Shaaban Robert: Ashiki Kitabu Hiki
Shaaban Robert: Ashiki Kitabu Hiki
SURA YA NANE
Kabla ya kuanza kuyachambua masuala mbalimbali yanayojitokeza katika mashairi ya diwani hii ya Ashiki Kitabu Hiki, tuichunguze kwanza kwa kifupi historia ya Shaaban Robert.
Shaaban Robert alizaliwa tarehe 1 Januari 1909 huko Vibambani, Tanga. Alisoma katika shule mbalimbali Dar es Salaam tangu 1922 hadi 1926, na baada ya hapo alifanya kazi huko Pangani, Longido, na baadaye Tanga. Alifariki tarehe 20 Juni, 1962.
Zaidi ya kuandika riwaya na insha, Shaaban Robert aliandika vitabu vingi sana vya mashairi; na kwa kweli ushairi ndio hasa uliompa umaarufu mwandishi huyu. Kati ya vitabu au tuseme diwani za ushairi za mwandishi buyu zipo za Pambo ta Lugha (1948), Marudi Mema (1952), Uhuru (1967), Ashiki Kitabu Hiki (1968), Mashairi ya Shaaban Rohert (1968), Mwafrika Aimba (1969) na Sanaa ya Ushairi (1972).
Ili kuweza kupata undani wa mashairi ya diwani yoyote ya Shaaban Robert ni vizuri kusoma baadhi kubwa ya diwani hizo zilizotajwa, au hata zote, kwani dhamira mbalimbali alizozishughulikia mshairi huyu katika maisha yake ya uandishi zimejitokeza karibu katika kila diwani.
DHAMIRA KUU
Jambo moja linalojitokeza sana katika mashairi mengi ya diwani hii ni lile la malumbano. Malumbano ni majibizano kati ya washairi kuhusu mambo mbalimbali, na aghalabu malumbano hayo huwa na kujisifu kwirigi kunakotolewa kiushairi. Kujisifu huku kulikuwa kwa kawaida sana kati ya washairi ambao waliandika kuringia na kujigambia ushaha wao katika uwanja wa ushairi.
Katika diwani hii mashairi yafuatayo tunaweza kuyaweka katika kundi hfli la malumbano: "Utangulizi" (uk. xi-xii), "Sichi" (uk. 1), "Wapinzi" (uk. 3), "Ngozi ya Simba" (uk. 3-5), "Bahati" (uk. 10), "Ni Wapuzi" (uk. 27-28), "Tosa Haitatukuka" (uk. 35-36). "Situmii Shoka Ukucha Unapofaa" (uk. 37-39), "Mwezi Hauwi Jua" (uk. 39-40), na "Si Kweli" (uk. 40-41).
Ni wazi kuwa mashairi haya ya malumbano hayaishilii katika kiwango cha kujitapa tu kwani zaidi ya kuringia usanii, hapohapo iliwabidi wanaolumbana kuonyesha ujuzi wao wa mambo waliyokuwa wanayajadili. Kwa mfano katika mashairi ya "Situmii Shoka Ukucha Unapofaa" na "Mwezi Hauwi Jua" suala la umuhimu wa ndoa na ubaya wa ujane linajadiliwa kimalumbano. Mojawapo ya mbinu kubwa zinazotumiwa na washairi wakati wa malumbano ni ile ya kufumba kwa kutumia lugha ya kilinge na sanaa ya hali ya juu. Kwa hiyo katika mashairi haya tunakuta matumizi ya tamathali za usemi, nahau, methali, na mifano mingi ya lugha nzito inayozidisha hali ya shairi kuwa tambo. Nia wakati mwingine ni ya kuwadunisha "maadui" hadi wajione kuwa wao ni chawa wadogo tu ambao hawastahili kuuawa kwa shoka wakati ukucha unatosha.
