UTAFITI:UTAFITI: UFASIHI SIMULIZI KATIKA RIWAYA ZA SHAABAN ROBERT: Mifano kutoka Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad


2.3 Pengo la utafiti
Tunapoyatalii maandiko hayo, tunabaini kuwa hakuna mtafiti aliyeshughulikia moja kwa moja suala la ufasihi simulizi katika ya riwaya za Shaaban Robert. Watafiti na waandishi wachache wamejaribu kulieleza kidogo suala la dhamira na fani, na kuacha vipengele vingine vidodo vidogo vinavyojenga kazi za riwaya teule za Shaaban Robert. Watafiti na waandishi hawa wamechambua dhamira na fani na kuonyesha ujumla wake, bila ya kuonyesha ufasihi simulizi uliomo ndani ya kazi hizo. Hata hivyo fasihi andishi hujengwa na vitu vingi, na pia ina mambo mengi ya kuchunguzwa katika muuundo wa riwaya, kwa kutizama fani ya jamii husika pamoja na historia, mahusiano na muundo wake. Hivyo utafiti huu umeziba pengo hilo kwa kuchunguza ufasihi simulizi katika riwaya za Shaaban Robert, ili kubaini jinsi msanii huyo anavyotumia vipengele vya fasihi simulizi kama malighafi ya utunzi wa riwaya zake. 2.4 Kiunzi cha Nadharia Katika utafiti wa kazi ya fasihi, zipo nadharia ambazo zinaweza kutumika kuchunguza na kuchambua kazi ya fasihi. Kila nadharia inaweza kufaa au kutokufaa kuzichambua kazi ya fasihi, Kwa kuzingatia lengo la utafiti unaotaka kufanywa. Katika utafiti tunaweza kutumia nadharia mbali mbali kama vile Ufemenisti, Uumbaji, Mwitiko wa msomaji, Simiotiki au kiujumi, na nadharia ya mwingilianomatini. Hata hivyo kutokana na malengo ya utafiti huu, tuliona kuwa misingi ya nadharia nyingine zisingetufaa katika kubaini ufasihi simulizi katika riwaya. Kwa hiyo tuliona kuwa nadharia ya mwingilianomatini inafaa kwa utafiti wetu. Sehemu ifuatayo inajadili kuhusu nadharia ya mwingilianomatini. 32 2.4.1 Nadharia ya Mwingilianomatini Kwa mujibu wa Wamitila (2002), Njogu na Wafula (2007) na Ndumbaro (2013), wanasema Mwingilianomatini ni moja ya nadharia za fasihi, ambayo hutumika katika kuchunguza, kuchambua data za utafiti na kubaini kazi moja ndani ya kazi nyengine katika kazi za fashi. Wamitila (2002), Njogu na Wafula (2007) na Ndumbaro (2013), hii iliyoasisiwa na mfaransa, Julia Kristeva, alizaliwa 24/06/1941 huko Bulgaria, Kristeva aliizua nadharia hii ya Mwingilianomatini kutokana na fikra zilizotokana na nadharia ya Usemezano ya Mrusi Mikhail Bakhtin (1895 – 1975). Bakhtin, anaamini katika nadharia hiyo ya Usemezano kuwa kazi ya fasihi ina alama ya sauti ambazo huingiliana na kupiga mwangwi katika kazi nyingine zilizopita, zilizopo kwa sasa au zitakazotungwa baada hizo zilizotangulia. Hii ina maana kuwa athari ya kazi moja huweza kuonekana katika kazi nyingine zilizopo kwa sasa au zitakazotungwa baada hizo zilizotangulia. Hivyo mawazo ya Bakhtin yalifanya kuzuka kwa mawazo ya Kristeva, Kristeva aliyaendeleza na kuyatanua mawazo hayo na ndipo ilipozuka nadharia yake ya mwingilianomatini mnamo mwaka 1960. Kristeva katika nadharia yake hiyo anaamini kuwa, katika kazi yoyote inayomuhusu mwanadamu haiwezi kuangaliwa peke yake, hivyo matini hiyo itakuwa na mafungamano na kazi nyengine inayochangiana nayo na kukamilishana katika miktadha mbali mbali. Hii ina maana kuwa katika kazi za kisanaa za fasihi kuna mafungamano ya kuhusiana na kutegemeana, hivyo si rahisi kuchunguza chanzo au upekee wa kazi ya fasihi, kwani kwa hali yoyote ile kutakuwa kuna mambo yanayochangiana katika kazi zilizopo au zilizotangulia kubuniwa. 