TASWIRA YA JAGINA KATIKA TENDI: ULINGANISHI WA FUMO LIYONGO
SURA YA NNE
UMUHIMU WA FUMO LIYONGO NA NABII ISA KWA JAMII ZAO. 4.0 Utangulizi Baada ya kutalii historia za mashujaa hawa wawili, kueleza salua za jamii zao na sifa zao na sifa bia za kimashujaa, itatubidi tupige hatua kwa kuangazia michango yao kwa jamii zao husika, na katika ulimwengu wote kwa jumla. Jamii ni kama mfumo au kiunzi imara ambacho huwa na taasisi au mifumo midogomidogo mingi ndani yake. Taasisi hizi ni kama vile, taasisi ya utamaduni, ambayo pia, huwa na taasisi nyingi ndani yake. Ili mfumo mzima uwe mkamilifu, ni lazima kuwe na kila nia ya kudumisha na kusawazisha hali mbalimbali katika jamii. Taasisi ya ushujaa kwa hivyo, huwa na nafasi kubwa mno ya kurekebisha mambo na kuleta mabadiliko fulani katika hali ambazo zimeenda kombo katika jamii. Jagina huzuka kwa ajili ya wanajamii, kila kitu anachokitenda hulenga kuwanufaisha wanajamii kwa jumla. Fumo Liyongo na Nabii Isa walikuwa na umuhimu mkubwa kwa jamii ya Waswahili na Wayahudi Mtawalia. 4.1.1 Kitambulisho cha Kitaifa/Kijamii Mara nyingi, shujaa huwa kitambulisho cha taifa au jamii yake. Shujaa mmoja kwa mfano, katika jamii husika huwa kipengele kikuu kinachowakilisha mfumo mzima wa jamii hiyo. Kwa kulitaja tu jina la Nabii Isa au Fumo Liyongo, itakuwa kana kwamba unarejelea kwa jumla jamii wanazoziwakilisha. Jamii ya Wakristo na Waislamu inatambulika kote duniani kutokana na jina la Nabii Isa na vivyo hivyo, jamii ya Waswahili kutambulika kwa kulitaja jina la Fumo Iyongo ni kipengele kimoja muhimu kabisa ambacho aghalabu kikitolewa, jamii husika itabaki “uchi”. 84 Huenda mtu yeyote asilijue jambo lolote lingine au hata mila za Waswahili au Wayahudi bila kuwataja nabii Isa na Fumo Liyongo. Liyongo, kwa mfano, ana umuhimu mkubwa katika kutambulisha jamii ya Waswahili katika ngazi za kimataifa ingawa aliishi miaka mingi iliyopita, sifa zake, maumbile na matendo yake yaliwavutia watu wa kawaida na wengine wengi kutoka nchi za mbali (kimataifa). Edward Steere (1970), miongoni mwa wazungu wengine huwakusita kukusanya habari kuhusu Liyongo na kuziweka katika maandishi. Steere (1870; VI) anadai kuwa Waswahili wanajitambulisha pakubwa na Liyongo. Hata baada ya miaka mingi ya mauko yake, bado anaathiri nafsi za watu katika jamii ya Waswahili, hata ingawa, Wapokomo, Wajabuni, na Wasegeju wanadai kuwa Liyongo alikuwa shujaa wao, yeye sanasana alionekana kujihusisha na kujitambulisha na jamii ya Waswahili ambayo inampenda na kumwajabia mno. Wapokomo walidai kuwa Liyongo ni mbaya ilhali Waswahili kwa upande wao, wanamwonea fahari kwa vile aiwasaidia kujikomboa kutoka mikononi mwa maadui zao. Vivyo hivyo Nabii Isa alichukuliwa na adui zake kuwa mbaya kwa kuwa alikufuru kwa kujiita “mwana wa Mungu”, ilhali kwa wafuasi wake alikuwa Masihi aliyetabiriwa katika Agano la Kale na ambaye angewakomboa na kuwaelekeza katika ufalme usio na mwisho. 4.1.2 Ukombozi na Muungano wa Jamii Kama tulivyotangulia kusema katika sura ya pili, hakuna jagina anayezuka katika ombwe tupu.Kila jagina huzuka katika hali na kipindi maalum katika jamii maalum ili kuikomboa kutokana na masaibu fulani. 