Katika diwani hii. Shaaban Robert anazungumzia hasa mambo yafuatayo
1. Suala la Wanawake
2. Athari za Pesa katika jamii
3. Falsafa kuhusu maisha
4. Hakidhidiyauovu.
Suala la Wanawake
Shaaban Robert ni mmoja wa washairi wa Kiswahili ambao kalamu zao zimelishughulikia sana suala la mwanamke na nafasi yake.katika jamii. Tunaugundua utetezi wake wa mwanamke si katika ushairi tu bali pia katika kazi zake zingine, kwa mfano katika Wasifu wa Siti Binti Saad (1955) na Siku ya Watenzi Wote (1968). Katika kazi hizi anajaribu kuonyesha kuwa haifai mwanamke anyanyaswe au kunyonywa na kugandamizwa na mwanamume. Yafaa - na kwa kweli ni lazima - apate haki na nafasi sawa na ya mwanamume katika nyanja zote za maisha kisiasa, kiutamaduni, na kiuchumi katika jamii. Hata katika Utenzi wa Hati Shaaban Robert anasisitiza kuhusu umuhimu wa kujitegemca na kujiendeleza kwa mwanamke ili asibaki jikoni na kitandani tu.
Katika diwani hii ya Ashiki Kitabu Hiki mashairi yaliyomshughulikia mwanamke ni kama vile "Sijui" (uk. 5), "Nani Atakutendea" (uk. 13). "Kuoa" (uk. 18-22), "Maango" (uk. 22-24) na "Mwanamke" (uk. 32-33).
Katika shairi la "Milango" (uk. 22-24) mshairi anamtetea mwanamke kwa kuonyesha vile ambavyo taasisi ya ndoa inampa nafasi duni. Anasema katika ubeti wa 3.
Ndoa mlango wa tatu,
Mume humiliki vitu,
Ila mke hawi mtu,
Huwa baa kwa kupoa
Taasisi hii katika jamii yenye maisha ya kimwinyi na kibepari humgeuza mwanamke knwa kitu kimojawapo kinachomilikiwa na mwanamume. Na haya yote hutokca ijapokuwa ni kweli kwamba mwanamke ndiye hasa chanzo kikuu cha uhai wa jamii kwani ndiye abebaye mimba na kuzaa - ndiye aliye na jukumu kubwa la kutimiliza jambo la kwanza kati ya matatu muhimu yaelezwayo na mshairi katika shairi la "Matatu Muhimu" (uk.42).
Katika jamii ambayo imezingwa na utamaduni wa kibepari unaoabudu pesa, kila kitu kinachowezckana kugeuzwa kuwa bidhaa ya kuuzika hufanywa hivyo. Mwanamke hali kadhalika huuzwa ama hulazimika kujiuza kama bidhaa zinginezo. Ndiyo sababu katika shairi la "Sijui" mwandishi anauliza:
Bilashi msijivune
Nanyi ni makurumbesa
Hamna jambo jingine
Ila kudai mapesa!
Sijui mwauza nini
Hata mkataka pesa?
Na kuwapasha madeni
Waume makubwa hasa?
Dhamira hii inajitokeza pia katika shairi "Mwanamke" hasa beti za 2 na 5:
Mwanamume kinyozi,
Dada mimi simwezi,
Heri nipande ngazi,
Nende japo kwa Goa.
Sinifanyie kelele,
Maneno mapesa mbele
Nikanunue mchele,
Huko nitakofikia.
Kwa hiyo mashairi mengi yamhusuyo mwanamke katika diwani hii si ya kumtetea hasa bali yanamwonyesha vile ambavyo katumbukia katika maisha ya kibepari yanayoifanya pesa kuwa kiungo pekee kati ya mtu na mtu. Kwa sababu dhamira hii ya fedha ina uzito wake, tuipe nafasi yake mahsusi katika mjadala wetu.
Athari za Pesa Katika Jamii
Mashairi yote katika diwani hii ambayo yameongelea kuhusu pesa yanatupa taswira ya maisha ya kibepari ya kuabudu fedha na kuzifanya kuwa Mungu pekee wa jamii.
Mashairi tuliyokwishayataja ya "Sijui" pamoja na ya "Nyumba za Ngoma" (uk. 12-13), na "Nani Atakutendea?" (uk. 13-14) yanaonyesha jinsi ambavyo imani hii juu ya pesa imeunda soko la kuuzia kila kitu. Ili kuonyesha kuwa si kwa wanawake tu bali pia kwa wanaume, mshairi kaweka beti mbili za mashairi mawili ambazo zina ushabihiano. Ubeti wa mwisho wa "Nyumba za Ngoma" unasema:
Wana wake magunge,
Wamezidi pangapunge,
Heri tusiwahonge,
Wataka kutuibia.