33 Vile vile nadharia ya mwingilianomatini inashikilia msimamo kwamba, matini kufanana na kuchangizana na kuamini kuwa matini ya kifasihi haiwezi kujitegemea kipekee. Pamoja na hayo mitindo fulani ya kiusemi na misimbo mwingilianomatini huhusisha pia, ambayo imesaidia katika uashiriaji wa kazi zitakozotungwa. Hii inamaanisha kuwa nadharia ya mwingilianomatini sio urejelezi wa kazi fulani katika kazi nyingine tu, bali pia ni ile tajriba ya uingiliano wa mitindo ya kitaashira. Kwa ujumla, mawazo ya Kristeva kuhusu na nadharia ya mwingilianomatini ni jumla ya maarifa na mbinu zinazoifanya kazi kuwa na maana kamili, ambapo dhana ya matini huangaliwa kama ina utegemezi na matini nyengine kwa kuitwa “mwanda wa ki – mwingilianomatini”. Hii ina maana, kwa mujibu wa Kristeva, matini yoyote ile huchukua au kujipamba kutokana na kazi nyingine kwa kuzichawanya katika mawanda ya kimwingilianomatini. Hivyo nadharia hii ilitufaa kwa utafiti wetu kwasababu tulichunguza ufasihi simulizi uliomo ndani ya fasihi andishi, ni sawa na kusema kuwa matini moja imo ndani ya matini nyengine. Kulingana na malengo ya utafiti huu tuliona kwamba nadharia zilizotufaa zaidi ni nadharia ya Mwingilianomatini. Katika utafiti huu tulitumia nadharia ya mwingilianomatini ili kuchunguza na kubainisha matumizi ya mbinu ya fasihi simulizi katika riwaya ya Adili na Nguguze na Wasifu wa Siti binti Saad. Ijapokuwa nadharia yoyote yaweza kufaa katika utafiti, lakini sababu ya kuchagua nadharia hii, ni kutokana na kuona kuwa misingi yake ilihusiana sana na malengo ya utafiti wetu. Kwa hiyo tuliona kwamba, kwa kutumia nadharia hii tutaweza kufikia malengo ya utafiti huu kwa kuonyesha uhusiano na kuathiriana kwa kazi za fasihi simulizi katika riwaya 34 kukamilisha utafiti wetu. Vilevile tuliona kuwa, misingi ya nadharia mwingilianomatini misingi yake itatuongoza katika kuchambua, kubaini na kujadili matumizi ya vipengele vya fasihi katika riwaya teule. Kwa kutumia nadharia hii, tuliweza kubainisha vipengele vya fasihi simulizi kama vile; nyimbo/ushairi, wahusika, matani, masimulizi, hadithi, methali, semi, mandhari, wahusika na ishara. Nadharia hii pia ilitusaidia kubaini dhamira zilizojiegemeza katika matumizi ya fasihi simulizi katika utunzi wa riwaya. Hivyo, nadharia ya mwingilianomatini ilitumika kuchunguza na kubaini ufasihi simulizi uliomo katika fasihi andishi kwa kutumia vitabu vya riwaya za Shaaban Robert ya Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Bint Saad. Tulichunguza ni jinsi gani fasihi simulizi ilivyoijenga jamii ndani ya fasihi andishi kulingana na mila, silka, desturi na utamaduni wa jamii. 2.5 Hitimisho Sura hii imepitia na kujadili juu ya maaandiko mbalimbali kuhusu dhana ya fasihi simulizi, tafiti za riwaya ya Kiswahili na hatimaye kuibua pengo la kimaarifa ambalo utafiti huu ulikusudia kuliziba. Katika sura hii imeelezwa kuwa nadharia ambayo imeongoza utafiti. Hivyo basi, sura inayofuata inabainisha kuchambua na kujadili mbinu za utafiti zilizotumika kukusanya data za utafiti huu. 35 SURA YA TATU MBINU ZA UTAFITI 3.0 Utangulizi Sura hii inajadili juu ya mkabala wa utafiti, mbinu, na vifaa ambavyo vilitumika katika utafiti huu. Sura hii imegawanyika katika sehemu kuu saba; sehemu ya