E. Kezilahabi: Kichomi
E. Kezilahabi: Kichomi
SURA YA TISA
Kwanza kuna umuhimu wa kuelewa kwa kifupi historia ya mwandishi wa kitabu hiki cha Kichomi kabla ya kukichunguza kitabu chenyewe.
Euphrase Kezilahabi alizaliwa mwaka wa 1943 katika Idsiwa kimoja kwenye Ziwa Victoria, Wilaya ya Ukerewe, Musoma, Tanzania. Baada ya masomo yake ya sekondari na Chuo Kikuu alifundisha Kiswahili katika shule za Sekondari za Mzumbe (Morogoro) na Mkwawa (Iringa), kabla ya kujiunga na Idara ya Kiswahili tangu mwaka 1974 hadi sasa.
Kati ya kazi alizokwishaandika mwandishi huyu, ni pamoja na riwaya za Rosa Mistika (1971), Kichwamaji (1974), Dunia Uwanja wa Fujo, na Gamba la Nyoka (1978); pamoja na hadithi fupifupi mbalimbali. Kazi hizi ndizo ambazo zimempa jina na umaarufu katika uwanja wa fasihi. Zote hizi zimeshughulikia masuala muhimu yanayohusu Tanzania ya wakati huu tulio nao. Masuala haya muhimu yameshughulikiwa pia, kama tutakavyoona, katika mashairi mbalimbali ya Kichomi.
DHAMIRA KUU
Maudhui ya Kichomi yameshughulikia nyanja mbalimbali za maisha ya Watanzania. Humu tunagundua masuala ya kisiasa, kidini, kiuchumi, na falsafa zihusuzo maana ya maisha.
Mshairi katizama masuala kadhaa katika diwani hii, ambayo ni pamoja na:
1. Harakati za ujenzi wa jamii mpya
2. Ukoloni mamboleo
3. Falsafa ya maisha
4. Ndoa na Mapenzi.
Harakati za Ujenzi wa Jamli Mpya
Mashairi kadhaa yameshughulikia suala la harakati za ujenzi wa jamii mpya ya Tanzania Mashairi yafuatayo yanaweza kuwa mifano mizuri ya maudhui ya aina hiyo: "Hadithi ya Mzce" (uk. 69), "Mto wa Haki" (uk. 17), "Ukweli" (uk. 31), na "Kuchambua Mchele" (uk. 63).
Madhalani, tunaweza kaichukua beti kadhaa za shairi la "Kuchambua Mchele:"
Habari zilifika kutoka Arusha
Tukaanza kuchambua mchele wa
Ujamaa Macho mbele, macho pembeni tukitoa mchanga
Tukafanya kaburi dogo la mchanga.Tukaanza kutoa chenga, moja moja,
Vidole vikafanya kazi kama cherehani
Usiku na mchana; machoyakauma
Tukafanya kichuguu kidogo cheupe.
Beti hizi mbili za mwanzo zinatoa kielelezo dhahiri cha jitihada za Watanzania za kujenga ujamaa na kuufyeka mfumo wa kinyonyaji wa kibepari. Ni dhahiri kuwa mchele hapa ni ujamaa, ni usawa wa binadamu, ni maisha yasiyo na unyonyaji kati ya mtu na mtu. Na chenga zilizotajwa ni vikwazo vyote ambavyo hujitokeza katika harakati za ujenzi wa ujamaa, ni mfumo wa kibepari unaoruhusu unyonyaji baina ya watu na watu. Hata hivyo shairi halikuishia hapo. Beti za nne na tano zinaeleza jambo lingine:
Chenga na mchanga vikawa vingi sana
Tukapika baada ya muda mrefu wa kazi
Tukaanw kula,
Tukakuta bado mchanga na chenga
Lini tutaula bila mchanga,
Bila chenga?
