UTAFITI: UFASIHI SIMULIZI KATIKA RIWAYA ZA SHAABAN ROBERT: Mifano kutoka Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad
SURA YA PILI MAPITIO YA MAANDIKO TANGULIZI
2.0 Utangulizi
Sura hii inahusu mapitio ya maandiko tangulizi yanayohusiana na mada ya utafiti. Sura hii imegawanyika katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni mapitio ya tafiti za riwaya na fasihi simulizi na sehemu ya pili ni kiunzi cha nadharia. 2.1 Dhana ya Fasihi Simulizi na Nafasi yake katika Fasihi Andishi Wataalamu kadhaa wamewahi kuielezea dhana ya fasihi simulizi. Mathalan, Sengo (1978), Mulokozi (1996), Matteru (1983), Kenguru (2013), Sengo na Kiango (1977), huku wakiwa na mitazamo iliyokaribiana au kutafautiana juu ya dhana hii ya fasihi simulizi. Kwa mfano, Ndungo na Wafula (1993), wanaeleza kuwa, fasihi simulizi ni kongwe, fasihi andishi ilikuja wakati wa uvamizi wa wageni wa Kiarabu na Wazungu na pia Shaaban Robert na James Mbotela ndio waandishi wa kwanza wa hadithi ndefu za Kiswahili katika Upwa wa Afrika Mashariki. Maelezo hayo tunakubaliana nayo kwani tunaamini kuwa dhana ya fasihi andishi ililetwa na wageni, kwa jina la “Literature,” wakiwa na maana ya “uandishi” au “herufi,” bila kuzingatia vielezea vya fasihi ya Kiafrika, katika upwa huu wa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla. Hivyo, dhana hii ya fasihi andishi haikuwapo hadi palipoanza maandishi. Mulokozi (1996), anaeleza kuwa, fasihi simulizi ni taasisi inayofungamana na muktadha fulani wa kijamii na kutawaliwa na muingiliano wa mambo kama vile, fanani, hadhira, 11 fani, tukio, pahala na wakati. Na huweza kuwekwa katika kumbo za semi, mazungumzo, masimulizi, maigizo, ushairi na ngomezi. Maelezo yanayofafanua sifa bainifu za fasihi simulizi ni muhimu sana katika utafiti wetu huu. Hiii ni kwasababu, Mulokozi amegusia vipengele muhimu ambavyo vitatuongoza katika kufanya uchunguzi wetu wa vipengele hivyo vya fasihi simulizi ndani ya riwaya hizo teule. Taassisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) (1985) inaeleza kuwa fasihi hujishughulisha na taratibu za jumuiya. Fasihi ni kazi ya sanaa inayochukua jukumu la kutudhihirishia na pengine kututatulia hali zetu za kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Kwa ujumla fasihi ni mdhihirisho ama kioo cha maisha ya jamii na uhusiano wao katika muktadha wa mazingira na maumbile yao. Hivyo ni kwamba fasihi inatunza na kutumbuiza. Maelezo haya yanamaanisha kwamba maendeleo ya fasihi hayana budi kuzingatiwa kuambatana kwa mujibu wa maendeleo ya Jumuiya yenyewe na utamaduni wake. Maelezo haya yalimsaidia mtafiti kuona na kuweza kuchambua kwamba ufasihi simulizi uliomo kwenye vitabu teule vilivyojadiliwa na utafiti huu. Hii inaonyesha kwamba ugunduzi wa maandishi hauna budi kuchota tajriba ya masimulizi ya jamii husika kimaelezo, kimtindo na kimuundo. Mwai na Ndungo (1991), wamekubaliana kwamba waandishi wengi wa fasihi andishi wameathiriwa na fasihi simulizi, kwa njia moja au nyengine, kuna wale ambao wameathiriwa kifani na kuna wale ambao wameathiriwa kimaudhui au kwa njia zote mbili. Kifani kuna wale ambao wanatumia wahusika kama mazimwi, majini au usimuliaji wa hadithi wa moja kwa moja. Kwa mfano Kezilahabi (1976) katika Gamba la Nyoka ametumia mtindo huo. Wengine wanatumia mtindo wa paukwa pakawa au 12 vitendawili kama inavyofanyika katika fasihi simulizi. Mfano Hussein (1976), katika Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi zimechota mitindo ya fasihi simulizi. Kimaudhui kuna uwiyano mkubwa kati ya fasihi simulizi na fasihi andishi. Dhamira nyingi wanazozijidali waandishi wa leo zilikwisha jadiliwa zamani katika fasihi simulizi, kama mapenzi, harakati za kikabila, uchawi na kadhalika. Wanaendelea kusema fasihi andishi haijagundua dhamira mapya kabisa ambayo haijitokezi katika fasihi simulizi. Mulokozi (1996), anasema kuwa fasihi andishi hutegemea maandishi, ni wazi kuwa fasihi andishi ni changa zaidi kwa vile haikuwepo kabla ya kugunduliwa kwa maandishi. Isitoshe, ilianza kwa kukopa mbinu kutoka katika fasihi simulizi, na mpaka leo bado inaathiriwa na fasihi simulizi. Kadhalika fasihi simulizi kwa kiasi fulani, huathiriwa na fasihi andishi. Kwa mfano baadhi ya hadithi au misemo ya waandishi