kwanza inahusu eneo ambalo utafiti ulifanyika, sehemu ya pili ni kundi lengwa, sehemu ya tatu ni sampuli na mbinu za uteuzi wa sampuli, sehemu ya nne ni mbinu za ukusanyaji data, sehemu ya tano inabainisha zana zilizotumika kukusanyia data na sehemu ya sita inajadili juu ya mbinu za uchambuzi wa data wakati sehemu ya mwisho ya sura hii inatoa hitimisho la sura. 3.1 Sampuli na Mbinu za Uteuzi wa Sampuli Uteuzi wa sampuli, kama unavyoelezwa na Bryman (2004), ni mwendelezo wa kuchagua kikundi cha vitu au watu ili kitumike katika utafiti kama kiwakilishi cha kundi lolote linalotafitiwa kwani sio rahisi kutafiti kundi zima. Mchakato wa kuteua sampuli kutoka katika kundi lengwa unajulikana kama mbinu ya uteuzi wa sampuli. Mbinu yenye madhumuni maalumu na dhamira zinahusisha uteuzi wa vitu kama sampuli unaofanywa na mtafiti kwa madhumuni maalumu na dhamira kutegemeana na taarifa zinazohitajika kupatikana kwa ajili ya utafiti. Kothari (1990) anaeleza kuwa siyo rahisi kukusanya taarifa zote kutoka kwenye kundi zima, yaani kundi lengwa. Na anasema kuwa zipo mbinu mbalimbali za uteuzi wa sampuli. Sampuli ya utafiti huu iliteuliwa kwa kutumia mbinu tatu, yaani: mbinu ya uteuzi wa madhumuni maalumu, uteuzi rahisi wa sampuli na uteuzi bahatishi. Matumizi 36 ya mbinu hizi, yalitokana na malengo ya utafiti huu kwa kuzingatia nadharia inayoongoza utafiti huu. Utafiti huu ulitumia mkabala wa utafiti usio wa kitakwimu. Hivyo matumizi ya mbinu hizi tatu za uteuzi wa sampuli yana umuhimu mkubwa ili kufikia lengo ya utafiti huu. 3.2 Eneo la Utafiti Utafiti huu ulifanyikia katika maeneo ya jiji la Dare-es-salaam (Chuo Kikuu Huria) na Pemba (Zanzibar). Uteuzi wa maeneo haya ya utafiti ulitokana na sababu zifuatazo; kwanza kwa upande wa Dar es salaam ni eneo ambalo kuna maktaba za kutosha, upatikanaji wa vitabu, wataalamu wa fasihi ya Kiswahili ambao pia wanatarajiwa wataweza kumpatia mtafiti data za kutosha mtunzi wa kazi hizi kwa sababu ya kumbukumbu zao nyingi zimehifadhiwa katika sehemu hizo. Pia kwa kutumia Pemba kama eneo la utafiti, tuliamini kuwa itakuwa rahisi kuwapata wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria wanaosoma fasihi ya Kiswahili. Dar es salaam ni eneo ambalo kuna Maktaba kuu ya Chuo Kikuu Huria na Chuo Kikuu Cha Dae-es –salaam. Kwa maana hiyo, ilikuwa rahisi kupata vielelezo vinavyomuhusu Shaaban Robert, kwa kusoma taarifa zake zinazohitajika katika utafiti huu. Vile vile ilikuwa rahisi kuwapata watu ambao waliwahi kusoma kazi zake, kwa kuandika makala au kuzifanyia utafiti. Kwa hiyo tulitegemea kupata data za kutosha. Kwa upande wa Pemba ilikuwa rahisi kupata data za mwandishi wa kitabu cha Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad, kwasababu vitabu hivi viliwahi kutumiwa mashuleni na bado vinatumika na pia watu wa kawaida wanendelea kuvisoma. Hivyo, Dar es salaam na Pemba ndio maeneo tuliyoyaona kuwa ni muhimu na kufaa kukamilisha utafiti huu. 37 3.3 Uteuzi wa Sampuli Katika uteuzi wa sampuli utafiti ulitumia sampuli tatu: uteuzi wa madhumuni maalumu, uteuzi wa nasibu/mbinu bahatishi na mbinu ya uteuzi rahisi, zimejadiliwa kama ifuatavyo : 3.3.1 Kundi Lengwa Kulingana na (Kothari, 2004; Bryman, 2004; Komba na Tromp, 2006) kundi lengwa ni jumla ya watu wote ambao huhusishwa katika utafiti. Cooper (1989) na Vans (1990), wanaeleza