SURA YA PILI HISTORIA YA FUMO LIYONGO



SURA YA PILI
HISTORIA YA FUMO LIYONGO NA NABII ISA PAMOJA NA ILE YA JAMII ILIYOWAZAA NA KUWAKUZA 2.0 Utangulizi Majagina huzuka katika mfumo na hali fulani mahsusi za kijamii, kama tulivyodokeza katika sura ya kwanza. Hivyo, ni muhimu kuielewa historia za jamii walimopatikana Fumo Liyongo na Nabii Isa. Historia hii itachangia katika kuwaelewa mashujaa hawa kwa kina hususan, maisha yao, mazingira na hali zilizowazaa pamoja na vipindi vya wakati walipozuka. Hivyo, katika sura hii tumeangazia vipengele vya maisha yao, kama vile miondoko yao, vitushi walivyovitenda na mahusiano kati yao na wanajamii wengine. Tumemulika mitafaruku ya kisiasa ya jamii zilizowazaa. Tumeangazia vilevile, historia ya Waswahili, na pia ile ya Wayahudi, katika vipindi mbalimbali kama vile, kabla ya kuzuka kwa majagina hawa, vipindi walimoishi na hata baada ya vifo vyao. 2.1 Historia ya Waswahili Historia ya Waswahili imeundwa kutokana na visasili pamoja na visakale vilivyopitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya utambaji. Fasihi simulizi kama vile visasili na visakale vilisaidia pakubwa kuunda historia ya Kiswahili. Aidha, wazungu kama vile Werner (1915), Dammann (1940), Sutton (1966), Nurse (1994), Knappert (1970 na 1970) Lyndon (1962), Greenville (1954 na 1955), Allen (1977), Spear (1985), miongoni mwa wengine walikusanya tamaduni za Waswahili kutoka kwa wenyeji wa pwani na kuzihifadhi katika maandishi. Vilevile, mwanaakiolojia Chitick (1984), kutokana na uchimbaji wake wa kitaalam wa maeneo kama Gedi, Manda na Pate yaliyoachwa kama mahame au magofu kutokana na misukosuko mingi 25 iliyotokea katika eneo la pwani hapo awali, pia umechangia pakubwa katika uelewaji wa baadhi ya tamaduni za watu waliokuwa wakiishi katika maeneo hayo. Chittick (1984) katika uchimbaji wake alikusanya vyombo kama vile, vyungu, mifupa, mbao, vyombo vya mawe, vioo, shanga, vifaa vya vyuma, sarafu n.k.Vifaa hivi vinasaidia katika uelewaji wa tamaduni za jamii za pwani na Waswahili wa awali pamoja na historia zao. Visasili vya jamii jirani na Waswahili kama vile, Wapokomo, Wasegeju na Wamijikenda na hata maandishi ya awali ya watalii wa kwanza kabisa kuzuru maeneo ya pwani na Afrika Mashariki yalichangia pakubwa. Mathalan, kijitabu cha The Periplus of the Erythrean Sea, kilichoandikwa baina ya karne ya kwanza na ile ya tatu baada ya Kristo na Mgiriki asiyejulikana kwa jina, kilichangia pakubwa katika uelewaji wa historia ya Waswahili. Kitabu hiki, kwa mujibu wa Sutton (1966:6), kinaelezea baadhi ya sehemu za upwa na bahari ya Hindi zikiwemo sehemu za bandari zilizoko katika bahari ya Shamu na Ghuba la Aden, pamoja na maelezo kuhusu safari za mashua kuelekea Uhindi zikitegemea pepo za misimu (pepo za Kaskazi na Kusi). Mgiriki huyu aliurejelea Upwa na Upembe wa Afrika kama Azania. Kijitabu hiki kilikuwa nguzo muhimu katika maelezo ya Ptolemy kuhusiana na Jiografia ya Upwa wa Afrika Mashariki. Waswahili ni Wabantu. Asili ya Wabantu ni katika eneo ambalo hivi sasa linakaliwa na nchi ya Cameroon na eneo la Mashariki mwa nchi ya Nigeria. Nurse na Spear (1985) wanadai kuwa baadhi yao walihamia katika janibu za Kusini mwa Afrika, ilhali wengine wakiwemo Waswahili, walihamia Mashariki na kukalia eneo la Shungwaya.Wanadai kuwa Khoisan (Bushmen na Hottentots) ndio walikuwa jamii ya awali kabisa katika eneo la Afrika Masharaki, kabla ya Wabantu, Wakushi na Wanailoti kuhamia kutoka hivyo, kabla ya kuwasili kwa Wabantu katika 26 maeneo ya Afrika Mashariki, Wakushi wa kusini tayari walikuwa wakimiliki maeneo haya kwa mujibu wa Nurse na Spear (khj 45) . Walsh (1987:21), akinukuliwa na Gichamba (2005:26), anaeleza kuwa wazungumzaji wa lugha ya Sabaki waliotoka katika sehemu zilizoko kwenye meaneo ya Kaskazini Mashariki ya Tanzania, walipokuwa wakipitia kwenye maeneo yaliyokuwa yamekaliwa na kumilikiwa na Wakushi hao, hawakuwa na maathiriano wala maingiliano kati yao. Walsh (khj: 21) anadai kuwa Wasabaki walitengana na Wabantu wengine katika eneo la Kaskazini mwa nchi ya Tanzania na kuelekea katika maeneo ya Kaskazini katika kipindi cha karne ya kwanza baada ya Kristo. Mwishoni wa karne ya kwanza, kutoka eneo la Wasabaki lilitengana katika makabila tofauti tofauti kama vile, Waswahili, Wapokomo, Waelwana na Wamijikenda. Baada ya kipindi kifupi, Waswahili walihamia sehemu za Kusini mkabala wa bahari ya Hindi. Hata hivyo, Wamijikenda, Wapokomo waliwafuata tu baadaye. Ni katika kipindi hiki ambapo Wakushi waliokataa kumiliki maeneo ya kusini waliingiliana na Wabantu na baadhi yao wakasilimishwa kuwa Wabantu. Tamaduni za jamii mbalimbali za Waswahili zinadai kuwa kugura kwao hadi katika maeneo ya Pwani kulitokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Wagalla. Stilahi (1981:858) akinukuliwa na Gichamba (2005:26), anadokeza kuwa Wabajuni katika tamaduni zao wanadai kwa yakini kuwa Wagalla ndio waliowafukuza kutoka eneo la Shungwaya. Aidha, Werner (1915:328) anashadidia kwa kusema kuwa mashambulizi mara kwa mara ya Wagalla ndiyo yaliyowafanya Wasabaki kukimbilia katika sehemu za Kusini. Hata hivyo, mashambulizi haya hayakusita hata baada ya kuhamia pande za kusini. Nurse (1994:48) anadai kuwa magurio ya Waswahili na Wabantu wengine kusini zaidi yalizidishwa na vamio la ghafla la Waarabu. 