Na ubeti wa mwisho wa shairi la "Nani Atakutendea?" nao unasema:
Na wanaume magunge
Wamezidi pangapunge,
Kina dada tujitenge
Hasara itatujia.
Uhusiano huu wa kibiashara kati ya wanaume na wanawake ndio unaomfanya Shaaban Robert awaite "magunge" na "pangapunge."
Shairi la "Fedha" (uk. 8 - 9) ni kielelezo dhahiri cha vile ambavyo fedha imeyatawala maisha ya jamii. Ubeti wa 4 unatoa muhtasari wa milki hiyo ya fedha:
Fedha imevunja nguu,
Milima ikatambaa,
Fedha ni kitu kikuu,
Aliye nayo shujaa,
Hutiiwa na wajuu,
Wa chini wakaridhia.
Halafu mshairi anaendelea kutueleza jinsi ambavyo fedha zimeua utu wa watu, na kuwafanya watu wabaya walio nazo waheshimiwe:
Mtu aliye nafedha,
Japo duni ni kubeli,
Asemafo lina ladha,
Neno lake ikibali,
Hazukiwi na bughudha,
Uongowe huwa kweli.
Hata hivyo baadaye mshairi anatueleza katika ubeti wa 8 kuwa athari za fedha zina ncha mbili: ncha moja huwafikisha watu jehanam, na ya pili huwapeleka peponi.
Shairi la "Simwezi" (uk. 24-25) hali kadhalika linashughulikia suala la athari za fedha na vile ambavyo huumba watu wenye tamaa nyingi, tamaa ishindayo hata ile ya fisi (ubeti wa 5).
Ndoa
Suala la ndoa nalo lilimshughulisha sana Shaaban Robert katika maisha yake ya uandishi. Katika riwaya za Utubora Mkulima na Siku ya Watenzi Wote, na pia katika mashairi yake mengi, Shaaban Robert ameiona ndoa kuwa ni wajibu kwa watu, mradi tu wanaooana wawe watu kufu. Ndiyo sababu hata katika ubeti wa 6 wa shairi la "Kuoa" (uk. 20) mshairi anatuambia:
Kuoa mke si kufu,
Atakuliza machozi,
Kwa mambo yake dhaifu,
Ukonde ubaki ngozi,
Huwezi kumsarifu.
Cheo chako hakiwazi,
Kwake kama upuuzi,
Yafahamu yasemwayo.
Hata hivyo tunagundua kwamba mawazo na falsafa ya mshairi huyu kuhusu ndoa si yale yale daima - uko wakati yanapingana. Kwa mfano, wakati anapopinga ujane na kusisitiza kuhusu umuhimu wa ndoa (tazama mashairi ya "Halali Kitu Akram," "Situmii Shoka Ukucha Unapofaa" na "Mwezi Hauwi Jua") bapohapo yapo mashairi ambayo yanaonyesha kuwa ndoa haina maana sana kwani furaha yake ni adimu sana kupatikana. Shairi la "Kuoa" (uk. 18-22) linaonyesha vile ambavyo ni vigumu kupata mke anayefaa ndoani; shairi la "Simwezi" na la "Milango" yanasisitiza jinsi ambavyo ni vigumu kuwa na ndoa yenye furaha. Kwa hiyo tunaelezwa katika ubeti wa kwanza wa "Milango" kwa mfano, kuwa ndoa ina matata na giza. Kwa ujumla mashairi haya yanasisitizajinsi ambavyo taasisi ya ndoa imeharibika. Ila mshairi haingii ndani zaidi kuchambua hasa chanzo na mzizi wa kuharibika huko.
Falsafa Kuhusu Maisha
Mashairi kadhaa katika diwani hii yanajishughulisha na suala la maana ya maisha. Shairi la "Nyuso Mbili" (uk. 1), kwa mfano, linasisitiza wazo kuwa maisha yana nyuso mbili na kwamba maisha lazima yana mwisho kwani "Maisha ni matembezi ya kukoma tasihili." Kwa hiyo, katika shairi la "Kubadilishana Zamu" (uk. 30) umuhimu wa mabadiliko katika maisha umesisitizwa; na shairi hili linatuasa kuwa hakuna refu lisilo na ncha.