Hata baada ya Azimio la Arusha kutangazwa bado upo "mchanga na chenga" katika mchele. Ujumbe upatikanao hapa ni kuwa upo umuhimu wa kuwa macho wakati wa kujaribu kujenga jamii ya kijamaa kwani vikwazo na upinzani daima utakuwapo kutoka kwa akina "mchanga na chenga" ambao maslahi yao yanahatarishwa na nguvu hizo za kijamaa.
Dhamira hii imepewa nyuso mbalimbali; kwa mfano, sifa za matendo bora ya mashujaa, sifa za harakati za ukombozi, sifa za utamaduni hasa upande wa lugha, na sifa za amali mbalimbali za kitaifa. Baadhi ya mashairi yanayoshughulikia dhamira hii ni haya yafuatayo: "Jinamizi (uk.l), "Afrika na Watu Wake" (uk.19), "Kumbukumbu" - 1 (uk.39), "Kumbukumbu - II" (uk.40), "Dakika 15 za Uzalendo" (uk. 51), "Mkwawa' (uk. 59), "Namagondo (uk. 67), na "Hadithi ya Mzee" (uk. 69).
Tuchukue shairi la "Mkwawa", kwa mfano. Tuanzie ubeti wa 2:
Jasiri Mkwawa. Ulisafiri kumwona huyo ketilt
Na kwa surc tabiri uliyokuwa nayo
Alikucheka kujicheka
Kwani tangu siku hizo wingu zito
Lilishuka juu ya himaya yake
Na lilipotanduka kweli ikaonekana
Anguko la himaya.
Halafu ubeti wa 4:
Jasiri Mkwawa. Wewe ni sime ya dhahabu
Iliyofuliwa ndaniya moto wa dhawabu,
Uliowashwa kwa nguvu za mahoka
Tone lako moja la damu lilitosha
Kuandika vitabu vingi vya uzalendo
Katika mioyoya vizazi vilivyofuata
Urithi mkubwa wa Taifa la Tanzania na Afrika.
Kwa kutumia mtindo wa majigambo, mshairi ameonyesha na kuyasifu matendo ya kizalendo aliyoyafanya Mkwawa wa Uhehe kupinga utawala dhalimu wa kikoloni.
Katika Ngonjera ya "Dakika 15 za Uzalendo" mshairi kaendeleza dhamira hiyo ya "Mkwawa" kwa kuwataja wazalendo wengine waliofanya matendo bora ya kijasiri. Hapa wapo akina Bushiri, Kinjeketile, Mirambo na Mbumi (ubeti wa 6) na Nyerere (ubeti wa 8). Ngonjera hii pia inalisifu Azimio la Arusha na kuwapinga wapinzani wa Azimio hilo.
Katika "Dibaji" aliyoiandika Farouk Topan twayakuta maneno haya:
Mawazo ya Kezilahabi yaliyomo katika mashairi haya ni mawazo ya kisasa, ni mawazo ya kijana aliyezungukwa na mazingira ya kisasa va kisiasa, kislimu, kijamii na hata ya kidini. Mambo aliyoyaona na kumpata maishani na fikira zilizomjia kichwani zaelezwa katika mashairi haya (uk. x-xi).
Ukoloni Mamboleo
Mazingira yaliyomzunguka na ambayo yamemkuza Kezilahabi ni ya mfumo wa kibepan unaojitokeza katika umbo la ukoloni mamboleo. Kwa hiyo basi, baadhi kubwa ya mashairi katika Kichomi yameshughulikia suala la maana ya ukoloni mamboleo. Kujishughulisha kwa mshairi na ukoioni mamboleo kumelinganishwa na kulinganuliwa na mkabsla wa mshairi mwingine maarufu, Abdilatifu Abdalla, mwandishi wa Sauti ya Dhiki. Mmoja wa wahakiki waliowalinganisha na kuwalinganua washain hawa, M.M. Mulokozi, kasema haya yafuatayo katika jarida la Kiswahili, (Na. 45/2, uk. 103):
Kufanana kwa dhamira wazishughulikiazo washairi hawa wawili siyo jambo lililotokea tu kwa bahati. Washairi hawa wawili wamezaliwa na kukulia katika jamii zilizo na matatizo yale yale ya kisiasa, kiuchumi na kuitamaduni, (matatizo ya ukoloni mamboleo); na nionavyo mimi, wote wanachukizwa na hali halisi za Afrika leo.
