na watu ambao walimuona kama si mwimbaji bora kwa sababu ya wivu na chuki walizokuwa nazo dhidi yake. Katika shairi hili tunaona kuwa Siti alidharauliwa kwa sura yake na pia alidharauliwa kwa umaskini wake, isipokuwa alisifiwa kwa sauti yake. Umasikini wake unaonekana 67 kuwa sio tatizo bali ni miongoni mwa utamaduni wake katika mavazi ya kuvaa kaniki na miguuni kuwa hana hata kiatu, dharua hii ni hali ya baadhi ya watu kudharau sehemu moja na kuitukuza sehemu nyengine. Swali lilosababisha kupatikana kwa jawabu ambalo lilijibiwa kama ifuatavyo; (24) Si hoja uzuri Na sura jamali Kuwa mtukufu Na jadi kubeli, Hasara ya mtu. Kukosa akili, (Ukurasa wa 29, Wasifu wa siti Binti Saad) Aidha, kwa kutumia ushairi mtunzi anaonesha majibizano baina ya Siti na maadui wake. Mtunzi anatumia mbinu ya ushairi kuibua dhamira ya elimu na kujitambua. Hapa msanii anaonesha kuwa elimu na kujitambua kiakili na kiutamaduni ndiyo silaha ya ushindi katika mapinduzi yoyote kwa mtu binafsi ama jamii nzima. Vile vile, utafiti huu ulibaini kuwa katika majibizano hayo ya kishairi msanii anaibua dhamira ya imani ya dini. Tazama mfano ufuatao; (25) Sikusudi langu Kuvunja utani, Enyi walimwengu, Mwajua yakini, Apendalo Mungu, Haliwezekani. 68 (Ukurasa wa 30, Wasifu wa siti Binti Saad) Katika mfano namba 25 tunaona majibu ya Siti kwa madui zake. Hapa msanii anatumia mbinu ya ushairi kuonesha imani ya dini na kuwepo kwa nguvu na uwezo wa Mungu katika maisha ya binadamu. Imani ambayo alikuwa nayo Siti kuwa kila linalomfika binadamu ni mapenzi ya Mungu. Siti alijitambua na kujua yeye ni nani na ana hadhi gani kwa jamii, pia kwa Muumba wa Ardhi na Mbingu na vilivyomo. Pia utafiti umebaini kuwa kutokana na tajriba ya maisha kila mwanajamii ana kipaji fulani alichonacho, ambacho amepewa na muumba wake. Mbinu ya ushairi pia imetumika kuonesha heshima na tuzo ya ushindi. Tazama mistari ifuatayo; (26) Siti wa sitiwa Na amaarufu, Na wingi wa haya Na ujamilifu, Pokea hidaya Ingawa dhaifu. (Ukurasa wa 32, Wasifu wa siti Binti Saad) Katika mfano namba 15 hapo juu, msanii anaibua dhamira ya heshima na tuzo. Hapa msanii anaonesha kuwa, kila mwenye kufanya jitihada ya kazi yoyote hupewa heshima na tuzo ya jitihada zake na mafanikio yake. Dhamira hii ina lengo la kufunza jamii kuthamini mchango wanayoitoa wanajamii katika kujenga na kuitambulisha jamii kwa jamii zingine duniani. 69 Katika kielelezo 27 vile vile dhamira ya kuombeana mema imejitokeza. Utafiti unalithibitisha hili kwa kupitia shairi lifuatalo; (27) Umetoka ushiridu Dua ladhaa adhima, Kurejea Al Amiri Sultani muwadhama, Jamii twamshukuru Mola Haya El Kiyama, Astahiki salama Maulana Al amiri. Bwana ulipondoka Raia tuliinama, Sote tulidhoofika Tulihadhiri jasama, Nasasa umefika Mwili utarudi nyama, Astahiki salama Maulana El Amiri. (Ukurasa wa 38 nz 39, Wasifu wa Siti Binti Saad) Utafiti umebaini kuwa katika shairi hili