Shairi la "Maswali na Majibu" (uk. 14-18), linatukumbusha shairi lingine maarufu la mshairi huyu huyu liitwalo "Gharika" (linapatikana katika kitabu cha Masomo Yenye Adili). Nalo linaonyesha wasiwasi na machafuko yaliyoenea katika dunia. Katika ubeti wa 3 wa shairi la "Maswali na Majibu" kwa mfano, mshairi anasema:
Dunia imetubana,
Imetuvika masombo.
Tulikwenda kwa mapana,
Tukapiga watu fimbo,
Ngoma ikivuma sana,
Ni kupasuka kiwambo,
Roho vmejaa mambo,
Radha ziko wapi tena?
Malalamiko haya yanarudiwa kwa namna nyingine katika shairi la "Hai" ambamo mshairi anaomboleza kifo cha mwanae, ingawa hapa mshairi anaonyesha pia tumaini jema la faraja ya maisha baada ya kifo. Anasema kuwa japokuwa uhai ni kitu kidogo sana, lakini faraja ipo katika uhai uliopo "huko Ng'ambo hiyo." Mawazo haya ni sawa na yale ayatoayo mwandishi huyuhuyu katika riwaya yake ya Siku ya Watenzi Wote - faraja yake yote iko juu ya siku ya ufufuo wakati watenzi wote watakapopangwa mbele ya Mola wao kupewa thawabu za matendo yao bora. Kwa Shaaban Robert tofauti baina ya masikini na matajiri zitaondolewa tu na Mwenyezi Murigu siku hiyo ya ufufuo. Utatuzi huu wa "kiutopia" ndio msingi mkubwa wa falsafa ya Shaaban Robert kuhusu maisha.
Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa Shaaban Robert kakata tamaa kabisa kuhusu maisha ya hapa duniani. Bado yapo mashairi machache ambayo yanaonyesha kuwa maisha hapa duniani yana uzuri wake. Kwa mfano, shairi la "Dunia Njema" (uk. 28) linaeleza kuhusu uzuri wa maisha. Beti za 2 na 3 zinasisitiza jambo hilo:
Dunia nzuri na mambo yake,
Yana fahari ya peke yake,
Juu sayari ni taa zake,
Chinijohari ardhi yake.
Zulia lake nyasi kijani,
Na majiyake mvua mbinguni,
Kushuka kwake milele shani,
Sifa ni zake Mola Manani.
Kutetea Haki na Kupinga Uovu
Shaaban Robert alijishughulisha pia na masuala ya kisiasa ya kutetea haki na kupinga unyonyaji, unyanyasaji, na uovu mwingine wote. Katika kitabu chake cha Maisha Yangi na Baada ya Miaka Hamsini tunaona jinsi alivyokuwa anapinga ubaguzi wa rangi uliomfanya Mwafrika kudunishwa, kudharauliwa na kunyanyaswa kutokana na rangi yake. Hate riwaya zake za Kusadikika (1951) na Kufikirika(1951) kimsingi zinatetea haki na kupinga ukoloni.
Katika diwani hii pia yapo mashairi ambayo yanapinga dhuluma na uayonyaji, japokuwa si mengi. Shairi la "Nani Atakutendea" (uk. 13), japokuwa linaeleza mambo mengi mengineyo, hapohapo linapinga unyonyaji wa mtu kufanyishwa kazi bila kupewa malipo:
Kazi bila manufaa,
Nani atakutendea
Sinifanyie hadaa,
Kungwi hakuniusia.Sinifanye hamaki,
Shetani wangu hataki,
Sharti unipe haki,
Ndipo ataputulia.
Hata hivyo ni shairi la mwisho katika diwani hii, shairi la "Shukrani," ndilo linaloiongelea dhamira ya vita baina ya uovu na wema kwa kirefu raidi ya mengine. Shairi hili ni la chereko chereko na lelemama za kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika. Katika kuupokea uhuru huo mshairi anaturudisha ayuma na kutueleza madhambi ya ukoloni mkongwe. Anatueleza jinsi ambavyo wakulima wanatoka jasho kwa faida ya watu wengine. Anasema katika ubeti wa 2 na wa 3:
Kulima na kuchimbua halivunji mapatano,
Hasa tukikumbukia mapito mazito mno:
Na kulima kwa beluwa hali si yetu mavuno,
Wala halikuwa neno kwa wenye kututumia.Kwa wenye kututumia hatukuwa na maneno,
Mchana kutwa wa jua katika ngwe ya mbono;
Kwa jazila ilikuwa ujira senti tano!