mashuhuri hutokea kupendwa sana na watu hadi kuingia katika mkondo wa fasihi simulizi ya watu hao. Kadhalika mfano Biblia na Misahafu ni miongoni mwa fasihi andishi ambayo imekuwa na athari kubwa kwenye fasihi simulizi ya mataifa mengine. Nkwera (1979) anasema Fasihi ni moja, lakini kutoka na jinsi taarifa zilizohifadhiwa na kuathiriwa katika jamii huonekana kuwa kuna fasihi simulizi; mapokeo ya mdomo, na fasihi andishi; habari za kubuni zilizoandikwa, baadhi ya habari hizo zikiwa zinatokana na fasihi simuizi. Nkwera anaendelea kusema kuwa jamii na utamaduni wake, watu na amali zao (ni mambo yanayoathiriwa na kuhifadhiwa na jamii, dini, mila, ujuzi, siasa, sanaa ya jadi na lugha). Kuingiliana kwa utamaduni wa jadi na ukoloni au athari nyengine (nguvu na ushawishi). Husababisha matatizo na migogoro pia maendeleo 13 duni ya jamii yaletwayo na uchumi, aidha mtindo mzima wa uzalishaji mali na jinsi mali inavyogawanywa. Hali ya kisiasa, utamaduni wa kigeni na ushirikina. Vile vile harakati za kikabila, yaani msuguano, mvutano na maingiliano katika jamii na matokeo yake ni zalio la athari za jamii na amali zake. Pia majibu na mawaidha ya mwandishi kuhusu kukabili matatizo hayo, ili kuleta na kudumisha furaha na maendeleo ya jamii na pia watu binafsi. Hivyo mazingira na fikra zilizotawala wakati wa mwandishi na ambazo zinamwathiri, Kama vile harakati za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Maelezo ya Nkwera yanaonyesha kuwa fasihi andishi ni lazima kuchota na kuibua mbinu za fasihi simulizi katika kuonyesha uzuri na ubaya ambao unafanywa katika jamii husika. Hali hii ilimsaidia mtafiti kwa urahsi kuweza kuibua na kuelezea ni kwa jinsi gani mwandishi hutumia ufasihi simulizi uliomo katika fashi andishi kulingana na vitabu teule vya Shaaban Robert: Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Naye Kihore (1996), anaona kuwa fasihi andishi na fasihi simulizi ni kazi moja tu. Kwani kazi hizo huweza kutoka katika hali moja na kwenda hali nyengine. Mathalani, fasihi andishi huwasilishwa kwa maandishi na fasihi simulizi huwasilishwa kwa masimulizi. Hivyo, utata huzuka kwa hoja kwamba ziko kazi zilizosimuliwa baadaye, zikaandikwa, na ziko zilizoandikwa baadaye, zikasimuliwa. Mawazo hayo ya Kihore ni kuntu kwa kusema kuwa, hiyo inayosemwa ni fasihi simulizi na hiyo iliyoandikwa ni fasihi andishi zina maingiliano makubwa kwani tofauti yake hujitokeza kwa namna zinavyowasilishwa na kuhifadhiwa. 14 Kwa upande mwengine TUMI (1988), wana mawazo tofauti na Kihore, wao wanasema kuwa, kazi ya fasihi simulizi, hata ikiandikwa haibadiliki hadhi, huwa imehifadhiwa tu kwa njia hiyo. Maelezo hayo ya TUMI yana mchango mkubwa katika kusukuma mbele utafiti huu. Mtafiti atachunguza tanzu za fasihi simulizi zinazohusishwa katika fasihi simulizi, kama zinavyojidhihirisha katika riwaya ya za Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. TUKI (1988:116) inaeleza kuwa fasihi andishi ina misingi yake katika maandishi. Kwa hiyo uzuri wa kazi ya mtunzi utategemea kwa kiasi kikubwa historia. Kihistoria binaadamu alipitia hatua nyingi na ngumu katika maendeleo yake katika enzi za ujima na unokoa maelekezo ya utawala yaliendeshwa kwa maelezo ya mdomo. Kadri maendeleo yalivyojitokeza watu waligundua mambo mengi, pamoja na maandishi. Hapo awali maandishi yalinakili masimulizi, yaani fasihi simulizi iliyohifadhiwa katika maandishi. Maelezo haya yalimsaidia mtafiti kwa kiasi kikubwa, kwa sababu yanaeleza nadharia inayosema chanzo cha fasihi ni jamii yenyewe na mambo yake katika harakati za kila siku. Vile vile yalithibitisha kuwa bila ya vipengele vya fasihi simulizi basi fasihi andishi haina uhai. Hali hii ilimsaidia mtafiti kufafanua vipengele vya fasihi simulizi na jinsi vilivyotumika katika kuibu dhamira, vilivyojitikeza katika kazi teule; Adlii na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad, vilivyotungwa na Shaaban Robert. TAKILUKI (1981:32) wanaeleza kuwa waandishi hutegemea zaidi habari wanayoipata katika mazungumzo na pia katika vitabu wanavyovisoma juu ya watu mbali mbali. Waandishi wa riwaya za aina yoyote wanaweza kutegemea habari za namna hii katika kubuni wahusika wao. Waandishi wa riwaya ambazo zinaelezea watu wa kale na 15 vitendo