K.H.A. Akilimali Snow-White: Diwani ya Akilimali



K.H.A. Akilimali Snow-White: Diwani ya Akilimali

SURA YA SABA
Utangulizi
Akilimali Snowhite ni miongoni mwa washairi wachache wa enzi wa akina Sbaaban Robert ambao tuna bahati ya kuwa nao leo hii. Wenzake wengine tunaowcza kuwataja ni akina Sheikh Saadani A. Kandoro, na Shaha wa Malenga Mwinyihatibu Amiri. Hawa na wengine kama akina Shaaban Robert, Mathias Mnyambala na K. Amri Abedi ndio walioendeleza jadi ya kimapokeo katika ushairi wa Kiswahili. Kwa mfano, katika ushairi wao kanuni za vina na mizani zilizingatiwa kuwa ni sheria, ijapokuwa hapa na pale baadhi yao (akiwemo Shaaban Robert) walikiuka "miiko" hiyo. Haya yote yanajitokeza kwa namna hii ama ile katika Diwani wa Akilimali.
DHAMIRA KUU
Katika "utangulizi" wa diwani hii, K. Amri Abedi ametoa muhtasari mzuri kuhusu maudui wa mashairi ya Diwani ya Akilimali kama ifuatavyo katika (uk.iii):
Mashairi haya mazuri yanaeleza kwa wingi mwendo wa siasa wa vijana, na maonyo na maagizo, pamoja na hekima ya mambo yenyewe kwa namna yanavyofasirika katika maoni ya mtungaji wetu stadi. Baadhi ya mashairi ni jawabu ya mashairi yaliyoandikwa na watungaji wengine... Baadhi ya mashairi haya ni mashangilio au masimango. Baadhi ni maombi au dua. Na merigine ni mashairi yanayohusu mapenzi, ndoa na talaka. Mashairi merigine yamo katika sura ya fumbo...
Kwa maneno haya, K. Amri Abedi amemrahisishia mwalimu na nwanafunzi kuyagawa mashairi haya kidhamira, japokuwa si lazima kufuata mpango huu.
Katika kuyajadili maudhui ya diwani hii, sura hii itachunguza jumla ya dhamira sita ambazo ndizo kuu bumu:
1. Mapenzi
2. Maadili na maana ya maisha
3. Ndoa na nafasi ya Mwanamke katika jamii
4. Umuhimu wa kazi
5. Siasa
6. Dini na Mungu.
Mapenzi
Karibu theluthi nzima ya mashairi ya Diwani ya Akilimali inashughulika na dhamira ya mapenzi au mahaba baina ya wanaume na wanawake. Kati ya mashairi havo yamo ya "Daima Nilikiwaza" (uk. 5), "Enenda Mwana Kunenda" (uk. 8), "Gud Bai Mai Diri" (uk. 11), "Kupenda Kimasikini" (uk. 27), "Kwako Nina Tadhalali" (uk. 30), "Laiti ukisubiri Utapoa Moyo Wako", (uk. 30), "Mapenzi Niliyo Nayo" (uk. 31), "Nala Nikimetameta Moyo Wangu Umetua" (uk. 49), "Nini Dawa ya Mapenzi" (uk. 50), "Nisipomtunza Wangu Nikamtunze wa Nani?" (uk. 52), "Ni Tangu Huniulizi Nimekonda Taabani" (uk. 52), "Nimemshika Mnana" (uk. 53), "Nisalimiye Hidaya" (uk. 55), "Pendo" (uk. 57), "Penzi" (uk. 57), "Sipotaka Niwe Nawe" (Uk. 65), "Simbulizi" (uk. 65), "Tangu Tumefarakana" (uk, 66), "Ua la Moyoni Ua" (uk. 67), "Usiponipenda Wewe" (uk. 70), "Umenipunguwa Hiba" (uk. 70), na "Wazuri Wanao Semwa" (uk. 76).
Mashairi yote hayo yanatoa nyuso mbalimbali za mapenzi na mahaba. Kwa mfano, shairi la "Daima Nilikiwaza" linaonyesha dukuduku linalokuwapo baina ya wapendanao, hasa pale ambapo ulikuwapo ukimya wa kutokuandikiana kati yao.
Katika shairi la "Enenda Mwana Kunenda" tunauona uso wa pili wa sarafu ya mapenzi: kuwa mapenzi siyo mito ya asali na maziwa daima dumu. Katika mapenzi kuna kufarakana na kugombana, pamoja na kukwaruzana hadi hata kuamua kutengana:
Nimechoshwa na vituko, daima vina nikifu,
Moyo sinapumvko, bali mwingi usumbufu,
Enenda ondoka vyako, moyoni unanikifu,

Enenda mwana kunenda, wendako nisalimie.

.................................................................................
Enenda nitapumua, na kubwa sumbuko hili,
Kama mapenzi yaua, kheri potelea mbali,
Na kama ni kuugua, nitapoa siku mbili,

Enenda mwana kunenda, wendako nisalimie.
Shairi lingine linaloonyesha kufarakana kwa wapenzi ni lile la "Sipotaka Niwe Nawe" ambalo linamtaka mmoja wa wapenzi arudishe vyote alivyopewa na mwenziwe.
Hata hivyo, kuagana kwa wawili wapendanao si lazima kuwe kwa shari bali kwaweza kuwa kwa heri, kama tuoneshwavyo katika shairi la "Gud Bai Mai Diri", ambamo mmoja wa wapenzi anamuasa mwenziwe kuwa wakumbukane kwa barua.
Masuala ya mapenzi yameshikamana sana na yale ya hali ya mtu ilivyo, hasa kiuchumi. Hili tunaonyeshwa na mshairi katika shairi la "Kupenda Kimasikini" ambamo twaonyeshwa kuwa katika "kupenda kimasikini, apendwae hana raha." Umasikini hauleti matatizo katika masuala ya mapenzi tu bali hata katika ndoa, kama ubeti wa mwisho wa shairi hili la "Kupenda Kimasikini" unavyosisitiza:
Mpe mema maikazi, nafusi ipate wanda,
Awe nao vijakazi, shamba asiwe wa kwenda,
Mke mfanye azizi, mapenzi si kumdunda,

