TASWIRA YA JAGINA KATIKA TENDI: ULINGANISHI WA FUMO LIYONGO
Meyer (1993 na 2010), anaeleza kuwa nadharia hii huhusishwa sana na uhakiki wa visasili.
Anadai kuwa wahakiki wa visasili hujishughulisha na ruwaza ambazo hujirudiarudia na ambazo
hudhihirisha maana bia na tajriba za kimsingi za binadamu licha ya wakati au mahali
wanamoishi. Kwa jumla, sifa, taswira, na mada zinazojumlisha maana na tajriba hizi ndizo
hujulikana kama vikale. Vikale hushirikisha ishara bia ambazo huibua hisia na athari nzito
kwenye akili laza ya msomaji wa fasihi.
Katika uhakiki wa kifasihi, vikale hutumiwa katika ruwaza ya aina za wahusika au taswira
ambazo zinafanana katika tungo mbalimbali za kifasihi na pia katika visasili na mitindo anuwai
ya kijamii. Kufanana katika maswala haya anuwai huchukuliwa kuakisi seti ya ruwaza bia
ambazo zimekuwepo tangu jadi. Nadharia ya uhakiki wa vikale kwa hivyo inaeleza kuwa
binadamu wote ni sawa popote walipo. Tofauti ni ndogo za kufikirika ambazo husababishwa na
tofauti za kihistoria na za kimazingira.
Kwa mujibu wa Mutiso (1999:2), vikale kwa jumla hurejelea ruwaza za kimsingi. Ruwaza za
jumla au bia za aina moja au nyingine ambazo aghalabu hudhihirika katika jamii za watu
mbalimbali duniani. Anashikilia kuwa vikale humvuta msomaji vikitumiwa vizuri katika kazi ya
fasihi.
Waitifaki wa nadharia ya vikale wanashikilia kwamba umaarufu wa kazi ya sanaa unatokana na
wahusika, maudhui na taswira zinazorudiwarudiwa katika kazi husika. Baadhi ya wahusika
wanaotumiwa kudhihirisha vikale ni kama: jaribosi au nguli anayeandaa safari ambayo mara
15
nyingi huanzia utotoni hadi anapofika utu uzima ambapo safari hii inaweza kuwa ya kikweli pale
nguli anajizatiti kukisaka kitu au kujisaka mwenyewe. Katika nadharia ya vikale, mkinzani wa
nguli huwa ni mhusika wa kikale ambaye hujifunga kibwebwe kuiharibu mipango ya nguli kwa
kujaribu kumwangamiza. Aghalabu mhusika huyu huwa mzinzi, mlafi na wakati mwingine huwa
tajiri. Hii inaafikiana na sifa za mkinzani wa mhusika mkuu katika Utenzi wa Fumo Liyongo
ambaye ni Daudi Mringwari na kwa kiasi fulani Wafarisayo na Wayahudi waliompinga
,kumkataa na hata kumfanyia njama ya kumuua Nabii Isa.
Kwa mujibu wa nadharia hii, jamii zote duniani huwa na mashujaa ambao aghalabu hupewa sifa
zilizo karibu sawa. Shujaa, kwa kawaida, huwa ni kiumbe wa kawaida. Walakini, kutokana na
mawazo yaliyo katika akili laza za wanadamu kutoka jadi,shujaa huchukuliwa kama kiumbe
asiyekuwa wa kawaida.Yeye huchukuliwa kuwa kiumbe aliye na sifa za kiajabuajabu na za
kipekee tofauti na wanajamii wengine wote. Kwa hivyo, sifa wapewazo mashujaa katika jamii
mbalimbali duniani hushabahiana sana.
Nadharia ya vikale kutokana na ubia wake imekuwa yenye umuhimu katika utafiti huu kwa vile
imetuongoza katika kulinganisha sifa za kishujaa za Fumo Liyongo na za Nabii Isa na umuhimu
wao kwa jamii zao.