inaibuka dhamira ya kutenda mema. Mwandishi anaonyesha kuwa iliyeombewa duwa, ilitenda mema, kuwapenda na kuwathamini wenzake na yeye alistahili kuombewa dua kutokana na aliyoyatenda. Utafiti umebaini 70 pia sio jambo zuri kuomba dua mbaya kwa wengine. Hii inamaanisha kwamba wema hauozi na hata ukioza hauwezi kuchakaa, kwasababu mtenda mema hutendea nafsi yake na pia mtenda maovu huitendea nafsi yake. Wema hauozi na uovu hauchakai ila kwa kuomba radhi. 4.2.2.3 Matumizi Utani katika Wasifu wa Siti Binti Saad. Kwa upande mwengine utafiti ulibaaini Mazungumzo (Matani) yalitumika kuibua dhamira. Dhamira ni sawa na zile zilizotumiwa na fasihi simulizi, lakini zimetumika katika kazi ya Wasifu wa Siti Binti Saad. Matani katika kielelezo 28 ni kuwa mwandishi ametumia kwa ufundi mkubwa, kiasi ambacho utafiti umebainu kuwa mtunzi Shaaban Robert kuwa alikuwa fundi mkubwa katika kuipamba kazi yake kwa kutumia lugha. Haya yanajibainisha kwa kuangalia maneno yafuatayo; (28) Siti binti Saad Ulikuwa mtu lini? Ulitoka shamba, Na kaniki mbili chini, Kama si sauti, Ungekula nini? (Ukurasa wa 22, Wasifu wa Siti Binti Saad) Maelezo yaliyopita, yaliyowasilishwa kwa muundo wa shairi yanaonyesha kuwa muhuska Siti alikuwa anabishana na kuzungumza na mtu ambaye alifanya matani na Siti, kutokana na utani wa kijadi. Ndipo utafiti ulipobaini Dhamira ya matani. Matani yaliibuka na kuonyesha uhalisia wa mambo yaliyopo katika jamii. Ama kwa maumbile 71 yake mabaya, sura yake, tabia yake, umasikini na hata eneo alilotoka. Hali ambayo inaonyesha matani fulani baina ya watani wawili wanapokutana katika matani yao ya kimila, kutokana na utamaduni wao na jinsi makabila hayo yanavyofanana na pia kutofautiana kwa hali tofauti. Hivyo kulingana na malengo ya utafiti tunapata dhamira ya utamaduni. Dhamira inasema kuwa matani ndio msingi mkuu wa kujenga udugu baina ya pande mbili zinazohasimiana, pia matani ndio kitu kinachojenga upendo na urafiki miongoni mwa wanajamii miongoni mwao. Kwani unapotaja sifa na utamaduni wa jamii fulani huwa sio ila bali sifa kulingana na tamaduni za watu fulani. Kwani kutaja kivazi na tabia na hulka za mtu, huwa unataja sifa za kabila fulani. Hiyo huwa ni sifa na utambulisho wa kabila fulani. Vile vile katika kielelezo 29 kinachofuata, dhamira ya ukweli wa mambo unayoambiwa, utafiti unalithibitisha hili kupitia kipande cha shairi kinachosema; (29) Si hoja uzuri Na sura jamali, Kuwa mtukufu Na jadi kubeli, Hasara ya mtu Kuokosa akili. (Ukurasa wa 29, Wasifu wa siti Binti Saad) Kutokana na kipande hicho utafiti umebaini kuwa mazungumzo au malumbano yaliendelea baina ya pande mbili zenye kutaniana baina yao. Dhamira ya ukweli ndipo ilipoibuliwa. Dhamira ya Ukweli ni hali ya kuwa, ukweli unatakiwa kuzungumzwa juu 72 ya hali ya mwanajamii ya kuwa hatopata umaarufu kwa sura yake, kuwa na nasabu bora au hata kutoka kabila lilobora zaidi ya