Kupenda kimasikini, apendwae hana raha.
Kwa hiyo basi, sawa na vile ambavyo maisha ya kuiabudu fedha yametawala nyanja zingine za uhai wa jamii, vivyohivyo taasisi ya ndoa imekumbwa na nguvu hii pamoja na mahusiano ya kimapenzi. Mshairi ameirudia dhamira hii ya mapenzi ya pesa katika shairi la "Penzi" ambamo anaonyesha tena jinsi ambavyo pendo kwa mtu fakiri ni kujiumbua bure. Suala hili tutaliangalia vizuri zaidi wakati wa kuishughulikia dhamira ya ndoa na nafasi ya mwanamke katika jamii.
Baadhi ya mashairi ya mapenzi katika diwani hii hapohapo r.i ya kimaadili. Mathalani shairi la "Kwako Nina Tadhalali" linasisitiza umuhimu wa wapenzi kupatana hata kama wamegombana, wakati lile la "Laiti Ukisubiri Utapoa Moyo Wako" linaasa kwamba katika mapenzi kuna haja ya kuwa na subira kwani harakaharaka haina baraka. Katika shairi hilihili mshairi anayakosoa mapenzi ya nyakati zake kuwa yamegeuka kuwa utani mtupu:
Penzi la sasa utani, sionl wafaidio,
Umebakia utani, kufanya kisingiziio,
Asili hauwaoni, wapenzi wapendanao,

Laiti ukisubiri, utapoa moyo wako.
Mashairi mengi ya mapenzi katika Diwani ya Akilimali yanaonyesha dhahiri ujana mwirigi aliokuwa nao mshairi alipoyaandika. Haya ni yale tunayoweza kuyaita ya "mapenzi ya sili silali" ambayo maneno yake yametiwa chumvi ili kukoleza mapenzi yenyewe. Mathalani, katika shairi la "Mapenzi Niliyo Nayo," mshairi anamweleza mpenziwe:
Mchana kutwa nalia, kwa fikirazo benati,
Moyo wanichechemea, kwa penzi sili siketi,

Mapenzi niliyo nayo, kwako hayana kiyasi.
Kwa wingi yamefurika, mapenzi nikupendayo,
Mwili damu nakauka, kwa kwikwi hata kiliyo,
Na kisha ninasumbuka, haunitulii moyo
Kauli za namna hii zinajitokeza pia katika shairi la "Tangu Tumefarakana," hasa katika ubeti wa pili na wa tatu:
Kwa raha sili silali, si usiku si mchana,
Nimedhoofika hali, sili nisipokuona,
Mpenzi nambiye kweli, lini nitapokuona,

Tangu tumefarakana, nimekonda sina hali.
Nimekonda takiraba, hali nimebadilika,
Sili mwana nikashiba, tangu ulipoondoka,
Rejea nipate tiba, huenda nikatibika,

Tangu tumefarakana, nimekonda sina hali.
Ijapokuwa haya na mashairi mengine tuliyokwishayataja yanaonyesha nguvu za mapenzi, ni wazi kuwa mtu hawezi kuwa analia kila siku kwa siku nzima kwamba hali chakula na halali eti kwa sababu ya mapenzi. Akifanya hivyo hufa. Hata hivyo lugha hii ya "sili silali" ni ya kawaida kwa wapenzi, hasa miongoni mwa vijana ambao ndio kwanza wanauingia ulimwengu wa urafiki baina ya wasichana na wavulana.
Maadili na Maana ya Maisha
Mashairi mengi pia katika Diwani ya Akilimali yanashughulikia maadili na maoni kuhusu maisha kwa jumla. Shairi la kwanza, kwa mfano, linasisitiza juu ya umuhimu wa kufanya na kuheshimu kazi, jambo ambalo lina umuhimu sana katika maisha ya Watanzania hata leo hii. Pia shairi linakazia kuwa mtu hawezi kupata uzoefu wa mambo yote yahusuyo maisha kutoka kwa wazazi wake: lazima awe tayari kufunzwa na ulimwengu, yaani kujifunza kutoka kwa wengine zaidi ya baba na mama yake. Mshairi anasema:
Kazi nilizojifunza, babangu hakuzijua,
Hakujua Kingereza, kuuza na kununua,
Bali kujipendekeza, ndipo mwana nikajua,

Asofunzwa na wazazi, hufunzwa na walimwengu.
Katika shairi la "Aso Sudi na Bahati" mshairi anaeleza jambo tata lihusulo dhana ya "bahati": kuwa kila mwenye kupata jambo huwa analipata kwa "bahati", na kwamba asiye na bahati habahatishi. Shairi hili ni zuri sana kwa majadiliano. Je, mwandishi si anajipinga mwcnyewe anaposisitiza katika baadhi ya mashairi yake kuwa mafanikio yanatokana na juhudi na uhodari katika kazi wakati ambapo hapohapo anadai kuwa ili kufanikiwa maishani mtu hana budi kuwa na bahati?
Shairi la "Ajionae Mbora" (uk.3) linashauri kuwa hakuna haja ya kujiona au kuwa na majivuno. Kwa vile hili ni shairi fupi sana tunaweza kulidondoa lote:
Ajionae mbora, mbora wa jadi yake,
Milele ana hasara, anavunja utu wake,
Apite kihangarara, watu wasimtunulce,