Hali hizi halisi twaziona katika mashairi kama yale ya "Afrika na Watu Wake," "Hadithi ya Kitoto," na "Hadithi ya Mzee." Shairi la "Jinamizi" ni mfano mzuri sana kati ya hayo:
Aliinua kichwa chakejuu ya maji
Utawala wa chuma ulimtoboa fuu,
La kichwa na kutupwa mtumbwni
Halafu nilifikiria Afrika Na siasa kwa ujumla
- Mafuvu
Utawala huu wa nguvu na mabavu - utawala wa kinyonyaji unaoshamiri kwa mtutu wa bunduki - umelalamikiwa zaidi na mshairi katika ubeti huu ufuatao, wa shairi la "Upepo wa Wakati" (uk. 4):
Tazama wanavyojinyakulia madaraka
Wanavyoshika pesa kama watoto
Ni picha ya bandia
Askari mwehu na bunduki yake
Na kutunyamazisha!
Kilio hiki kinatukumbusha kile cha waandishi wengine maarufu kama vile akina Ngugi wa Thiong'o, Ayi Kwei Annah, Penina Muhando (Mlama), Ebrahim Hussein, na kadhalika, ambao baadhi ya maandishi yao yameonyesha dhahiri tanzia hii ya Afrika: tanzia ya uhuru uliosalitiwa na baadhi ya viongozi ambao wamejitenga na kuwasahau wananchi waliopigania uhuru huo. Hawa wanashirikiana na mfumo wa kinyonyaji wa ukoloni mamboleo kuzidi kuwanyonya na kuwagandamiza wananchi wa matabaka ya chini - matabaka ya wakulima na wafanyakazi.
Mfumo huu wa ukoloni mamboleo umejaa "uhuru," "demokrasi," "umoja" na "ushirikiano" - vyote vya bandia tupu kama anavyosisitiza mwandishi:
Patulivu, patulivu!
Lakini! Lakini! Lakini! (uk. 5)
Suala hili la mfumo wa ukoloni mamboleo basi, limeshikamana na dhamira ya dhuluma itokanayo na "tawala za chuma" zenye watu wanaowalazimisha wanyonge wawabebe mabegani mwao. Kwa mfano, mistari kadhaa ya "Mto wa Haki" (uk. 17) inatueleza:
Alimpanda mabegani bwana alimkalia
Alipepea hewani kama kidevu cha kabaila
Alinenepa kama kiboko cha Mjerumani
Alipepea kama bendera ya Mwingereza
Sautiyakejuu, elimu kichwani, na pesa mfukoni.
Kumbe basi hata baada ya uhuru wa bendera bado hali za videvu vinene vya kabaila, viboko vya Wajerumani, bendera ya Mwingereza, na elimu itenganishayo wasomi na jamii zao zimeshamiri na kusitawi katikati ya jamii, japokuwa mengine ni kwa kujifichaficha.
Suala zima la ukoloni mamboleo, kama tutakavyoona, limeelezwa na mwandishi kwa kutumia taswira ya "nzige" (uk.71-2) walao bila kikomo, pamoja na "vimatu" - watoto wa nzige ambao wanazidi kuzaliwa kila uchao. Picha hizi zinawakilisha tabaka la vibwanyenye wenye mali na vyeo.