1.8 Yaliyoandikwa Kuhusu Mada
Kuna data kubwa ya yaliyoandikwa kuhusu majagina duniani. Nyingi za kazi hizi ni za
kinadharia na zimefafanua masuala anuwai kuhusiana na majagina kwa jumla. Kunazo tendi
nyingi ambazo zina wahusika ambao wamesawiriwa kama majagina. Majagina au mashujaa wa
16
utendi wa Kiswahili ni kama vile Fumo Liyongo katika Utendi wa Fumo Liyongo wa Mohamed
Kijumwa (1913), na Abushiri bin Salim katika Utendi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mrima,
wake Hemed Abdallah (1895), mtume Muhamadi na masahaba wake kama Utendi wa Rasil
Ghuli na mashujaa wa kubuni kwa mfano Tajiri katika Utendi wa Masahibu. Tendi hizi pamoja
na zingine kama vile Utenzi wa Katirifu, Utenzi wa Siri li Asilali, na Utenzi wa kutawafu Nabii,
zina wahusika ambao wamechorwa kama majagina. Kazi zingine ni mahsusi na zinawamulika
mashujaa wa jamii fulani, kama vile Shaka Zulu, Fumo Liyongo, Sundiata, Gautama Buddha na
kadhalika. Tafiti nyingi zinaelezea jamii zilizowazaa na kuwakuza majagina hawa. Kazi hizi zote
ni muhimu katika kuzipambanua sifa za majagina wa utafiti wetu na kuelezea umuhimu wao kwa
jamii zilizowazaa na kuwalea.
Katika utafiti wetu hatukupata makala yaliyoandikwa yakimuangazia Nabii Isa kama shujaa.
Makala ambayo tulipata kuyarejelea na ambayo yalitufaa sana katika kuelezea mazingira ya
kuzaliwa, kukua na matendo ya Nabii Isa bali na Utenzi wa Nabii Isa, ni Qurani na Bibilia
takatifu.
Kazi za mwanzo zilizoandikwa kumhusu shujaa Fumo Liyongo zilifanywa na Steere (1870),
ambaye alikusanya katika maandishi ngano za Waswahili kama zilivyosimuliwa kwake na
wakaaji wa Unguja. Ngano alizozichapisha ni kama Hadithi ya Liyongo (uk 456-471), Mashairi
ya Liyongo (uk 456-471) na Utumbuizo wa Gungu (uk 474-483). Kazi hizi zimeufaa utafiti huu
kwa kutupambanulia sifa za Fumo Liyongo na umuhimu wake kwa jamii ya Waswahili.
17
Kulingana na Gichamba (2005) Werner (1968), ni kazi inayotoa mkusanyiko wa maelezo kuhusu
visasili na visakale vya baadhi ya Wabantu, Waswahili wakiwa baadhi yao. Mwandishi anadai
kuwa Wabantu, licha ya uhusiano katika lugha, wana mila na desturi nyingi zinazofanana. Kazi
hii imetufaa katika utafiti huu kwani kufanana huku kumetuwezesha kuwatazama majagina wa
utafiti wetu kiulinganishi. Katika kuirejelea Hadithi ya Liyongo (uk. 145-154), ametoa maelezo
muhimu kwa utafiti huu kuhusu aila ya Liyongo na mgogoro uliokuwepo baina yake na nduguye
Daudi Mringwari. Mgogoro huu ni muhimu katika kuiunda historia ya shujaa huyu. Werner
(khj), vilevile amewazungumzia mashujaa wengine wa Kibantu na kuzungumzia shughuli na
fenomena mbalimbali katika jamii ya wabantu anamotoka shujaa Fumo Liyongo.
Knapert (1979), ametoa maelezo kuhusu kipindi alichoishi Fumo Liyongo pamoja na maelezo
mengine muhimu kumhusu Liyongo na tungo zake. Kazi nyingine ya mwandishi huyu iliyofaa
utafiti wetu ni ile ya mkusanyiko wa visasili na visakale vya Waswahili (Myths and Legends of
the Swahili (1970). Kazi hizi za fasihi simulizi ya hapo kale zilichota kwa upana maudhui yake
kutokana na hali na migogoro ya kijamii iliyopo. Mtalaa wa kazi hizi umetupa taswira angavu ya
jamii zinazopatikana.