Ajionae mbora, daima ana hasara.
Hili limeungana na la "Akiba si Mbaya" (uk. 3) linaloonyesha umuhimu wa kuweka akiba. Tatizo la shairi la "Akiba si Mbaya" ni kwamba linajaribu kuwaeleza watu kuwa kupata au kukosa kwao hutokana na majaliwa ya Mungu (ubeti wa 5), jambo ambalo leo hii si rahisi kukubalika miongoni mwa wasomaji wengi.
Shairi la "Dunia Rangi Rangile" (uk. 6) ni mfano mzuri pia wa shairi la maadili. Humu mshairi anaeleza umuhimu wa kuheshimu na kujituma katika ufanyaji kazi. Ni shairi linalosisitiza juu ya kujitegcmea, kama asemavyo mshairi katika ubeti wa pili:
Dunia kwa mwanamume, yataka kujichumia,
Kila pembe ujitume, nawe kujisaidia,
Siyo ungoje wachume, ukaliye kutumia,

Dunia rangi rangile, yataka kujichumia.
Katika shairi la "Dunia si Uungwana" (uk. 7), mshairi kaunga mkono maadili anayoyatoa katika "Dunia Rangi Rarigile" ambamo anatuasa kuwa maisha yanataka taratibu, ustaarabu na kuishi vizuri na watu. Maadlii haya yameendelezwa katika shairi la "Dunia Ndiyo Ni Njema" (uk. 8) ambamo mshairi anatueleza kuwa kwa asili mtu si mwema. Shairi hili nalo linatoa kauli tata inayoweza kuonekana ni ya kujipinga yenyewe inaposema "Dunia ndiyo ni njema, wanaadamu si wema." Je, inawezekana tuwe na "dunia njema" yenye "wanadamu wabaya"?
Hata hivyo, katika shairi hilihili Akilimali anasisitiza kuwa ni tabia ya kawaida kwa mwanadamu kuwa karibu nawe wakati wa raha na kukukimbia wakati wa janga:
Wanadamu si wema, zingatia nisadiki,
Sione kukuengama, moyo ukataharuki,
Mtapendana pa nema, pa dhiki hawaoneki,

Dunia ndiyo ni njema, wanaadamu si wema.
Kuwa na fahari kumepigwa vita katika shairi lingine la kimaadili la "Fahari Inafilisi" (uk 9). Shairi hili linasuta tabia ya mtu kujiona kwa mambo ambayo si ya kweli Ubeti wa 3, kwa mfano, unashauri:
Humpotei kundini upendae kusifiwa,
Ingawa awe ngomani, fahari ataitoa,
"Mimikwangu khamsini, nitayari kuzitou",

Fahari inafilisi, hadharini na fahari.
Pamoja na kuepuka ufahari, mshairi anashauri pia kuwa kuna umuhimu wa kufanya mambo kwa uangalifu. Haya anayaeleza katika shairi lake la "Ghafula Inaumiza," shairi ambalo linaungana na lile la "Hasira Ina Hasara" (uk. 11) linalosisitiza kuwa kama mtu asingeyakabili mambo kipupa na kwa hasira hata pale panapoudhi, angekuwa na maisha mazuri sana. Maadili, ya namna hii yanaibuka pia katika shairi la "Hujafa Hujaumbika" ambalo linaeleza umuhimu wa heshima kwa watu, na kusisitiza kuwa kuna haja ya kukwepa majitapo, ujeuri, ufahari na kiburi. Wakati huohuo shain hili ni kama linaeleza pia maana ya maisha: kuwa maisha ya mtu yamo katika mabadiliko mengi kiasi ambacho ni vigumu kwa mtu huyo kujidai kuwa amekamilika kabla hajafa.
Utenzi wa "Hisani" pia ni wa kimaadili unaosisitiza juu ya umuhimu kwa watu kuwa na hisani, fadhili na huruma. Hisani imepewa sifa nyingi katika utenzi huu. Mathalani, imeitwa "tamu kama zabibu," "tamu kama sharubati," nayo "yavuma kama zumari", "husitawi kama shamba" na "hunukia kama tunda".
Katika utenzi huu pia, sawa na tuonavyo katika shairi la "Jalisi Ukiandisi" (uk. 19), mwandishi anasisitiza umuhimu wa kuisbi na watu kiutaratibu, bila mabavu au ugomvi. Ametumia mifano wa Bwana Msosi katika mashairi yote mawili kulisisitiza jambo hili:
Watemi wamefilia, akina Bwana Msosi,
Nguvu walikitumia, wakinyang'anya kwa fosi,
Na wanao wandamia, wawangojea mkosi,

Jalisi ukiandisi, ichungue dunia
("Jalisi Ukiandisi")
Basi dunia sifosi,
Yataka mwendo wa ngisi,
Wawapi kina Msosi,
Nguvu walikitumia?
("Hisani")
Katika beti hizi mbili mshairi anagusia suala la uongozi bora kuwa hautakiwi uwe wa "fosi" na mabavu kama ahokuwa nao Mtemi Bwana Msosi. Utumiaji mabavu umepingwa pia katika shairi la "Kila Mtaka Uluwa" ambamo adili kubwa lipatikanalo ni lile Sa kuwaasa watu wasitumie nguvu bali wawe wavumilivu:
Kupata huwa si nguvu, si vishindo na ghasia,
Kwataka uvumilivu, uukosapo tulia,
Autakae kwa nguvu, jela inamngojea,

