TASWIRA YA JAGINA KATIKA TENDI: ULINGANISHI WA FUMO LIYONGO
SURA YA TATU
KULINGANISHA NA KUTOFAUTISHA SIFA ZA KIJAGINA ZA NABII ISA NA FUMO LIYONGO 3.0 Utangulizi Gichamba (2005:67) akiwanukuu Chiraghdin, Nabhany na Baruwa (1975:63), anasema kuwa tenzi ambazo huandikwa kuhusiana na mashujaa au tukio lingine lolote la kijamii, hufumbata na kusawiri kwa kina masuala muhimu ya kihistoria. Wanaendelea kusema kuwa, maudhui ya tenzi katika fasihi mbalimbali za ulimwengu ni kutukuza utaifa katika historia za jamii, na pia kuwatukuza watu waliotenda vitendo vikubwa (mashujaa) katika historia zao. Ni kwa mintarafu hii ambapo katika sura hii, tutaangazia sifa za kishujaa za Fumo Liyongo na Nabii Isa. Tutaonyesha kushabahiana kwa sifa za kijagina za mashujaa hawa wawili, pamoja na kutofautiana kwao. Ili kupata sifa jumlishi za kishujaa za Fumo Liyongo, tumerejelea Utenzi wa Fumo Liyongo pamoja na tungo zingine zilizotungwa na waandishi wengine kumhusu. Aidha, tumerejelea tungo muhimu ambazo zinadaiwa kutungwa na Liyongo mwenyewe. Katika kuainisha sifa za kishujaa za Nabii Isa, tumeangazia sifa zinazojitokeza katika Utenzi wa Nabii Isa. Huu ni utenzi ambao msingi wake ni katika Qurani. Hivyo, shujaa Isa katika utenzi huu amesawiriwa kwa njia sawa na alivyoangaziwa katika Qurani tukufu. Hata hivyo, tumerejelea Qurani, na inapobidi, Bibilia, ili kuchangia sifa za kijagina za shujaa huyu ambazo hazijajitokeza kikamilifu katika utenzi huu. Aidha, tumetalii mitandao tofauti ili kuchangia historia, maisha na matendo ya kimiujiza ya shujaa Isa. 48 3.1 Kuzuka kwa Mashujaa Jamii ni mfumo ambao huwa na mahitaji mengi. Mahitaji haya huzua taasisi mbalimbali, mojawapo ikiwa ni taasisi ya mashujaa. Taasisi hii ni muhimu katika kusawazisha hali zilizoenda kombo katika jamii. Shujaa wa kihistoria wa jamii huwa hazuki katika ombwe tupu, bali huzuka katika kipindi, mazingira na wakati maalumu katika jamii yake na huishi hadi pale ambapo atatekeleza dhamira yake. Ni kutokana na sababu hii ambapo wanajamii wanamtazama shujaa kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Wengi wa mashujaa, kama vile wa kidini na hata wa kihistoria, huzuka katika mazingira ambamo mna vita. Lwanda Magere alizuka kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Wanandi, Dedan Kimathi, kwa mfano, pia alizuka katika mazingira ya kivita, na vivyo hivyo Fumo Liyongo aliyezuka kwa sababu ya misukosuko ya kivita kati ya Waswahili wenyewe, na hata kati yao na majirani zao. Nabii Isa anazuka kama shujaa kwa Wayahudi ambao baada ya kutawaliwa na kulipishwa kodi na mataifa mengine na hata kutumika kama watumwa, walitarajia kutimizwa kwa ubashiri wa Nabii Isaya kuhusu kuzaliwa kwa mfalme wa wafalme ambaye angewakomboa kutoka kwa maadui zao. Wayahudi walitarajia kiongozi wa kijeshi. 3.1.1 Utabiri wa Kuzaliwa kwa Majagina Mutiso (1999:4), anasema kuwa kuzaliwa kwa jagina huwa kumebashiriwa na kusipobashiriwa, huthibitishwa baada ya jagina kuzaliwa. Hali hii ya ubashiri inadhihirika sana katika kuzaliwa kwa mashujaa wa kidini ambapo kabla hawajazaliwa, kunatokea mbashiri ambaye anawatia moyo wanajamii wazidi kuwa na ustahimilifu, huku akiwaambia kuwa jagina atazaliwa. Jagina huyu ataasisi ufalme ambao utakuwa mkubwa mno ukilinganishwa na falme zingine na kisha atawakomboa kutoka kwa dhiki zao. 49 Kuzaliwa kwa Nabii Isa kulibashiriwa katika Agano la Kale na kunathibitishwa na Yahya Mtakatifu. Unabii huu umedokezwa katika Isaya vii:14, xi:3 Yeremiah xxiii:5,Micah v:2. Tangu utabiri wa Isaya hadi kuzaliwa kwa Isa, inakadiriwa kuwa ni miaka 400. Utabiri wa nabii Isaya ulitimia katika kitabu cha Mathayo 2:1 ambapo inaeleza kuwa shujaa alizaliwa Bethlehemu ya Uyahudi, zamani za mfalme Herode. Mutiso (khj) anasema kuwa hata kuzaliwa kwa mashujaa wengine wa kidini huwa kumetabiriwa. Kuzaliwa kwa Gautama Buddha kwa mfano, kulitabiriwa na watabiri sitini na wanne walioifasiri ndoto ya mamake hata kabla ya kuzaliwa kwake. Kuzaliwa kwa Samsoni aliyewakomboa Waisraeli kutoka kwa Wafilisti (taz kitabu cha Waamuzi 13:3 kwenye Biblia), kulitabiriwa na malaika. Shujaa anapozaliwa kunakuwa na ishara inayoonyesha kuwa mtoto aliyezaliwa ni mtoto wa kipekee. Sifa hii inajitokeza vyema zaidi katika Biblia. Baada ya Yesu kuzaliwa, malaika wa Mungu aliwatokea wachungaji waliokuwa wakichunga makundi yao karibu na Bethlehemu. Malaika huyo alitangaza: “Leo katika jiji la Daudi, Mwokozi ambaye ni Kristo Bwana amezaliwa kwenu.” (Luka 2:8-11) Kisha, “..umati wa jeshi la mbingu ukawa pamoja na yule malaika, ukimsifu Mungu na kusema: ‘Utukufu katika vilele vilivyo juu kwa Mungu, na juu ya dunia amani kati ya watu wa nia njema.’ Luka 2:13, 14. 50 Vilevile, Isa alipozaliwa, makuhani walienda kumwabudu wakielekezwa na nyota iliyong’aa kutoka Magharibi na kutua mahali alikozaliwa (Mathayo 2:1‒3). Ishara hizi zinaoana na sifa kuwa majagina wanapozaliwa kunakuwa na ishara kuonyesha kuwa hawa ni watoto wa kipekee. Katika utafiti wetu, hatukupata ushahidi wowote kuonyesha kuwa kuzaliwa kwa Fumo Liyongo kulikuwa kumetabiriwa. Utenzi huu pia haujazungumzia matukio yaliyozunguka kuzaliwa kwa Fumo Liyongo au ishara zozote zilizoonyesha kuwa Liyongo angekuja kuwa mtu wa pekee katika maisha ya baadaye. 3.1.2 Jagina kwa Kawaida ni Mwanamume Aghalabu kote duniani majagina huwa ni wa kiume. Pale ambapo ni mwanamke, basi hana sifa bia za kishujaa kama walizo nazo wanaume ambao hurejelewa kama mashujaa (sifa za toka utabiri wa kuzaliwa kwao hadi kifo chao). Pengine mwanamke shujaa utapata kuwa alitenda tendo moja tu la kijisajiri. Hata hivyo, ujasiri ni sifa moja tu ya kishujaa wala haiwezi kumfanya mtu kuwa shujaa. Shujaa Fumo Liyongo na Nabii Isa walikuwa mwanamume.Mashujaa wa kidini pia huwa ni wanaume. Kwa mfano Musa, Samsoni, Buddha, Mtume Muhammadi na wengine wengi. Aidha, waumini wa dini mbalibali duniani humchukulia Mungu (ambaye ni shujaa wa mashujaa) kuwa ni mwanamume. Hali hii ya kumchukulia jagina kuwa mwanaume inatokana na akililaza kuwa mwanamume kwa wakati wowote yu juu ya mwanamke na kwa hivyo, uongozi pamoja na ukombozi ni lazima 51 utokane na mwanamume. Kadhalika, wanawake kote duniani husawiriwa kama watu waoga na wadhaifu, tofauti na mwanamume ambaye mara nyingi huwa mstahimilifu na hukabiliana na mambo na masaula magumu katika jamii.kama vile, vita na mambo mengine magumu. Ndiposa kukatokea msemo wa “jikaze kiume”. 