Hii ndiyo hali halisi ya Afrika. Tofauti baina ya ushairi wa E. Kezilahabi katika Kichomi, na wa Abdilatifu Abdalla katika Sauti ya Dhik imo katika utatuzi wa matatizo waliyoyashughulikia. Wakati Sauti ya Dhiki inaelekea kuwa na uhakika wa utatuzi wa hayo matatizo, wakati mwingine katika Kichomi hakuna uhakika huo, na hata utokeapo, ni potofu. Njia mojawapo ya utatuzi aipendekezayo Kezilahabi ni ile ya kurudia "utamaduni" wetu "wa asili." Anasema:
Sikilizeni, simba aliyeumizwa
Bila haya alijikokota kwa unyonge
Mpaka nyumbani, vidonda vikalambwa
Vikapona kwa mateya nyumbani.
Japokuwanjia hii ya kuurudia "uzamani" ili kujipatia utambulisho halisi yaweza kuwa hatua muhimu ya mwanzo wa kujikomboa, lakini hii hatuwezi kuichukulia kuwa ndiyo tu ukombozi kamili.
Dawa ya "vidonda vya ukoloni" ambavyo mshairi katueleza kuwa kwa muda mrefu vimelisumbua bara la Afrika (shain la "Mgomba," uk. 8) 'imeonyeshwa katika shairi la "Afrika na Watu Wake" (uk. 19):
Mimi naona mgonjwa
Bado amelala kitandani
Kama hatutamtoa miiba iliyobaki
Mgonjwa hataweka miguu yake chini
Ili kutembea bila kujiegemeza.
K.K, Kahigi, mmoja wa wahakiki wa E. Kezilahabi, kapendekeza kuwa "kutembea bila kujiegemeza" ni kujitegemea - siasa ambayo ndiyo Tanzania inajitahidi kuijenga. Japokuwa mshairi haonyeshi dhahiri juu ya kujitegemea huko, lakini pendekezo lake twaweza kuliita la kimaendeleo hasa tunapoliunganisha na "dawa" ya Azimio la Arusha, dawa aionayo kuwa itatibu "ugonjwa" wa kijamii wa Tanzania na wa nchi zilizo sawa na Tanzania.
Pia, ili kuondoa matatizo aliyoyashughulikia kama yale ya unyonyaji, unafiki, na mengi mengineyo, mshairi anapendekeza umuhimu wa kuunga mkono harakati zote zinazotetea haki, usawa na amani kote duniani:
Ningekuwa askari ningeoga damu na maji
Ningekanyaga kichwa cha msaliti....................................................................Ningekuwa wa kwanza kutimiza
malalamiko ya watu
Ningeku wa askari wa haki, amani na
mapenzi duniani.
Hata hivyo shairi hili la "Kichwa na Mwili" kidogo linatatanisha kimsimamo kwani, zaidi ya kugusia kuwa ushujaa hautokani na akili bali na mwili tu (angalia ubeti wa pili na wa tatu kwa mfano), shairi hili pia halielekei kuutambua ukweli kuwa vita vya ukombozi vina misingi ya kitabaka kati ya wagandamizaji na wagandamizwaji. Ndiyo sababu mshairi hasemi kuwa ana nia ya kuogelea "katika damu ya wasio katika hatia kwa manufaa ya umma.''
Falsafa ya Maisha
Zaidi ya mashairi yahusuyo uzalendo, ukoloni mamboleo na dhuluma, katika Kichomi kunayo mashain yanayojishughulisha na falsafa zihusuzo maisha kwa jumla. Shairi la "Nimechoka" ni kielelezo kizuri cha mtazamo na falsafa ya mwandishi kuhusu maisha. Katika shairi hili, mshairi anayaona maisha kuwa ni adhabu na tanzia kali: ni kichomi. Maisha yameonyeshwa kuwa yamejaa na kufurika upweke wa ajabu. Haya yote yanamsukuma mshairi katika shairi la "Kisu Mkononi" hadi kwenye hatuaya kutaka kujiua kwa kisu, japokuwa mwishoni anaghairi uamuzi huo.