Kila mtaka uluwa, dunia aichukia.
Zaidi ya uvumilivu, mshairi pia anahubiri juu ya umubimu wa ujirani mwema na kusaidiana. Pia ahasuta tabia ya watu kutetane ar hata kuingiliana katika unyumba. Haya anayasema hasa katika shairi la "Jirani Yako Ni Ndugu" (uk. 20).
Maadili mengineyo ni yale yanayoeleza umuhimu wa kuwa na tahadhari na uhakika wa matendo yetu, na umuhimu wa kuwapa watoto malezi mema kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo ("Kitendo Ni Majuto" uk. 24); tusiropoke maneno ovyo ("Kinywa Humponza Kichwa," uk. 25); tukwepe upokeaji hongo na rushwa ("Kila Mpenda Rushuwa," uk. 27); uzuri wa subira maishani ("Mume Asiye Subira," uk. 32); na pia tunaaswa kuwa ijapokuwa tabia ya upole na ukimya kwa jumla ni nzuri, lakini sifa hizi ni lazima ziwe za wasiani kwani upole na ukimya unapozidi huweza kuwa na hasara kwetu ("Upole Wachusha," uk. 69).
Kwa jumla, mashairi haya ya maadili ni mazuri kwani yanajaribu kujenga tabia nzuri na mahusiano mazuri pia miongoni mwa wanajamii, Tatizo moja kubwa la maadili ya namna hii ni kwamba yanatoleva kimahubiri mno bila hasa kuchambua chanzo cha matatizo yahusikayo. Kwa mfano, siyo vizuri kusema tu "usiibe'' biia kuangalia ni mambo gani katika jamii yanayomfanya mtu aamue kuiba Inawezekana kabisa kwamba yako matatizo yanayotokana na jamii kugawanyika kati ya matajiri sana waisbio kwa jasho la wengine, na wengine kwa kutoa jasho la mchana kutwa kuwatumikia hao matajiri. Hawa watoa jasho haitakuwa jambo laajabu "waibapo" kutokakwa matajiri hao, na wala si sahihi kuwahubiria na kuwakemea kuwa wasiibe.
Kwa hiyo basi, japokuwa maadili mengi katika mashairi ya Diwani ya Akilimali yanasikilika vizuri sana masikioni, mengi ya hayo pia yamekosa misingi ya kijamii kwa hiyo yanapwaya
Ndoa na Nafasi ya Mwanamke Katika Jamii
Kwa vile suala la ndoa linashirikiana sana na lile la natasi ya mwanamke katika jamii, tutazichambua dhamira hizi kwa pamoja.
Katika shairi la "Mume Asiye Subira" (uk. 32) Akilimali anasema kuwa maisha ya ndoa yanahitaji subira na uvumilivu mwingi:
Subira kitu azizi, ni vyema kisiachiwe,
Subirs ni utoshezi, na mkubwa msadawe,
Wenye subira wapeno, wanaishi pasi yowe,

Mume asiye subira, maisha yumashakani.
Suala la ndoa lilizishughulisha sana kalamu za washairi wa enzi za Shaabn Robert akiwemo Akilimali Snow-White. Hili lilijadiliwa na kulumbaniwa hasa katika gazeti la Mambo Leo. Mashairi merigi yaliyolijadili jambo hili yalieleza ubaya wa ujane, na yalisisitiza kuwa naoa ni wajibu kwa watu wote. Hili tunaliona, kwa mfano, katika shairi la "Oa Mwana Kwetu Oa" (uk. 56).
Mashairi mbalimbali yanayozungumzia ndoa pamoja na uhusiano wa mume na mke, hapohapo yanagusia suala lililokuwa muhimu sana enzi za akina Shaaban Robert: suala la nafasi ya mwanamke katika jamii. Wakati ambapo Shaaban Robert aliwatetea wanawake bila kujipinga sana katika msimamo wake juu ya suala hili, Akilimali amejitahidi kumwinua mwanamke bila kujua kuwa aina ya utetezi aitoayo hapohapo inamdhalilisha sana mwanamke. Tuangalie mifano michache ya jambo hili. Katika shairi la "Mume Asiye Subira" beti za 5 na 7 zasema hivi:
Kazi ya mume kwa mke, ni kumfuza mkewe,
Muradi mlimike, mkeo aongokewe,
Sio kucha kekereke, mkeo umsumbuwe,

Mume asiye subira, maisha yumashakani.
Mke sikumwacha fuvi, sabiliaachiliwe,
Japo mke mjuvi, mfunde pasipo yowe,
Kisha maneno si chumvi, siku moja ayajuwe,

Mume asiye subira maisha yumashakani.
Taswira tuipatayo ya mwanamke napa ni sawa na ya mtoto mdogo mjin'ga ambaye mwalimu wake daima ni mwanamume. Taswira hii imerudiwa katika shairi la "Mke Ni Fingo la Nyumba" (uk. 35), hasa katika beti za 7, 8 na 9:
Muwekee matumizi, sanaa zisiwe haba,
Jitume ufanye kazi, mke apate kushiba,
Na ikifikia mwezi, apate cha kujipamba,

Mke ni fingo la nyumba, hadhari kumchezea.

Umpe mema malezi, atuwe katika nyumba,
Awe nao vijakazi, na vitwana kumpamba,
Msabiliye ghawazi, atumiye kujiramba,

Mke ni fingo la nyuma, hadhari kumchezea.

Kumchezea maizi, mtunze mfano shamba,
Mpambe kwa vidarizi, vya dhahabu kumpamba,
Na kama hivyo huwezi, mpambe japo vya shaba,

Mke ni fingo la nyumba, hadhari kumchezea.
Katika beti hizi tatu, licha ya mwanamke kuonekana kuwa yu kiumbe duni cha kutunzwa na kulelewa, pia iko taswira imdunishayo, ya kumwona kuwa ni pambo la kuyafurahisha macho ya mwanamume. Mwanamke tumwonaye hapa hatofautiani na yule tumkutaye katika Utenv wa Mwanakupona, kwani, aghalabu vijakazi na vitwana hawa waliotajwa huwa wa kike. Hawa tunakutana nao pia katika utenzi wa Sayyid Abdallah A. Nassir wa Al Inkishafi, (Oxford, 1939) wakiwapepea, kuwakanda na kuwaimbia nyimbo za kuwabembeleza wafalme wa mji wa Pate.
Utii, unyenyekevu, na unyorige huo wa mwanamke umesisitizwa pia katika utenzi wa "Mke na Mume" (uk. 42-49). Haya yamejitokeza hasa katika beti za 19-23, za 30-38, na za 44 na 49. Katika beti hizi mwanamke hatakiwi awaze, anahitajiwa angoje "cha kuwaziwa":
19. Mwanamke hapasiki,
Kutaka hiki na hiki,
Mwanamke ana haki,

Kungoja cha kuwaziwa.