mwenzake, kwasababu hili hutofautisha kwasababu ya wanajamii kujuana. Pia utafiti umebaini kuwa mwanajamii ambaye hana akili ndiye ambaye atafikwa na kupatwa na taabu, lakini kwa mwenye akili anaweza kufanya analolitaka kilifanya tena kwa manufaa kabisa, isipokuwa kuweka mikakati juu ya jambo hilo, kulingana na jamii fulani. Dhamira hii ya ukweli, inasisitiza juu ya kuwa mkweli wakati wowote wa maisha kulingana na sifa ya kitu kilivyo unatakiwa kutopotosha, kwani inawezekana kuleta mapambano dhidi ya wanajami na kwasababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, kwasababu ukweli siku zote ni wenye kujenga, na wala hauwezi kubomoa. Msema kweli ndiye mpenzi kwa viumbe wenzake na msema uwongo huchukiza kwa wenzake. Malumbano (Matani) yaliendelea tena na kuibuliwa kwa dhamira kuomba radhi. Kuomba radhi juu ya kitu au jambo unalotaka kulisema kabla kulisema jambo hilo, uthibitisho wa hayo ni kilelelezo 30. Kama ifuatavyo; (30) Sikusudi langu Kuvunja watani, Enyi walimwengu Mwajua yakini, Apendalo Mungu Haliwezekani. (Ukurasa wa 29, Wasifu wa siti Binti Saad) Kipande hicho cha shairi kinathibitisha kulingana na malengo ya utafiti ya kuwa uzuri wa kitu unapotaka kusema basi ni lazima kuomba radhi mwanzo ndio uendelee kusema 73 kitu fulani na ndio utaratibu mzuri wa maisha, sio kuomba msamaha baada ya kufanya jambo. Unatikwa kuomba radhi kabla ya kufanya jambo inawezekana kukera na kuwa kosa lakini linafutwa na ile samahani ya mwanzo kabla ya kulifanya hilo. Hali inayoonyesha kuibua wa msemo unaosema “Ashakum si matusi” hata mzungumzaji alisema neno ambalo halikubaliki basi huwa tayari ameshaomba msamha kwa jambo hilo. Hivyo kila kitu kina utaratibu wake na mipango yake kulingana watu walivyokubaliana kufanya. Kutokana na kipande cha shairi kifuatacho utafiti umegundua dhamira ya pongezi. Pongezi ni dhamira inayosisitiza kwamba aisyekubali kushindwa sio mshindani. Pongezi hapa ni lie hali ya kukubali kwa yule anayeshindwa ukweli juu ya kushindwa. Baada ya kushindana baina ya wanajamii wawili ni lazima mmojawapo akubali kushindwa, na ndipo panapopatikana ukweli juu ya jambo fualani linaloshindaniwa. Utafiti umegundua kwamba ni lazima kwa wanaoshindana baada ya kupitikana ukweli ni juu ya mmoja kukubali kuwa ameshindwa juu ya hilo, kutokana na kutolewa kwa sifa za kinachoshindaniwa. Mfano hulka, tabia mila na hata desturi. Pia kupeana zawadi ni jambo jema au hidaya baada ya kufanikiwa kwa kitu fulani ndani yake ijapokuwa kitakuwa hakina thamani kubwa lakini atakaepewa apokee hata kama kina upungufu, hili ndilo jambo jema kwa wanaofuata mila na desturi za jamii. Kwani kutunikiwa ni bora kuliko kuomba. Kuomba ni pingamizi katika maisha ya mtu isipokuwa kwa dharura. 