kuwa kundi lengwa ni wanachama wote, mtu mmoja, kikundi au elementi ambazo mtafiti amekusudia kuzihusisha katika utafiti wake. Walengwa waliohusishwa katika utafiti huu ni walimu na wanafunzi wa umahiri katika fasihi ya Kiswahili Chuo Kikuu Huria hususani Idara ya Fasihi Taaluma za Kiswahili Pemba, wanafunzi wa Sekondari ya Uweleni kidato cha tano (5) na kidato cha sita (6) ambako tuliweza kuwapata wanafunzi wa fasihi ya Kiswahili. Kwa upande wa walimu, mtafiti aliwateua kulingana na madhumuni maalumu. Hapa mtafiti alizingatia ufahamu na taarifa alizopata kuwa nani ni mwalimu wa fasihi ya Kiswahili hususan riwaya kwa Kiswahili na nani ni mwalimu anayefundisha fasihi kwa jumla. Kundi lengwa la utafiti huu liliteuliwa kulingana na sifa na umuhimu wa kundi hilo katika utafiti huu; kwanza kwa mwanafunzi lazima awe anasoma au kulifahamu vyema somo la fasihi ya Kiswahili na umuhimu wa kila kundi katika utafiti huu. Kwa mfano, wanafunzi wa umahiri katika fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu Huria waliteuliwa kwa kigezo kuwa ni wanafunzi wanaosoma fasihi, wana maarifa ya nadharia za uchambuzi wa kazi za fasihi na pia wana ujuzi na maarifa katika matumizi ya nadharia 38 na mbinu za uhakiki wa kazi za fasihi. Vile vile kigezo cha kuwa wanafunzi hawa wanasoma riwaya kwa Kiswahili kilifanya kundi hili kuwa ni rasilimali ya kutosha katika utoaji wa data za utafiti huu. Sifa nyingine ya wanafunzi wa umahiri katika fasihi ya Kiswahili wa fasihi Chuo Kikuu Huria ni kwamba walipatikana kwa urahisi. Lakini pia ilikuwa rahisi kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria kwa sababu wanasoma darasani na kuna eneo mahsusi la kuweza kuwapata na kuwatambua kuwa hawa ni wanafunzi wa fasihi ya Kiswahili. Hivyo basi, sababu hizi ndizo zilizomfanya mtafiti kuchagua wanafunzi wa umahiri katika fasihi ya Kiswahili wa Chuo Kikuu Huria, kuwa wahojiwa wake katika utafiti huu. Walimu na wahadhiri wa fasihi wa muda mrefu ni kundi muhimu katika utafiti huu kwa sababu wao ndio wanaofundisha kozi ya fasihi, wana ujuzi na maarifa ya kutosha katika nadharia na vitendo kuhusu fasihi ya Kiswahili na uhakiki wa kazi za fasihi kwa jumla. Hivyo kwa kutumia kundi hili tuliweza kupata data za kutosha kuhusu Shaaban Robert kutokana na vitabu vyake teule katika utafiti huu. Kwa upande mwingine, walimu wa fasihi wa muda mrefu ni kundi muhimu katika utafiti huu kwa sababu wao ndio wanaofundisha kozi ya fasihi, wana ujuzi na maarifa katika nadharia na vitendo kuhusu fasihi ya Kiswahili na uhakiki wa kazi za fasihi kwa jumla. Vile vile uliwahusisha wazee na vijana wanaoishi nje ya eneo la Mkoani – Pemba, wazee ambao ni kawaida kutamba hadithi kwa vijana na pia vijana ambao hutolewa hadithi za kale, ambao huwa na uzoefu wa kutoa hadithi na wanosimuliwa kuweza kuhifadhi hadithi hizo na kusimulia wenzao, hadithi kama zile za safari, 39 vichekesho, ujanja na pia za watu mashujaa waliokuwepo Ukanda wa Pwani Afrika Mashariki. Zikiwemo zile ambazo baadae ziliandikwa kama riwaya, mfano Adili na Nduguze, hadithi ya Mkama Ndume, Mwana wa Mwana, Mwinyi Mkuu, Siti Binti Saad n.k. Hivyo kwa kutumia kundi hili tuliweza kupata data za kutosha kuhusu vitabu vya Adili na Nduguze pamoja na wasifu wa Siti binti Saad kwani hadithi zao sio ngeni kwa wasimulizi wa hadithi na wasikiliza hadithi za utamaduni wa watu wa Afrika Mashariki. 