23. Mume ni yako hirizi,
Yakupasa kumuenzi,
Mtii kwa kila kav,

Asemalo nyenyekea.

24. Linalompasa mke,
Ndiyo nyumba uishike,
Nyumba ni mume na mke,

Nyumba si mume pekee.
Hapa mwanamke anatakiwa anyenyekee lolote lisemwalo na mumews; atii kama mtoto mdogo tu.
Beti za 24-29 zinasisitiza kuwa nafasi ya mwanamke ni nyumbani, naye hana budi kuisafisha nyumba vizuri. Amalizapo kufanya hivyo ametakiwa asiranderande ovyo bali atulie nyumbani na ajipambe:
31. Unapopata wasaa,
Kupumzika kukaa,
Uwache kugaagaa,

Jikoshe ukipumua.
32. Ebu jitiye utuli,
Unawiri wako mwili,
Uwe mke kulihali,

Jasho baya kuondoa.
Japokuwa kijuujuu mawaidha baya ya kujipamba na kujifanya msafi huweza kusifiwa kwaai hulandana na kaida za afya bora. tuyachunguzapo kwa undani tunagundua kuwa yanamdhalilisha mwanamke kwani anatakiwa ayafanye hayo yote ili kumridhisha mwanamume. Haya yametiliwa mkazo katika ubeti wa 44:
44. Nenda mwendo maridhia,
Mume ukimsikia
Alitakalo sikia,

Mume ukimridhia.
Katika shairi, la "Nala Nikimetameta, Moyo Wangu Umetua'' jambo hilo limerudiwa. Mshairi anafurahi kuwa ana mke anayefuata lolote asemalo:
Moyo wangu umetua, nala nikimetameta,
Mke nilio muoa, mpole hana matata,
Mpole hana udhia, nimwambialo hufata,

Nala nikimetameta, moyo wangu umetua.

Kicheko nakiangua, kwa mke niliopata,
Ndio wangu maridhawa, dumu nikimlafuta,
Mke wangu ni mtawa, nje hapendi kupita,

Nala nikimetameta, moyo wangu umetua.
Taswira sawa na ya beti hizi mbili inajitokeza pia katika shairi la "Nisipomtunza Wangu Nikamtunze wa Nani?" (uk. 52), hasa katika ubeti wa 3.
Kwa Akilimali, ni ushindi mkubwa sana kuwa amepata mke anayefua kwa adabu na upole lolote analomwambia; mke anayetawa ndani ya nyumba Huu ni utamaduni wa kipwani wenye asili ya Uarabu na Uislamu. Leo hii utawa huu pamoja na upole anaoufurahia Snovv-White utaonekana na unyonge wa mwanamke, vitu ambavyo vafaa vipigwe vita. Ukombozi wa mwanamke ambao ni mada muhimu katika mikutano na makongamano mbalimbali duniani unapinga sana adili. Hata tamathali azitumiazo mshairi kumhusu mwanamke leo hii zinaweza zionekane kwa baadhi ya watu kuwa ni za kumdhalilisha zaidi mwanamke badala ya kuwa sifa za kimaendeleo. Mathalani, kumfananisha mwanamke na ua zuri au ndege mzuri (angani ubeti wa 2 wa "Nimcmshika Mnana", uk. 53) kunamgeuza mwanamke na kumfanya pambo tu la kuyafurahisha macho ya mwanamume, kwa hivyo kutaonekana kuwa kunapingana na ukombozi wa mwanamke kutoka katika unyonge wake.
Hata hivyo, kuna mashairi machache ambayo tunaweza kuyaita ya kimaendeleo kuhusu suala la nafasi ya mwanamke katika familia na jamii. Shairi la "Wapenzi Shangilieni Uzazi" (uk. 75), zaidi ya kuonyesha jinsi ambavyo furaha ya ndoa ni kupata watoto, linaungana na lile la "Mke Mzazi Nyumbani" (uk. 41) kuonyesha umuhimu wa mwanamke hasa katika jukumu lake la umama la kuendeleza uhai; jukumu ambalo linataka aheshimiwe na pia apate haki zote, hata za urithi. Umuhimu wa jukumu hili la umama limesisitizwa katika beti za 40-47 za utenzi wa "Radhi" ambamo mshairi anaeleza kuhusu uchungu na maumivu ya uzazi, mzigo ambao kina mama huuvumilia ilimradi waendeleze maisha na uhai wa jamaa na jamii.
Shairi lingine ambalo limeendeleza utetezi huo ni la "Wapeni Vyeo Mabibi" (uk. 74). Ijapokuwa huenda kwa baadhi ya wasomaji utetezi huu leo hautaonekana kuwa na uzito kwani kwa sasa hivi wako viongozi wa kikc serikalini na pia katika mashirika na makampuni, tuzirigatiapo wakari alipoandika bwana Snow White itadhihirika kuwa huu uiikuwa utetezi thabiti ambao pia ni hatua muhimu ya mwanzo katika ukombozi wa mwanamke.
Umuhimu wa Kazi
Hapa na pale katika mashairi ya Diwani ya Akilimali upo msisitizo kuhusu umuhimu wa kufanya na kuheshimu kazi.
Katika shairi la kwanza kabisa la "Asofuzwa na "Wazazi Hufunzwa na UIimwengu" anasema haya kuhusu kazi:
Kiasi nilijifunza, si haba kwa kubabia
Nitokapo napendeza, kazi njema natumia
Ni vigumu kuibeza, jinsi inanielea
..........................................................
Haifai kupuuza, kwa kitu usichojua,
Jaribu kupeleleza, na kisha ukichungua
Nia unapoikaza, hushindwi kitu kujua