Hapakuwa na miguno yote yalivuniliwa.
Shairi hili pia linaonyesha jiasi ambavyo hali hiyo iliathiri hata mahusiano baina ya mke na mume (ubeti wa 4) kukawa na kutoelewana na kutotoshelezana kati yao. Twaelezwa vilevile kwamba, wananchi walizidi kukondeana kwa kutumikishwa katika mashamba ya mbono, ngano, katani, miwa, na kadhalika; mazao ambayo yote yalisafirishwa na kuyanufaisha mataifa ya nje.
Shaaban Robert, basi, anashangilia kupatikana kwa huo uhuru ambao anasema umefutilia mbali unyonyaji na unyanyaswaji huo. Kwa hiyo anamshukuru Mungu kwa huo uhuru; na baada ya napo anaishukuru Uingereza kwa kuikirimia Tanzania. Wakati ambapo ni rahisi kuelewa kwa nini Shaaban Robert anamshukuru Mungu hasa tukijua kuhusu maisha na malezi ya kidini aliyoyapata mshairi huyu, inakuwa vigumu kuzikubali shukrani azitoazo kwa Waingereza katika ubeti wa mwisho. Waingereza hawakukaribishwa na Watanganyika waje kututawala. Walitawala kwa nguvu; ndio wao waliowalimisha na kuwanyanyasa wananchi. Badala ya kuwashukuru dhalimu hawa ingefaa walaumiwe kwa ukoloni wao! Hapa basi, msimamo wa mshairi kuhusu suala la uhusiano baina ya mkoloni na mtawaliwa kuwanyenyekea wakoloni unatetereka.
Dhamira Zinginezo
Zaidi ya dhamira kuu tulizokwishachunguza, diwani hu imeshughulikia dhamira nyinginc ndogondogo kama furaha ("Kama Mfaime," uk. 10), bahati ("Bahati," uk. 10), kweli ("Nyuso Mbili," uk. 1), mahaba na mapenzi ("Nasadiki," uk. 6, "Siwezi," uk. 24; "Nyakati," uk. 26); umalaya ("Nyumba za Ngoma," uk. 12), na mcagineyo.
MATUMIZI YA VIPENGELE VYA FANI
Katika diwani hii, kama ilivyo katika diwani zinginezo za Shaaban Robert, mshairi ameonyesha ustadi wakc wa kutumia mitindo mbalimbali ya ushairi.
Wakati ambapo waumini wa ushairi wa kimapokco wameviita vigezo vya mizani kumi na sita na vina kuwa ndivyo roho ya ushairi wa Kiswahili, Shaaban Robert amepevuka zaidi kwani katuonyesha kuwa si vizuri mshairi atawaliwe na muundo ule ule mmoja daima.
Katika diwani hii mshairi kaandika mashairi ya mizani minne hadi ishirini. Shairi la "Ni Wapuzi"' (uk. 27), kwa nafano, ni la mizani minne tu, na la "Nani Atakutendea" (uk. 13-14) ni la mizani 8, wakati ambapo yako ya mizani 12, 16 na kadhalika.
Kuhusu vina, mashairi mengi humu yamefuatia muundo wa vina wa ab/ab/ab/ab, Muundo huu unamaanisha kuwa vina vya kati vya kila mstari vinafanana katika kiia ubeti, na vya mwisho hali kadhalika. Muundo huu wa vina pamoja na ule wa ab/ba/ab/ba mara nyingi huonekana katika mashairi ya tarbia (au ya unne). Hapo hapa upo muundo wa kufuata jozi za vina ambapo mistari miwili ya kwanza ina vina vyake tofauti na vile vya mistari miwili ya mwisho ya ubeti. Hapa tunapata muundo wa ab/ab/cd/cd.