Ni wazi kwamba falsafa ya namna hii kuhusu maisha imepotoka kwani haisaidii kuendeleza mbele harakati za kujikomboa kwa mkulima na mfanyakazi.
Ndoa na Mapenzi
Kichomi kimeshughulikia pia dhamira ya ndoa na mapenzi. Hapa mshairi kachambua na kubeua kanuni za dini kuhusu ndoa. Angalia shairi lake la "Bikira Mwenye Huzuni" (uk.3), kwa mfano. Katika shairi hili mlshairi anaonyesha vile ambavyo nguvu za kimaumbile zinapingana na zile za kanuni za kujinyima za dini, na vile ambavyo za maumbile hushinda:
Buibui, kanisa, alikuwa
Amekwisha wasomea kitabu cha wmani
Na kusema aliweza kumwoa: lakini
Bila, kwa nguvu za shetanl, kwanza
Kuvunja ule wavu wa uchawi.
Hapohapo ugumu wa maisha ya ndoa umeonyeshwa katika baadhi ya mashairi; kwa mtano shairi la "Wimbo wa Kunguni" (uk. 20), na lile la "Hadithi ya Kitoto" (uk. 42). Ugumu wa ndoa umelinganishwa na ule wa kuingiza bao kwa viatu vilivyochanika, huku mpira ukiwa ni tofali, na goli lenyewe likiwa na upana wa futi moja, tena katika uwanja uliojaa wazomeaji huko kijijini
Kwa kifupi, mashairi mengi yahusuyo ndoa katika Kichomi yanao uelekeo sawa na ule wa falsafa ikatishayo tamaa kuhusu maisha. Mshairi kaichukulia taasisi ya ndoa si kama kitu mahsusi kilichozuka katika mazingira mahsusi bali ni cha watu binafsi tu, cha mtu mmojammoja.
Mtazamo huo wa kukatisha tamaa pia unajitokeza katika mashairi yahusuyo mapenzi. Kwa mfano mashairi ya "Barua ya Mkata kwa Rehema" (kuhusu matatizo ya umasikini katika mambo ya mapenzi); "Hutanihadaa" (matatizo ya mapenzi yaliyochujuka); na "Hadija" (msiba wa mke aliyemuua mumewe) - yote haya yana welekeo unaokatisha tamaa kuhusu mapenzi.
MATUMIZI YA BAADHI YA VIPENGELE VYA FANI
Katika Kichomi Kezilahabi katumia ushairi unaotofautiana na wa kimapokeo. Jambo hili limeelezwa na F. Topan katika "Dibaji" ya kitabu hiki hivi:
Muundo anaoutumia Kezilahabi haukuftingika upande wa mistari: si lazima kila ubeti wa shairi uwe na idadi maalumu ya mistari; haukufungika upande wa vina; si lazima mistari yenyewe iwe na vina; haukufungika upande wa mizani: si lazima kila mstari uwe na idadi sawa ya mizani. Mashairi yale (yaani ya mapokeo) yaimbwa, haya hayaimbwi.
Mashairi ya Kichomi hayakufungwa na kanuni za urari wa vina na mizani wala aina za beti zilizozoweleka katika ushairi wa kimapokeo. Kwa sababu hiyo, mashairi mengi ya Kichomi hayaimbiki kwa mahadhi yaliyozoweleka redioni.
Tofauti hizo za kimuundo zimezusha ugomvi na rnfarakano mkubwa kati ya washairi wa kimapokeo na washairi wa kisasa. Washairi wa kimapokeo hawakubali kuwa haya yaliyomo katika Kichomi nii mashairi. Kwao, kama asemavyo mshairi wctu maarufu J.M.M. Mayoka, vina na mizani ni uti wa ushairi wa Kiswahili; kwao viegezo hivi viwili ndivyo maana ya ushairi. Kundi la akika Kezilahabi na wenzao walisisitiza kuwa vina na mizani siyo roho ya ushairi wa Kiswahili. Wanasisitiza pia kuwa jambo walilolifanya si la uzushi bali wamechota tu amali za kifasihi simulizi na kuzitumia katika fasihi andishi ya Kiswabili, kwani mtindo wautumiao ni wa kawaida sana katika ushairi na nyimbo zinazojitokeza katika fasihi simulizi za makabila yetu mengi. Pia wanaeleza na kudhihirisha kuwa mapambo ya vina na mizani hayapatikani tu kwenye ushairi wa kimapokeo wa Kiswahili, bali pia katika ushairi wa watu wa mataifa mengine kama vile Waarabu.