Asofunzawa na wazazi, hufunzwa na walimwengu
Kazi nilizojifunza, babangu hakuzijua
Hakujua Kingereza, kuuza na kununua
Bali kujipendekeza, ndipo mwana nikajua.
Mawaidha haya yamesisitizwa katika shairi la "Dunia Rangi Rarigile" ambalo lote linatilia mkazo tabia ya kujituma na kuwajibika katika ufanyaji kazi. Shairi hili linasisitiza juu ya umuhimu wa mtu kujitegemea kwa kutolea jasho kila kitu badala ya kusubiri kusaidiwa. Mshairi anasema:
3. Jitume huku na huku, upate kujichumia
Si wajibu kila siku, mwanadamu kungojea
Na usingoje usiku, kakayo kumlilia
Dunia rangi rangile, yataka kujichumia.
8. Kiwacho cha jasho lako, ni chema kwa kutumia
Kulikoni cha mwenzako, kitu cha kusimangia
Akunyimapo mwenzako, lipi litakufalia
Duniarangirangile, yataka kujichumia.
Japokuwa katika shairi la "Unapokosa Shukuru" (uk. 71) kuna mawazo yanayoweza kupingwa na baadhi ya wasomaji kutokana na udhaifu wake wa kuhusisha "kupata" au "kukosa" na mipango ya Mwenyezi Mungu, lakini baadhi ya beti zake (hasa ule wa mwisho) zinapinga uvivu na kusisitiza kuwa mtu hana budi kufanya kazi:
Kazi zote njema sana, sioni wake ubovu
Hata hiyo ya kushona, bali usiwe mvivu
Kazi yeyote kijana, yataka shime na nguvu
Mashairi haya yote, japokuwa ni machache katika diwani hii, yanamfanya Akilimali Snow-White awe na nafasi muhimu katika jamii ya Tanzania ya leo ambamo kazi inathaminiwa kuwa ni kipimo cha utu.
Siasa
Japokuwa dhamira ya siasa tumeitenga hapa, kwa hakika si sahihi kuitenganisha na ile ya umuhimu wa kazi, kwani siasa ni mfumo wa kiitikadi unaofuatwa na jamii, kikundi au tabaka fulani katikajamii, na ufanyaji kazi pamoja na ugawanyaji wa mali ni sehemu ya itikadi. Hata hivyo neno "siasa" hapa tunalihusisha hasa na hali ilivyokuwa nchini katika enzi za ukoloni, wakati Snow-White alipoandika baadhi kubwa ya mashairi yake. Je, mshairi aliisawiri vipi hali hiyo?
Labda tuanze na shairi la "Hongera Kuini Wetu" (uk. 11). Shairi hili lina utata kidogo, kwani tujuavyo, kuini huyo alikuwa mkuu wa Dola ya Uingereza, naye ndiye hasa kiongozi wa ukoloni ulioinyonya na kuigandamiza Tanganyika. Iweje basi mshairi wa Kitanganyika amsifu adui huyu?
Hata hivyo, kwa upande mwingine, inawezekana kabisa kuwa Akilimali alipoandika shairi hili alilitumia kikejeli na labda kuwataka wasomaji wake walisome kila neno katika kinyume chake. Msomaji afanyapo hivyo atagundua ujumbe wa kumlaani kabisa "kuini" huyo.
Shairi la "Kila Ndege na Tundule" (uk. 22) ambalo ni tambo, huweza kuwa la kisiasa pia. Hili linajikita katika uzalendo wa kila mtu kupenda nchi na utamaduni wake ("tundu"), na hili tunaling'amua hasa katika ubeti wa mwisho:
Rabi naomba kabuli, tujalie heri njema
Tuzidishe ikibali, tujifunze taaluma
Tuishi na Kiswahili, lugha ngeni kuzitema

Kila ndege na tundule, tundujingine karaha.
Maudhui ya "Kila Ndege na Tundule" yamesisitizwa pia katika shairi la "Kila Mdharau Chake" (uk. 24) ambalo hali kadhalika tunaweza kulihusisha na uzalendo wa mshairi; na pia katika lile la "Mcheza Kwao" ambamo mshairi anaasa kuwa mtu hana budi kujenga na kuimarisha nchi yake.
Mashairi ya "Nafingwa Ningali Hai" (uk.51), "Rabi Humlipizia Mnyonge Mkosa Haki" (uk.58) na "Walimwengu Tutendeje" (uk.75) ni ya kisiasa yanayotetea haki za wanyongc. Wakati ambapo inaelekea lile la "Walimwengu Tutendeje" limetumiwa kuwafumbia wakoloni kwani "shida" itajwayo yaweza kuwa ukoloni na madhila yake, wakati ambapo "nguruwe" wanaojitokeza kula miche ya mahindi ipandwayo na wananchi huweza kuwawakilisha wakoloni na unyonyaji wao; katika mashairi ya "Nafingwa" na "Rabi Humlipizia" mshairi 'amepinga dhuluma moja kuwa moja. Anasema katika shairi la "Nafingwa":
Napigwa pigo la goti, miguu nimelemewa
Kilicho changu sipati, naomba bila kupewa
Nafingwa kama kijili, nanyimwa kwa kuonewa

Nafingwa ningali hai, kinywa nazibwa kunena.
Zaidi ya kupinga uonevu wa kutoruhusiwa hata kulalamikia maovu yaiiyopo nchini wakati wa ukoloni, mshairi ananung'unikia pia ubaguzi wa rangi uliokuwa umezagaa wakati huo katika shairi hili:
Japo navuta sauti, kauli kutaka toa
Natishwa Snowaiti, kwa rangi niliopewa
Kwa kunifunga kijiti, bila sababu kujua