27 Mashambulizi haya yaliwafanya Wabantu kuhamia katika eneo lililoko baina ya Juba kati ya eneo la kusini mwa Wabantu, kuhamia katika eneo lililoko baina ya Mto juba, ulio kati ya eneo la Kusini mwa Somalia na mto Tana. Katika maeneo ya pwani, Waswahili walijikusanya katika makundi madogomadogo kwenye visiwa na sehemu nyingine mbali kidogo na ufuko. Walitapakaa pwani kote kuanzia Somalia na kuteremka hadi Msumbiji, mazingira yao ya bahari na mito ikiwatumbukiza katika shughuli za uvuvi. Kwa hivyo, walijingiza katika utengenezaji wa mitumbwi, jahazi, makasia, nyavu, nyugwe, nk. Bali na uvuvi, kama njia ya kiuchumi, shughuli zingine za asili za kibantu zilikuwa pamoja na ufugaji wa wanyama kama vile, mbuzi, ng’ombe, kondoo na kuku. Kilimo cha mpunga, malenge, mtama, nazi, mboga na matunda, mawele na jamii ya kunde kama vile njegere na maharagwe, pia kiliendelezwa na Waswahili. Ndizi na yugwa zililetwa hapo baadaye kutoka sehemu za kusini mashariki ya bara la Asia. Shughuli za uhunzi ziliwawezesha kuunda na kutengeneza zana za kilimo kama vile mashoka, majembe, panga na visu. Vifaa hivi vilitumiwa kufyeka mashamba bikira, kupanda, kuvuna na kupalilia. Isitoshe, walishughulika na uudanji wa zana za kivita kama mishale, nyuta, mafumo, vitara, jambia, ngao, misu na panga. Baadhi ya vifaa vingine walivyoviunda ni pamoja na vinu, mchi, kamba, vyano vya kupepetea na vinoo/tupa. Useremara pia uliendelezwa ili kuunda baadhi ya vifaa vya nyumbani. Mandhari ya bahari yaliwezesha usafiri au safari ya Waswahili kutoka sehemu moja hadi nyingine katika shughuli mbalimbali kama vile, shughuli za kibiashara na kuwatembelea jamaa zao. Aidha, wageni kutoka maeneo mengine ya ulimwengu walifika hadi pwani ya Afrika Mashariki, Mazingira haya yalileta mabadiliko makubwa katika utamaduni na muundo wa 28 kijamii ya Waswahili, kisiasa na kiuchumi. Wageni wa awali katika maeneo haya walikuwa ni wafanyi biashara, wasomi (wanajiografia), wamishenari na watalii walioabiri mashua. Hao wageni walitoka sehemu kama vile, Uarabuni, Ghuba ya Uajemi, Uhindi, Ugiriki, Ureno zikiwemo sehemu nyingine ulimwenguni haswa maeneo ambayo yamepakana na fukwe za bahari. Wareno walifika baadaye, na mwisho kufika walikuwa Waingereza waliokuwa na nia ya kujitwalia maeneo muhimu pamoja na kusambaza dini. Miongoni mwa waandishi na wanajiografia wote wa kiarabu wa enzi za kati (baina ya miaka 1100 – 1500) wanaoirejelea Afrika Mashariki, Freeman Greenville (1954 – 1955:1) akinukuliwa na Gichamba (2005:28), anadai kuwa hakuna mwandishi aliyeitembelea pwani ya Afrika Mashariki ambayo kwa sasa inajumuisha pwani za Somalia, Kenya na Tanzania ila tu Muhammed ibn Abdallah ibn Batuta ambaye aghalabu hujulikana kama ibn Batuta. Uhusiano wake na wenyeji, ustaarabu wake na uelewa wa mandhari ya Afrika Masharaki ulisaidia pakubwa kuelewa historia ya watu wa pwani ya Afrika Masharaki. Wafanyi biashara walisaidiwa na pepo za Kusi na Kaskazi katika safari yao ya kuja na kuondoka pwani mtawalia.Waarabu,Wahindi na Wajemi walitumia msimu wa pepo za Kaskazi zilizokuwa zikianza kuvuma katika mwezi wa Novemba hadi mwezi wa Februari ili kufika pwani ya Afrika Mashariki. Baada ya shughuli zao za biashara kukamilika, walirudi makwao kwa pepo za Kusi zilizoanza kuvuma baaada ya pepo za Kaskazi kutua. Bidhaa kama mbao, dhahabu, pembe za ndovu, magome ya kobe, watumwa waliotekwa kutoka bara, rangi za nguo, manukato, miongoni mwa bidhaa zingine zilinunuliwa na wageni waliofika 29 pwani ya Afrika Mashariki kwa shughuli ya biashara. Waswahili nao, walinunua bidhaa kama majora ya vitambaa, vyungu, shanga za vioo, vitara, vyombo vya vioo vya nyumbani, mvinyo, shaba na ngano miongoni mwa bidhaa zingine kutoka kwa wageni hao. Vijiji vilianza kupanuka na kuwa miji tu biashara ilipozidi kushamiri. Miji ilikuwa kama vile Mogadishu, Lamu, Pemba, Unguja, Malindi, Barawa, Kilwa, Gedi, Pate nk. Baadhi ya wageni kama vile Waarabu walikuja na familia zao na kustakimu katika eneo la pwani. Allen (1993:7), anadai kuwa Waajemi na Waarabu ndio waliokuwa waasisi wa ustaarabu katika eneo hilo. Walikuwa wakitumia pepo za misimu katika bahari ya Hindi ili kufika