3.1.3 Utoto na Ujana wa Jagina Aghalabu utoto na ujana wa jagina huwa hauelezwi. Kama utaelezwa, utapata kuwa ni kwa kijuujuu tu na wakati mwingine utapata wanahistoria huchanganya utoto wa kuzaliwa kwa shujaa na ujana wake na kufanywa kuwa kitu kimoja. Hii ni kwa sababu shujaa anapozaliwa, hukua kama mtu kawaida tu. Lakini baadaye ndipo watu hugutuka kutokana na matendo, tabia na uwezo wake usio wa kawaida na ndipo watu huanza kumtukuza. Kazi zinazohusishwa na Fumo Liyongo, kwa mifano hazielezi kuhusu utoto wake wala ujana wake. Mathalani, hutuelezwi mazingira ya nyumbani kwao, uhusiano wake na vijana wengine akiwa mtoto, maeneo aliyoyatembelea akiwa kijana, hulka na matamanio yake. Tunatajiwa katika Utenzi wa Fumo Liyongo kuwa Liyongo alibaleghe na kuwa mwanamume mwenye haiba, kimo kirefu, mpana na maarufu hivi kwamba watu walienda kumwangalia. Katika Utenzi wa Nabii Isa hakuna mengi yanayosemwa kuhusu ujana na utoto wa Nabii Isa, ila tu kwamba alilelewa katika ibada na kwamba alisema akiwa mdogo sana.Utenzi wa Nabii Isa unatufafanulia kuwa mamake Maryam binti Imrani alipohisi njaa akiwa shinani mwa mtende punde tu baada ya kumzaa, mwanawe nalimuuliza autikise mtende ambao haukuwa na tende lakini Mungu alimruzukia akavuna tende tamu, maalum tena mbivu na vivyo kumwepusha na njaa. 52 Nabii Isa alifahamu toka utotoni mwake kuwa alikuwa na nafasi muhimu kama masihi na hivyo hakushiriki michezo kama watoto wengineyo: 288 Kwa wadogo si katiti, Alikuwa tafauti, Hakupoteza wakati, Machezo kuhudhuria. 289 Mchezo wake dhabiti, Alo akijisharuti, Ni yeye ni msikiti, Ibada kuhudhuria. 3.1.4 Shujaa Hutokana na Ukoo wa Kifalme au nasaba bora. Mara nyingi shujaa hutoka katika ukoo ambao unachukuliwa kuwa ni ukoo ambao umetengwa na kuteuliwa na Mwenyezi Mungu, ili uongoze jamii na kuikomboa kutokana na shida na misukosuko inayowakumba wanajamii husika. Mutiso (1999:4) anaeleza kuwa kuzaliwa kwa jagina huwa kumebashiriwa na kusipobashiriwa huthibitishwa baada ya ya jagina kuzaliwa. Anadai kuwa ithibati kwamba atakayezaliwa au aliyezaliwa atatokana na ukoo au mlango wa kureshi, Sakya, Gandhi, Amaterasu. Omikami, Daudi, n.k. Kila jamii katika ulimwengu mzima huhusudu asili ya jagina ake na hutilia maanani umuhimu wa mambo ya kadimu. Kwa kuitaja shajara yake, mwanadamu hujihisi kama amezaliwa upya tena. 53 Baada ya kiongozi kufa, jamaa mmoja kutoka katika ukoo wa kiongozi huyo ndiye huurithi utawala. Kwa hivyo, kwa kawaida jagina hutokana ukoo bora au wa kifalme ambapo baba ya jagina aghalabu huwa mfalme au kiongozi wa jamii yake. Uongozi wa utawala huu hauji vivi hivi tu, lakini inabidi kuwe na utetezi wa cheo cha uongozi kama ambavyo tutathibitisha hapa baadaye. Fumo Liyongo alitokana na ukoo wa Al Bauri (Allen: 1993:121). Ukoo ambao ulichukuliwa kuwa bora na kupewa jukumu la kuiongoza jamii, haswa jamii ya Waswahili wa Pate. Baba yake Liyongo, aliyeitwa Mringwari wa kwanza, alikuwa sultani wa dola ya Pate. Baada ya kifo chake, Daudi Mringwari aliyechukua hatamu za uongozi pia, alitoka katika ukoo wa Al Bauri. Mashujaa wengine na hasa wa kidini, akiwepo Nabii Isa, mtume Muhammadi na Gautama Buddha, walitokana na ukoo bora. Nabii Isa alitokana na ukoo wa mfalme Daudi. Mashujaa wengine ambao wametokana na koo bora ni kama vile Mtume Muhammadi, aliyetokana na ukoo wa kabila la Kikureshi, na Gautama Buddha, aliyetokana na ukoo bora ulioitwa Sakya, ulioaminika kutokana na mayai yaliyoanguliwa na jua (Mutiso 1999:5). 3.1.5 Utetezi wa Cheo Shujaa mara nyingi huwa hakipati cheo chake kwa njia ya urahisi. Huwa lazima akipiganie na akitetee dhidi ya maadui wake. Aghalabu shujaa akiwa kiongozi ndipo hupata nafasi nzuri ya mabadiliko na kuitumikia jamii yake jinsi atakavyo hadi katika ufanisi wa ukombozi. Shujaa kwa hivyo anaweza kufanya jambo lolote, bora tu litamsadia kuhifadhi kiti chake, anaweza hata kuua. 54 Utetezi wa cheo cha ufalme wa Fumo Liyongo unadhihirika vizuri sana katika Takhmisa ya Liyongo ambapo suala hili limeangaziwa kwa kina katika beti mbalimbali. Gichamba (2005:75), anatoa maelezo ya utetezi wa cheo kwa kurejelea jinsi Shaka Zulu alivyopigana ili kuona kuwa ameurithi uongozi wa Wazulu baada ya kifo cha babake. Anasema kuwa babake alipofariki, Sigujana (ndugu wa kambo wa Shaka) ndiye alichukua hatamu za uongozi. Hata hivyo, Shaka alijiona kama mrithi halali na kwa kibali cha Dingiswayo, alikichukua kikosi cha Izichwe na kuelekea hadi nyumbani kwao na kumwondoa Sigujana kutoka uongozini. Baada ya kushika hatamu za uongozi, wasaliti wake waliadhibiwa kwa mujibu wa sheria kali alizoweka. Mberia (1989:25), anasema kuwa Liyongo wa takhimisa anadhihirika kama jabari na jasiri ambaye hakunywea mbele ya maadui zake hata walipokuwa wengi na wenye silaha kali. Daima alikuwa tayari kukabiliana nao kwa moyo wa ushupavu. Kwani woga ulikuwa kitu cha kuepukana nacho na waoga watu wa kuepukana nao. Msimamo wake ulikuwa kwamba Mungu pekee ndiye aliye na uwezo wa kuangamiza binadamu na wala sio binadamu wengine. Hivyo basi anashauri: Wazi ata kicho na wachao sandaye nao Nao fawithi umuri kwa Mungu anusurao Siche ya ziumbe na zituko wakutishao Kufa kwa Mungu na shabuka limkutao Si kwa walimwengu mivi kikwi ingakufuma 55 Liyongo hakupigana kwa ajili ya kupenda kupigana au kwa kutaka kusifiwa. Sifa za namna hiyo aliziona ni mbaya. Alipigana kulipokuwa na sababu nzuri ya kufanya hivyo. Inaonekana kwamba miongoni mwa sababu hizi ni utetezi wa cheo. Pia, inaelekea kuwa, kwake, kutokuwa na cheo alichokuwa alichokuwa akipigania kulikuwa sawa na kuteremshwa katika ngazi ya hadhi. Alikiona cheo hicho kuwa ni stahiki yake. Tunaambiwa: Ana ndimi simba mfiliye jaba na cheo Naipiga kati kawanesa wajibagao Siche aduizo kukutana kwa ungi wao Sichi kikwi chao nami ume ndio nilio moyo Wangu kikwi kwa ajili ya kushagama. Hata hivyo, haijitokezi wazi iwapo Liyongo alikuwa anawekewa vikwazo ili asikipate cheo hicho au tayari alikuwa nacho akawa anapokonywa. Japo shujaa Isa alitokana na ukoo bora na wa kifalme wa Daudi, hakutetea cheo chake kwa njia ya vita vya kimwili kama walivyofanya Liyongo na Shaka. Badala yake aliwakabili wapinzani wake kwa kutoa mafundisho, ambayo mengi yaliwasuta watawala pamoja na Wayahudi ambao walimpinga na kumkataa kama mtume huyu wa Illahi. 