vyao wategemee kabisa habari zinazopatikana katika vitabu vya historia, na vitabu vinavyoelezea maisha ya watu wa kale. Tunapoangalia muhusika wa kitabu cha Mohmed Suleiman Abdalla, anawaelezea wahusika kama walivyo tu pasi na kuonesha dharau au mapenzi. Mfano ni Mwana wa Ging‟ingi katika kitabu kiitwacho Kisima cha King’ingi labda Mwatenga katika Siri ya Sufuri. Katika riwaya inawezekana pia kukutana na muhusika ambaye sifa au ila zake zimepita mipaka ya kawaida. Wahusika kama hawa huwa kama karagosi au vichekesho badala ya kuonekana kama ni watu wanaolingana na watu wa kweli ndani ya jamii, Mfano muhusika Melikizadeki katika kitabu cha riwaya Siri za Maisha kilichotungwa na Emmanueli Mbogo. Hali hii ilimsaidia mtafiti kubaini kuwa hata wahusika wanaobuniwa ndani ya kazi ya fasihi andishi ni wale ambao wanatoka katika fasihi simulizi na pia ilimsaidia kuchunguza vipengele vyengine vya fasihi simulizi vilivyomo ndani ya kazi za Shaban Robert, Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Matteru (1983:31), anaeleza kuwa fasihi simulizi ndiyo data ya fasihi andishi. Fasihi andishi hutumia fasihi simulizi kuunda maudhui ya maandishi yake. Fasihi simulizi huweza kuwa ni msingi mzuri wa kutoa data itakayotumika kama malighafi ya fasihi andishi. Waandishi wa fasihi ya Kiswahili wananufaika kwa kutumia miundo na fani mbali mbali za fasihi simulizi. Katika kufafanua dhana hiyo, Matteru anawatumia waandishi kama; Shaaban Robert, akitaja vitabu vya Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad, kuwa mwandishi ametumia miundo ya kiasili. Kenguru (2013), anaeleza kuwa tanzu za mwanzo kabisa katika jamii zote ni zile zinazohusiana moja kwa moja na fasihi simulizi, kama vile, mashairi, ngano, 16 vitendawili, visaasili, uigizaji na kadhalika. Kenguru anaeleza kuwa, baadaye tanzu hizi zilijitokeza katika hadithi za maandishi. Maelezo haya ya Kenguru yalimsaidia mtafiti kuchunguza namna tanzu za fasihi simulizi zilizotajwa na zilivyojitokeza katika kazi teule zinazotafitiwa; Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Mtafiti mwengine aliyewahi kufanya uchunguzi wa fasihi simulizi ni Zaja (1986), aliyenukuliwa na Kenguru (2013), akieleza kuwa, ngano za awali nyingi zilikuwa na wahusika binaadamu na wanyama. Sababu kuu ni kuwa fasihi simulizi ilikuwa njia ya kuelewa na kutawala mazingira au matukio ya mara kwa mara, waandishi wa kazi za kubuni walichukuwa malighafi yao kutoka katika mazingira yao. Maelezo haya ya Zaja yalimpatia mtafiti muelekeo mzuri wa kuchunguza ufasihi simulizi uliomo katika fasihi iliyoandikwa. Ingawa Zaja aligusia vipengele vichache tu, yaani wahusika, mandhari na maudhui, ni dhahiri kuwa, mtafiti alichunguza wahusika na mandhari ya kifasihi simulizi ili kutambua namna yanavyodhihirika katika riwaya teule za Shaaba Robert; Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad zilizofanyiwa uchunguzi. Maelezo hayo yana umuhimu mkubwa kwani, pamoja na kwamba fasihi simulizi hutumiwa na waandishi wa kazi za fasihi andishi katika ujenzi wa kazi zao, pia vipengele hivyo ndivyo vinavyotumika kufikisha dhamira za mwandishi. Kwa hivyo, katika utafiti huu vilichunguzwa namna vipengele hivyo vilivyotumiwa na muandishi kufikisha dhamira kwa jamii. 2.1.1 Vipengele vya Fasihi Simulizi Kwa vile kazi hii imenuia kuchunguza vipengele vya Fasihi Simulizi vilivyojitokeza katika riwaya ya Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad. Hivyo, ni vyema kabla 17 ya kufanya uchambuzi wa uchunguzi, kwanza, vielezwe vipengele hivyo vya fasihi simulizi. Wataalamu kama vile Mulokozi (1996), TAKILUKI (1981), Balisidya (1987), TUKI (1988), Nkwera (1979), wamejaribu kueleza vipengele ambavyo huwa vinahusishwa na fasihi simulizi. Mulokozi (1996), amejaribu kugawa vipengele vya fasihi simulizi katika kumbo na kila kumbo ina vipengele vidogo vidogo, ni semi, mazungumzo, masimulizi, maigizo, ushairi nyimbo, ushairi maghani na ngomezi 2.1.1.1 Semi Semi ni tungo au kauli fupi fupi za kisanii zenye kubeba maana au mafunzo muhimu ya kijamii. Kumbo hii hutunza, kama vile; methali, vitendawili, mafumbo na misimu. 