pwani ya Afrika Mashariki kwa muda wa miaka elfu mbili au zaidi. Fauka ya biashara, Waarabu walichukua Waswahili kuwa makafiri kwa sababu ya imani zao katika mapango, sayari za anga ya juu, nyota jua hata mwezi. Kwa sababu hiyo, walisambaza dini ya kiislamu. Dini ya kiislamu ilikuja na athari zake katika janibu hizo ambapo hadi sasa baadhi ya watu hawawezi kubainisha kati ya Uislamu (dini) na Uswahili (utamaduni wa Waswahili), matambiko na sherehe nyingine, mathalan, Maulidi zinahusishwa na Uislamu. Katika mpito wa vipindi mbalimbali vya kihistoria, jamii ya Waswahili imekuwa na hali, misukosuko ya kila aina na mafarakano yaliyozuka na kusababisha vita kati ya jamii ya Waswahili wenyewe. Vita hivi vilisababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali. Aidha, mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa majirani hasa walioishi bara kama vile Wasanye (Waboni), Walangulo, Wadahalo, Wagalla na Wasegeju yalikithiri. Mitafaruku hii ilitokea baina ya karne ya kumi na mbili na karne ya kumi na tano ambapo Waswahili walikuwa na taabu na 30 maisha yao kuvurugika kiasi cha kumtaka mtu wa kuwaongoza na kuwaunganisha. Ni kwa sababu hii, ndipo shujaa wao, Fumo Liyongo akazuka. 2.2 Historia ya Fumo Liyongo Fumo Liyongo alizuka kutokana na misukosuko ya kivita iliyokuwa imeshamiri katika upwa wa Afrika Masharaki kwa muda mrefu. Maelezo yake yanapatikana hapa na pale na yametokana na tamaduni za jamii mbalimbali za pwani. Hata hivyo, kuna ukuruba au uwiano wa aina fulani kuhusiana na maelezo tofautitofauti ambayo yalipitishwa kwa muda mrefu kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya utambaji. Kuna maandishi chungu nzima ambayo yameandikwa na maulama mbalimbali kumhusu Fumo Liyongo. Isitoshe, kumekuwepo na mijadala mirefu kuhusu iwapo shujaa huyu wa Waswahili aliwahi kuishi na ikiwa kweli aliishi, kama alikuwa na sifa ambazo amepewa. Kwetu sisi, hatuna shaka kwamba Fumo Liyongo aliwahi kuishi na kwamba alikuwa na sifa za kipekee - sifa zilizokuwa tofauti na zile za wanajamii wengine. Yumkini, sifa hizi zinaweza zikatiliwa chumvi katika maandishi ya kifasihi yanayomsawiri na hii ni kaida ya mashujaa wote duniani. Shujaa hukuzwa na wanajamii ambao humwona kama kiumbe wa ajabu mno. Licha ya hayo, tumeyadokeza mazingira na hali ya kijamii ambayo ilimzua Fumo Liyongo. Hali kama hii hudhihirika katika uzukaji wa majagina wengine duniani. Mengi ya maandishi ya awali yanayomhusu Liyongo yalikusanywa na Wazungu kana vile: Werner (1915), Dammann (1940), Sutton (1966), Nurse (1994), Knappert (1970 na 1970) Lyndon (1962), Greenville (1954 na 1955), Allen (1977), Spear (1985) miongoni mwa Wazungu wengine. Waafrika wa awali walioandika masuala kumhusu Liyongo, kwa mfano Muhammad Kijumwa (katika Utenzi wa Fumo Liyongo), walifanya hivyo kwa hisani ya Wazungu ambao 31 walikuwa wakifanya utafiti kuhusu Liyongo. Wazungu walikusanya fani mbalimbali za fasihi simulizi ya Kiswahili na kuzitia katika maandishi. Miehe na wenzake (2004:8) wanaeleza kuwa, licha ya juhudi za Wazungu za kukusanya tamaduni kumhusu Liyongo na kuziweka katika maandishi, Waafrika wachache kama vile Ahmed Nabahany na Ahmed Nassir pasipo utegemezi wa Wazungu wamefanya juhudi za kukusanya na kuweka katika maandishi baadhi ya tamaduni za watu wa Lamu na Mombasa zikiwemo tamaduni kumhusu Liyongo. Haijulikani kwa yakini ni lini Liyongo alizaliwa lakini wasomi wanakisia kwamba aliishi takribani kati ya karne ya kumi na tatu na kumi na tano. Liyongo hakuwa shujaa wa Waswahili tu, bali anatajwa pia katika utamaduni, kwa mfano wa Wapokomo. Ikumbukwe kwamba, Waswahili walioona na baadhi ya majirani zao na kwa hivyo, mengi ya makabila yalidai kuwa Liyongo alikuwa shujaa wao. Ni kawaida kwamba, mwanadamu yeyote duniani hupenda kujihusisha na mtu ambaye ni maarufu. Mamake alijulikana kwa jina Mwana Mbwasho ilhali babake alikuwa Mringwari wa kwanza. Kijakazi wake alikuwa Saada na anadhihirika mno katika tungo ambazo zinadaiwa Liyongo amezitunga. Mpenzi wake alijulikana kwa jina Kundazi. Kwa mujibu wa Miehe na wenzake (khj: 5), tamaduni kumhusu Liyongo na jamaa wake wa karibu kama vile mamake, kijakazi chake, mpenziwe na mpinzani na adui wake mkubwa kwa jina Daudi Mringwari, zimehifadhiwa akilini mwa watu wa pwani, na zimekuwa sehemu muhimu ya urithi wa utamaduni wa kitaifa wa Kenya na hata Tanzania, Isitoshe, kiini cha utamaduni wa Liyongo huhusishwa na nyimbo za sifa na uchezaji ngoma na nyingi za nyimbo hizi bado zipo kwenye fikra za wazee waliokoma wa Mombasa na Lamu. 32 Wapokomo katika tamaduni zao wanadai kuwa Liyongo alikuwa mtawala wa dola ya Ozi (katika karne ya kumi na tano) iliyokuwa katika upande wa chini wa Mto Tana, (kuna madai kwamba Liyongo alikuwa