74 4.2.2.4 Matumizi ya Semi katika Wasifu wa Siti binti Saad. Kwa upande wa kitabu cha Wasifu wa Siti Binti Saad, utafiti umebaini kuwa, kuna semi ambazo zimetumika kubebeshwa dhamira na kuibua dhamira kwa mitindo tofauti. Methali kama mbinu inayotumiwa na fasihi simulizi kwa kawaida, kulingana na kielelezo 31 na 32 vinavyofuata kuwa methali ni aina moja ya fasihi simulizi, hii inamanisha kuwa baadhi ya methali zimeonekana ndani ya riwaya hii ya Wasifu wa Siti Binti Saad. Methali zinazosema; (31) “Asiyeweza kutuumba na kutuumbua hawezi”. (Ukurasa wa 23, Wasifu wa Siti Binti Saad) (32) “Cheka uchafu usicheke kilema”. (Ukurasa wa 23, Wasifu wa Siti Binti Saad) Methali hizo zinaonyesha kuwa ni hali gani mtu anavyotakiwa kwasababu kabla ya kufa basi mtu ajue hajaumbika; vile vile kila kitu kina mwanzo na mwisho wake na kila kitu pia kina muanzilishi na pia mwenye kuweza kukibadilisha umbile lake lilivyo. Methali hizo zinatoa dhamira ya ukweli wa maisha. Na ndipo unapatikana ukweli kwamba kila kitu kina wakati wake na muda wake na kuwa bila ya kulazimisha, kikilazimishwa kinaweza kikaleta madhara katika jamii. Hivyo kila kitu kinaweza kubadilika na kuweza kuleta sura nyingine kuliko kilivyokuwa hapo mwanzo. Vile vile, kwa upande wa misemo iliyopatikana katika kitabu cha Wasifu wa Siti Binti Saad, inathibitisha kuibuliwa kwa dhamira kama ifuatavyo; (33) “Siti alikuwa si mmoja wa wahuni waliozoea kutoroka kwao wakakimbilia katika miji kukaa kama chaza, au kama kupe na mkia wa ng’ombe”. 75 (Ukurasa wa 13, Wasifu wa Siti Binti Saad) Methali katika kielelezo 33, zinatupatia dhamira ya mafanikio. Mafanikio katika maisha ni dhamira inayoonyesha kuwa mafanikio yanapatikana kwa njia moja ya kuwepo na kuwasikiliza wazee na kukaa nao pamoja, hii ni sababu ya mafanikio, wote ambao wamekwenda kinyume na wazee wao au kuwakimbia na wakakimbilia mijini basi wameshindwa kupata mafaniko yaliyo bora kulingana na silka, desturi, silka na utamaduni wa jamii husika. Hii inamaanisha kukimbia tatizo sio kusuluhisha tatizo bali ni kuzidisha matatizo zaidi, kila kitu kinaweza kisiwe pale unapotaka kukifanya, kinaweza kukupa tabu pale ambapo una shida nacho, vile vile jambo baya linaweza kutokezea wakati wawote katika maisha, isipokuwa ni kujipanga katika kukitatua kitu hicho kwa uangalifu na kwa umakini wa hali ya juu, kwa hali ya kuwasikiliza wazee na jamii kwa ujumla. Vile vile Mafankio kwa kawaida ni ile hali ya kupata kile unachotaka na kutatua shida iliyokabili. Kupata na kukosa ni hali pia ya mafanikio katika maisha kwani kukosea ndio njia ya kujifunza na kukijua unachojifunza, lakini jamii ndiye mwalimu wa kwanza katika maisha, mtu hujifunza kutokana na makosa yaliyomkabili kutokana na silka, desturi na utamaduni wa jamii. Hali inayothibitisha kuwa mafanikio hayapatikani ispokuwa kuwasikiliza wakubwa katika jamii, kulingana na jamii inavyotaka. Semi nyngine ni ile tamathali ya semi ya takriri, takriri inayoonekana hapa ni ile inayoenyesha msisitizo ni ile inayoenyesha msisitizo. Dhamira ya namna ya kujifunza inapatikana, kwa kawaida