2.1.1.2 Mazungumzo Mulokozi (ameshatajwa) anaeleza kuwa, mazungumzo ni maongezi, katika lugha ya kawaida, juu ya jambo lolote lile. Hata hivyo si kila mazungumzo ni fasihi. Ili mazungumzo yaitwe fasihi lazima yawe na usanii wa aina fulani, yanayomithilisha uhalisia badala ya kuunakili. Hali hii hujidhihirisha katika lugha, katika muundo na mtiririko wa mazungumzo yenyewe na katika namna yanavyotolewa. Mifano ya tanzu zinazoingia hapa ni; hotuba, malumbano ya watani, mizaha na sala. 2.1.1.3 Masimulizi Masimulizi ni taaluma yenye kusimulia habari fulani yakiwa na usanii ndani yake. Hivyo, hii taalimu ya kisimulizi na fani zake huwa na sifa kama vile; kueleza matukio 18 kwa mpangilio fulani mahususi, huwa na wahusika yaani watendaji au watendwaji, katika matukio yanayosimuliwa. Aidha hutumia lugha ya kimaelezo. Lugha hiyo wakati mwengine huchanganywa na mazungumzo. Vile vile utambaji au utoaji wake huweza kuambatana na vitendo au ishara. Pia huwa na maelezo ya kweli au ya kubuni na yenye funzo fulani kwa jamii. Masimulizi yana tanzu nyingi. Hata hivyo Mulokozi (1996) anaeleza kuwa, tanzu zinazofahamika zaidi ni kama vile; hadithi za kubuni ambazo hujumuisha ngano, istiara, michapo na hekaya. 2.1.1.3 Maigizo Pia, Mulokozi (1996), anaeleza utanzu mwengine wa fasihi simulizi ni utanzu wa umithilishaji. Anaeleza kuwa, umithilishaji unatumia watendaji kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe. Mara nyingi natiki za Kiafrika ni kma vile; ngoma, utambaji wa hadithi, nyimbo na matendo ya kimila, kwa mfano, jando na unyago. Yapo pia matukio yanayoambatana na michezo ya watoto, matanga, uwindaji, kilimo. Natiki nyingi hutumia mapambo maalumu. 2.1.1.4 Ushairi Simulizi Mulokozi (1996), anaeleza kuwa ushairi simulizi wenye kufuata kanuni fulani za urari wa sauti, mapigo ya lugha, na mpangilio wa vipashio vya lugha. Lugha ya ushairi katika fasihi simulizi hupambanuliwa na lugha ya kawaida kwa namna inavyopangiliwa na namna inavyoingiliana na muktadha wa utendaji. Mulokozi anaendelea kusema kuwa, tanzu za ushairi simulizi ni nyimbo na tenzi. 19 Katika kufafanuwa kipengele cha wimbo Mulokozi (ameshatajwa) anasema kuwa, wimbo ni kila kinachoimbwa. Hii ni dhana pana ambayo hujumuisha tanzu nyingi. Hata baadhi ya tanzu za kinathari, kama vile hadithi zinaweza kuingia katika kumbo ya wimbo pindi zinapoimbwa. Aina kuu za nyimbo hapa Afrika Mashariki ni tumbuizo; nyimbo za kuliwaza, bembea; nyimbo za kubembeleza watoto, nyimbo za kilimo au maombolezi, nyimbo za jando na unyago, nyimbo za siasa; hizi ni nyimbo zinazoimbwa kwenye shughuli za kisiasa, nyimbo za kuaga mwaka au kuadhimisha mwezi muandamo. Pia kuna nyimbo za dini; hizo huweza kuwa nyimbo za Waislamu, Wakiristo na hata ibada za kijadi. Aidha tanzu vyengine za nyimbo ni kama vile; nyimbo za taifa; hizi ni nyimbo za kusifia taifa au kabila, Chapuzo; hizi ni nyimbo za kuhamasisha shughuli fulani kama vile kilimo, uvuvi, kutwanga na kadhalika. Pia kuna nyimbo za kazi. Hapa tunapata nyimbo kama vile kimai; nyimbo zihusuzo shughuli za bahari, nyimbo za vita; hizi ni zile ziimbwazo na askari wakati wa vita. Pia kuna nyimbo za watoto; nyimbo hizi ni zile ziimbwazo na watoto wakati wa michezo yao. Vile vile kuna tenzi au tendi: hizi ni nyimbo refu zinazosimulia jambo fulani. Zile zinazosimulia visa vya mashujaa huitwa tendi. Vile vile katika kufafanua kipengele cha maghani Mulokozi (ameshatajwa) anaeleza kuwa maghani ni ushairi unaoghaniwa au kutambwa hadharani. Mara nyingi sauti ya maghani huwa kati ya uzungumzaji na uimbaji. Aghalabu maghani hutambwa hadharani pamoja na ala ya muziki au bila ala. Baadhi ya ghani huwa refu sana zenye kusimulia 20 hadithi au historia. Ghani za aina hiyo huweza kuwa tendi-simulizi, sifo, visaasili nakadhalika. Kimaudhui maghani hayana tofauti na nyimbo. 