akitembelea ufuko wa mto Tana ili kufua nguo zake pamoja na kuoga), lakini baadaye alipinduliwa na dola ya Pate na ufalme wake kutwaliwa (Allen 1993:95). Mji mkuu wa dola hii ulikuwa Shaka kwa mujibu wa Tarihi ya Pate, Inadaiwa kuwa Liyongo alipanua ufalme wake kutoka Malindi hadi janibu za Wapokomo, eneo ambalo ni mkabala na hori la kisiwa cha Pate. Liyongo mwenyewe, kama mtawala wa dola hii, hakupendwa na Wapokomo. Jambo hili lillitokana hasa na kodi aliyowatoza. Vijiji vikubwa vilitozwa kodi ya wasichana wawili na wavulana wawili, ilhali vijiji vidogo vilitozwa kodi ya msichana mmoja na mvulana mmoja kutoka kila kijiji, miongoni mwa kodi zingine na hasa kutoka kwa mazao ya kilimo. Hali hii ya kumchukia inadhirika katika maelezo ya Hadithi ya Liyongo (Steere 1970:339 – 452). Katika hadithi hii anasawiriwa kama mtu mbaya-aliyekuwa anawaudhi watu sana. Hadithi hii ilisimuliwa kwake Steere na Hamisi wa Kayi (Khamis bin Abubakar) huko Unguja. Hata hivyo, utamaduni wa Waswahili unadai kuwa Liyongo alipendwa sana na watu. Hali hii inadhihirika katika Utenzi wa Fumo Liyongo, pale ambapo baada ya kifo chake, watu wengi walisikitika na kuhuzunika. Hata hivyo, kama ilivyo kawaida ya wanadamu kote duniani, si watu wote walihuzunika. Maadui zake walifurahia kwa vile tisho lao kubwa lilikuwa tayari limeondolewa. 33 2.3 Misukosuko ya Kivita Iliyomzua Fumo Liyongo Jamii ya Waswahili awali ilipitia taabu na misukosuko mingi. Vita mbalimbali vimeelezwa haswa katika visasili na visakale vya jamii ya Waswahili wakiwemo majirani zao kama Wagalla, Wasegeju na Wapokomo kuhusika. Biashara ya watumwa iliyoendelezwa na Waarabu ilisababisha mitafaruku katika jamii mbalimbali zikiwemo za bara na za pwani. Waarabu waliokuwa na bunduki na panga waliwashika na kuwateka nyara Waafrika na kuwasafirisha hadi eneo la Mashariki ya Kati zikiwemo sehemu nyingine ulimwenguni. Aidha, Waarabu walishirikiana na baadhi ya Waafrika kuwasaidia katika shughuli zao za utekaji wa watumwa kutoka bara. Watumwa hawa walifunganishwa kwa kamba au minyororo shingoni. Hatimaye walisafirishwa kwenye mazingira yenye hatari mno wakiwa wametwikwa baadhi ya bidhaa kutoka pwani. Nyumba zao zilichomwa kwa moto na watoto wao kuuawa. Wengi wa mateka hawa walijifilia njiani. Waliokuwa hawajiwezi kwa sababu ya uchovu au ugonjwa walitumbukizwa baharini wakiwa wamefungwa kwa kamba na minyororo miguuni au mikononi. Maelezo haya ni kwa mujibu wa Mbotela (1934). Shughuli za utekaji wa watumwa ilikuwa ni sababu ya vita vya mara kwa mara kati ya Waarabu na wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki, Waswahili wakiwemo, na hata watu wa bara. Licha ya hayo, jamii za Waswahili kutoka sehemu mbalimbali zilipigana vita.Wafalme wa dola mbalimbali walichukua kila hatua kuimarisha utawala wao. Kwa mfano Utenzi wa Fumo Liyongo unaeleza kuwa Daudi Mringwari (binamuye Liyongo), alihofia Fumo Liyongo angefanya mapinduzi dhidi ya utawala wake, kwa hivyo, alifanya njama zilizomwangamiza 34 Liyongo. Sutton (1966:18-19) anaeleza kuwa kati ya miaka 1200 na 1500B.K, kulikuwepo na ugomvi, mitafaruku na mashambulizi baina ya dola mbalimbali au baina ya makundi yaliyokuwa yakizozana katika dola hizo. Anaendelea kusema kuwa masultani wa awali wa Kilwa walikuwa na matatizo na majirani zao. Anadai kuwa hata Tarihi ya Pate inatueleza kuhusu mapigano, uporaji na mapinduzi katika visiwa vya Bajuni ukiwemo umwagikaji mwingi wa damu na uharibifu wa mali katika kisiwa cha Pate. Pia, Malindi ilizozana na Mombasa hadi baada ya Wareno kuingilia kati kwa kutumia bunduki ambapo uporaji mkubwa ulitokea katika mji wa Mombasa. Kumekuwa na madai kuwa kudorora kiuchumi na kisiasa kwa mji wa Kilwa mwishoni mwa karne ya kumi na nne kulilingana na kuinuka kwa mji wa Pate kulisababisha utekaji katika maeneo mbalimbali ya pwani kutoka Mogadishu hadi katika Visiwa vya Kirimba vilivyo pande za Kusini. Majirani wa Waswahili pia kama tulivyodokeza awali, walikuwa tisho kwa usalama na utangamano wa Waswahili. Mashambulizi haya hayakutelelezwa dhidi ya Waswahili pekee bali pia Wapokomo, Wasegeju na makundi mengine ya Wamijikenda. Kwa mfano, Wagalla wanaelezwa katika tamaduni mbalimbali katika janibu za pwani kama watu wakatili. Hata baada ya Wagalla hao kuwatimua Waswahili na makundi mengine kutoka Shungwaya, bado waliwafuata hadi sehemu za Kusini na kuzidisha mashambulizi yao. Werner (1915:328) anatoa mfano wa Wasegeju na Wakauma waliotoroka makao yao ili kuhepa Wagalla waliokuwa wakatili na wenye nguvu za kivita. Anadokeza kuwa baadhi ya Wapokomo walitekwa na Wagalla na kufanywa watumwa wao. Tamaduni za Wapokomo hata hivyo, zinaeleza kuwa Wapokomo wengine walijificha mashimoni karibu na fuo za mito kisha Wagalla waliokuja