85 Masaibu kuwa pamoja na uvamizi wa mara kwa mara na maadui, unyakuzi wa ardhi na rasilmali zingine za wanjamii kama walivyofanya mabeberu barani Afrika, mizozo katika utawala wa jamii, matatizo ya kiuchumi, dhuluma zinazojitokeza kutokana na ukabila katika jamii, matatizo ya kiuchumi, dhuluma zinazojitokeza kutokana na ukabila katika jamii. Kutokana na haya masaibu yote, ni lazima shujaa azauke ili kuleta umoja na kuunganisha wanajamii na kusawazisha mfumo ulioenda kombo. Pia ukosefu wa vitu au vifaa muhimu hurekebishwa na shujaa hata kuwaelekeza wanajamii kuhusiana na masuala ya kidini, miongoni mwa mambo mengine ambayo iwapo jagina hatazuka katika kipindi anapohitajika, kuna uwezekano kuwa jamii hiyo itabakia katika shida zizo hizo. Wanaamii walijitokeza kwa wingi kila mara waliposikia kuwa Fumo Liyongo angezitongoa nyimbo zake, kwa mfano, alipokuwa gerezani akingojea kuuawa na Sultani (Utenzi wa Fumo Liyongo beti, 111, 112, 113, na 114), kuwa watu walijitokeza kwa wingi na mshairi alilinganisha hafla hiyo na ile ya harusi. Ngoma za gungu ziliendelea kuitambulisha jamii ya Waswahili na kuwaunganisha katika sherehe mbalimbali hata baada ya kifo cha Liyongo. Aidha, kifo chake kiliwahuzunisha watu wengi waliomwona kama ngao yao dhidi ya maadui zao. (Utenzi wa Fumo Liyongo ub 225 na 226). Nabii Isa, kwa mujibu wa utenzi, alinusuriwa na mola wake kwa kupaa juu mbinguni lakini waislamu wanaamini kuwa atarejea kukamilisha kazi aliyoianzisha ulimwenguni. Wakristo wanaamini kuwa aliwakomboa waumini na wafuasi wake. Alipokufa, wengi walisikitikia kifo chake. Kutokana na kifo chake, wanaamini kuwa wataurithi ufalme wa mbinguni. Ni kutokana na jukumu la kuwakomboa wanajamii ndiposa shujaa huchukuliwa kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo, kuwafanya waabudiwe hata baada ya mauko yao. 86 4.1.3 Kioo cha Jamii/Historia ya Jamii Tunaweza kudai kuwa shujaa, kama ilivyo fasihi, ni kioo cha jamii. Shujaa huwa kama kiwakilishi cha jamii haswa katika kipindi cha historia alichozuka na kuishi. Kwa kuelewa historia ya shujaa wa jamii fulani katika kipindi fulani, basi tunaweza kupata taswira kuhusu mfumo wa jamii ile. Kwa kawaida, madhila, mateso, dhuluma, ufanisi na masuala mengine yote yanayomkumba shujaa hutupatia picha kuhusu hali ilivyo katika mfumo mzima wa jamii yake. Mifumo kama ya siasa, mila, uchumi na masuala mengine ya kitamaduni hujulikana tu baada ya kumtalii shujaa wa jamii husika. Kwa vile shujaa huzuka katika jamii fulani katika kipindi na hali Fulani kutimiza malengo na dhamira fulani haswa ya ukombozi katika jamii yake, hivyo basi, kwa kuangazia shujaa huyo, kabla ya kuzuka kwake, wakati wa enzi zake na baada ya kifo chake, (maisha yake kwa jumla) kutusaidia kuelewa historia ya jamii yake. Maelezo kuhusiana na sifa na historia ya mashujaa hawa wawili yametupatia nafasi nzuri ya kuihakiki jamii ya Waswahili pamoja na Wayahudi. Kwa kupitia kwao haswa, tumepata kuwa jamii hizo zote zilikumbwa na mizozo na mivutano