3.1.6 Maadui wa Shujaa Njogu na Chimera (1999:156), wanasema kuwa hakuna jagina yeyote ulimwenguni ambaye hana adui. Kwa kawaida, mtu huwa na watu wanaompenda na wasiompenda.Hata Mwenyezi Mungu 56 (shujaa wa mashujaa, pia ana adui wake mkubwa ambaye ni shetani. Katika maisha ya kawaida, lazima ikumbukwe kuwa, ingawa mtu fulani anaweza kuwa mashuhuri na kipenzi cha watu au ambaye ana ufanisi mkubwa, hakosi watu wakumtakia mabaya, wanaomwonea wivu na hata wenye nia ya kumwua. Shujaa aghalabu anaweza kuwa na jamii nzima kama adui wake, mtu mmoja tu au watu wengi. Kwa kawaida, maadui hawa ni muhimu kwa sababu mtu hawezi kuwa shujaa bila kuwa na waoga.Vilevile, mtu hawezi kuwa mzuri kama hakuna wale wabaya. Huenda shujaa naye asiwepo kama hakutakuwa na maadui wake. Shujaa huwa na jukumu la kuikomboa jamii yake kutokana na mashambulizi au maovu ya maadui. Mara nyingi maadui wa shujaa humwogopa na hufanya njama za kisirisiri ili kumwangamiza, kwa sababu shujaa huwa na sifa za kipekee tofauti na za wapinzani wake. Fumo Liyongo kwa mfano, alikuwa na maadui wengi kama vile: Wagalla waliowashambulia Waswahili pamoja na jamii zingine za pwani, binamuye (Daudi Mringwari), na hata mwanawe ambaye katika Uteuzi wa Fumo Liyongo (Ub. 214), amerejelewa pia kama adui wa Mwenyezi Mungu. Kwa kawaida, maadui za jamii anayowakilisha au kuitawala shujaa huwa maadui wa shujaa huyo.Tunaweza kudai kuwa ushujaa pia huwa na ngazi mbalimbali, kwa mfano, Wagalla walikuwa mashujaa wa mwituni, lakini waliingiwa na hofu na hata kuogopa vibaya pindi walipomtazama Liyongo. Ngazi hizi za ushujaa huanzia kwenye matawi ya chini (shujaa wa kiwango cha chini) na kupanda hadi katika kiwango cha juu kabisa cha ushujaa kinachomilikiwa na Mungu. Shujaa wa chini kwa kawaida humcha shujaa wa kiwango cha juu. 57 Daudi Mringwari aliyekuwa binamu wa Fumo Liyongo, pia alikuwa ni adui wake mkubwa. Alipanga njama za kumwangamiza Liyongo kwani alimwona kama tishio dhidi ya utawala wake. Alimtumia mwanawe Liyongo kumsaliti baba yake. Kama alivyo Fumo Liyongo na maadui wengi, vivyo hivyo alivyokuwa Nabii Isa ambaye alipangiwa njama ya kuuawa, jambo ambalo Mola alilibadilisha kwa kumleta mtu ambaye alimfananisha na Nabii Isa kisura. Baadaye mtu huyu aliteswa, akauawa, akasulubiwa msalabani na wahalifu wale wakidai kuwa huyu alikuwa ni Nabii Isa mwenyewe. Kwa mujibu wa Bibilia, Wayahudi walifanikiwa kumsulubisha na kumuua Isa. Wayahudi, Waandishi na Mafarisayo waliona kama wamemkomoa kwa kuwa walidai kuwa alijikweza kwa kujifanya mwana wa Mungu. Pia watawala walifurahi maana watu wengi walimfuata na kumsikiliza, na hivyo kumuona kama hatari kwa utawala wao. 3.1.7 Shujaa huwa Kipenzi cha Wanajamii Hata ikiwa majagina huwa na maadui zao, pia huwa kipenzi cha jamii (umma) na ladha maadui zake huwa na wivu kuona jinsi wanajamii wanavyomchukulia kama mkombozi wao na hivyo kumwenzi na vilevile kutarajia mambo makubwa zaidi kutoka kwake, hasa kuleta mabadiliko yana yotarajiwa kuwapeleka hadi katika ufanisi wa hali ya juu. Si ajabu kuwa wanajamii wengi huhusisha mambo yote mazuri katika jamii na shujaa wao, kwa hivyo, umaarufu wa jagina huenea kila mahali. Fumo Liyongo, alikuwa maarufu sana miongoni mwa jamii Waswahili na hata miongoni mwa watu wengine kutoka jamii zingine. Tunaelezewa haya katika ubeti wa saba wa Uteuzi wa Fumo Liyongo. 58 7 Kimo kawa mtukufu Mpaka sana mrefu Majimboni yu maarufu Watu huya kumwangaliya. Fumo Liyongo alipokamatwa na kutiwa gerezani, Sultani aliomba ushauri kutoka kwa wanajamii kuhusu kuuawa kwake.Wanajamii walijaribu kumtetea kwa kila njia, walisema kuwa badala ya yeye kuuawa, aachiliwe huru na afanywe amiri jeshi. Walimwona kama mtetezi wao dhidi ya maadui zao (beti za 88 na 89 katika Utenzi wa Fumo Liyongo.Habari za kifo chake zilipowafikia Waswahili, walihuzunika sana. Mshairi wa Uteuzi wa Fumo Liyongo ametumia fumbo kwa kusema, imeanguka pazia (ub.226) kumaanisha kuwa jamii imeachwa bila mtu wa kuongoza au kuwaunganisha. Maelezo haya yako katika Uteuzi wa Fumo Liyongo kama ifuatavyo; 224 Make Liyongo hakika Matanga aliyaweka Watu wakasikitika Kwa Liyongo kuifiya 225 Liyongo silaha yetu Kwa wut’e khasimu zetu Alikuwa ngao yetu Wut’e wakinena haya. 59 226 Mui walisikitika Hakuna wa kutosheka Kwa Liyongo kutoweka Imeanguka paziya. Kifo cha Isa kwa mujibu wa Bibilia, kilipoteza matumaini ya watu waliokuwa wakimwamini, ndugu zake pamoja na wanafunzi na wafuasi wake. Watu walilia na kuomboleza pale msalabani kwa kuwa mtetezi wao ametoweka japokuwa waliahidiwa kuwa siku ya tatu atafufuka. 3.1.8 Jina la Shujaa Mara nyingi shujaa hupewa jina linaloakisi hulka, matendo na tabia yake. Huwa ni majina ya kimajazi pamoja na lakabu mbalimbali kwa kutegemea mitazamo ya wanajamii kuhusiana na sifa za jagina wao. Mutiso (1999:16) anasema jagina hupewa jina hili pindi tu anapozaliwa.Yumkini apewe jina la muda na wazazi wake, baada ya kuzaliwa, hadi kufikia pale ambapo ataweza kujitambulisha na kujipa jina mwenyewe au Mungu au kiumbe mwenye uwezo na utambuzi atakapompa jina. Mifano ya majagina wenye majina ya sifa zao ni kama vile, Achillesi (Ujasiri), Orkoiyot (Mwenye nguvu) na Musa (Aliyeokotwa). Fumo Liyongo pia alipewa jina kulingana na sifa zake. Kwa mfano, jina “Fumo” linarejelea mkuki wenye ncha pana mno ambao hutumika kama vita. Fumo pia linaweza kuwa na maana ya kufuma. Alipokuwa kisimani alipatikana akilenga mshale kama anayetaka kumfuma adui wake huku akipiga magoti. Jina Fumo pia linaweza kuwa na maana ya mfalme, kwa sababu baba yake 60 alikuwa mfalme na hivyo, akapewa jina hilo. Katika utenzi huu pia, Liyongo anaitwa simba wa miji na ngao. Allen (1993:228) kama alivyonukuliwa na Gichamba (khj), anaeleza kuwa neno “Fumo” linalofasiriwa kama mwana mfalme lilitumiwa na familia ya kifalme ya Pate kwa jina Nababani, kama neno la heshima na huenda walitoa jina hilo kutokana na jina Fumo Liyongo, baada ya ushindi wao dhidi yake katika karne ya kumi na tano. Liyongo mwenyewe alikuwa mwana wa mfalme na akawa mfalme wa dola ya Ozi.Uteuzi wa Fumo Liyongo pia unatueleza kuwa Liyongo alikuwa ni mtume wa heshima na adabu. Aliitwa na sultani wa Pate afike mjini Pate ili Wagalla wamtazame na alifanya hivyo. Si ajabu kuwa Nabahani walitumia neno “Fumo” kuashiria heshima. Kila jina la shujaa lina siri ya ushujaa kama vile urembo, umaarufu, uganga uchawi, ujasiri n.k. Katika Utenzi wa Nabii Isa, Isa pia alipewa majina mengi kama Rasuli (ubeti 792), Rasili, Mtume (ubeti 347). Katika Bibilia Nabii Isa anitwa Simba wa Yuda, Mshauri mwema, Mwalimu, Emanueli (Mungu pamoja nasi). Sifa hizi zote zinamtambua sifa za nabii Isa Nabii Isa kama Shujaa halisi wa kidini. 