kulisha mifugo yao walifumwa na mishale yenye sumu. Hatimaye, Wagalla walitorokea sehemu 35 za chini za mto.Wapokomo nao wakawafuata mara tu usiku ulipoingia kwa kutumia mitumbwi midogomidogo na kuwaua. Baada ya mauaji, walificha mitumbwi yao chini ya mto kwenye mchanga. Baadaye Wagalla walichoka na vita kisha wakajaribu kufanya urafiki na Wapokomo. Kila kundi hatimaye liliapa kutolishambulia lingine. Kwa mujibu wa tamaduni za Wamijikenda na Waswahili, nyumba zao (Waswahili) awali zilikuwa zimeezekwa kwa nyasi kwenye paa na hata kwenye pande zake. Kwa hivyo, ilikuwa rahisi kwa Wagallla kuwafuma mikuki kutoka nje walipokuwa wakilala. Allen (1993:218), anadai kuwepo kwa hadithi mojawapo kuhusu kijiji cha hapo awali ya Wagiriama kwa jina Kaya Murikwa iliyokuwa na nyumba za sampuli hiyo ambayo ilishambuliwa na Wagalla kikatili, kisha ikabadilishwa jina kuitwa Kaya Mwijo (Kaya ya dhahabu). Wagalla waliwashambulia majirani zao kwa sababu nyingi. Kwanza ilikuwa ni fahari yao walipoona mikuki ikipasua ngozi nyororo na kisha kufanya maadui kuwa maiti. Pili, walitaka kutwaa mifugo yao. Werner (1915:335) anaeleza kwamba Wagalla walipowaona Wapokomo wakiwa na ng’ombe wengi, hawakufurahia hadi walipowachukua ng’ombe hao na kuwafanya Wapokomo kuwa watumwa wao. Ni bayana kuwa misukosuko ya kivita iliyoshuhudiwa na Waswahili pamoja na jamii zingine kutoka pwani ilihitaji mtu wa kutoa uongozi au wa kujitambulisha naye na hata kuwakinga kutokana na mashambulizi ya maadui zao. Aidha, palihitajika mtu wa kuwaunganisha Wapokomo, Wasegeju na jamii nyingine za pwani kama familia moja ndiposa bali na Waswahili kujitambulisha na Fumo Liyongo, hata Wapokomo, Wasegeju na jamii zingine za pwani wanamtambua Fumo Liyongo kama shujaa wao hata katika tamaduni zao. 36 2.4 Historia ya Wayahudi hadi Kuzaliwa kwa Nabii Isa Asili ya watu wa Israeli ambao wanaitwa Wayahudi pia ni Abraham, mwanawe Yitshak, na mjukuu wake Ya`aquub (Israili). Wote hawa waliishi nchi ya Kanaani, ambayo ilikuja kujulikana kama Israili.Jina Israil linalotokana na nabii wa Mwenyezi Mungu Ya`aquub. Mwenyezi Mungu aliwatumia wana wa Israeli mitume wengi sana, mmoja baada ya mwingine. Kati yao, nabii aliyejulikana zaidi kuliko wote alikuwa ni nabii Musa, ambaye aliteremshiwa kitabu cha Taurati ambacho kilikuwa na hukumu za dini yao na desturi zao kama vile umma wa Muhammad uliteremshiwa Qurani tukufu. Baada ya nabii Musa, walifuatia mitume wengine wakihukumu kufuatia kile Kitabu cha Taurati.Baada ya Musa, akatumwa nabii Daudi na kuteremshiwa kitabu cha Zaburi. Wana wa Israil walikuwa wakaidi Mungu na mitume wake, wenye khiyana na vilevile walikuwa wadanganyifu. Hivyo, waliwakadhibisha baadhi ya mitume wao na baadhi yao wakawauwa bila haki. Baada ya Nabii Musa kuwaokoa wana wa Israil kutoka kwa Firauni ambaye aliwaadhibu kwa adhabu za kila nui, walipokuwa njiani wakienda nchi ya ahadi (Falastina), walikutana na watu wakiabudu masanamu, na wakamwomba Musa awatengenezee masanamu kama hayo ili nao wapate kuyaabudu badala ya kumwabudu Mungu wao aliyewaokoa. Baadaye, walimwomba mtume wao awaonyeshe wamuone Mwenyezi Mungu wazi wazi ili wapate kumwamini mtume wao Musa. Ombi hilo liliwasababishia mola kuwaadhibu kwa kuwauwa na umeme wa radi na wengi wakafa. Lakini baadaye aliwahuisha wote ili wapate kumshukuru. 37 Allah alipotaka kuwafungulia nchi takatifu (L-Qudsi) kwa mikono yao kutoka kwa majabari, walikataa wakati kupambana nao kama walivyoamrishwa na badala yake wakamwambia Musa aende na mola wake akapigane na wao wangojee pale.Mungu alitaka kuwaangamiza lakini nabii Musa alimwomba awasamehe. Hivyo, Mungu akawaadhibu kwa kuwaharamishia wasiingie nchi takatifu kwa miaka arubaini. Baada ya kukamilisha hiyo miaka arubaini, Mungu akataka waingie ile nchi takatifu chini ya uongozi wa mtume Youshua baada ya nabii Musa kufa huku wakiwa wamenyenyekea na kwa kuomba msamaha. Lakini walivunja amri ile na wakaingia kwa kiburi na ukaidi. Mwenyezi Mungu alighadhabika na akawaangamiza kwa kuwatumia ugonjwa wa tauni uliowauwa watu sabini elfu kwa saa moja kwa sababu ya ukaidi wao. Wakati wa zama za Mtume Hezaqiil walipoamrishwa kupigana vita, walitoka idadi kubwa majumbani mwao wakakimbilia jangwani kwa kuogopa mauti. Mungu aliwaua lakini baadaye kwa fadhila zake juu yao, aliwahuisha baada ya mtume wake kuwaombea na wakapata kujua kwamba kufa si lazima kutokane na kupigana vita tu. Kisha baadaye, Mwenyezi Mungu aliwatumia Nabii Ilyaas. Nabii huyu aliwaita katika ibada ya Mungu mmoja na kuwahimiza waache ile ibada ya masanamu. Waliukataa mwito wake na wakataka kumuuwa. Alipokata tamaa kwamba hawatamwamini, akamwomba mola wake na Mungu akawaadhibu kwa njaa kwa kuifunga mvua kwa miaka mitatu. 