ya hapa na pale ikiwemo ya kivita, kiuongozi, kiuchumi, kidini, kitamaduni n.k. mathalan, dola mbalimbali zilizotawaliwa na wafalme kulikuwa na ung’ang’aniaji wa madaraka ambao ulisababisha njama na hila mbalimbali za usaliti kutumiwa, uvuziaji na uvinjari pia, kulikuwepo na masuala mengi kama vile uvamizi, dini, biashara, tohara, mapenzi, mauaji, kilimo, ufugaji, sheria, ngoma na masuala mengine mengi ya kitamaduni ya jamii zilizowazaa mashujaa wetu wa utafiti. Mashairi, misemo pamoja na nyimbo mablimbali zilizotungwa na waja wengine au hata zilizodaiwa kutungwa na mashujaa hawa ukwahusu hutusaidia kuelewa aina ya mazingira 87 yaliyomo katika jamii zao. Kwa mfano, tunapata kujua baadhi ya miji ambayo Fumo Liyongo aliwahi kutembelea katika harakati zake za kugura hapa na pale. Tumetajiwa miji kama vile Pate, Shaka, Ozi, miongoni mwa miji mingine. Aidha, tumeelewa kuwa kulikuwa na milima na mito. Mto Tana ni mojawapo ambamo Liyongo alienda mara kwa mara kuoga. Bali na hayo, tunatajiwa majina ya vifaa mbalimbali kama vyungu, mafiga, mimea, miti na misitu katika mazingira ya Fumo Liyongo. Vilevile, hali za maisha za majirani wake Wasanye na Wadahalo pia zimeangaziwa. Tunaambiwa waliishi mwituni wakila matunda mbalimbali kama makoma. Hata hivyo, utamaduni ya jamii yoyote ile unaweza kubadilika kutokana na hali mbalimbali katika jamii kama vile, vipindi mbalimbali, mpito wa wakati, utangamano na maingiliano na jamii nyingine, elimu, dini n.k. Mara nyingi, kutokanana na nafasi ya hadhi ya juu aliyopewa jagina katika jamii yake pamoja na kutegemewa katika kila jambo maishani, yeye huwa na uwezo wa kubadilisha mkondo wa maisha ya jamii yake atakavyo (kwa sababu anategemewa katika kila kipengele cha utamaduni wao). Licha ya kuzikomboa jamii zao kutokana na tishio la maadui, Nabii Isa na Fumo Liyongo walileta mabadiliko makubwa katika vipengele mbalimbali vya utamaduni (maisha) vya jamii zao. Nabii Isa na Fumo Liyongo walijitokeza bayana kama watetezi na watekelezaji wa imani, mila na desturi mbalimbali za jamii zao. Kwa njia za mafundisho, nyimbo, mighani na ughani wa mashairi huku wakishirikiana na wanajamii wengine. 88 Liyongo mwenyewe alikuza, kuendeleza na kuimarisha utamaduni wa Waswahili kwa kuasisi gungu wa mwao, ngoma ambazo zimekuwa hai katika jamii ya Waswahili huku zikichezwa katika shrehe mablimbali na haswa wakati wa harusi. Frankl (1993:130). Akinukuliwa na Gichamba (2005:124), anaeleza kuwa ngoma ya gungu (ikijumlisha nyimbo za Liyongo), huwa inachezwa saa za asubuhi wakati wa kuamkia siku ya kila mwaka. Nabii Isa kwa upande mwingine amekuwa kielelezo kwa jamii yake na ulimwengu mzima kwa jumla. Huyu ni shujaa wa kidini, ambaye maisha na matendo yake yameangaziwa katika dini mbili zilizo na ufuasi mkubwa ulimwenguni. Kitabu cha Injili alichokiachia umma wake kama zawadi ya jagina, kingali kinashikilia sehemu kubwa ya imani ya waumini wa imani zote mbili. Kwa hivyo, imani na shughuli za kitamaduni zilidumisha umoja, mashikamano na utangamano baina ya watu. Maadili pia yaliendelezwa. Fumo Liyongo na Nabii Isa walitumia tamaduni hizo ili kuziweka jamii zao katika mfumo mmoja imara. 