3.3.2 Uteuzi wa Madhumuni Maalumu Uteuzi, kwa kigezo cha madhumuni maalumu, ni uteuzi wa kuzingatia sababu mahsusi. Kombo na Tromp (2006) wanasema, ni uteuzi ambao mtafiti, kwa makusudi, hulenga kuteua kundi la watu ambao anafikiri kuwa ni rasilimali inayotegemewa katika utafiti wake. Kwa hiyo, mbinu hii ni bora na ya muhimu katika utafiti kwa sababu, baadhi ya watu, katika kundi lengwa, walionekana kuwa na uwezo na ni rasilimali kubwa zaidi katika kutoa data za utafiti huu kuliko wengine. Kwa mfano, suala la kiwango cha ufahamu wa fasihi, nadharia na uhakiki kati ya wanafunzi wanaosoma fasihi na wale wasiosoma fasihi, kati ya walimu wanaofundisha fasihi, hususani riwaya. Katika uteuzi wenye madhumuni maalumu uteuzi hufanywa kwa kuzingatia vigezo ambavyo vinahusu na maswali ya utafiti, kuliko kigezo cha uteuzi nasibu au wa kubahatisha. Hivyo, Katika mbinu hii, wahojiwa waliteuliwa kwa madhumuni maalumu kutokana na nafasi zao kwa kujuwa kuwa wao ndio rasilimali ya jamii juu ya data ya utafiti. Sababu nyingine iliyomfanya mtafiti kutumia mbinu hii ni kwamba; mtafiti alikuwa na taarifa juu ya kuwapo kwa makundi yenye ujuzi, maarifa na uzoefu katika fasihi kwa Kiswahili na riwaya kwa Kiswahili, makundi hayo ndiyo yaliyokuwa rasilimali ya data 40 ya utafiti huu. Hivyo basi, mbinu hii ilitumika kufanya uteuzi kutoka kwa walengwa wa utafiti huu. Kwa upande mwingine, wanafunzi wanaosoma riwaya kwa Kiswahili waliteuliwa kwa kigezo kuwa wanaelewa nadharia za uchambuzi wa riwaya ya Kiswahili. Wanafunzi walioteuliwa ni wale wenye maarifa ya riwaya kwa Kiswahili, historia na mabadiliko yake na hivyo, wana uwezo wa stadi za uchambuzi wa vipengele vya fasihi simulizi katika kitabu cha Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Kigezo hiki pia kilitumika kwa walimu wa fasihi waliobobea katika riwaya kwa kuzingatia uzoefu na maarifa na ujuzi juu ya nadharia za uchambuzi na uhakiki wa riwaya. Kwa jumla, mbinu ya uteuzi kwa madhumuni maalumu, ilimsaidia mtafiti kupata kundi la watu wenye uzoefu, stadi na maarifa katika nadharia na uhakiki wa fasihi na riwaya kwa Kiswahili, na hatimaye, kupata data ambazo ni mhimili wa utafiti huu. Vile vile, data zilizopatikana katika makundi hayo, zilimsaidia mtafiti kupata na kufanya majumuisho mahususi aliyoyakusudiwa kulingana na madhumuni ya utafiti. 3.3.3 Uteuzi nasibu/Mbinu bahatishi Mbinu nyingine ambayo ilitumika katika uteuzi ni mbinu ya uteuzi nasibu. Kombo na Tromp (2006) wanaielezea mbinu hii kuwa, ni mbinu ambayo hutumia watu ambao ni hadhira iliyomilikiwa, yaani watu ambao mtafiti alikutana nao bila kutarajia. Katika mbinu hii, wahojiwa huwa ni wale watu ambao walipita na kuonesha kupendezwa na utafiti unaofanywa. Mbinu hii ilitumika kuwateua wahojiwa ambao ni watoa hadithi na wapenda kusoma vitabu vya fasihi hususan vitabu vya Shaaban Robert. Kwa kuwa siyo rahisi, kuwafahamu watu hao, mbinu hii ilimsaidia mtafiti kuwashirikisha pale tu mtafiti 41 alipokutana nao na alipata taarifa kuhusu kitabu cha Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Mbinu hii ilimsaidia mtafiti kupata data na taarifa za kutosha kuhusu hadithi ambazo Shaaban Robert kaziandika na kuwa riwaya. 