38 Mungu baadaye, aliwatumia nabii Al-Yasa`a aliyewaita katika ibada ya Mungu mmoja kwa sheria aliyokuja nayo Ilyaas na wakamwamini na kumtukuza. Baada ya L-Yasa`a akaja nabii Dhil-Kifl. Wakaendelea na hali ile ile kama walivyokuwa kwa nabii L-Yasa`a. Lakini baadaye wakavunja ahadi zao na kumfanyia makosa. Wakati ule, walikuwa na Tabuut (Sanduku la Taurati) walilokuwa wakirithiana tokea wakati wa nabii Musa. Walipozidisha uasi wao, Mwenyezi Mungu akawapa nguvu L-`Amaalika wakawanyang`anya sanduku hilo mpaka wakati alipotumwa nabii Shamueli. Baada ya hapo Mwenyezi Mungu aliwatumia nabii Daud na nabii Suleiman na manabii wengi wengineo kama Nabii Uzeir na Nabii Zakaria na Yahya waliowaua, na mwishowe Nabii Issa waliyemuudhi na kutaka kumuuwa, lakini Mwenyezi Mungu alimpaza mbingu 2.5 Misukosuko ya Kivita Iliyowakumba Wayahudi Abdilatif abdalla katika utangulizi wa Utenzi wa nabii Isa anakariri kuwa utenzi huu unahusu kuzaliwa kwake nabii Isa, kupawa kwake utume, misukosuko kadha wa kadha aliyoipata katika kuwalingania watu wake – Mayahudi, ili wamuandame na kuiandama njia ya uongofu, kuhitilafiana kwa mayahudi juuu ya kumuamini nabii Isa na kujaribu kwao kutaka kumuua.Wayahudi kama watu na taifa walipitia misukosuko mingi mikononi mwa mataifa mengine kama tutakavyoonyesha hapa chini. Katika mwaka wa 587 K.K, jeshi la Babiloni walingia mji wa Jerusalem, wakaliharibu hekalu na kuwateka nyara Wayahudi na kuwahamishia nchi ya Babiloni. Mwaka wa ndio ulileta mabadiliko katika historia ya eneo hili. Kuanzia mwaka huu na kuendelea katika miaka iliyofuata, nchi hii ilitawaliwa na mataifa yenye uwezo zaidi, moja baada ya lingine kuanzia 39 Babiloni, Shamu, Ugiriki, himaya za Roma na Byzantini, Ufalme wa Ottoman na Uingereza. Katika mwaka wa 587 K.K, Wayahudi walitawaliwa na Babiloni, na chini ya utawala huu, hekalu la kwanza liliharibiwa. Kati ya mwaka wa 538–333 K.K, chini ya utawala wa Shamu, hekalu la pili lilijengwa baada ya Wayahudi waliotekwa nchini Babiloni walirejea makwao. Nchi hii ilitwaliwa na majeshi ya Ugiriki chini ya Alexander katika mwaka wa 333 K.K. Kati ya mwaka wa 333 na 63K.K, hekalu la pili. Jeshi la Warumi likiongozwa na Tito lilivamia Jerusalem na kuliharibu hekalu la pili. Wayahudi walishikwa mateka na kuhamishwa ughaibuni. Katika mwaka wa 132, Bar Kokhba alipanga vita vya kuususia utawala wa Warumi, lakini aliuawa katika vita vya Bethar katika milima ya Judea. Kutokana na haya, Warumi waliamua kuumaliza utambulisho wa Wayahudi kabisa katika nchi yao. Walifanya hivi kwa kubadili jina la jiji la Jerusalem na kuliita Aelia Capitolina na Judea kuitwa Palestina (jina hili lina asili ya Kirumi). Wayahudi waliosalia walihamia katika miji ya Kaskazini ya Galilee. Baada ya utekaji wa Warumi, Wayahudi walihamia Uropa na Afrika Kaskazini. Wakiwa ughaibuni waliendelea na dini na tamaduni zao. Masaibu haya waliyoyapitia Wayahudi wakiwa kwao nchini na ugenini kuliwafanya wamtamani shujaa aliyetabiriwa na Nabii Isaya katika Agano la kale. Walimtarajia Masihi ambaye walimwamini angekuwa shujaa wa kivita, ambaye angewapigania kutoka kwa maadui wao, na kuuanzisha ufalme ambao haungekuwa na kikomo. 40 2.6 Historia Ya Nabii Isa Utenzi wa Nabii Isa ni kisa kinachohusu maisha ya Mariyamu Binti Imrani ambaye baada ya kuzaliwa katika familia ya Imrani na mamake waliabudu msikitini kila mara, alichukuliwa na mtume Zakaria aliyeishi naye kwa mafunzo mengi ya kidini na hata kumlea kwa ibada kila mara msikitini. Kabla ya Mariyamu kukutana na mtume wa Mungu aliyemtabiria kuhusu kuzaliwa kwa Nabii Isa na kumvivia nguo na baadaye akapata mimba ya mwana ambaye ndiye Nabii Isa bila kuonana na mume yeyote kimwili. Utenzi huu ni utenzi uliojikita katika mafundisho ya dini ya Kiislamu kuhusu maisha ya mtume Isa. Hivyo, Nabii Isa katika utenzi huu amechorwa kwa njia sawa na alivyosawiriwa katika Qurani tukufu. Ingawa Waislamu sawa na Wakristo wanakiri pia vitabu vitakatifu vya Torati, Zaburi na Injili, katika ibada wanatumia Qurani tu na kwa kawaida ndiyo chanzo chao cha habari juu ya watu na matukio ya kabla yake. Mengi ya matukio haya yanaoana na jinsi yalivyoangaziwa katika Bibilia. Kwa mintarafu hii, tutaangazia historia ya Nabii Isa kama alivyosawiriwa katika Utenzi wa Nabii Isa, na vilevile kwa kurejelea Qurani tukufu pamoja na Bibilia ili kushadidia historia hii. Qurani iliandikwa miaka 600 hivi baada ya Kristo na ina aya 93 zinazomhusu Nabii Isa, lakini haileti mfululizo wa habari za maisha yake wala za mafundisho yake maalumu. Nabii Isa kwa Waislamu ni mtume anayeaminiwa kuwa mmojawapo wa mfululizo wa mitume na manabii watukufu 124,000 wa Mwenyezi Mungu walioletwa ulimwenguni kuwapasha wanadamu ujumbe wa upweke na umoja wake, ili wamuabudu akiwa ndiye