4.1.4 Mabadiliko Katika Mfumo Mzima wa Jamii Baada ya shujaa kutekeleza jukumu la kuikomboa jamii yake kutokana na misukosuko mbalimbali, huwa hachoki, bali huunda mikakati na sheria kabambe na mpya za kumwezesha kubadilisha maisha ya jamii yake kwa jumla. Kama kulikuwa na sheria ambazo ziliwafinya na kuwadhulumu wanajamii, huziondoa, na kuleta nyingine mpya. Hata hivyo, kuna wakati ambapo shujaa anaweza kuzua mikakati, sheria mpya na mabadiliko yasiyoungwa mkono na wanajamii. Kwa mfano, Liyongo aliwatoza Wapokomo kodi ya juu, jambo ambalo liliwasinya sana.. 89 Mabadiliko ambayo yanaweza kuletwa na shujaa ni pamoja na mabadiliko katika mikakati ya kivita, uzalishaji mali, sheria, mahusiano na jamii zingine pamoja na kuleta amani na kufanya biashara n.k. Fumo Liyongo na Nabii isa walileta mabadiliko makubwa katika jamii zao.Mabadiliko haya ni kama kuleta umoja miongoni mwa jamii. 4.1.5 Ruwaza Bora ya Kufuatwa na Wanajamii Kama tulivyodokeza hapo mwanzo, shujaa ni mtu ambaye yu tayari kuhatarisha maisha yake kwa manufaa ya jamii yake. Ni yule mtu ambaye ana mapenzi kwa wanajamii, jambo ambalo huwafanya wanajamii kutaka kujitambulisha naye hata baada ya mauko yake. Matendo, sifa na hulka za kiajabuajabu za jagina hupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia za masimulizi na hata kupitia kwa watoto wengi ambao aghalabu huvutiwa na ngano katika maandishi na masimulizi na hata filamu zinazowasawiri mashujaa. Majagina hawa huwa ni ruwaza bora bora kwa watoto mbalimbali, ikiwa kazi hizi zitawasawiri katika uigizaji wa hadithi za kazi bunilizi au zile zinazowasawiri mashujaa wa kihistoria. Bali na hayo, mashujaa huathiri maisha ya mtu binafsi, jinsi mtu anavyotazama mambo. Huenda mtazamo wake ukabadilika baada ya hisia zake kuvutiwa na shujaa wao. Shujaa kwa kawaida huyafanya mambo kwa ajili ya manufaa ya jamii nzima si kwa manufaa yake mwenyewe. Huenda mtu akapata mshawasha wa kufanya hivyo pia. Huenda baadhi ya wanajamii wakaiga vitushi vya shujaa wao, utaratibu wa mbinu zake. 4.1.6 Fahari ya Jamii Zao Kama tulivyodokeza hapo awali katika sura ya kwanza, kila jamii huwa na shujaa wao, humkuza, humwona kama mkombozi wao, humwaajabia na kumwonea fahari. Juhudi za jagina, 90 mara nyingi, hufurahiwa na kukumbukwa milele. Si ajabu kupata wanajamii wakifunza vizazi vijavyo kuhusu matendo, historia na sifa za jagina wao hususan pale ambapo huyo jagina alitekeleza dhamira yake vizuri kwa umma. Jamii huajabia maisha yake yote hata baada ya mauko yake, kwa mfano katika kufundisha kuhusu jagina ulimwenguni, walimu wa Kiafrika katika shule hulinganisha majagina wa Kiafrika na kujaribu kuonyesha ukuruba uliopo baina ya vitushi na maumbile ya majagina hao wote. Waama, Fumo Liyongo na Nabii Isa wakiwa majagina miongoni mwa wengine wa Kiafrika na wa kidini mtawalia, waliwatetea watu wengi kote duniani. Ni fahari kubwa wala sio tu kwa Waswahili na Wayahudi kwa kupitia uwezo wao, vitushi na maumbile yao, bali pia kwa ulimwengu