Nafingwa ningali hai, kinywa nazibwa kunena.
Kwa jumla, mashairi ya aina hii si mengi katika diwani hii, lakini haya machache yanatoa maudhui mazito mno ambayo yanafifisha udhaifu wa mashairi ya aina va lile la "Hongera Kuini Wetu."
Dini na Mungu
Katika uchambuzi wa dhamira mbalimbali tuliokwishafanya tuligusia hapa na pale kuhusu mawazo ya mwandishi huyu juu ya nafasi ya dini au Mungu katika maisha ya jamii. Hapa tutaendeleza tu mjadala huo kwa kuuhusisha na mashairi yanayoshughulikia dhamira hii ama moja kwa moja, au kwa kuitaja tu.
Karibu mashairi yote ya kimaadili yanagusia suala la dini na Mungu. Mwandishi inaelekea yu muumini mkubwa wa dini, naye anaamini kabisa kuwa jambo lolote linalotokea duniani ni kwa amri ya Mungu.
Shairi la "Ikuze Dini ya Kiislamu" (uk. 16) moja kwa moja ni la kuitangaza dini hiyo ambayo mshairi anaamini ndiyo sahihi yenye "nuru" ya kuwaangaza watu wakati zingine zote ni za kikafiri. Anasema haya katika ubeti wa mwisho wa shairi hili:
Yarabi tusheheneze, Isilamu twasongeka
Farijiko tueneze, dhiki hizi kututoka
Ukafiri ukimbize, ukome na kutoweka

Ikuze na inyanyuze, dini ya Kiislamu.
Bwana Shaaban Robert, mshairi mwenzake Akilimali, ubeti kama huo anaupinga kwani alikwishavuka mipaka ya kanisa na msikiti na kusema, hasa katika kitabu chake cha Siku ya Watenzi Wote, kwamba watu wote, bila kujali dini, rangi au taifa, hawana budi kuungana katika juhudi za kuleta maendeleo ya jamii.
Katika shairi la "Nisipomtunza Wangu Nikamtunze wa Nani?" ubeti wa mwisho unasema:
Tamati hapa ni basi, daima nashukurani
Naujutia ukwasi. Mungu alio nihini
Mke wangu angepasi, kwa kila la tamaduni.
Hapa mshairi anaeleza kuwa mtu kuwa tajiri au masikini ni matakwa ya Mungu. Ujumbe huu anaurudia katika shairi la "Unapokosa Shukuru" (uk. 71) anapodai:
Shukuru unachopata, japo ukipata mbovu
Mungu mwenyewe tafeta, nzima pasipo ya nguvu
Bure pesa hutapata, pasipo uelekevu
Unapokosa shukuru, kupata kuna Rabuka.
Mashairi ya namna hii yanaweza kurudisha nyuma maendeleo ya baiakati za watu za ujenzi wa jamii zao hasa watakapohitimisha kuwa matatizo yao na hali zao zote ni mipango ya Mungu.
Katika utenzi wa "Radhi" mshairi kaanza na mtindo wa kimapokeo unaomwita Mungu na kumwomba ampe msaada na baraka katika utunzi wake. Iliaminika miongoni mwa washairi wa kimapokeo kuwa mtunzi wa tenzi hupata kipaji kutoka kwa Mungu, jambo ambalo linazidi kupoteza waumini wengi kila uchao, hasa kwa washairi wa kizazi kipya cha leo. Hawa wanaamini kuwa kila jambo hutokana na mtu mwenyewe, kwa juhudi pamoja na maarifa yake.
Dhamira Zinginezo
Tulizoziangalia si dhamira pekee zijitokezazo katika diwani hii. Ziko zingine ambazo zinajitokeza katika shairi moja moja au mawili hivi. Nyingi ya hizi ni zile zinazojitokeza katika mashairi ya tambo. Mathalani umuhimu wa kujali na kutunza kile alicho nacho mtu ("Bora Shaba Sibadili na Dhahabu," uk. 4); kuheshimu ndoa ("Jozi," uk. 18); hasara za kudodosa mambo, hasa yamhusuyo mtu wa karibu nawe ("Kuku Ukimchungua," uk. 27); na umuhimu wa kutunza siri ("Panapo Wingi wa Ndege," uk. 56).
Shairi la "Kiswahili" (uk. 29) linaungana na yale ya kizalendo kwani linausifu na kuutukuza utamaduni wa Mtanganyika. Mshairi kasema kwamba Kiswahili ni kama "zamaradi", na kuendelea kwamba:
Katika yangu fuadi, Kiswahili ndiyo memo
Nakipenda sina budi, kwafasaha na upimo
Lugha nyingine fisadi, yanivuruga msemo