3.1.9 Shujaa Huwa na Akili Pevu Mashujaa ulimwenguni huwa wenye akili pevu na kung’amua mambo yaliyofichika. Vilevile, uwezo huu, mara nyingi huwasaidia kunusurika kutokana na njama za maadui zao na kwa hivyo huwawezesha kuishi hadi pale watakapokamilisha majukumu yao katika jamii. Fauka ya hayo, shujaa huweza kutabiri yale ambayo yatatokea baadaye. Isa, shujaa wa wakristo, kwa mfano 61 aliyatabiri mambo mengi ambayo hatimaye yalitokea, kwa mfano, alitabiri kifo chake, kufufuka na hata kupaa kwake mbinguni. Fumo Liyongo naye, akili zake pevu zilimwezesha kuhepa mitego ya adui yake Daudi Mringwari. Sultani wa Pate (Mringwari) alitaka kumwangamiza kwa sababu alihofia kuwa Liyongo angempokonya ufalme wake. Liyongo aling’amua njama hizo na kuhamia mwituni. Maelezo haya yanapatikana katika Uteuzi wa Fumo Liyongo katika beti za 49 na 50. Wadaho na Wasanye walipewa ahadi na sultani ya reale mia moja baada tu ya kumwua Liyongo. Kwa sababu ya ushupavu wake katika vita, Wasanye na Wadahalo walijua kwamba haingewezekana kumuua Liyongo kwa njia ya ana kwa ana. Kwa hivyo walifanya njama ya kumuua kwa hila. Walipoenda bara, walimwendea kwa urafiki wakamwomba awe pamoja nao. Walipanga wawe wakila makoma, hivi kwamba, kwa zamu, kila mmojawao, (akiwemo Liyongo) angepanda juu ya mkoma na kuyatunda makoma. Kila mmoja miongoni mwao isipokuwa Liyongo alitekeleza tarajio la mpango huo. Ikabakia zamu ya Liyongo. Njama yao ilikuwa kwamba, akipanda mkoma wamfume mishale kwa pamoja. Liyongo alitambua nia yao na badala ya kukwea juu ya mkoma, alitumia mishale na kuyaangusha makoma mengi. (Uteuzi wa Fumo Liyongo beti za 136 na 140). Kwa mara nyingine akili arifu ya Liyongo ilimwezesha kuepukana na kifo. Kwa ushairi, alimtuma kijakazi aliyekuwa akimletea chakula gerezani kwamba akamwambie mama yake aupike mkate wa wishwa na humo ndani afiche tupa ili aitumie kukereza minyororo aliyokuwa amefungwa kwayo gerezani. Kila alipotumwa kumpelekea Liyongo chakula kitamu, kijakazi Saada alipokonywa chakula kile na walinzi na kukila. Liyongo alifahamu fika kuwa mkate wa 62 wishwa si mtamu na walinzi hawangetaka kula chakula ambacho si kitamu. Saada alipouleta mkate ule (ukiwa na tupa ndani), askari walimtukana kwa dhihaka na kumruhusu Saada kumpelekea Liyongo mkate ule. Japo ni bayana katika utenzi huu kuwa Liyongo alikuwa na akili pevu, haieleweki ni kwa nini anamfunulia mwanawe siri ya kifo chake, licha ya kung’amua ukweli kuwa mwanawe alikuwa na nia ya kumwua. Tunaambiwa: 136 Babake akamwambiya Wewe kuuliza haya Dhana nimekudhaniya Kuniuwa huzengenya. 140. Akamwambia nayuwa Kijana umefundiwa Na wewe utahadawa Hayo wamezokwambiya Kupevuka kwa akili ya Nabii Isa kunaweza kuthibitishwa na mafundisho aliyoyatoa. Alifunza kwa kutumia vielelezo mbazi ambavyo viliufanya umati uliomfuata kuajabia mafundisho yake. Umati uliohutubiwa na Nabii Isa uliajabia mafundisho ambayo yalitokana na mtu ambaye mwandishi wa Utenzi wa Nabii Isa anadai kuwa hakusoma sana. 544 ‟Kwa maneno ya kutimu, Fasaha na ya ilimu, Kutujuza tufahamu Kuwa yeye ni nabia. 63 546 ‟ Ni mwingi wa taaluma, Wala sana hakusoma Na mambo chungu nzima, Yeye yanamuelea. 3.2.0 Kugura kwa Shujaa Mara nyingi shujaa hutoroka makwao na kuishi ugenini. Mashujaa hufanya hivi ili kuwahepa mahasimu wao ambao mara nyingi huwa ni viongozi. Kwa kuwa majagina mara nyingi huwa na uwezo usio wa kawaida, viongozi wengi huhofia kuwa majagina hawa huenda wakapindua dola zao. Safari ya jagina humtayarisha kutekeleza majukumu au dhima yake katika jamii. Hivyo, safari hizi ni muhimu sana. Mutiso (1999:31), anaeleza kuwa safari ya shujaa inaweza kuwa ya kiwakati, kimahali, kifikra au kisaikolijia. Katika safari ya kisaikolojia jagina huzinduka kutokana na elimu au mawazo mapya anayopata. Baadaye, huwafunza wafuasi wake mambo wanayostahili kutenda na hivyo kubadilisha mfumo wa jamii. Aghalabu shujaa akigura huenda katika nchi au sehemu nyingine, huwa anapata mazingira au hali nyingine tofauti na ya nyumbani. Hivyo, anakuwa na mtazamo mwingine. Wakati mwingine huenda shujaa asirejee kwao baada ya kugura kama alivyofanya Mbega shujaa wa Washambaa aliyegura kutoka kwao Nguu, baada ya jamaa wake kupanga kumuua. Daudi Mringwari yule Sultani wa Pate, alipanga njama ya kumwangamiza Fumo Liyongo. Liyongo alipotanabahi hatari iliyomkuba, alitorokea porini ambapo aliishi na Wasanye na Wadahalo. Sifa ya kugura kwa shujaa haijitokezi vyema katika utenzi huu lakini imeelezewa 64 kikamilifu katika Bibilia. Kama ilivyo desturi ya mashujaa wengi, punde tu baada ya kuzaliwa, Nabii Isa alikutana na vikwazo vya kutaka kuuawa na Mfalme Herode, ambaye alihofia kunyang’anywa madaraka, shujaa huyu atakapokuwa mkubwa (Mathayo 2:13). Malaika wa Bwana alimtokea Yusufu (Baba wa Isa) katika ndoto na kumweleza amchukue mtoto Isa na mama yake (Mariam) kisha wakimbilie Misri. Ndivyo ilivyo hata kwa mashujaa wengine, misukosuko inapozidi kukimbilia uhamishoni. Baada ya Mfalme Herode kufa, shujaa Isa alirudishwa na wazazi wake kwao Galilaya katika mji wa Nazareti. 3.2.1 Mashujaa kwa Kawaida Huwa ni Washairi Mutiso (1999:21), anasema kuwa kila jagina ni mshairi,mwanafalsafa, mwenye elimu (hata kama hajasoma) na mwenye sifa zote za uzuri na ubaya. Ubaya wake huonekana na maadui wake tu. Baadhi ya sifa za jaginani kama vile urembo, ustahamala, usamehevu, umaasumu, ufukara, ujasiri, ufasaha wa kusema, ujanja, ufadhili na sifa zingine nzuri na mbaya. Mara nyingi mashujaa huwa na kipawa cha ushairi. Mshairi, kwa kawaida huwa na falsafa nzito kuhusiana na jamii. Mashairi huwa yanakubaliwa na wanajamii na hivyo hupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mashairi haya huwa zawadi kwa wanajami kwani hudumu hata baada ya kifo cha jagina. Mashujaa wengi hutungiwa nyimbo za kuwasifu zikielezea historia na umuhimu wao kwa jamii. Japo nabii Isa hakuwa mshairi, na hakuna mashairi au nyimbo alizozitunga, mafundisho yake yamesheheni jumbe zenye falsafa nzito. Alifundisha kwa kutumia vigano mbazi na mifano iliyooana na tajriba za aliowafunza na ndiposa kwingineko anadaiwa kama mwalimu kielelezo. 65 Fumo Liyongo alikuwa mshairi stadi. Miehe na wenzake (2004) walikusanya nyimbo na mashairi yanayodaiwa kutungwa na Fumo Liyongo. Mashairi haya yanatupa taswira na hulka ya mtunzi, uhusiano wake na jamii, tajriba yake maishani na hata mila na desturi za jamii ya mtunzi.Fumo alikuwa stadi wa gungu na mwao. Hata hivyo, kama tulivyoona hapo awali, chochote kizuri kinachotukia katika jamii huhusishwa na jagina. Hivyo, kuna uwezekano kuwa nyimbo na mashairi yanayohusishwa na Fumo Liyongo huenda kwa hakika iwe kwamba hakuyatunga mwenyewe. 3.2.2 Maisha ya Shujaa Huwa ni Dhiki Tupu Lengo kuu la jagina huwa ni kuikomboa jamii yake kutokana na madhila yanayoikumba. Katika jitihada hizi, majagina hukumbana na upinzani na mateso ya kila nui kutoka kwa wapinzani wao. Mateso haya huwa ni pamoja na kuonewa, kudhulumiwa, kushtumiwa, kusingiziwa, kusalitiwa na hata kuuawa. Kawaida ulimwenguni majagina huishi maisha ya dhiki kutoka kuzaliwa kwao hadi kufa kwao kutokana na majaribio wanayoyapitia. Kama tulivyoona hapo mbeleni, majagina hutoroka makwao ili kuwaepuka maadui wanaowasaka ili kuwaua au kuwaangamiza.Wakiwa uhamishoni, wanaishi maisha ya upweke. Shujaa huwa haoni raha hasa anapoiona jamii yake ikiteseka na anaweza kufanya lolote kadri ya uwezo wake kuhakikisha kuwa anaikomboa jamii yake kutoka mikononi mwa adui. Matarajio waliyo nayo wanajamii juu ya jagina wao, humkuza na kumtia shime zaidi jagina. Nabii Isa alizaliwa shinani mwa mtende kulingana na utenzi huu. Bibilia kwa upande mwingine, husema kuwa Isa alizaliwa horini mwa ng’ombe kwa sababu wazazi wake walikuwa wamesafiri Bethlehemu kwa sababu ya sensa iliyokuweko na hawangemudu kukodisha chumba cha malazi. 