Pamoja na wingi wa miundo ya vina pia upo ule wa jumla ya mistari ya kila ubeti wa mashairi mbalimbali. Hapa pia ni rahisi kwa msomaji kuainisha mashairi tangu ya uwili hadi yale ya mistari ishirini kwa kila ubeti. Ila yatubidi tu tuelewe kuwa wingi au uchache wa naistari iundayo beti hutegemea jambo linaloongelewa. Wazo dogo tu hupewa mistari michache itakayolifanya liweze kunasa akilini mwa msomaji haraka. Jambo linalohitaji maelezo marefu hupewa mistari mingi, tena mirefu, na aghalabu huwa na beti nyingi zaidi ya zile za mawazo madogo madogo.
Matumizi ya taswira na ya misemo mbalimbali iliyoundwa ndani ya methali na nahau yamesaidia sana katika kuleta uzito wa mawazo yatolewayo. Shairi la "Mnyomele" (uk. 5) ni mfano wa fumbo lililofichika vizuri sana kutokana na matumizi yake ya taswira iniayowakilisha kitu kingine kabisa maishani.
Mshairi pia katumia taswira za maumbile kutoa maudhui ya mashairi yake. Kwa mfano tukiangalia shairi la "Dunia Njema" (uk. 28) tunaona vile ambavyo maumbile yamepewa jina la zulia. Twaiona dunia kuwa kama jengo zuri linalowahifadhi watu.
Katika shairi la "Nyakati" (uk. 26) mshairi katumia taswira ihusuyo fuajira na vile ambavyo lazima yanabadilika, halafu akatumia ustadi wa kulinganisha na kulinganua kwa kutumia tabaini kwa kila jambo. L'fundi huu umefaulu kumdanganya msomaji hadi sehemu ya mwisho ya ubeti wa mwisho ambapo ndipo ukweli kuwa shairi linaongelea mapenzi hujitokeza.
Mashairi mengi ya malumbano ama hutumia taswira nzito nzito au lugha ya kimafumbomafumbo ya kimethali. Mfano ni shairi la "Nazi" (uk. 7') linavyodai kuwa kamwe nazi haiwezi kuvunja jiwe; au lile la "Silumii Shoka Ukucha Unapofaa" (uk. 37-39) ambalo moja kwa moja linafaulu kuwanyamazisha wapinzani kwa kuwafanya wajisikie wadogo wasiofaa mbele ya mshairi huyu. Katika fungu hili tunaweza kuyaweka pia mashairi ya "Wapinzi" (uk. 3), "Ngozi ya Simba" (uk. 3-5), Mwezi Hauwi Jua" (uk. 39-40), na kadhalika.
Shairi la "Halali Kuca" twaweza kulichukua kuwa mfano mzuri wa matumizi ya lugha ya kinahau. Ndoa imeitwa kuwa ni "Nyama ya mafuta.'' Ilivyo, nyama ya mafuta ni nono inayotamaniwa na watu wengi. Mfano huu unaifanya ndoa ionekane kitu bora sana ikilinganishwa na ujane.
Matumizi ya aina hii ya lugha, ishara na taswira, pamoja na upana ws miundo ya vina na mizani katika ushairi wa Shaaban Robert, ndivyo vigezo vilivyosaidia sana kuvafanya maudhui ya mashairi yake yaeleweke vizuri, na kuyafanya mashairi yake kwa jumla yapendwe sana na yampe sifa ya shaha wa malenga.
Maswali
1. Zijadili dhamira muhimu ambazo zimeibuka katika Ashiki Kitabu Hiki. Je, mwandishi kafaulu au kashindwa vipi kuzichambua dhamira hizo?
2. Jadili msimamo wa Shaaban Robert kuhusu wanawake kama ujitokezavyo katika Ashiki Kitabu Hiki.
3. Taswira ya athari za maisha ya kibepari inajitokezaje katika Ashiki Kitabu Hiki?
4. Zijadili falsafa za mwandishi kuhusu ndoa na maisha kama zijitokezavyo katika Ashiki Kitabu Hiki.
5. Yajadili matumizi ya vipengee vifuatavyovya fani kama yalivyojitokeza katika Ashiki Kitabu Hiki:
a) vina na mizani
b) mistari
c) matumizi ya picha (taswira)
d) lughakwajumla
e) ishara.