Muumba na mruzuku wao hapa duniani. Mitume na manabii hawa wameletwa katika zama mbalimbali na kwa watu, kaumu na umma 41 mbalimbali, na mfululizo huu ulianza na Adamu, baba wa wanadamu wote, hadi Mtume Muhammad akiwa ndiye wa mwisho. Nabii Isa(anayefahamika kama Yesu Kristo na Wakristo) ni miongoni mwa mitume wakubwa kama Nabii Nuhu, Ibrahimu, Musa na Muhammad, ambao Mwenyezi Mungu amewasifu kwa subira yao na ustahimilivu wao mkubwa: Tena ni miongoni mwa Mitume waliopewa Kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kiitwacho Injili. Kuzaliwa kwa Nabii Isa, kama ilivyo kwa majagina wengi, kulikuwa kwa kulikuwa kwa kimiujiza. Nabii Isa alizaliwa na bibi Maryam bila ya baba, kwa amri ya Mola wake ambaye alimtuma malaika Jibrili, kumtangazia kumpata mtoto mtukufu. Kama tutakavyoona hapa baadaye, kuzaliwa kwa majagina wengi huwa kumetabiriwa. Qurani pamoja na Bibilia zinatoa maelezo kuhusu utabiri uliofanywa na nabii Isaya kuhusu kuzaliwa kwa Nabii Isa. Utabiri huu unatimia miaka mia nne baadaye. Kwa mujibu wa Bibilia, utabiri wa nabii Isaya ulitimia katika kitabu cha Mathayo 2:1, ambapo inaeleza kuwa shujaa alizaliwa huko Bethlehemu ya Uyahudi, zamani za Mfalme Herode. Kama ilivyo desturi ya mashujaa wengi wa kidini, baada tu ya kuzaliwa, alikutana na kikwazo cha kutaka kuuawa na Mfalme Herode ambaye alihofia kunyang’anywa madaraka, shujaa huyu atakapokuwa mkubwa (Mathayo 2:13). Malaika wa Bwana alimtokea Yusufu (Babake Isa) katika ndoto na kumweleza amchukue mtoto Yesu na mama yake (Mariam), kisha wakimbilie Misri. Ndivyo ilivyo hata kwa mashujaa wengine misukosuko inapozidi, kugura au kukimbilia 42 uhamishoni. Baada ya Mfalme Herode kufa, shujaa Yesu alirudishwa na wazazi wake Galilaya katika mji wa Nazareti. Baada ya kuzaliwa, Nabii Isa, kama walivyo baadhi ya majagina, alisema utotoni mwake akiwa bado mchanga, huu ukiwa ni muujiza mwingine kwa watu ili kuwaonyesha kuwa yeye si mtoto wa kawaida, na kuwa mamake hana dhambi ya kuja kwake bila ya baba. Huu ni mfano mmoja katika mifano minne ya uumbaji aliyoonyesha Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu alimuumba Adamu bila ya baba wala mama, akamuumba Hawa bila ya mama, akamuumba Isa bila ya baba, na akawaumba wanadamu wote waliobakia kutokana na baba na mama. Habari za kuzaliwa kwake Nabii Isa zinapatikana katika Qurani, Surat "Maryamu" (19) kuanzia aya 16 - 35. Na mtaje Maryamu katika Kitabu, pale alipojitenga na jamaa zake mahali upande wa mashariki.Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea Roho wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu. (Maryamu) akasema: Hakika mimi najikinga kwa Mwingi wa Rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mcha Mungu. (Malaika) Akasema: Hakika mimi ni mwenye kutumwa na Mola wako ili nikubashirie tunu ya mwana aliyetakasika. Akasema: Nitampataje mwana hali mwanamume yeyote hajanigusa, wala mimi si kahaba? (Malaika) akasema: Ni kama hivyo! Mola wako mlezi amesema: Haya ni mepesi kwangu! Na ili tumfanye kuwa ni Ishara kwa watu, na Rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo lililokwishaamuliwa. Basi akachukua mimba yake, na akaondoka nayo mpaka mahali pa 43 mbali. Kisha uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende; akasema: Laiti ningelikufa kabla ya haya, na nikawa niliye sahaulika kabisa! Pakatangazwa kutoka chini yake: Usihuzunike! Hakika Mola wako amejaalia chini yako kijito kidogo cha maji! Na litikise kwako hilo shina la mtende, utakuangushia tende nzuri zilizo mbivu. Basi kula, na kunywa, na litue jicho lako. Na pindi ukimwona mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwenyezi Mungu ya kufunga; kwa hivyo leo sitasema na mtu. Akenda naye (mwanawe) kwa jamaa zake amembeba. Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu! Ewe dada yake Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba.Akawaashiria (mtoto).Wakasema: Vipi tumsemeze aliye bado mdogo yumo katika mlezi? (Mtoto) akasema: Hakika mimi ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu. Amenipa Kitabu, na amenifanya Nabii. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo. Na ameniusia Sala Na Zaka maadamu ni hai, Na nimtendee wema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri, mwovu.Na amani iko juu yangu siku niliyo zaliwa, na siku nitakayo kufa, na siku nitakayo fufuliwa kuwa hai. Huyo ndiye Isa mwana wa Maryamu. Ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka.Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa Na mwana, Subhanahu, Yeye ametakasika! Anapolihukumia jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa. Nabii Isa aliletwa kwa wanadamu kufikisha ujumbe kwao wa kuwafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja, hana mwenzake, na kuwa yeye pekee ndiye mwenye kustahili kuabudiwa kwa haki, na ujumbe huu ndio ujumbe uleule uliotumwa kwa Mitume na manabii wote kwa wanadamu ili kuwaongoza, naye alikuja kutilia mkazo na kusisitiza jambo hili na kuzipa nguvu 44 tume za mitume na manabii waliopita. Kadiri ya sura ya 3 aya ya 50 alisema ni "msadikishaji wa yale yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na ili niwahalalishieni baadhi ya yale mliyoharimishiwa, na nimewajieni na Ishara kutoka kwa Mola wenu, kwa hiyo mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii". Alitabiri kuwa baada yake atakuja mmoja ambaye atawafundisha wanadamu ukweli wote na kuwaongoza kwenye haki na kuwaeleza kila wanalolihitaji katika maisha yao. Ujumbe wake ulikuwa ni wa mwisho kabla ya ule wa mtume Muhammad ambao ndio wa mwisho kabisa kwa wanadamu wote.Mwenyezi Mungu ameleta mitume na manabii wengi ulimwenguni, lakini alichagua baadhi yao na kuwateremshia vitabu vya uongozi na sharia na hekima kwa wafuasi wao. Katika vitabu vilivyoteremshwa kwa Manabii mbalimbali ni Taurati kwa Nabii Musa, Zaburi kwa Nabii Daudi, Injili kwa Nabii Isa, na Qurani kwa Nabii Muhammad. Kitabu cha Nabii Isa kiliteremshiwa Wayahudi ambao ndio walengwa wake wa kwanza wa Nabii Isa, kama ilivyothibitishwa na Qurani wakati aliposema: Enyi Wana wa Israili! Hakika Mimi Ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninayethibitisha yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria Mtume atakayekuja baada yangu jina lake ni Ahmad! Lakini alipowaletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio wazi! Majagina kwa kawaida hufanya miujiza au mambo ya ajabuajabu. Nabii Isa alipewa na Mwenyezi Mungu miujiza mbalimbali kumsaidia katika kazi yake ya kutangaza dini ya Mwenyezi Mungu, kwani ilikuwa ni kawaida kwa Mtume au Nabii kuonyesha miujiza kwa watu 45 au kaumu yake ili awathibitishie kuwa yeye kweli ni mjumbe aliyeletwa na Mola wa ulimwengu huu. Mitume waliomtangulia Nabii Isa, kama Nuhu na Ibrahim na Musa na wengine walikuja na miujiza mbalimbali. Baadhi ya miujiza ya Nabii Isa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu ni kuumba ndege kutokana na udongo, kuponyesha vipofu wakaweza kuona, na kuwaondoshea ukoma wale wenye ukoma, na kuhuisha mtu aliyekufa, na kuwateremshia wafuasi wake chakula kutoka mbinguni ili iwe ni dalili kwao wote. Ingawa Isa alichukua muda mwingi msikitini katika ibada (beti 289, 299), wengi bado hawakuacha kutenda maovu na kila asubuhi hao walitafuta njia ya kuhalalisha ibada haramu ya kuabudu masanamu (ubeti 310). Licha ya kufanya miujiza, wana wa Israeli walihitilafiana iwapo yeye ni nabii au la. Hili jambo lilileta upinzani mkali miongoni mwao na wengi walizua njama ya kumuua. Moja kati ya sifa bia za majagina ni kwamba wanakumbana na usaliti kutoka kwa aila au watu walio karibu sana na wao. Shujaa Isa alifanya huduma kwa muda wa miaka mitatu kisha akafa. Wakati wa huduma ya kuwakomboa watu na dhambi zao, wapo Wayahudi waliomkubali na kumfuata na wengine walimchukia na kumshutumu kuwa alikufuru kwa kujiita mwana wa Mungu.Wale waliomchukia ndio waliofanya njama za kumuua. Hatimaye walimtumia mmoja wa wanafunzi wake aliyeitwa Yuda kwa kumpa vipande thelathini vya fedha ili amsaliti kisha wamkamate. Yuda aliwaambia, nitakayembusu ndiye, na hapo ndipo Wayahudi walipomkamata shujaa huyu na kumsulubisha hadi kifo chake (Marko 14:10-72 na 15:1-37). Baada ya siku tatu, alifufuka na kupaa juu mbinguni ambapo wakristo wanaamini kuwa anakaa katika upande wa kulia wa Mungu baba na kwamba atarudi hapa duniani kuwahukumu walio hai na waliokufa. Qurani inatoa maelezo tofauti kuhusu kifo cha Isa kwani inasema kuwa Isa alichukuliwa na mola 46 wake na kupandishwa kwake mbinguni baada ya Wayahudi kutaka kumuua, na kwa hivyo hawakuweza kumuua wala kumsulubu. Waislamu pamoja na Wakristo wanaamini kuwa Isa atarudi tena ulimwenguni kukamilisha kazi yake aliyoiacha baada ya kupaa kwenda kwa Mola wake, na haya yanaelezwa katika vitabu vya dini vya Kiislamu na vya Kikristo.Muhimu hapa ni kujua kuwa sawa na umma wa majagina, waumini wa Isa katika dini zote mbili wanaamini kuwa atarudi tena duniani kukamilisha kazi aliyopewa na Mwenyezi Mungu. 2.7 Hitimisho Katika sura hii, tumeangazia historia, vipindi walivyoishi na mazingira yaliyowazaa mashujaa Fumo Liyongo na Nabii Isa.Kama tulivyotangulia kusema shujaa huzuka ili kutatua tatizo fulani linaloisibu jamii au umma wake. Katika sura hii tumeonyesha ni kwa nini majagina hawa walizuka wakati walipozuka na matarajio ya umma wao. Katika sura inayofuata, tutalinganisha kufanana na kutofanana kwa majagina hawa wawili kwa mujibu wa sifa bia za majagina.


>>>>>>>>>ITAENDELEA>>>>>>>>>>>
Powered by Blogger.