Katika kuelewa kwa kina historia ya Pate alikotembelea Fumo Liyongo, tumerejelea Utenzi wa
Al- Inkishafi. Utenzi huu unarejelea maanguko ya mji huo chini ya utawala wa Wareno. Vile
vile, utenzi huu unatusawiria hali ya mji huu kabla ya maanguko na kutuonyesha ustawi wake.
Hali hii imetusaidia kuelewa mfumo wa kijamii wa mji huu wakati alipoishi Liyongo.
18
Nurse na Spear (1985), kama walivyonukuliwa na Gichamba (2004), waliangazia historia ya
Waswahili pamoja na lugha ya Kiswahili baina ya karne ya saba na kumi na nne (800-1400
B.K). Waandishi hawa wameelezea maswala muhimu kama vile, utamaduni asilia wa
Waswahili, asili ya lahaja mbalimbali za Kiswahili, kuibuka kwa miji mbalimbali ya Waswahili
kama vile Mogadishu, Kilwa, Pate, Lamu, Malindi na Mombasa kutokana na kupanuka kwa
jamii ya Waswahili; miundo ya kijamii na kiutawala katika miji mbalimbali; hali ya kiuchumi
katika jamii hii; na maingiliano baina ya Waswahili na watu kutoka jamii zingine za Kiafrika, za
Mashariki ya Kati na sehemu zingine ulimwenguni. Kazi hii imefaa sana utafiti wetu kwani ilitoa
mwanga kuhusu hali ilivyokuwa katika kipindi alichoishi Liyongo.
Tasnifu zinazotalii suala la majagina na zilizochapishwa katika lugha ya Kiswahili si nyingi.
Mutiso (1985) aliangalia hurafa - linganishi juu ya majagina. Aliirejelea Kasida ya Hamziyya
katika kumlinganisha mtume Muhammed na mashujaa wengine katika hurafa na uyakinifu
katika kasida hiyo. Kazi hii ni muhimu kwetu kwani ni mojawapo wa kazi ambazo
zimeorodhesha sifa bia za majagina, ambazo ndizo msingi tulioutumia katika kuwafafanulia
majagina wetu Fumo Liyongo na Nabii Isa.
Mberia (1989), anamtazama Liyongo kama shujaa wa masimulizi katika ngano za Waswahili.
Katika makala haya, mwandishi ametoa sifa tano za Liyongo na kudai kuwa sifa hizi ni bia kwa
mashujaa wote na kwamba zinapatikana katika masimulizi ya mataifa mengine duniani. Sifa hizi
ni ujasiri au ushupavu, nguvu za kimwili, nasaba au cheo, wepesi wa akili na usanii (stadi katika
gungu na mwao). Aidha, anatoa ngano kumhusu Sundiata ili kuonyesha ulinganifu kati ya
mashujaa hawa wawili. Utafiti wetu ni tofauti na utafiti huu kwa kuwa bali na sifa tano
19
alizoziorodhesha mtafiti huyu, tutadhibitisha kuwa zipo sifa nyingine za mashujaa kama urijali,
kupenda haki, “uungu-mtu” n.k. Aidha, utafiti huu umemwangazia Liyongo kama mhusika wa
kihistoria na wala si mhusika katika ngano, na ambaye tumemlinganisha na Isa, ambaye ni
shujaa wa kidini.
Mutiso (1999), anatazama kiulinganishi maisha na sifa za majagina wawili wa kidini,
Muhammadi na Buddha, huku akirejelea sifa bia za mashujaa. Katika kuwaangazia majagina
hawa, makala haya yamewataja majagina wengine duniani kama vile Nabii Musa, Nabii Isa,
Samshoni, Shaka Zulu na Fumo Liyongo miongoni mwa wengine. Utafiti wetu umelinganisha
sifa za Fumo Liyongo kama shujaa wa kihistoria, na Nabii Isa kama shujaa wa kidini, na
kuelezea umuhimu wao kwa jamii zao. Mambo haya hayajashughulikiwa na makala haya. Hata
hivyo, makala haya ni muhimu kwetu kwani yameelezea kuhusu zawadi ya jagina kwa umma
wake, kama mojawapo ya sifa za jagina. Anadai kuwa Waswahili waliachiwa gungu na Fumo
Liyongo.