66 Hali hii ni mfano mmoja tu wa kutudhihirishia mazingira ya dhiki ya majagina. Majagina vilevile katika kupambana na wanaoendeleza dhuluma dhidi ya umma wao, inabidi waishi maisha ya mateso na dhiki kuu. Madai ya wahakiki wengi kama Mberia (1989), na Achieng (2012), kuwa majagina wanakumbwa na masaibu mengi na vilevile wana maadui wengi ni ya kweli kwani Nabii Isa katika Utenzi wa Nabii Isa alikumbwa na matatizo mengi, sio kutofautiana kuhusu unabii wake kwa wana wa Israeli, Waisraeli walihitilafiana kuhusu iwapo Isa ni Nabii au sio (beti 528-630), sio njaa akiwa pamoja na wanafunzi wake, sio kusalitiwa kwake na mmoja wa wanafunzi wake (beti 785-790). 3.2.3 Maisha na Matendo ya Shujaa Huwa ni ya Kimiujiza Mdee na wenzake (2011), wanaelezea muujiza kama jambo la ajabu; kioja, shali, nduli au dungudungu. Nayo Kamusi ya Tuki (2004) inasema muujiza ni jambo lisilokuwa la kawaida; shali, ajabu, kioja au dungudungu. Tunakubaliana na maelezo haya kuhusu maana ya neno hili,ila tunaongeza kuwa katika miujiza kuna sifa za uhalisiajabu. Katika Utenzi wa Nabii Isa, baadhi ya matendo ya Nabii Isa yamefanya utenzi huu kupata sifa za kiuhalisia ajabu. Uhalisia ajabu kulingana na Wamitila (2003:274), ni dhana iliyobuniwa na msanii wa Ujerumani, Franz Roh inayohusishwa na sifa mbalimbali za kuyaelezea matukio ya kifantasia au ya kiajabu au kichawi kwa namna ya moja kwa moja kwa namna inayoyafanya yaonekane kama ya kawaida. Anadai kuwa mpaka uliopo kati ya mambo yanayoweza kupatikana katika ulimwengu halisi na yasiyowezekana huwa mdogo sana. 67 Nabii Isa alitenda matendo ya ajabu kama vile kuwawezesha vipofu kuona. Nabii Isa aliwaponya watu wenye macho pofu na kuwafunulia macho yao (ubeti 422, 425). Miujiza hii ya Nabii Isa pia umeangaziwa kwenye kitabu cha Mathayo 9:27-31 ambapo Biblia inaeleza kuwa Yesu alipoingia chumbani, alifuatwa na vipofu wawili waliomlilia na kumwomba kuwa, “Yesu mwana wa Nazareti, tuonee huruma”.Yesu alipowauliza kama walikuwa na imani kuwa angewaponya, walionyesha imani yao kwa kuitikia.Yesu aliwagusa kwenye macho na wakaweza kuona. Nabii Isa aliwaumba ndege kwa udongo aliofinyanga na ndege hao wakaweza kupaa waliporushwa. Baadhi ya sifa hizi ni za kiuhalisia ajabu na zilidhihirisha kuwa Nabii Isa alikuwa na uwezo zaidi kuliko binadamu wa kawaida (beti 452,472). Jambo jingine la kimiujiza alilolifanya Nabii Isa ni kumtajia yule jamaa aliyeuliza chakula alichokila wakati wa asubuhi na chajio, maji aliyoyatumia, pesa za mfukoni na hata akiba ambayo huyo jamaa alikuwa nayo nyumbani. Huyo mtu alipodhibitisha ukweli wa mambo aliyotajiwa, alikosa kinywa cha kusema na baadaye akakubali kuwa kweli Isa ni Nabii (beti 380-382). Kule kuzaliwa kwa Nabii Isa bila baba pia ni jambo la kiajabu kwani ni kinyume na hali halisi katika jamii; Nabii Isa alizaliwa bila mama yake kuonana kimwili na mume, (ubeti 588) ila kwa mtume kumvivia tu Mariyamu nguo na akapata mimba ya mtoto Nabii Isa. Nabii Isa na wanafunzi wake wakiwa jangwani waliomba ili wapate chakula na mwishowe walipewa kutokana na maombi aliyofanya Nabii Isa. Chakula chenyewe kikiwa kinaitwa Maida na kilikuwa kitamu kisichomithilika (beti 746-761). 68 3.2.4 Shujaa Huwa Hawaeleweki kwa Uwazi Watu katika jamii mbalimbali huwa na mitazamo mbalimbali kuwahusu mashujaa wao. Jambo hili linakubalika haswa katika fasihi simulizi ambapo mtu ana huru wa kueleza masuala kwa namna ambayo anaona yanafaa. Mathalani, kila shujaa huwa na adui pamoja na wafuasi wake wanaompenda. Kila jamii kwa hivyo huchukua mielekeo tofauti kuhusiana na usawiri wa majagina. Kila jamii ina uhuru wa kumlimbikizia jagina wake sifa sufufu na hata kuna uwezekano wa wengine kuzitilia sifa hizo chumvi. Lakini maadui zake, huenda wakampatia jagina sifa chache na za kumkashifu na hivyo kuwafanya majagina kuwa na mitazamo mingi ya kuwasawiri. Hivyo basi, kuwafanya kutoeleweka kwa uwazi, maadamu, kuna mitazamo mingi kuhusiana na mashujaa. Hatuna budi kuelewa kuwa mashujaa watabaki katika hali ya kutoeleweka kwa uwazi jambo ambalo katika usomi lina kubalika. Kuna masuala kumhusu Fumo Liyongo ambayo yanazua utata. Kuna baadhi ya watu wanaofikiria kuwa Fumo Liyongo hakuwahi kuishi duniani na kuwa ni mhusika tu wa kubuni katika simulizi za Waswahili. Suala la kipindi alichoishi, mwaka aliozaliwa, sifa alizo nazo yakiwemo masuala mengine ni baadhi ya mambo yanayochanganya hadi leo. Kila maulama anatoa maelezo yake kuhusiana na masuala haya kwa misingi ya mtazamo wake tu. Yumkini shujaa mwenyewe huenda asijulikane asili yake, malengo au dhamira yake, wazazi wake, hususan baba mzazi. Aghalabu mama wa shujaa awe siri pia (kama alivyo mama yake Fumo Liyongo). 69 Nabii Isa vilevile aliwakanganya Wayahudi ambao hawakumuelewa. Kwao walitarajia Masihi ambaye angalikuwa amiri jeshi mkuu ambaye angaliwaongoza katika vita vya ukombozi kutoka kwa Warumi waliokuwa wamewanyanyasa kwa muda mrefu. 3.2.5 Mapenzi ya Mama kwa Shujaa Kwa kawaida jagina hupendana na mama yake kwa dhati na huwa wanashiriki katika mambo mengi ya siri ambayo wanajamii wengine hawafahamu. Mama yake jagina humpa motisha ili atekeleze dhamira yake na huwa kitulizo cha kumliwaza wakati ana dhiki. Wengine huchukulia kuwa mamaye jagina pia ni jagina kutokana na ukaribu wake na jagina. Hata hivyo, huenda asiwe na sifa bia za mashujaa. Kuna dhana ya kisaikolojia ambayo inadai kuwa mwana wa kiume huvutiwa kimapenzi kwa mama yake (Oedipal complex) ilhali mwana wa kike, huvutiwa kimapenzi kwa babaye (Electra complex). Hii humfanya jagina kumwona babake kama adui yake, kwa hivyo hana budi kumwangamiza panapo patikana nafasi. Liyongo walipendana sana na mamaye kiasi cha hata mamaye kuelewa hisia zake za ndani. Liyongo akiwa gerezani, mamaye angemtayarishia chakula kitamu na kumpatia Saada ampelekee. Hata hivyo, kutokana na utamu wa chakula, maaskari walikuwa wakila na kumsazia Liyongo makombo. Baada ya siku kadhaa, Liyongo aligundua kuwa maisha yake yamo hatarini akamtuma Saada kwa kumtongolea shairi au wimbo uliofumbwa na ni mamake pekee ndiye aliweza kuelewa habari hiyo. Hata askari (“makozi” kwa mujibu wa Utenzi wa Fumo Liyongo), hawangeweza kutanzua fumbo lililogubikwa kwenye ufumbo huo. Hayo yote, yalidhihirisha kuwa mamaye Liyongo pia alikuwa mshairi kama mwanawe. Baada ya kupokea ujumbe huo, alifanya jinsi alivyoagizwa na kusaidia kukomesha jaribio la Sultani la kumwua mwanawe. 