2.1.1.5 Ngomezi Mulokozi (1996), anaeleza ngomezi kuwa ni namna ya kupeleka ujumbe kwa kutumia ngoma, midundo fulani ya ngoma huwakilisha kauli fulani katika lugha ya jamii husika. Mara nyingi kauli hizo ni za kishairi au kimafumbo. Huimbwa wakati wa dharura, aghalabu hutangazwa vita kwa kutumia Ngomezi katika kabila fulani kwa kutumia ngoma. Balisidya (Matteru) (1987) anagawanya fasihi simulizi katika tanzu tatu ambazo ni nathari, ushairi na semi. Katika kila utanzu kuna vipera vyake ambavyo navyo vina vijipera pia vidogo vidogo ndani yake, uanishaji wake ni nathari, nudhumu na ushairi. Amegawa vipengele hivi kwa upande wa nathari, kuna ngano ambayo ndani yake ina istiara, hekaya na kharafa. Katika tarihi kuna kumbukumbu, shajara, hadithi, historia na epik. Na kwa upande wa visaasili kuna kumbukumbu, tenzi. Kwa nini na kwa maana gani? Kundi la pili la ushairi lina nyimbo ambayo nyimbo imejumuisha bembea, tumbuizo, ngoma, kwaya na miviga. Kwa upande wa maghani kuna majigambo, shajara, vijaghani na tenzi. Katika uainishaji wake huu baadhi ya tanzu hazionekani, ama tunaweza kusema zimeondolewa kabisa. Mfano visakale na ngomezi. Aidha, Balisidya (ameshatajwa) anaweka utenzi kuwa ni kipera cha visaasili katika kundi la nathari. Hapa anaibua mjadala, kwani kama tujuavyo kuwa utenzi katika fasihi simulizi huhusisha uimbaji 21 kwa hivyo swali la kujiuliza ni utenzi au ni nathari. Vile vile kuna kuingiliana kwa tanzu, Mfano kumbukumbu na kwanini na kwa namna gani ni tanzu ambazo zinajitokeza katika kundi zaidi ya moja. TUKI (1988), wanasema ugawaji wa tanzu na fani ya fasihi simulizi si wa moja kwa moja. Hii ni kwasababu ya utendaji na uwasilishaji wake, ni vigumu tanzu hizo kubakia katika hali moja. Tanzu na fani ya fasihi simulizi huingiliana. Wimbo huweza kuwa hadithi na hadithi kuwa methali, msemo na kuwa kitendawili. Tunaweza kugawa tanzu na vipera vya fasihi simulizi kwa kugawanya kutokana na kusadifu matumizi. Kulingana na aina ya lugha iliyotumiwa kuziwasilisha mwanzo wa kuumbwa lugha ya tanzu hiyo. Kwa hivyo, tanzu na fani ya zote zitaingia katika mafungu matatu ya awali, kulingana na aina ya lugha ya uwasilishaji katika fashi simulizi, na kupata nathari, semi na ushairi. Tanzu hizi zote za fasihi simulizi zimegawika katika makundi mawili nudhumu na nathari. Nathari hujumuisha tanzu na vipera ambavyo ni hadithi, ngano, tarihi, visakale, vigano na masimulizi ya utani. Nudhumu nayo hujumuisha ushairi, nyimbo na maghani. TUKI (1988), wamegawa fasihi simulizi katika tanzu tatu na pia kila utanzu una aina nyengine ya vipera vidogo vidogo, kuna hadithi ambayo ina ngano, tarihi, visaasili, vigano na soga. Ushairi au nudhumu una ngonjera, maghani, nyimbo na ushairi. Vile vile kundi la semi lina vipera vya misemo, misimu, mafumbo, methali, nahau, vitendawili na mizungu. Kama inavyoonekana katika tanzu hizi tatu, kuna aina nyengine mbali mbali ambapo kila kipera kimoja chaweza kuwa ni mkusanyo wa vipera 22 mbali mbali vyenye wasifu wa aina moja wa muundo na mbinu za uundaji na namna ya uwasilishaji katika masimulizi. Hivyo basi, mawazo haya yanahitaji kuchunguzwa kwa kina jinsi ya ugawaji wa tanzu za fasihi. Tunahitajika kuangalia wakati pamoja na kuangalia muingiliano wa tanzu. Muingiliano huu hufanya baadhi ya jamii kuwa na jina moja tu kwa fani zaidi ya moja, au majina zaidi ya moja kwa fani ile ile moja. Nkwera (1979), amegawa fasihi simulizi katika makundi matatu, anaona kuwa kunamakundi matatu ya kazi ya fasihi, anaona kuwa kuna habari za kweli na za kubuni katika fasihi huitwa kazi bunilizi. Kazi zenyewe ni hadithi, ushairi na michezo ya kuigiza. Anaendela kusema kuwa hadithi zimegawika katika visa, ngano na hekaya. Ushairi ni mashairi, tenzi na nyimbo. Katika michezo ya kuigiza ni futuhi, tanzia, yuga na rasma. Nkwera (kashatajwa), anasema futuhi ni mchezo wa furaha au ushindi wa kitu kilichokuwa kimawaniwa, na watu au makundi ya watu tofauti. Tanzia ni mchezo ya kuhuzunisha au kupatwa na janga. Hivyo michezo hii huchezwa kuonesha huzuni juu ya jambo fulani. Yuga ni michezo inayoonyesha furaha na pia huzuni. Ramsa ni michezo inayochezwa kwa namna ya kukejeliana miongoni mwa watu na vile vile kufanyiana mizaha mbali mbali, kulingana na jamii. Kutokana na maelezo hayo, yameweza kumsaidia mtafifi kupata uwelewa juu ya uchambuzi wa tanzu za fasihi simulizi na kumsaidia katika kukamilisha malengo yake ya utafifi. Hali hii imeweza kumfanya mtafiti kukamilisha kazi yake kwa usahihi. Vile 23 vile maelezo hayo yalimsaidia katika kuelewa aina mbali mbali za tanzu za fasihi simulizi. Mawazo haya ya Mulokozi, TUMI, TUKI, Nkwera na Balisidya yalitusaidia sana katika kufanya utafiti na kusukuma mbele uchunguzi wa vipengele vya fasihi simulizi katika kazi hizi teule. Hii ni kwa sababu vipengele alivyovieleza