3.3.4 Mbinu ya Uteuzi Rahisi Mbinu hii ilitumika katika kupata uteuzi wa utafiti huu. Kwa kutumia mbinu hii ya uteuzi rahisi, Mtafiti alichukua orodha ya majina ya wanafunzi wa sekondari, na alitumia nafasi kila baada ya mwanafunzi wa nne, aliteua jina la mwanafunzi ambaye alishiriki katika kutoa data za utafiti. Hivyo, kwa ujumla utafiti huu ulikuwa na jumla ya wahojiwa 64 na mchanganuo wake ni kama inavyojionyesha katika jedwali lifuatalo namba 2: Jedwali namba 2 - Idadi ya Washiriki wa Utafiti Namba Aina Jinsia Jumla Ke Me 1. Wanafunzi wa umahiri wa Chuo Kikuu wanaosoma riwaya kwa Kiswahili 09 09 18 2. Wanafunzi wa sekondari (Uweleni) 15 15 30 3. Wlimu chuo Kikuu Huria 00 02 02 4. Walimu wa fasihi Sekondari Uweleni 04 04 10 5. Waliowahi kusoma kazi za Shaaban Robert 03 03 06 6. Wazee wasimulizi hadithi 01 01 02 7. Vijana wasikiliza hadithi 01 01 02 JUMLA 70 Chanzo kutoka data za Utafiti 3.4 Mbinu za Ukusanyaji wa Data Ukusanyaji wa data ni zoezi linalohitaji mbinu muafaka zinazokubalika kutokana utafiti husika. Bila matumizi ya mbinu stahili data stahili za utafiti haziwezi kupatikana. 42 Hivyo, katika kukusanya data za utafiti huu mbinu mbalimbali za ukusanyaji data zilihusishwa ambazo ni usomaji wa machapisho, majadiliano ya vikundi, usaili na dodoso. 3.4.1 Mbinu ya Usomaji wa Machapisho Mbinu hii ni mbinu kuu iliyotumika kukusanya data za utafiti huu. Kwa kutumia mbinu hii mtafiti aliweza kusoma na kuchambua kitabu cha riwaya cha Adili na Nduguze na kitabu cha riwaya cha Wasifu wa Siti Binti Saad. Katika kuchambua riwaya hizi, mtafiti alibainisha vipengele vya fasihi simulizi katika vitabu vya Shaaban Robert. Baaada kubainisha vipengele vya fasihi simulizi alipanga katika makundi mahususi, mbinu hii ilitusaidia sana kubaini vipengele hivyo. Pamoja na ubora wake bado ilionekana kuwa kuna haja ya kupata data zaidi kuhusu vipengele vya fasihi simulizi katika riwaya. Hivyo tuliamua kutumia mbinu ya usaili ili kupata data zaidi. 3.4.2. Mbinu ya Usaili Babbie (1992) anasema kuwa usaili unahusisha mawasiliano ya moja kwa moja baina ya mtafiti na wahojiwa na mtafiti hupata maelezo mazuri kuhusu baadhi ya mambo ambayo yasingeweza kuwekwa bayana kupitia mbinu nyingine ya utafiti. Mbinu hii inaruhusu unyumbukaji katika mwendelezo wa kuuliza maswali, kuweka bayana istilahi ambazo zinaonekana hazieleweki kwa watu na kupata taarifa za ziada na za kina zaidi, hususan pale ambapo majibu ya watu wanaosailiwa hayaeleweki (Kothari, 1990 na 2004). Hivyo, mbinu hii ilimsadia mtafiti kukusanya data za kutosha na zilizo yakini zaidi. Katika utafiti huu, usaili wa aina mbili ulitumika yaani, usaili rasmi na usaili usio rasmi. Usaili rasmi ulitumika kwa sababu walichaguliwa wahojiwa ambao walikuwa 43 wametayarishwa kujibu maswali yaliyokusudiwa kujibiwa, kama vile wanafunzi wa sekondari na wanafunzi wa Chuo Kikuu. Usaili usio rasmi uliandaliwa kwa wahojiwa ambao walihojiwa kwa vikundi kulingana na mahitaji ya utafiti. Kwa kutumia usaili rasmi seti ya maswali huandaliwa katika mpangilio na maswali huulizwa hatua kwa hatua kufuatana na mpangilio huo (Kothari, 2004). Katika utafiti huu, mtafiti aliandaa maswali ambayo yalikuwa ni maswali ya mwongozo wakati wa kufanya usaili. Maswali hayo yaliulizwa kwa mpangilio wa kufuata hatua kwa hatua kulingana na kundi la wahojiwa. Kila kundi lilikuwa na maswali yake ambayo yalikuwa yameandaliwa kulingana na madhumuni ya utafiti. Hivyo, wahojiwa