70 Baada ya Liyongo kupatikana kisimani na kuwafanya watu kutoteka maji, ni mama yake ndiye aliyeitwa ili aende kumrai ili atoke watu wapate kuchota maji. Mamake alimlongolea mashairi ya kumbembeleza akiwa mbali kwani aliogopa na kutetemeka kwa kutowahi kumwona Liyongo katika hali kama hiyo. Liyongo hakuwa na tabia ya kukaidi amri ya mama yake, ndiyo sababu mama yake aliogopa sana wakati huo.Mama yake hakujua kuwa alishakufa.Alifikiria kuwa wanajamii ndio waliokuwa wamekosea mwanawe. Mama yake alieleza (Utenzi wa Fumo Liyongo ub.197 na ub 198) kuwa Liyongo hukasirika kwa nadra sana, lakini akikasirika, hasira zake huwa ni za moyoni. Aidha, baada ya mamaye kugundua kuwa Liyongo alikufa, alilia sana na hatimaye aliandaa matanga ili waombolezaji watoe rambirambi zao. Ukuruba baina ya Nabii Isa na mamake Maryamu unajitokeza kwa bayana zaidi katika Bibilia kuliko katika Utenzi na Qurani. Katika Bibilia, muujiza wa kwanza alioufaanya Isa ni kufuatia shinikizo kutoka kwa mamake. Walikuwa wamehudhuria sherehe ya arusi katika Kana ya Galileya na divai iliyokuwa imeandaliwa wageni ikaisha. Mamake alipoona hivyo akamuuliza asaidia na hapo akageuza maji kuwa divai. Tukio huli pamoja na kuwa Maryamu alikuwa mmoja waliokuwa wakiomboleza baada ya kifo cha mwanawe ni dhihirisho kuwa Nabii Isa alikuwa kipenzi cha mamake. 3.2.6 Kimo na Nguvu za Shujaa Mashujaa kwa kawaida huzaliwa akiwa na nguvu nyingi.Hata hivyo, anaweza kuzaliwa akiwa dhaifu au mlemavu. Mutiso (khj: 12) anasema kuwa ulemavu huu ni onyo kwa wanadamu kuwa “huyu si kiumbe wa kawaida na atakuwa na nguvu nyingi za ajabu baadaye”. Majagina wa 71 kihistoria kwa kawaida huwa majitu amabayo yana nguvu na vimo virefu mno. Vimo hivi virefu ndivyo huwafanya wanajamii wamuajabie jagina wao. Majagina wengine huwa na vimo vifupi kuliko watu wa kawaida na hili ni jambo pia linalowafanya wanajamii kumuajabia pia. Sundiata, jagina wa jamii moja huko Mali alikuwa mwembamba na tena mlemavu lakini alikuwa na nguvu za ajabu. Fumo Liyongo na hata Nabii Isa walidhihiri nguvu za ajabu. Liyongo alidhihiri nguvu za kimwili. Akiwaelezea Wagala kuhusu ushupavu wa Liyongo, mfalme wa Pate anamsifia kwa kusema kwamba alikuwa kama simba, na kwake kutembea usiku na mchana ni mamoja. Kumtokea mtu ghafla kungesababisha mtu huyo kutapa na kulia kwa woga. Kukodoa macho yake kungemfanya binadamu kuzimia. Wagala, ambao pia walikuwa mashujaa wa vita, walicheka kwa dhihaka wakifikiria sultani alikuwa anawafanyia mzaha. Walimwambia sultani kwamba wangependa kumwona Liyongo. Sultani alikubali na akamtumia Liyongo mwaliko. Liyongo alikubali mwaliko na kusafiri hadi Pate. Katika maelezo ya ziara hiyo ya Pate, picha ya Liyongo tunayoipata ni ile ya mtu mwenye nguvu zisizo za kawaida. Kwanza, tunafahamishwa kwamba safari ya kutoka Shaka, ambako alikuwa akiishi Liyongo hadi Pate, ilimchukua siku mbili badala ya siku nne ambazo zingechukuliwa na binadamu wa kawaida. Pili, anafika Pate akiwa amebeba panda tatu ambazo anazipasua nguvu ya pumzi na mapafu yake: Liyongo kenda muini Akipata mlangoni Panda katia kanwani Kivuzia kapasua 72 Kiivuzia hakika Muini wakashtuka Panda ikapasuka Wagala wakasikiya Liyongo asimuhuli Akaipiya ya pili Pandaye isihimili Na ya pili kapasuwa Aidha, picha ya Liyongo kama mtu aliyekuwa na nguvu zisizo za kawaida inajengeka zaidi kutokana na maelezo ya vitu alivyovibeba mkobani katika ziara yake ya Pate. Tunaelezewa kuwa kwenye mkoba wake kulikuwa na vitu kama kinu na mchi, aina tofauti tofauti za vyungu, mafiga, kipeto cha mtama na nazi. Kwa kawaida, Wagala walikuwa mashujaa wa misituni na watu wenye vimo virefu. Lakini tunaelezewa kuwa waliokuwa warefu miongoni mwao walikuwa wanamfika Liyongo magotini. Fumo Liyongo anatofautiana na Nabii Isa katika kimo kwa kuwa kimo cha Isa kilikuwa cha kawaida tu. Lakini alikuwa na nguvu za kufanya mambo ya ajabu kama tuliyoyaangazia katika sehemu ya miujiza ya jagina hapo juu. 3.2.7 Majagina Aghalabu Huwa Magwiji Katika Vita Mashujaa aghalabu huwa magwiji katika vita kwa sababu wanazuka ili kukomboa jamii zao dhidi ya maadui zao. Mashujaa huwa hawaogopi chochote. Ni kutokana na hali ya kivita ndipo 73 ushujaa wao hudhihirika, hususan mashujaa wa kijamii. Samson katika Bibilia, kwa mfano, anasawiriwa kama shujaa wa kivita aliyetumia utaya wa punda na kuwauwa Wafilisti elfu moja (taz. Kitabu cha Waamuzi 15:14-17). Uwezo wake wa kivita uliwawezesha Waisraeli kujikomboa kutoka kwa wafilisti baada ya miaka mingi ya dhuluma na unyanyasaji. Vivyo hivyo, Lwanda Magare, Dedan Kimanthi na Fumo Liyongo miongoni mwa mashujaa wengine walifurahia vita. Fumo Liyongo, Shaka Zulu, Sundiata, Lwanda Magere walizuka katika kipindi cha misukosuko ya kivita. Liyongo aliweza kuwakabili watu wengi kwa wakati mmoja, (Utenzi wa Fumo Liyongo ub 12 na ub. 35). Aidha, Liyongo anajitokeza kama gwiji katika ufumaji wa mishale. Anayafuma na kuyaangusha makoma kwa wingi akiwa chini Liyongo pia anakufa akiwa na mishale mikononi huku akipiga goti moja chini tayari kufuma (utenzi wa Fumo Liyongo beti za 65, 66, 180 na 181), unatoa haya maelezo. Takhmisa ya Liyongo inamsawiri Liyongo kama asiyeogopa mikuki wala mishale na anakiona kifo kama kitokanacho tu na Mwenyezi Mungu. Lakini si kutokana na kufumwa mikuki na mwanadamu. Aidha, Liyongo anasawiriwa kama mtu anayependa vita sana na anajilinganisha na “mwana kozi”. Maelezo haya yanapatikana katika (Takhmisa ya Liyongo katika beti zifutazo: 8, 9, 14, 16, 22, 23 na 24. Kinyume na alivyochorwa Fumo Liyongo, Nabii Isa hakutumia nguvu za kimwili kupigana na maadui wake. Japo amesawiriwa kama mtu jasiri, anapambana na maadui wake kwa vita vya kiroho. 74 3.2.8 Shujaa na Suala la Ndoa Mashujaa duniani kote, kwa kawaida hawaoi na wakioa huwa hawatilii maanani sana swala la ndoa. Hii inatokana na sababu kuwa shujaa huwa na jukumu la kukomboa jamii kutokana na dhuluma pamoja na taabu mbalimbali. Kwa hivyo, ili shujaa atekeleze dhamira yake, ni sharti awe huru. Ndoa kwa kawaida haimpatii mtu nafasi ya kushughulikia mambo mengine lakini shujaa huwa kwa ajili ya jamii nzima. Ni vigumu mno kukosa kuitumikia kwa madai ya kumliwaza mtu mmoja (mke wake) pekee. Matamanio ya wanajamii kuhusu ukombozi wao yako kwa shujaa wao, kwa hivyo, huchukuliwa kuwa shujaa “huioa jamii”. Isitoshe wanawake ndio huwa chanzo cha kuporomoka kwa mashujaa wengi, hata nguli katika kazi bunilizi. Hata hivyo, kuna baadhi ya mashujaa ambao huoa, japo ndoa yao mara nyingi haiwi dhabiti kwa sababu, jagina huwa hatulii mahali pamoja. Kimathi shujaa wa Wakikuyu, kwa mfano alioa na kuacha familia yake alipoingia msituni kutetea jamii yake. Ajabu ni mpaka leo hakuna anayejua kaburi lake liliko, kwa sababu alishikwa na mabeberu kuuawa. Fumo Liyongo kama alivyo Lwanda Magere alikuwa na wanawake wengi. Tunaelezewa katika Utenzi wa Fumo Liyongo (ub. 45 na ub. 46) kuwa Wagalla walimpa mke aliyechukua mimba na hatimaye kujifungua mwana wa kiume. Katika mashairi yanayodaiwa kutungwa na Liyongo, tunaelezwa kuwa alikuwa na mpenzi wake kwa jina Kundazi. Pia tunaarifiwa kuwa Liyongo alitilia maanani sana umuhimu wa mwanamke katika maisha ya mwanamume. Katika Utumbuizo wa Mwana Mnazi, Liyongo anatoa mfano kwa kumtumia mwanamke aliyekuwa mpenzi wake. Anasema kuwa yeye ndiye “mpangua hamu na simanzi”. Tunaona 75 kwamba Liyongo anapochelewa kufika nyumbani kipenzi chake aliwaambia vijakazi Saada na Rehema waandae chakula kizuri na kisha waende wakamtafute. Aidha kipenzi chake alienda hatua ya kumlisha akisaidiana na kijakazi wake mwingine katika Utenzi wa Mwana Ninga, utenzi ambao unadaiwa kutungwa na Liyongo. Liyongo anasifu sehemu mbalimbali za mwanamke kuanzia utosini na kuteremka hatua kwa hatua hadi nyayoni. Inadaiwa kuwa mwanamke huyo pia alikuwa mpenzi wa Liyongo. Kinyume na Fumo Liyongo, Nabii Isa hakuoa wala kupata watoto na hivyo kuingiana na sifa kuwa majagina wengi huwa hawaoi. 