mzima. Walitekeleza na kutimiza dhamira zao kwa kutumia nguvu, rasilimali na mbinu zenye taathira kubwa katika kutekeleza masuala makubwa na ya ajabu bila kutegemea usaidizi wa wageni kutoka ng’ambo. Kwa hivyo, Waswahili na Waafrika kwa jumla, bali na kujivunia utamaduni wao, wanaonea fahari juhudi za shujaa Liyongo hadi leo. Nabii Isa bali ni kuwa kuwakomboa Wayahudi, ni jagina ambaye ana ufuasi mkubwa sana ulimwenguni. Hata kama wazungu waliwachukulia waafrika kuwa watu wasiostaarabika na washenzi, ni dhahiri kuwa ndani ya huu “ushenzi” mlikuwemo na ufahari na ustadi mkubwa na hasusan kwenye mifumo ya miundo misingi ya waafrika wenyewe. Utawala bora wa majagina, upanuzi wa milki zao, ulinzi wa watu, utangamano wa umma wake, matumizi ya mbinu na mikakati maridhawa ya kivita na ukuzaji wa utamaduni ya jamii zao ni masuala yanayoonewa fahari na wanajamii na watu wengine kutoka uga wa kimataifa. Waafrika walikuwa na taasisi na tamaduni zilizofuata utaratibu fulani uliokubaliwa na wanajamii wake. 91 Kwa, hivyo, kwa mujibu wa mbeberu, mwafrika ni mshenzi pamoja na tamaduni zake ilhali kwa jicho la mwafrika, yeye na tamaduni zake ni zenye ustaarabu wa hali ya juu, ambao kwa kiasi kiukubwa umetetewa na kuendelezwa na majagina wao. Kulingana na Kenyatta (1922:), Waafrika walikuwa na mfumo faafu wa utozaji kodi, uamuzi wa kesi, njia za kuabudu, njia za uzalishaji mali (kilimo, biashara, uvuvi, utamaduni, useremala n.k), ndoa, tohara, maziko, uhifadhi wa mazingira, njia ya kuwakumbuka mashujaa wao, miongoni mwa mbeko na tamaduni zingine. Mzungu lazima atilie maanani uwezo wa mtu mweusi katika kujikomboa kutoka katika hali duni na kupaa juu hadi katika ngazi za ufanisi mkubwa uliodhihirishwa na sifa na matendo ya mashujaa Kiafrika, Fumo Liyongo na Nabii Isa wakiwemo. 4.2 Hitimisho Kama tulivyotangulia kusema katika sura ya kwanza, tendi nyingi huwajenga mashujaa wake katika hali ya kuwafungamanisha na matatizo yanayoikabili jamii husika. Hufanya hivyo kwa lengo la kuonyesha kuwa shujaa ni zao la jamii, na kama ni zao la jamii, hana budi kukumbana na matatizo kama wanajamii wengine. Pia, hufanya hivi kwa lengo la kuwaonyesha wanajamii ushujaa wa shujaa katika kukabiliana na matatizo mbalimbali, kwamba hutofautiana na watu wa kawaida. Aidha, hufanya hivyo kwa lengo la kuwaondolea wanajamii hofu na kuwahakikishia usalama wao pindi wapatwapo na matatizo, kuwa, wanaye mwokozi atakayewaokoa katika matatizo yao. Katika sura hii, tumejaribu kuyathibitisha haya kwa kujikita katika kuchambua ujagina wa wahusika wetu kama ulivyojitokeza katika Utenzi wa Nabii Isa, na Utenzi wa Fumo Liyongo. 