wote waliulizwa maswali sawa kulingana na maswali ya mwongozo wa usaili yaliyoandaliwa. Usaili ulifanyika kwa wanafunzi wa riwaya wa Chuo Kikuu cha Huria Pemba, walimu wa fasihi hususani riwaya na wanafunzi wa sekondari. Wakati wa usaili mtafiti alitumia karatasi na kalamu kuandika mambo muhimu katika mazungumzo baina yake na wahojiwa. Data zilizohifadhiwa katika zana hizo zilimsaidia mtafiti katika uchambuzi Hivyo, kwa kutumia mbinu hii, mtafiti aliweza kupata data ambazo zilimuongoza katika kufanya majumuisho ya data za utafiti wake. 3.4.3 Zana za Utafiti Katika utafiti huu, data zilikusanywa kwa kutumia zana ya hojaji. 3.4.4 Mbinu ya Dodoso Kwa mujibu wa Kothari (2004), mbinu hii huhusisha uandaaji wa maswali ya hojaji ambayo hutumwa kwa muhusika kwa maombi ya kumtaka mtafitiwa kujibu maswali 44 yaliyomo hatimaye kurudisha kwa mtafiti. Hojaji huhusisha orodha ya maswali ambayo huwekwa katika mpangilio maalumu. Kothari (1990) anasema kuwa, katika kiwango cha mahojiano ya msingi ya utafiti usio wa kitakwimu, undani na taarifa za ziada kuhusu hisia, uzoefu na maarifa ya wahojiwa hujionyesha vyema kupitia maswali funge. Hivyo, katika utafiti huu, mtafiti aliandaa maswali ili kuwapa uhuru na nafasi wahojiwa kujibu kwa uhuru na kuelezea hisia, uzoefu na maarifa waliyonayo juu ya mada husika. Sababu kubwa ya kuamua kutumia mbinu hii ni kwamba, mhojiwa huwa huru kuelezea hisia, mawazo na maoni yake juu ya jambo fulani kwa uwazi zaidi. Mbinu hii ilimsaidia mtafiti kupata data za kutosha na kwa uwazi zaidi kwa kuwapa wahojiwa nafasi ya kuelezea mawazo, hisia, mtazamo na uzoefu wao. Hivyo kutokana na mbinu hii mtafiti aliweza kupata data za kutosha kulingana maswali aliyoyatoa kulingana na malengo ya utafiti, ambayo yalimuezesha kuchambua data za utafiti kuilingana na malengo yake. Hata hivyo ili kukidhi malengo ya utafiti huu, tuliamua kutumia mbinu ya majadiliano ya vikundi. Mbinu ambayo tuliamini itaibua hisia, mtazamo na maoni ya wahojiwa. 3.4.5 Mbinu ya Majadiliano ya Vikundi Katika utafiti huu, mbinu ya majadiliano ya vikundi ilitumika kukusanya data za utafiti huu. Mtafiti alitumia majadiliano ya vikundi kwa kuwakusanya wanafunzi wa fasihi katika shule ya Sekondari ya Uweleni, iliyopo Mkoani Pemba. Makundi hayo yalihusisha watu watano hadi saba ambao waliwekwa katika chumba kwa muda tofauti. 45 Kwa kila kundi mtafiti alifanya majadiliano ya dakika ishrini na tano hadi dakika thelathini na tano. Sababu kubwa ya kuamua kutumia mbinu hii ni kwamba, katika majadiliano mtafiti alilenga kupata maoni, mtazamo na mielekeo juu ya riwaya ya Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Kwa hivyo, mbinu hii ilitufaa katika utafiti huu na ilitusaidia kupata data kuhusu ufasihi simulizi uliomo katika kazi hizo za Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. 3.4.6 Hojaji Kwa mujibu wa Kitula (2010), hojaji huandaliwa kwa lengo la kukusanya taarifa muhimu kutoka kwa watafitiwa. Aidha, Kothari (1990), anasisitiza kuwa hojaji iliyoandaliwa vizuri ni ile ambayo maswali yake yamepangwa katika mtiririko maalumu ili mtafitiwa aweze kujibu maswali hayo kwa urahisi. Mtafiti alichagua njia ya hojaji kwa sababu njia hii huweka ulinganifu wa majibu yatakayotolewa na watafitiwa wote. Njia hii ilirahisisha ukusanyaji wa taarifa kutoka kwa watafitiwa wengi tena kwa muda mfupi. Vilevile njia ya hojaji ilirahisisha kazi ya kufanya majumuisho ya majibu yaliyopatikana. Hojaji za maandishi ziliandaliwa kwa ajili ya walimu wa sekondari na chuo Kikuu Huria, wanafunzi wa fasihi na waliosoma kazi za mtunnzi ambao wanaoishi maeneo ya Mji wa Mkoani pamoja na Chake Chake Pemba. 