3.2.9 Kifuasi cha Shujaa Mara nyingi shujaa huwa na vifuasi ambavyo huandamana navyo. Vifuasi hivi ni muhimu sana maishani mwa mashujaa mbalimbali. Sahaba wa shujaa yumkini anaweza kuwa mnyama, kijana, dhana fulani, ndege, mti, mdudu, jiwe, kitu, mjinga na kwa nadra sana mwanamke. Kifuasi hawi na kazi muhimu sana bali kumsaidia shujaa kutekeleza lengo lake na yamkini apandishwe cheo kuwa shujaa baada ya shujaa kuwa mgonjwa, kufa au kupotea. Wanawake wengi huwa shujaa kwa sababu ya upelelezi au kwa mapenzi yao juu ya shujaa. Mashujaa halisi wa kike aghalabu walipatikana katika mfumo wa Ujima. Jambo hili linaonyesha vile wanawake wamekandamizwa kihistoria. Vifuasi husaidia katika kumkamilisha shujaa. Werner (1968: 133) anaeeleza kuwa Mbega shujaa wa Washambaa, aliandamana na mbwa wengi kila mahali alipoenda. Alikuwa anawafundisha mbinu za usasi wa nguruwe, wakiwemo wanyama wengine wa porini. Kuna mbwa fulani aliyempenda sana aliyejulikana kama “Chamfuu”. Anaendelea kudai kuwa jina hili limehifadhiwa na wanajamii hiyo hadi leo. Mbwa huyo alimsaidia Mbega sana katika usasi wa 76 nguruwe. Baada ya usasi, aliwapa wanajamii nyama ya nguruwe kwa wingi. Wanajamii walifurahi na kumwajabia. Bali na hayo, Mbega alikuwa na mkoba uliokuwa na hirizi ambazo alitumia kutenda mambo yasiyo ya kawaida. Mtume Musa shujaa wa Waisraeli naye alikuwa na kijiti alichokitumia kutenda miujiza katika harakati za kuwakomboa wana wa Israel kutoka huko Misri. Kijiti hiki hata kilikuwa kikigeuka nyoka wakati mwingine (taz kutoka 4:1–5 kwenye Bibilia takatifu). Aidha Yesu Kristo, alidaiwa kuandamana na Roho mtakatifu (taz Luka mtakatifu 3:22 kwenye Bibilia). Roho Mtakatifu alimwezesha kutenda miujiza pia. Fumo Liyongo ni vivyo hivyo. Fumo Liyongo kwa mfano alikuwa na mkoba aliopenda kubeba kila mahali aliopenda. Ndani ya mkoba huu mlikuwa na vitu kadhaa ikiwemo mishale aliyotumia vitani. Tunaelezwa katika Utenzi wa Fumo Liyongo kuwa katika ushirika wa kikoa, aliubeba mkoba ambao ulikuwa na uta na mishale (taz ub 65). Alipopatikana akiwa amekufa, alikuwa tayari ametia mshale kwenye uta huku akiwa tayari kufuma (Utenzi wa Fumo Liyongo) ub.180 na ub.181. 3.3.0 Shujaa Huhusishwa na Zaidi ya Jamii Moja Jagina mara nyingi hatambuliwi na kuhusishwa tu na watu wake bali pia na watu kutoka jamii zingine. Hata hivyo, jagina wa kijamii hujitolea kufa kupona ili kuilinda jamii yake na mara nyingi huwa karibu na jamii yake kuliko jamii nyingine ile. Huitetea kwa vyovyote ingawa hushirikiana na wafalme wa jamii nyingine katika kuimarisha hali ya amani, utangamano na kuendeleza maisha ya raia wake hadi kwenye ufanisi. Ni jambo la kawaida kupata baadhi ya 77 watu wakidai kuwa shujaa fulani hutoka katika ukoo wao. Madai haya yanakuwepo kwa sababu kila mtu, kama kaida ya watu hupenda kujihusisha na mtu maarufu au yule ambaye anafanya vitu visivyo vya kawaida au miujiza na kwa sababu hiyo, kila jamiii pia hupenda kujihusisha naye. Majagina wa kidini kwa mfano, Mtume Muhammadi, Isa (Yesu) na Buddha walikuwa si wa jamii moja bali wa ulimwengu mzima. Licha ya Yesu Kristu kutoka katika ukoo wa Daudi, alichukuliwa na Wakristo wote kama mkombozi wao. Aidha mtume Muhammad ni shujaa wa waislamu wote duniani naye Buddha ni shujaa wa wahindu wote duniani. Licha ya Fumo Liyongo kuwa shujaa wa Waswahili, Wasegeju, Wabajuni na Wapokomo pia hudai kuwa Fumo Liyongo alikuwa ni shujaa wao. Nurse (1994:69), anaeleza katika mahojiano yake na mmojawapo wa wabajuni, kuwa Fumo Liyongo alikuwa Mbajuni. Werner (1915:333) naye anadai kuwa alifahamishwa na mmojawapo wa kijumbe mtoa habari kuwa Fumo Liyongo alikuwa Msegeju. Watu wa kawaida hufa na kusahaulika baada ya miaka michache. Wanajamii huwa hawaamini kuwa shujaa wao ameaga na wengi huchukulia kuwa ameenda safari na kuwa atarudi siku moja. Kwamba utafiti huu unahusu mashujaa walioishi zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita ni idhibati tosha kuwa majagina huwa hai miongoni vizazi na vizazi. Fumo Liyongo na Nabii Isa watazidi kufanyiwa utafiti sio tu na watu kutoka jamii zao, bali pia na watafiti kutoka pande mbalimbali za ulimwengu. Wengi wa majagina wa kihistoria na wale wa kidini kama Buddha, Muhammad na Isa miongoni mwa wengine, hukumbukwa daima. Kila jamii inawajibika kuwafunza watoto kuwahusu 78 mashujaa wao, ambao huzuka katika katika vipindi na hali mbalimbali katika jamii hiyo. Jamii moja huenda ikawa na zaidi ya jagina mmoja lakini ni muhali kwa mashujaa wawili kuzuka katika hali na kipindi kimoja katika jamii. Aidha, katika kukumbukwa mashujaa hutungiwa nyimbo, tenzi, mashairi, pia, maandishi chungu nzima hutungwa kwa maumbo mbalimbali na kuhifadhiwa kama kumbukumbu kwa minajili ya vizazi vijavyo. Inaaminika miongoni mwa wakristo na waislamu kuwa kuwa Nabii Isa atarudi ulimwenguni kuikamilisha kazi alioianzisha. 3.3.1 Usaliti na Kifo cha Shujaa Dhana ya usaliti imejitokeza sana katika kazi za kifasihi na inaonekana kuwa ni silaha ya kumwangusha shujaa mfano Lwanda Magere katika kitabu cha Lwanda Magere, Samsoni na Yesu katika Bibilia. Mtoto wa Liyongo anamuuliza babaye siri ya nguvu zake, anapoambiwa kuwa ni kuchomwa sindano ya shaba kitovuni, anakubali kumchoma baba yake. Hatimaye Liyongo anakufa, kisha mwanawe naye anakufa kutokana na uovu wake. Baada ya shujaa Liyongo kufa watu walisikitika, waliomboleza na wengine walionekana kukata tamaa kwa kuwa shujaa huyu alikuwa ni mtetezi wa watu katika jamii. Beti za 224-226 zinaeleza vizuri jinsi watu walivyomwomboleza shujaa wao. Kwa upande mwingine dhana hii ya usaliti ina sura mbili yaani faida (anayenufaika baada ya usaliti) na hasara (anayeathirika baada ya usaliti). Kifo cha shujaa pamoja na usaliti vinatupatia motifu ya dhambi na mapatilizi. Ingawa mtoto wa Liyongo alimsaliti babaye ili apewe zawadi nono, hakutimiziwa ahadi hizo. Alinyanyaswa na hatimaye alikufa kama alivyokufa baba yake. Hii inaashiria kuwa katika mapigano kati ya wema na uovu, siku zote wema hushinda. 