njia moja ya kujifunza ni ile ya kurejea rejea kwa kile unachojifunza ambacho hakijulikani na ndio inayojenga kumbukumbu ya muda mrefu. Hili linathibitishwa pale Adili alipokwenda kutafuta na kujiuliza na kukariri yale 76 aliyokuwa anayaona, hali iliyomfanya kufanikiwa katika maisha yake. Utafiti umebaini kuwa mojawapo wa njia ya kujifunza ni kukariri kariri unachojifunza Vile vile katika katabu cha Wasifu wa Siti Binti Saad, dhamira ya elimu na umuhimu wake ndipo inapoibuliwa, kutokana na malengo ya utafiti, kwa maneno yafuatayo; (34) “Vyungu, vyungu, vyungu vizuri nunueni vyungu kwa bei rahisi”. (Ukurasa wa 05, Wasifu wa Siti Binti Saad) (35) “Mwanamke huyu ambaye hakusoma alikuwa na moyo wa kuhifadhi mambo kama umeme. Kisha aliweza kuyakariri baadaye neno kwa neno kwa namna iliyowashangaza kila aliyemsikia”. (Ukurasa wa 09, Wasifu wa Siti Binti Saad) (36) “Kwa kadri ya sauti ya kinanda ilivyokuwa nzuri, lakini ile ya mwanadamu ilikuwa bora. Hilo lilimfanya Siti kuwa kama Johari katika jumui ile”. - (Ukurasa wa 10, Wasifu wa Siti Binti Saad) Marudio hayo ya maneno yanaweza kuleta mafanikio ya aina yoyote, rejea kielelezo 34, 35, na 36 itakapokuwa yamefuta mila, desturi na utamaduni wa jamii. Mwandishi anasema kujitahidi kwa Siti katika kunadi kwa sauti nzuri na yakubembeleza iliyorudia rudia baadhi ya majina ya vile alivyoviuza ndio iliyomfanya kuhifadhi vitu vingi na kujifunza na kufanikiwa katika maisha. Utafiti unathibitisha kwamba kurejea rejea ni hali moja ya mafanikio katika maisha. Hivyo katika mchakato wa maisha hakuna jipya isipokuwa unapofuata sheria basi mafanikio hutokea kwa uhakika. Hivyo utafiti umebaini kuwa njia rahisi ya kujifunza ni ile ya kurejea rejea kwa kila unachojifunza. Na pia ni njia moja ya kujifunza sio lazima kuenda darasani, hata ukienda kwa watu wa 77 kawaida unaweza kujifunza tena kwa manufaa, na kuweza kukitumia kitu hicho kwa uzuri wa hali ya juu, kama alivyofanya Siti. 4.3 Hitimisho Katika sura hii tumejadili juu fasihi simulizi ilivyotumika kuiwasilisha fasihi andishi katika kuibua dhamira ndani ya katika kitabu cha Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Imeelezwa kuwa mwandishi anaweza kutumia kipengele chochote kile cha fasihi simulizi kwa ajili ya kufikisha dhamira. Aidha sura hii imejadili kuwa mwandishi anaweza kutumia mbinu mbali mbali za uteuzi wa vipingele vya fasihi simulizi katika ujenzi wa kazi za kifasihi. Sura hii imejadili kuwa msanii yoyote anaweza kuibua dhamira kutokana na kipengele chochote cha fasihi simulizi, hii inatokana na ukweli kwamba msanii yoyote anatoka katika jamii fulani, yenye kuonyesha historia yake, itikadi, uchumi, siasa, mambo ya kijamii, siasa, uchumi na utamaduni. Hivyo basi ni dhahiri kuwa jamii yoyote ina utamaduni wake na jinsi wanavyotumia baadhi ya mambo yao katika kupeleka dhamira kwa jamii kulingana na mahitaji yao

Powered by Blogger.