92 SURA YA TANO HITIMISHO NA MAPENDEKEZO 5.0 Hitimisho Katika sehemu hii, tutaangazia matokeo ya utafiti wetu, pamoja na masuala mengine ambayo yalijitokeza katika mchakato mzima wa utafiti huu, huku tukirejelea malengo ambayo tuliazimia kuyatekeleza mwanzoni mwa utafiti wenyewe. Ni bayana kuwa suala la mashujaa ni pana mno na huhitaji uelewa wa kina wa mazingira yanayowazaa, pamoja na historia, na falsafa zao za maisha. Mada hii ya majagina ina mvuto wa kipekee hasa tunapowatazama kwa mkabala wa kiulinganishi. Shujaa ni asasi au taasisi ambayo ina mchango mkubwa katika jamii. Majagina wa kidini na wa kihistoria wako na wamechangia pakubwa katika kuwepo kwa hali mbalimbali katika jamii za sasa. Hivyo, wanapaswa kumulikwa kwa jicho pevu, ili kuuweka wazi mchango wao kwa vizazi vijavyo. Utafiti wetu ulichukua mwelekeo ambao ulifumbata maswala kadhaa, ambayo, ni muhimu katika kutoa picha bayana ya jagina kwa jumla. Katika sura ya kwanza, tulitanguliza somo la utafiti wetu kwa kuangazia usuli wa utafiti na masuala muhimu na ya kijumla ambayo yangetoa mwongozo wa kufikia malengo ya utafiti wetu. Katika sura ya pili, tulilenga kuiangazia historia ya Nabii Isa, na ile ya Fumo Liyongo katika mkabala mzima wa historia ya jamii zao, huku tukionyesha mazingira, vipindi na hali za kijamii zilizowazaa. Tulipata kuwa mashujaa hawa walizuka kutokana na mahitaji fulani. Mashujaa 93 hawa wawili walizuka katika kipindi cha misukosuko katika jamii zao na kuwa walizuka ili kuitatua misukosuko hiyo. Katika sura ya tatu, tulitalii sifa za majagina hawa wawili kiulinganishi, na kupata kuwa shujaa Fumo Liyongo na Nabii Isa wana sifa zinazolingana kwa kiasi kikubwa. Tofauti zilizoko ni chache mno kama vile, kuhusu utabiri wa kuzaliwa kwao, swala la ndoa, kufa kwao na utetezi wa cheo. Hivyo, utafiti huu umechangia madai kuwa sifa za mashujaa duniani kote ni karibu sawa. Katika sura ya kwanza, Mberia (1989) na Mulokozi (1999) walitutolea baadhi ya sifa za kishujaa za Fumo Liyongo. Utafiti wetu umebaini sifa zaidi za Fumo Liyongo na Nabii Isa, ambazo zinaoana na za mashujaa wengine ulimwenguni ambao hatujawaangazia. Fumo Liyongo na Nabii Isa, wana sifa za kishujaa ambazo ni karibu sawa. Tumeona kuwa sifa hizi za kiajabu ajabu ndizo ziliwakuza pamoja na kukuzwa na jamii zao. Hivyo, kila mwanajamii humsawiri jagina wake apendavyo na kulingana na mtazamo wake. Kwa mintarafu hii, kuna wanajamii ambao walitiilia chumvi sifa za majagina wao, na wengine kuzipunguza, hasa wale ambao jagina alikuwa adui kwao. Kutokana na jinsi Liyongo amesawiriwa kwenye Utenzi wa Liyongo, umefanya baadhi wa watu kutoamini au kutiilia shaka kuwa aliweza kuishi. Utafiti wetu umebaini kuwa wanajamii humsawiri shujaa wapendavyo na hivyo hiki hakipaswi kuwa kigezo cha kupima iwapo jagina aliishi au la. Katika sura ya nne, tumepata kuwa shujaa huzuka ili kutekeleza wajibu fulani muhimu katika jamii. Hivyo, jagina ana umuhimu sana kwa jamii yake. Umuhimu huu unajitokeza siku nyingi 94 hata baada ya kifo chake. Hii ndiyo sababu sifa moja ya jagina ni kuwa ‘hafi’ na hukumbukwa daima na jamii yake. Matokeo yetu yamelingana na nadharia tete ambazo zilituongoza katika mchakato mzima wa utafiti wetu. Ilidhihirika katika matokeo ya utafiti wetu kuwa Liyongo na Isa ni mifano mizuri ya majagina wa kihistoria na wa kidini. Mashujaa hawa pia wana nafasi muhimu sana katika historia ya ulimwengu kwa jumla kwa sababu wanaweza kuwekwa katika kiwango sawa na cha mashujaa wengine ulimwenguni. Matokeo haya vilevile