Mulokozi ndio vilivyotuongoza katika kufanya utafiti wetu, na pia vilikuwa ni muhimili wa utafiti, ambavyo viliongoza namna ya kuvichunguza vipengele hivyo, ili kuona namna vilivyotumika katika riwaya hizo za Adili na Nduguze na Wasifu wa Siiti Binti Saad. Jadweli na 1 linaonesha vipengele vya fasihi simulizi kulingana na wataalamu, ambavyo vitachaguliwa vile vitakavyojitokeza kulingana na malengo ya utafiti na ndivyo vitakavyoongoza utafiti huu. Jadweli na 1: Vipengele vya Fasihi Simulizi Namba Vipengele Vya Fasihi Simulizi 1. SEMI - methali, vitendawili, simo, lakabu, kauli tauria 2. MAZUNGUMZO - malumbano wa kijamii, hotuba, sala 3. MASIMULIZI - muundo, lahaja, hekaya, kisa kale, kumbukumbu, istiara, hadithi, ngano, maigizo ya kidini, mandhari pamoja na dhamira 4. MAIGIZO - kutegemea shabaha ya miktadha. 5. NGOMEZI - Kutoa taarifa kwa kutumia ngoma kwa nyimbo 6. USHAIRI NYIMBO NA USHAIRI MAGHANI - Nyimbo za aina yoyote 7. WAHUSIKA - wanyama, miti, majabali, miungu, mashetani, mazimwi n.k 8. DHAMIRA – kujitolea, ushujaa, ukarimu, elimu, ubinafsi n.k Chanzo cha data: Mulokozi (1996) 2.2 Tafiti kuhusu Riwaya ya Kiswahili Utafiti aina mbalimbali umefanywa ambao unahusu riwaya za Kiswahili lakini utafiti huo umejikita katika kutoa maana ya riwaya, na uchambuzi wa riwaya, kuchambua vipengele vya fani na maudhui kwa ujumla na pia baadhi ya vipengele vya fani na 24 maudhui na si katika kuchunguza ufasihi simulizi uliomo katika riwaya. Maana ya riwaya imelezwa na wataalamu wengi, baadhi yao ni kama wafuatao; Hatuwezi kupata maana ya riwaya kwa kipimo cha ubainishaji wa urefu au wingi wa maneno kwa ukamilifu wa maana ya riwaya. Iwapo tutakubalina na Mphalale (1976) ili iwe riwaya ni lazima maneno 75,000 basi tutakuwa tunaungana kwamba hatuna riwaya katika fasihi ya Kiswahili. Chuachua (2011) anafasili kuwa riwaya ni kazi ya kubuni ya kinathari yenye uchangamani wa fikra, msuko, mandhari na uhusika unaosawiri binaadamu na maisha yake. Hii inaonyesha kwamba tunapozungumzia uchangamani, ni ile hali ya kuunda kazi kisanii kwa kutumia mbinu mbali mbali za kiubunifu (kiumbilizi), na ndipo unamfanya kumfikirisha msomaji na uchangamani ndio kigezo kikuuu kinachotofautisha riwaya na aina nyengine za nathari. Maelezo yaliyotangulia, yanakubalika kwa maoni yetu kwasababu yanaonyesha vigezo vilivyokusanya maana ya dhana ya riwaya kwa mkusanyiko mkubwa wa wataalamu wengi kuonyesha vigezo vya urefu, uhusika wa kina, uchangamano wa mtindo na uzito wa kidhamira, masimulizi kwa kugusa nyanja mbali mbali za maisha zinazohusu walimwengu na vitu vinavyowahusu, mawanada ya hadithi, suala la wakati na matumizi ya mandhari. Hatumaanishi ya kuwa ni lazima pawepo aina zote za vigezo vilivyotajwa lakini pawepo na asilimia ya kutosha (kubwa) kuikamilisha kazi hiyo. Tunakubaliana ya kuwa vigezo hivyo vitakamilisha kuijua dhana ya riwaya na kuitofautisha na aina nyengine ya nathari. Kitu kitachotuwezesha kusema kwa mawanda mapana kuwa vitabu vya Shaabani Robert cha Adili na Nduguze na Wasifu wa Siti Binti Saad ni miongoni mwa riwaya. 25 Ndungo na Mwai (1991) wanaeleza kuwa kuzuka miji na viwanda kulistawisha uandikaji wa riwaya na usomaji kupanuka. Maendeleo katika vipengele vyote vya maisha, kama vile kiuchumi, kisiasa na kijamii, yalizusha haja ya kuwa na utanzu wa fasihi ambao uchangamano wake wa kifani na kimaudhui ungedhibiti nyanja hizi zote. Aidha mabadiliko hayo yalileta matabaka, ambapo palizuka tabaka jipya la mwabwanyenye, walihodhi viwanda na nyenzo nyingine za kiuchumi. Hivyo tabaka hili lilitaka fani mpya katika fasihi kwa sababu ya kipato cha fedha za kununulia vitabu na magazeti, na kupata wakati wa ziada wa kujisomea. Fani hiyo ya riwaya ilitawaliwa na ubinafsi. Ubinafsi huu ulijidhihirisha kiitikadi, mfano riwaya ya Robinson Cruisoe (1719), hudhaniwa kuwa ni riwaya iliyosawiri mawazo ya juu ya kibepari, kwa kumtumia muhusika Friday ambaye alionekana bado kustaarabika. Vile vile ubinafsi ulionekana katika kanuni za utungaji wake kwa kuepukana na kanuni za jadi. Mulokozi (1996) anaeleza kuwa mageuzi ya kijamii na kisiasa pia yalifungamana na mabadiliko ya kiuchumi tuliyoyataja. Mataifa ya Ulaya yalianza kujitegemea kwa kuepukana na Dola iliyokuwa tukufu ya Kirumi. Hivyo Mataifa ya Ulaya yalianza kujipambanua kiutamadauni na kisiasa pia walijenga utamaduni wao kitaifa na mifumo ya elimu. Vile vile walianza kutumia mfumo wao wa maandishi katika lugha yao. Hata misahafu ya dini, kama vile Biblia ilianza kufasiriwa kwa lugha ya Kidachi mwaka elfu moja mia tano na thalathini na nne (1534), kila elimu ilipotanuka na ndipo watunzi walipoengezeka na hivyo kuwa hadhira nzuri ya watunzi wa riwaya. 