3.5 Matini Matini tulizozizungumzia hapa ni matini za riwaya ya Adili na Nduguze na Wasifi wa Siti Binti Saad. Mtafiti alitumia matini hizi kama chanzo cha data za upili kwa sababu katika matini kuna matumizi ya lugha na vipengele vya fasihi simulizi. 46 3.6 Uchambuzi wa Data Utafiti huu ni utafiti uliotumia sifa za utafiti usio wa kitakwimu. Zipo mbinu mbalimbali zilizotumika kuchambua data za utafiti wa aina hii. Hata hivyo, data ya utafiti huu zilichambuliwa kwa kutumia mbinu mbili, yaani uchambuzi maudhui na uchambuzi fafanuzi. Ntarangwi (2004) anaelezea uchambuzi maudhui kuwa ni mbinu ya uchambuzi ambayo huziweka mada kulingana na jinsi jamiii inavyohusiana na kazi hiyo katika mila, destuti, silka pamoja na utanmaduni wa jamii hiyo na kuhusiana na kuihusisha na kazi hiyo moja kwa moja. Sababu ya kutumia mbinu hii ni kwamba ilitusaidia kuweka maana zote zinazohusiana kutokana na data za dodoso na usaili ili kutoa mawazo ya jumla kulingana na malengo ya utafiti huu. Kwa upande mwingine, uchambuzi maudhui hutumika kumithilisha data kutoka kwa watu tofauti. Mbinu hii iliteuliwa kutumika kwa sababu ilisaidia kuweza kumithilisha vipengele vya fasihi simulizi ili kubainisha jinsi vinavyochangia kuibua riwaya za Kiswahili. Katika kazi za msanii na hatimaye kupata majumuisho ya matumizi ya vipengele vya fasihi simulizi vinavyotumiwa na msanii wa riwaya ya Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Katika uchambuzi wa data za utafiti huu mtafiti alifanya yafuatayo: (1) Kuchambua vipengele vya fasihi simulizi katika Riwaya ya Adili na Nduguze. (2) Kuchambua vipengele vya fasihi simulizi katika Riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad. 47 (3) Kufafanua vipengele vya fasihi simulizi katika kitabu cha Adili na Nduguze, kwa kuhusisha dhamira na kufasiri matokeo kwa kuweka majibu yanayofanana na kuhusiana katika kundi moja. (4) Kufafanua vipengele vya fasihi simulizi katika kitabu cha Wasifu wa Siti Binti Saad, kwa kuhusisha dhamira na kufasiri matokeo kwa kuweka majibu yanayofanana na kuhusiana katika kundi moja. (5) Kufasiri na kuchambua majibu ya mawsaili (usaili, dodoso na majadiliano) na kuweka majibu yanayofanana. (6) kuzifasiri na kuchambua data za maktaba na kuzijadili kwa kutumia maelezo, namba na chati. 3.7 Hitimisho Sura hii imejadili juu ya mbinu zilizotumika katika kukusanya data za utafiti huu. Imejadiliwa katika sura hii kuwa eneo la utafiti litakuwa ni Pemba na walengwa wa utafiti huu ni walimu wa fasihi, wanafunzi wa fasihi Sekondari, wasimulizi wa hadithi na wasikilizaji. Aidha, sura hii imejadili mbinu za ukusanyaji data ambazo ni mbinu ya usomaji machapisho, usaili, dodoso na majadiliano. Mbinu hizi zilitumika kwa kukamilishana na kujalizana kwa data ilizopatikana iliyotumika kutokana na mbinu moja na nyingine. Katika sura hii imejadiliwa kuwa nadharia ilikayotumika katika uchunguzi na uchambuzi wa data za utafiti huu ni nadharia ya mwingiliano matini
 >>>>>>>>>ITAENDELEA>>>>>>>>>>>>>>>>>>
Powered by Blogger.