Miehe na wenzake (2004), wamekusanya nyimbo pamoja na mashairi ambayo yanadaiwa
kutungwa na Fumo Liyongo. Mashairi haya pamoja na nyimbo hizi zilidondolewa kutoka kwa
kazi za awali zilizochapishwa, ilhali nyingine walizitoa kutoka maktaba na hifadhi za nyaraka
mbalimbali katika taasisi mbalimbali ulimwenguni. Kazi hii ni zao la warsha kadhaa
zilizofanyika huko Bayreuth Ujerumani, kati ya mwaka wa 2003 na 2004. Lengo kuu la warsha
hii lilikuwa ni kutalii na kuchambua mashairi na nyimbo zinazohusishwa na Fumo Liyongo ili
kuibuka na toleo kamilifu ambalo lingekidhi mahitaji ya kiusomi kote duniani. Bali na
kuzionyesha tungo hizo za Liyongo, wametoa maelezo kuhusiana na utamaduni wake, fani
20
zilizotumiwa katika tungo hizi, miongoni mwa masuala mengine muhimu katika utamaduni wa
Waswahili. Kazi hii ilikuwa msingi mmojawapo wa kufafanulia masuala kadhaa kuhusiana na
utamaduni wa Fumo Liyongo.
Gichamba (2004), amewalinganisha mashujaa wawili wa kihistoria - Fumo Liyongo wa
Waswahili, na Shaka Zulu wa Wazulu. Utafiti huu ni tofauti na wetu kwa sababu
amewalinganisha mashujaa wawili wa kihistoria na wa kutoka katika eneo moja la Afrika. Utafiti
huu ni tofauti na wetu kwa kuwa wetu unamlinganisha shujaa wa kidini, na mwingine wa
kihistoria. Aidha, mashujaa hawa ni wa kutoka maeneo mawili tofauti kijiografia.
Achieng (2012), pia aliangazia sifa za mashujaa na umuhimu wao kwa jamii zao huku
akimlinganisha Fumo Liyongo wa Waswahili na Lwanda Magere wa Wajaluo. Katika uhakiki
wake, aliweza kufafanua sifa za mashujaa wa kijamii na hii kazi yake ilitufaa zaidi katika
kufafanua sifa za mashujaa wa kidini na wa kihistoria katika Utenzi Nabii Isa.
Ndumbaro (2013), ameshughulikia dhana ya shujaa wa tendi kwa jumla, na matatizo mbalimbali
ya kijamii katika maisha ya shujaa. Katika utafiti huu, mtafiti anahitimisha kuwa shujaaa
hupatwa na matatizo kama wanavyopatwa watu wengine katika jamii, ila sihiri au nguvu alizo
nazo shujaa zisizoweza kuelezeka humfanya shujaa kuwa na upekee katika ufumbuzi wa
matatizo hayo. Utafiti huu ulitufaa katika utafiti wetu kwa sababu ulitutolea mwanga kuhusu
jinsi majagina huyakabili matatizo yanayowakuba.
21
Kalinjuma (2013), amejadili suala la jaala ya shujaa wa tendi za Kiafrika na shujaa wa tendi za
Kimagharibi. Alizingatia jaala ya tendi na ukweli kuhusu mambo yanayofungamana na jaala
yake. Mtafiti huyu anahitimisha kuwa jaala ya shujaa inaonekana kufanana kati ya majagina wa
Kiafrika na wa Kimagharibi kwani matukio wanayofanya ni yaleyale ya kishujaa yenye
kuambatana na matukio yanayofasiliwa kuwa si ya kawaida, na ni ya kushangaza kwa jamii zao.
Kazi hii inatuthibitishia kauli kuwa mashujaa wote huwa sifa zinazokaribiana sana.