26 Mulokozi (1996) anafafanua kuwa ugunduzi wa teknolojia ya upigaji chapa vitabu kwa kutumia herufi zinazohamishika, mathalani mgunduzi aitwae Gutenberg huko Ujerumani mwaka elfu moja mia nne na hamsini (1450) ulirahisisha kazi ya uchapaji vitabu, Hali iliyopelekea vitabu kuwa bei nafuu na kupatikana kwa wingi. Ndongo (1991) anaeleza kuwa kuzuka kwa viwanda kuliwafanya waandishi wengi kuandika maandiko yaliyo marefu hali hii ilisababisha kapatikana kwa wasomaji wengi hasa wanawake ambao waliachwa majumbani baada ya waume wao kwenda kufaya kazi viwandani. Kwa kuwa wanawake hasa wale wa tabaka la juu walikuwa na watumwa wa kuwafanyia kazi za nyumbani. Kwa hivyo kuzuka kwa riwaya tunaweza kusema kulifungamana na mfumo wa ubepari. Ndungo na Mwai (1991) wanaeleza kuwa kuzuka kwa mitambo ya kupigia chapa, viwanda pamoja na miji, hivi vilikuwa vyombo mahsusi vilivyokuza utanzu wa riwaya. Kulikuwa na uwezekano wa kuandika maandiko marefu marefu kwa urahisi kwa kutumia mitambo ya kupigia chapa. Hali iliyofanya nakala nyingi za maandiko hayo zingalitolewa na kusambazzwa kwa rahisi. Miongoni mwa riwaya za mwanzo kuandikwa kwa Kiswahili ni ile riwaya ya Uhuru wa Watumwa (1934), kilichoandikwa na Mbotela (1934), kinaelezea kwa kusimulia habari za watumwa na uhuru wake pamoja na harakati za biashara ya watumwa katika mwambao wa Afrika Mahariki. Kitabu hiki ijapokuwa kimeandika habari za watumwa lakini kina taathira kubwa za kikoloni. 27 Mashindano yaliyoanzishwa yalikuwa ni chachu ya kuanzishwa kwa riwaya ya Kiswahili. Kutokana na mashindano hayo yaliyoanzishwa na Taasisi, waandishi wengi wa Kiafrika walijitokeza na kuandika riwaya. Mifano ya waandishi hawa ni Shaaban Robert (1960), ambaye vitabu vyake vilichota kwa kiasi kikubwa utamaduni wa wageni, vitabu kama vile Kusadika na Kufikirika. Ali Jemadar naye aliandika riwaya ya Nahodha Fikirini, wengine walioshiriki katika mashindano haya ni Moh‟d Saleh Farsy (1960) alitoa kitabu cha Kurwa na Doto, Mohmed Suleiman Abdalla (1960), aliandika wa Watu na Wanawe. Katika maendeleo ya riwaya za Kiswahili, uandishi umepiga hatua fulani, hasa baada ya uhuru, nje ya ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki, Mantiki, imeongezeka maradufu. Kwani maudhui, mantiki, mtiririko hata mtindo inasonga mbele kila uchao. Hivyo riwaya nyingi zimeandikwa miaka ya sabiini na thamanini. Waandishi kama vile Euphrase Kezilahabi, Said Ahmed Mohamed, Suleiman Mohamed, Mohamed Said Abdalla, ndio washika bendera kwa kuzingatia kigezo cha maudhui na uumbaji wa kisanaa. Tunapochunguza maelezo hayo ni dhahiri kuwa chanzo cha riwaya za Kiswahili ni mchango mkubwa uliotokana na biashara na mapinduzi ya viwanda huko Ulaya. Hali hii ilianza Ulaya na kuja Afrika, kwa kutumia biashara ya baharini. Ambapo biashara hii ilipotokea Ulaya kuja Afrika iliathiri kwa kiasi kikubwa mila, silka na desturi za Waafrika. Hali iliyopelekea kufuata uhalisia wa Kiafrika na kuwa mchanganyiko kati ya Uafrika na Uzungu. Ndipo pakapatikana kitu kiitwacho riwaya inayotokana na fasihi andishi badala ya hadithi inayotokana na fasihi simulizi. 28 Kwa upande wa uchambuzi wa riwaya, kazi ambazo zimefanyika kuchambua riwaya ni pamoja na Chuachua (2008), Chuachua (2009), Senkoro (1976), Senkoro (1982), Msokile (1993), Sengo (1975), Taib (2008), Tiab (2009) na Mong‟eri (2000). Chuachua (2008), alifanya utafiti unaohusu “Taswira katika riwaya za Shaaban Robert”, alichunguza athari mbali mbali alizotumia Shaaban Robert katika riwaya zake. Kwa ujumla, kwa kuangalia taswira, hivyo alifanya uchambuzi wa dhamira na kuliacha suala la fani. Hivyo utafiti huu umetuachia pengo ambalo linahitajika kuzibwa. Chuachua na wenzake (2009), waliandika makala inatoitwa “Shaaban Robert Vita na Ukoloni”, walifanya uchambuzi katika vitabu vya Shaaban Robert