79 Jagina hudhurika mahali pamoja tu, kwa silaha ya aina moja tu au kwa njia ya kipekee tu (pia mara nyingi huweza kuponeshwa kwa silaha ya aina moja au kwa njia ya aina moja tu). Kwa mfano, ni sindano ya shaba tu amabayo ingeweza kumwua Fumo Liyongo. Katika Utenzi wa Nabii Isa, usaliti unajitokeza pale ambapo Nabii Isa pamoja na wanafunzi wake waliishi, kula na kunywa pamoja lakini baadaye mmoja miongoni mwa wafuasi wake ndiye aliyemchochea kwa kumtaja kwa wahalifu waliotarajia kumwua (beti 785-790). Nabii Isa alipangiwa njama ya kuuawa, jambo ambalo Mola alibadilisha kwa kuleta mtu ambaye alimfananisha na Nabii Isa kisura na baadaye mtu huyu akateswa, akasulubiwa msalabani na wahalifu wale wakidai kuwa huyu alikuwa ni Nabii Isa mwenyewe. Mutiso (1999:37) anasema kuwa majagina huwa hawaamini ya kwamba wanaweza kudhurika. Anadai kuwa si ajabu wao kuamini ya kwamba wataishi milele. Wanapopoteza imani hii, (yakutodhurika au kufa) wao huamua ya kwamba hakuna lingine ila watafute kisingizio cha kufa kwao. Anasema wao huamua kufa kikondoo au kuhatarisha maisha yao kwa sababu kifo ni muhimu kuliko maisha. Husema ya kwamba kufa kwao kulikuwa kumebashiriwa au kifo chao ni wokovu kwa ulimwengu mzima na jambo hili ni sharti alitekeleze Mungu. Isa alipaa mbinguni kwa mujibu wa Utenzi wa Nabii Isa. Wakristo wanaamini kuwa kifo cha Isa kilitabiriwa kwa kuwa Mungu aliamua kuwarudia tena wanadamu, lakini Yuda Iskariote ndiye aliyepelekea kifo hiki kutokea. Alimsaliti Isa kwa Wayahudi kwa ahadi ya vipande thelathini vya fedha. Kama ilivyokuwa kwa shujaa Liyongo, Isa naye alisalitiwa na mtu wa karibu (mwanafunzi wake). Yuda aliyemsaliti Yesu, baada ya kupewa vipande thelethini vya fedha, alimbusu Yesu, na Wayahudi, Waandishi na Mafarisayo wakamkamata, wakamsulubisha mtini na kumtesa hadi 80 alipokufa. Wakristo huamini kuwa kifo cha Isa msalabani ndicho gharama ya dhambi na kwamba yeyote amwaminiye na kumfuata, atapata maisha ya milele. Baada ya Isa kuuwa msalabani, pazia la Sinagogi lilipasuka mara mbili na hata kukaingia giza mchana.Ishara hizi zinaingiana na sifa kwamba vifo vya majagina huwa vya kimiujiza. Taswira ya kifo cha shujaa Isa kinajitokeza kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo: Kwanza Wayahudi, Waandishi na Mafarisayo waliona kama wamemkomoa kwa kuwa walidai kuwa anajikweza kwa kujifanya mwana wa Mungu. Pia watawala walifurahi maana watu wengi walimfuata na kumsikiliza. Kifo cha Fumo Liyongo kinatofautiana na cha Nabii Isa katika Bibilia kwa kuwa Isa alifufuka baada ya siku tatu ilhali Liyongo hakufufuka. 3.3.2 Anamoishi Jagina na Kurudi Kwake Safari ya Mwisho Shujaa Isa ni jagina wa kidini kama tulivyotangulia kusema. Mutiso (1999:39), anadai kuwa majagina wa kidini kwa kawaida huhubiri kuwa kuna ulimwengu mwingine ambao waliotenda matendo mema huenda baada ya mauko yao. Ulimwengu huu hauna matatizo, ila ni raha na shibe. Anaendelea kusema kuwa makazi haya katika dini ya Usiva huitwa Kilaisa, katika Ukristo ni mbinguni na katika Uislamu ni peponi. Ulimwengu huu ni ruwaza ya utakatifu, utulivu, amani, raha, uhuru, maisha ya milele, umoja, upenda, kutosheka, utangamano, na kila jambo nzuri. Mutiso (khj), anasema kuwa mahali hapa ndipo makao ya miungu, Mungu na majagina (kabla na baada ya kufa). Ni majagina, miungu na Mungu ambao wanaweza kufika huko. Ni hadi siku ya mwisho tu ambapo waliofuata sheria za 81 jagina wataweza kuingia mahali hapo. Mahali hapa viumbe wote huishi kwa utangamano, kama hapo mwanzoni. Wajibu wa jagina, hasa wa kidini ni kutoka katika ulimwengu huu wetu na kwenda katika ulimwengu mwingine au kuja katika ulimwengu wetu au kufanya yote mawili. Hii ni safari ya mwisho ya jagina. Ndio wakati wa kuwahukumu wale wote ambao hawakufuata sheria zae duniani na kuwaongoza wale waliomtii katika kuingia makazi ya raha mustarehe. Ndio wakati wa kuwafufua wafu na kuwaadhibu vikali wawi. Wakristo na Waislamu wanaamini kuwa Isa atarudi tena duniani kuikamilisha kazi alioanzisha ulimwenguni.Wakristo huamini kuwa anakaa kwenya upande wa kuume wa Mungu na kwamba atarudi duniani kuwahukumu wanadamu kulingana na matendo yao. Waliomkubali na kufuata nyendo zake, wataungana naye mbinguni na walioenda kinyume na mafundisho yake wataenda Jahanamu. Fumo Liyongo hakuwa jagina wa kidini na katika utafiti wetu, hatukupata habari zozote zunazozungumzia habari zake baada ya kifo na kuzikwa kwake katika sehemu ya Kipini. Kifo cha jagina ni sharti kionekane pigo kubwa kwa dunia nzima.Fumo Liyongo alipokufa Waswahili walisikitika sana kwa kumpoteza jagina wao. Kwa siku kadha Waswahili hawakuweza kuteka maji kisimani, kwa kuwa walidhani Fumo Liyongo alikuwa hai na alikuwa anawazuia kuteka maji. Wafuasi wa Isa pia walitamaushwa na kifo cha isa na Bibila inatoa maelezo kuhusu kusikitishwa kwa wanafunzi wake waliojifungia nyumbani na kuongea katika sauti za chini. 82 3.4 Hitimisho Katika sura hii, tumebainisha kuwa shujaa Isa na Fumo Liyongo wanafanana kwa njia zifuatazo; kuwa wote wanatumia nguvu isiyokuwa ya kawaida kutenda mambo ya ajabu (miujiza), walikuwa na ushirikiano mzuri na jamii zao, walipendwa na watu kiasi cha watawala kuwachukia, walifanyiwa njama za kuuawa, wote walisalitiwa na watu wao wa karibu, baada ya kufa watu waliwaombolezea, wasaliti wa mashujaa wanaahidiwa kupewa fedha, vyeo na mali nyingine baada ya kukamilisha kazi ya usaliti mfano Mfalme anaahidi kuwapa Wasanye, Wadahalo, Waboni na Watwa reale mia iwapo watamleta kichwa cha Liyongo. Pia mwanawe Liyongo anaahidiwa mali, mke na cheo cha uwaziri. Pia Yuda aliahidiwa vipande thelathini vya fedha iwapo atafanikisha kukamatwa kwa shujaa Isa.Waliowasaliti shujaa Liyongo na Isa walikufa baada ya kifo cha mashujaa hao. Hawakuwa waoga, wote ni majasiri. Kutofautiana kwao kunajitokeza kwa kuwa Fumo Liyongo alitumia nguvu ya uganga au sihiri. Hadhuriki kwa chochote isipokuwa kwa kudungwa sindano ya shaba kitovuni. (Ubeti 143 -144) Nabii Isa alitumia nguvu za Roho Mtakatifu kutenda mambo mbalimbali k.v, kutembea juu ya maji, kuponya watu wengine (Mathayo 3:13-17, Mathayo 4: 23 -25). Liyongo alioa mke na alikuwa na mtoto wa kiume, ana nguvu za kirijali ilhali Isa hakuoa wala hakuzaa. Baada ya kufa, Liyongo hakufufuka. Nabii Isa kwa mujibu wa utenzi hakufa ila alipaa mbinguni. Katika Bibilia, Isa alifufuka na aliwatokea watu mbalimbali ili kuwadhihirishia kwamba yuko hai (Marko 16:1-14). Japo alikufa, wafuasi wa Isa wanaamini kuwa kazi ya kuwakomboa wanadamu ilikamilika kwa kuwa kila anayemwamini anaokolewa na kupatanishwa na Mungu
>>>>>>>>>ITAENDELEA>>>>>>>>>