Katika utafiti wetu, kazi tuliyoipata inayomwangazia Nabii Isa kama shujaa wa kidini ni ile ya
Achieng (2013), aliyeyahakiki maudhui katika Utenzi wa Nabii Isa. Kazi hii Ilitufaa katika
utafiti wetu kwa sababu, moja kati ya maudhui yalioangaziwa katika utenzi huu ni ujagina.
Hivyo, kazi hii ilitutolea mwanga zaidi kuhusu ujagina wa Isa kama unavyojitokeza katika utenzi
huu.
Aidha, bali na Utenzi wa Nabii Isa, tumerejelea mtandao pamoja na Qurani tukufu na Bibilia
takatifu ili kuangazia sifa zaidi za ushujaa wa Isa pamoja na kujenga uelewa wa kina wa
mazingira yaliyomzaa shujaa Isa, pamoja na umuhimu wake kwa umma wake.
Kwa jumla, kunazo kazi nyingi sana ambazo zimeandikwa kuhusiana na Fumo Liyongo na Nabii
Isa. Kazi ambazo tumezirejelea ni baadhi tu ya kazi nyingi zinazowasawiri majagina wa utafiti
huu. Kwa kuwashughulikia Nabii Isa na Fumo Liyongo kiulinganishi, utafiti huu umenuia
kulijaza pengo la kiusomi ambalo limekuwepo. Hakuna utafiti tuujuao unaomlinganisha jagina
wa kidini na jagina wa kihistoria, na kuelezea kwa kina umuhimu au mchango wao kwa jamii
zao.
22
1.9 Mbinu za Utafiti
Utafiti wetu umekuwa ni wa maktabani. Tumesoma vitabu vya kihistoria kuhusu historia ya
Waswahili, Wayahudi, hali za kijamii na mazingira yaliyowazaa Fumo Liyongo na Nabii Isa.
Habari tulizozipata katika vitabu mbalimbali zimetusaidia kueleza historia ya Fumo Liyongo na
Nabii Isa, ikifungamanishwa na historia ya Waswahili na Wayahudi mtawalia.
Pia, kupitia usomaji wetu wa makala mbalimbali maktabani, tumejaribu kutambua, kuchunguza
na kujitokeza na sifa bia za kishujaa na umuhimu wa mashujaa wetu kwa jamii zao. Fauka ya
hayo, tumezisoma tasnifu, makala, na majarida mbalimbali yanayohusiana na somo letu la
utafiti.
Aidha tumeyasoma mashairi na nyimbo zilizotungwa na watu mbalimbali kuhusu Fumo
Liyongo, na hata yale yanayodaiwa kutungwa na yeye mwenyewe. Mashairi haya yametusaidia
kumwelewa Fumo Liyongo kwa kina. Tumeelewa sifa zake za kishujaa, historia yake
ikifungamanishwa na ya Waswahili, na hata umuhimu wake kwa jamii ya Waswahili.
Tumetafuta habari pia katika mitandao na tovuti mbalimbali ambazo tumeweza kuzifikia na
ambazo zinasheheni habari kuhusiana na utafiti wetu.
1.10 Hitimisho
Mada yetu ya utafiti inahusu taswira ya jagina katika tendi za Kiswahili, ambapo
tunamlinganisha Nabii Isa ambaye ni shujaa wa kidini, na Fumo Liyongo ambaye ni shujaa wa
kihistoria. Hawa ni mashujaa wa vipindi, jamii na maeneo tofauti. Ulinganishi wa jagina wa
kidini na wa kihistoria haujafanywa hapo mbeleni, na tafiti za aina hii zitachangia katika
23
kuthibitisha kuwa sira za majagina katika ulimwengu mzima zinafanana sana. Pia, utachangia
katika kudhihirisha umuhimu wa mashujaa hawa kwa jamii zao, na kwa ulimwengu mzima kwa
jumla.
>>>>>>>ITAENDELEA>>>>>>>>>>>>
>>>>>>>ITAENDELEA>>>>>>>>>>>>