na kuthibitisha kuwa kazi za Shaaban Robert zimejaa ukoloni. Kwa kuonyesha ni namna gani wakoloni walitesa, kuwakandamiza pamoja na kuwanyonya watu weusi kwa miaka mingi kadhaa. Katika uchambuzi wao, walionyesha vipengele vya dhamira ya kupinga ukoloni na kutafuta ukombozi, kwa kutumia vitabu vya Kusadikika (1951), Kufikirika (1909), Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini (1949) na Mwafrika Aimba (1969). Kazi hizi zote zilijishughulisha na itikadi ya Kisoshalisti tu. Senkoro (1976), aliandika makala inayoitwa “Utamaduni katika Riwaya za Kiswahii”, kwa ujumla aliangalia athari za utamaduni katika riwaya za Kiswahili, pamoja na mambo mengine. Alifafanua kwamba riwaya ya Adili na Nduguze ina umbo la ngano na wahusika wake ni majini na mashetani n.k. Pia anaeleza kuwa Shaaban Robert amezikashifu dini za Kiafrika kwa kuwa zina mila za kuabudu mizimu. Maelezo ya Senkoro (1976) yanafaa kujadiliwa kwa kina, kwani aliyoyasema yanaonyesha kuwa, 29 hakuangalia mila, desturi, silka pamoja na utamaduni wa Afrika, kwa wakati ambao ulikuwa haujapata athari kubwa za wageni walioingia Afrika. Senkoro (1982), alifanya kazi ya kuchambua kitabu cha Siku ya Watenzi Wote, na kuchambua kipengele cha dhamira na alifafanua kwamba, dhamira iliyotawala ni ile ya ujenzi wa jamii mpya itakoyokuwa ya kiutopia. Kwa maoni suala hili linahitajika kuangaliwa kwa jicho la ndani kabisa, kwani mbinu za masuluhisho ya kuweza kujenga jamii aliyoikusudia Shaaban Robert pengine zinatekelezeka. Senkoro (1982), inaonyesha hakuangalia itikadi kwa usahihi ya mwandishi wa kitabu cha Siku ya Watenzi Wote na jamii ambayo imeandikiwa kazi hiyo kwa kutazama mila, desturi, silka na utamaduni wa jamii. Sengo (1975), alifanya uhakiki wa kazi za Shaaban Robert, uhakiki wa Sengo unaweka bayana dhamira zilizotamalaki katika kazi zake. Japo kapigania utu bora, uungwana, ustaarabu, heshima, adabu, njema, haki na kila jema. Maelezo hayo yanaonyesha ujumla jumla, bado yanahitajika kujadiliwa kwa kina kwani hayakuonyesha ni kitu gani au msukumo gani uliomfanya Shaaban Robert kutunga kazi kwa kutumia dhamira hizo. Je? Jamii haina mambo yake wanayofuatwa katika kutengeneza au kufanya jambo fulani kutokana na mila, desturi, silka na utamaduni wake. Tiab (2008), alifanya uchambuzi wa kazi mbali mbali za Shaabani Robert, ambazo kwa maoni yake Taib, kazi hizi zina maudhui ya Kiislamu na kwamba zinafaa kuhakikiwa na kuchambuliwa kwa makabala wa nadharia ya Uislamu. Anafafanua kwamba hata kazi za Shaaban Robert, hazipaswi kuhakikiwa kwa mikabala ya Kimagharibi kwani mikabala hii ina nafasi kubwa ya kuweza kupotoa maudhui ya kazi zenye maadili ya 30 dini husika. Maelezo haya yanaweza kujadiliwa kwa ukweli, sio mikabala yote inapotosha Uislamu pale inapoteuliwa kufanyika kwa utafiti. Kutokana na maelezo hayo, inaonyesha kuwa unapochagua mkabala tuhakikishe kuwa utafaa kwa utafiti, mfano mwingilianamatini tunaweza kutumia bila ya kupotosha kazi za Shaaban Robert. Tunapoangalia mkabala wa kimuundo tunaangalia jinsi gani lugha inavyowiyana na maana iliyobeba kutokana na jamii yake. Pia mwingilianomatini tunaangalia kazi moja kutumika ndani ya kazi nyengine kulingana muktadha wa kijamii Taib (2009), alifanya uchambuzi kuhusu “Maisha ya Shaaban Robert na Falsafa yake katika Maandishi”, Mtafiti wa maandishi haya anasema msingi wa falsafa ya mwandishi huyu ni udhanifu, na kwamba dini ndio muelekeo wa vielelezo vyake. Mwandishi huyu ameigawa falsafa katika makundi matatu, utu wema, siasa na dini. Taib anaeleza kuwa lengo la Shaaban Robert ni kuelimisha jamii kuhusu uongozi mwema unaofaa na kulaumu dhuluma iletwayo na uongozi unaokandamiza raia. Tunajiuliza suala ni siasa ipi ifuatwe ili kujenga uongozi mzuri. Hapa tunasema tuiyangalie jamii kimuundo katika mamlaka yake katika fikra, mila, desturu, silka na utamaduni. Mong‟eri (2000), alifanya utafiti na kuchambua utetezi wa maadili katika nathari za Shaaban Robert pekee. Anaeleza kwamba tunaweza kugawa maadili katika makundi matatu, kundi la kisiasa, kiuchumi na kijamii. Lengo la utafiti huu ni kushughulikia suala la itikadi katika riwaya zake, tunaitazama itikadi kama zana ya utekelezaji wa majukumu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.