yamedhihirisha kuwa, sifa za mashujaa hawa kwa kiasi kikubwa hufanana. Pia mtazamo kuwa mashujaa hawa ni muhimu kwa jamii zao umedhihirika. Katika kuzipambanua sifa za kishujaa za Fumo Liyongo, tungo za kimsingi ambazo tulizirejelea ni pamoja na Utenzi wa Fumo Liyongo, Takhmisa ya Liyongo na mashairi na nyimbo zinazodaiwa kutungwa na Fumo Liyongo, miongoni mwa kazi zingine. Kwa upande wa Nabii Isa, tuliurejelea Utenzi wa Nabii Isa pamoja na Qurani na Bibilia ili kushadidia sifa, maisha na hata falsafa ya shujaa huyu. Pale tumemlinganisha shujaa huyu wa kidini na wengine wa kihistoria, si kwa nia ya kudhalalisha dini au imani ya mtu yeyote, bali ni katika kujaribu kuweka wazi sifa za kishujaa ambazo zinadhihirika kwa majagina wengine duniani. Hakuna utafiti wa kina tuujuao uliofanywa hapo awali unaomlinganisha shujaa wa kidini na wa kihistoria, pamoja na umuhimu wao kwa jamii zao. Hivyo basi, ni imani yetu kuwa pengo lililokuwepo kiusomi litazibwa kupitia kwa utafiti huu. 95 5.1 Mapendekezo ya Utafiti Katika utafiti wetu tumemlinganisha Isa ambaye ni jagina wa kidini wa jamii ya Wayahudi, na Fumo Liyongo ambaye ni jagina wa kihistoria wa jamii ya Waswahili. Majagina hawa wametoka katika janibu mbili ambazo ni tofauti kijiografia, kimila na kidesturi, na hata katika vipindi walivyoishi. Tungependekeza utafiti zaidi ufanywe unaowalinganisha mashujaa zaidi wa kidini kama vile Gautama Buddha au Mtume Muhhamad, na mashujaa wengine wa Kiafrika kama vile Kimathi, Magere, Mirambo, Kinjeketile, Kibwebanduka n.k ili kuonyesha ni kwa kiwango gani sifa zao za kijagina zinavyoambatana na sifa bia za mashujaa. Mashujaa wengi wa kihistoria na wa kijamii wa Kiafrika hawajafanyiwa utafiti wa kutosha. Hili ni pengo kubwa la kiusomi ambalo linastahili kujazwa. Ni bayana kwamba mashujaa hawa walichangia pakubwa katika harakati za ukombozi na ufanisi wa jamii zao. Mchango huu unafaa kuwekwa wazi ili vizazi vya sasa na vijavyo viweze kuzifahamu juhudi za mababu zao katika kupigania uhuru, ili kuzikomboa jamii zao na hivyo, kufuata nyayo zizo hizo. Majagina hawa ni kama vile, Kimathi, Magere, Mirambo, Kinjeketile, Kibwebanduka miongoni mwa wengine wengi, wanaoshikilia nafasi muhimu sana katika historia ya Afrika, na ulimwengu mzima kwa jumla. Ni vema ulinganishi wa kina uweze kufanywa baina ya majagina hawa na kuzipambanua sifa zao za kijagina na pia kuweka wazi michango yao kwa jamii zao. 96 MAREJEO Abdulaziz, M.H (1979) Muyaka: 19th Century Swahili Popular Poetry.Nairobi: Kenya Literature Bureau. Allen, J. V (1977) Al Inkishafi. Nairobi: East African Educational Publishers. _________ (1993) Swahili Origins: Swahili Culture and the Shungwaya Phenomenon. London: James Currey. Achieng, O.B (2012) Sifa za mashujaa na umuhimu wao kwa jamii zao: Ulinganishi wa Fumo Liyongo na Lwanda Magere.Chuo kikuu cha Nairobi. Haijachapishwa. Chiraghdin, S. Nabhany, A.S na Baruwa, A. (1975) Tarehe ya Ushairi wa Kiswahili, Mulika Na. 7 uk 59-67. Chittick, N (1984) Manda Excavations at an Island on the Kenyan Coast. Nairobi: B.I.E.A Freeman-Grenville (1954-1955) Ibn Batuta’s visit to East Africa A.D1332: A Translation.Ugandan Journal, uk 1-6. Gichamba, J.M (2005) Sifa za mashujaa na umuhimu wao kwa jamii zao: Ulinganishi wa Fumo Liyongo na Shaka Zulu.Chuo Kikuu Cha Nairobi. Haijachapishwa. Gunnep, A.V (1960) Rites of Passage.London: Routledge & Kegan Paul. Http / google (2013) The Classic Literary Hero, Mswada ambao haujachapishwa. Http / google (2005) Al Islam.Org/Kiswahili Vitabu: Usahihi wa Historia ya Uislamu na Waislamu. Mswada ambao haujachapishwa. Jung, C. J (1968) The Archetypes & The Collective Unconscious. London: Routledge & Kegan Paul Ltd Jung, C. J (1972) Four Archetypes: Mother, Rebirth, Spirit, Trickster. London: Routledge & Kegan Paul ltd Kalinjuma, D. (2013) Jaala ya Shujaa wa Tendi za Kiafrika na Ulaya. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Knappert, J. (1982) Myths and Legends of the Swahili.Nairobi: Heinemann Educational Books. _______ (1979) Four Centuries of Swahili Verse: A Literary History and Anthology. London: Heinemann Educational Publishers. Mbele, J.L (1986) The Liongo Fumo Epic and the Scholars’. Kiswahili 53/1 na 53/2 uk 128-145. 97 Mberia, K. (1989) Fumo Liyongo Mulika Na 21. Uk 25-43. Mbotela, J.J (1959) Uhuru wa Watumwa.Nairobi: Nelson. Mdee nw (2011): Kamusi ya karne ya 21.Nairobi: Longhorn Publishers. Miehe,G.N.,Abdalla,A,Bhalo,A.N.J.,Nabhany,A.,Baschiera,A.,Dittemer,C.,Topan,F., Abdulaziz, M.H., Khamis, S.A.M., Omar, Y.A. na AL-Bakary, Z.M.F (2004) Liongo Songs: Poems Attributed To Fumo Liyongo.Koln: Grudiger Koppe Verlag. Mulokozi, M.M. (1999) Tenzi Tatu za Kale.Dar es salaam: TUKI. Mutiso, K. (1985) ‘Hurafa na uyakinifu katika Hamziyyah’ Tasnifu ya Uzamili. Chuo Kikuu cha Nairobi. Haijachapishwa. ______ (1990) Fumo Liyongo na kazi zake. Haijachapishwa.1999) ______ (1999) Sira ya Majagina Buddha na Muhammed. Swahili Kolloquim Universitat, Bayreuth. Mei 14-15, 1999. Mzenga, M. (1977) Utenzi wa Nabii Isa.Nairobi: Fountain Books Ltd. Ndumbaro, E (2013) Shujaa wa Tendi na Matatizo ya Kijamii.Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Njogu, K na Chimera, R (1999) Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: J.K.F. Njogu, K na Wafula, R (2007) Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: JKF. Nurse, D (1994) Historical texts from the Swahili Coast “Swahili Forum 1 AAP Nam. 37 uk 47-85. Sheikh Abdullah Saley na Al farsy (1984). Qurani Takatifu. Nairobi: The Islamic Foundation Publication. Chapa ya nne. Steere, E. (1870) Swahili Tales as Told by the Natives of Zanzibar: London Sutton, J.E.G. (1966) The East African Coast: A Historical and Archeological Review. Nairobi: East African Publishing House. TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Toleo la pili) Nairobi: Oxford University Press. United Bible Societies (1952) Bibilia. Nairobi: Scripture Union. 98 Wamitila, K.W. (2002) Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi: Phoenix Werner, A. (1915) The Bantu Coast Tribes of The East African Protectorate.Journal of Royal Anthropological Institute XLV, uk 326-345.