Ingawa najitahidi, kusema sipati kimo.
Shairi la "Manahodha Kuwa Wengi, Ni Kuzamisha Mashuwa" linaibusha dhamira muhimu hata katika Afrika ya leo. Dhamira hii inahusu uongozi bora, nayo inaeleza kuwa mabavu hayafai katika majukumu ya uongozi.
Japokuwa suala la elimu ni dhamira ndogo kitabuni humu ilinganishwapo na zingine kama za "mapenzi" na "maadili"; linayo nafasi muhimu pia katika diwani hii.
Katika shairi la "Asofunzwa na Wazazi Hufunzwa na Ulimwengu" mshairi amegusia dhamira hii kwa kutuonyesha kuwa elimu si ya darasani tu bali pia hupatikana katika malezi ya wazazi na ya dunia.
FANI KATIKA DIWANI YA AKILIMALI
Wakati wa kujadili maudhui ya diwani hii hapohapo tulikuwa tunagusia kuhusu vipengele mbalimbali vya fani vilivyotumiwa na mshairi kuyaibushia maudhiu hayo. Mathalani, tulieleza juu ya kipengele cha picha au taswira ya mwanamke tuipatayo ambayo inapingana na ukombozi wa mwanamke alioukusudia Akilimali. Haya yote yametokana na ukweli kuwa maudhui na fani ya kazi ya fasihi ni vitu viwili visivyotenganika; kwa hiyo, mara tu mhakiki aanzapo kujadilj kipengele kimoja hujikuta akikihusisha na cha pili, apende asipende.
Katika sehemu hii basi, tutajaribu kugusia vipengele ambavyo hatukuvitaja vinavyochangia sana kwenye uundaji wa fani katika diwani hii.
Kwa jumla mshairi ametumia mtindo wa kimapokeo katika mashairi na tenzi zake zote. Kanuni za vina na mizani zimefuatwa kimapokeo, na mashairi mengi ni unne yenye vina vya kati na vya mwisho vilivyo sawa katika mistari mitatu ya kwanza kwa kila ubeti, lakini vyenye kubadilika katika mistari ya mwisho mwa beti.
Mwandishi amejitahidi kutumia tamathali za mlinganisho, kama hasa zile za sitiari na tashbiha. Hizi ni tamathali za mlinganisho, kama vile alivyouita ustaarabu kuwa ni dhahabu (ubeti wa 7 wa "Dunia Si Uungwana," uk.7). Pia amatumia sifa mbalimbali kuhusu hisani kwa kuiita "zabibu", "sharubati". "zumari", "juba" na kadhalika ("Hisani," uk. 14); mfano mwingine ni ule wa kumwita mke ni fingo la nyumba.Tamathali hizi na zinginezo ambazo msomaji atazigundua katika mashairi mengine, zaidi ya kuipamba lugha zimeongezea pia uzito katika kutupa picha ya kikamilifu zaidi ya jambo lihusikalo.
Zaidi ya tamathali, mshairi ametumia pia methali katika baadhi ya mashairi yake, hasa katika vichwa vya mashairi hayo. Mfano ni mashairi ya "Asofunzwa na Wazazi, Hufunzwa na Ulimwengu," "Hasira Hasara," "Hujafa Hujaumbika," "Haliwezi Mwanadamu Lishindalo Fisi," "Kila Ndege na Tundule," na mengi ya aina hii ambayo matumizi yake ya methali yamesaidia katika kuleta ujumbe uliokusudiwa.
Kuna baadhi ya mashairi ambayo matumizi yake ya vina ni tofauti kidogo. Mathalani, tunaweza kusema kuwa shairi la "Oa Mwanakwetu Oa" lina vina vitatu katika kila mstari kwa sababu neno "oa" linarudiwa katika sehemu zile zile kwenye kila mstari. Marudio haya yanafanya kuwe na kina cha a mwanzoni mwa kila mstari na pia katikati ya kila mstari, na kina kingine mwishoni mwa mstari. Hapa basi, tunapata mpangilio wa vina kama ifuatavyo:
Oa mwana kwetu oa, oa mrembo jamali
Oa mwana mlelewa, mwenye utu mwenye hali
Marudio haya ya neno "oa" hapohapo vanasisitiza umuhimu wa ndoa.
Mshairi anao mtindo wa kutumia maneno ya Kiingereza kwa kuyatohoa. Wakati mwingine haya yameleta ucheshi wa habari anazozieleza. Kwa mfano katika shairi la "Akiba Si Mbaya" katumia neno "poni" kwa maana ya lile la Kiingereza la "pawn", na katika shairi lingine ambalo kichwa chake kinachekesha katumia "Gud Bai Mai Diri" kwa maana ya "Goodbye My Dear" Haya pamoja na maneno "Twenti eiti" - kwa maana ya "Twenty eight" katika shairi la "Ndugu-Arusi'" (uk. 55) huenda kwa wengine yakaonekana kuwa ni kasumba badala ya ucheshi.
Hata hivyo, japokuwa tumevitaja viungo vyote hivyo vya fani, kwa hakika mashairi mengi katika diwani hii yanasomeka moja kwa moja tu bila kuwaha ile lugha ya mvutc ya "kishairi'" tuikutayo katika mashairi mengine ya kimapokeo kama vila ya akina Shaaban Robert au Mathias Mnyampala. Huenda tutakuwa tunamwonea Akilimali Snow-White, hata hivyo, kwa kumtaka awe na kiwango sawa na cha hao mashaha wa malenga kwani hata kiumri alikuwa mdogo sana kwao, na kuizoefu pia hizi zilikuwa juhudi zake za mwanzo. Ndiyo sababu tunamwona Akilimali wakati mwingine akikosa msamiati na kurudiarudia maneno hayohayo si kati -a shairi tu, bali hata ndani ya ubeti huohuo; marudio yanaonekana dhahiri kuwa si kwa ajili ya msisitizo, bali ni matokeo ya uchanga wa Akilimali Snow-White katika bahari ya ushairi wakati alipoandika mashairi ya diwani hii. Mathalani, katika ubeti wa mwisho wa "Dunia Rangi Rangile" neo "mwenzako" isingefaa lirudiwe; na neno "balia" isingefaa kutumiwa mara mbili katika beti zilizofuatana za 17 na 18 za utenzi wa "Mke na Mume."
Bila kujali udhaifu huo tulioutaja, ni dhahiri kuwa Akilimali Snow-White katika Diwani ya Akilimali ameshughulikia dhamira mbalimbali zilizo muhimu na ambazo huwavutia wasomaji wengi vijana.
Maswali
1. Chagua dhamira mbili kati ya zifuatazo ujadili zilivyoibushwa katika Diwani ya Akilimali:
1. Maadili na maana ya maisha
2. Ndoa
3. Siasa
4. Ukombozi wa mwanamke.
2. "Kutokana na kutapakaa kwa dhamira ya mapenzi katika diwani hii, tunaweza kusema kuwa Akilimali kawaandikia vijana zaidi kuliko wazee". Jadili.
3. Linganisha jinsi Akilimali na mshairi mmoja kati ya wafuatao walivyoishughulikia dhamira ya siasa.
1. Theobald Mvungi (Raha Karaha)
2. Saadani Kandoro (Diwani ya Saadani)
3. Francis Semghanga (Teuzi za Nafsi).
4. Je, ni nani kati ya Saadani Kandoro (Mashairi ya Saadani), Francis Semghanga (Teuzi za Nafsi), na Akilimali Snow-White (Diwani ya Akilimali), ambaye amefaulu zaidi katika kuoanisha fani na maudhui ya ushairi wake? Toa sababu na uthibitisho wa hoja zako.
Powered by Blogger.