Matumizi ya Taswira katika Kichomi
Kati ya viegezo vingi vya fani katika ushairi, matumizi ya taswira na ishara ni kiegezo muhimu sana. Hata Kezilahabi mwenyewe kakiri katika Utangulizi wa Kichomi juu ya umuhimu wa sifa hii (uk. xiv).
Taswira na ishara katika ushairi ni ule ufundi wa mshairi wa kusawiri hali au dhana anayoiongelea kwa njia inayogusa vionjo mbalimbali vya mtu, huku ikivipa vionjo hivyo umbo kamili akilini.
Ufundi huu umezagaa katika diwani hii. Shairi ambalo limetajwa na wahakiki wengi kuwa ni maarufu na ni kielelezo cha ufundi wa Kezilahabi wa matumizi ya taswira ni lile la "Nimechokal" Shairi hili lina taswira ambazo hujenga falsafa ya mwandishi kuhusu maisha tangu mwanzo tumwonapo akiwa kafungwa na "waya mgumu wa maisha" usio na mwanzo wala mwisho. Halafu twaelezwa kuwa mshairi kaning'inia "kama ndege" aliyenaswa na mtego wa mtoto mdogo.
Picha hii ya "ndege aliyenaswa" inadhihirisha wazi falsafa ya maisha yaliyo na mashaka, maisha ambayo chanzo wala mwishowe havijulikani. Mambo yanakuwa mabaya zaidi, wakati tumwonapo mshairi akishindwa kudondoka kutoka kwenye "waya mgumu" kwani, twaelezwa, chini yake ipo miti iliyochongoka iliyo tayari kumchoma "kama mshikaki." Kwa hiyo basi huko juu ni kubaya, na chini hali kadhalika ni kubaya.
Hali hii inamfanya mshairi aamue kuendelea kushikilia waya, hana hiari. Waya nao unamkata vidole hadi anatapakaa damu na jasho. Taswira ya damu inaongezea uzito wa dhiki ya maisha. Hata hivyo bado anaendelea kuning'inia hadi machozi yanamtoka, machozi ambayo hana hata uwezo wa kuyapangusa. Baada ya hatua hii tunamwona mshairi akigaragara huku akiomba msaada wa jamii. Hawa hawamjali, wako katika "harakati" za kujisalia wao na roho zao. Halafu ghafla mshairi anatupa picha ya "vichwa vyeupe" vinavyozuka "kati ya vitimbo." Mafuvu haya yanamzomea anapojaribu kuomba msaada, na kati ya wazomeaji inasikika sauti ya baba yake inayomuasa aendelee kushikilia waya; bila kukata tamaa. Mwishoni mshairi anaanza kufumua tabasamu; tabasamu linaloashiria utambuzi wa mshairi kuhusu maana ya maisha.
K.K. Kahigi ametoa muhtasari wa picha na ishara za "Nimechoka" kama ifuatavyo:
Waya mgumu unawakilisha dhiki na machungu ya maisha; mtu anayening'inia katika waya hiyo ana-wakilisha upweke; vitimbo vinawakilisha vitu vinavyo-sababisha kifo; watu wanaosali wanawakilisha mtazamo wa dini juu ya maisha; vichwa vyeupe vinawakilisha mauti, na kichomi kinawakilisha machungu na maumivu ya maisha.
Mchangamano huu wa taswira ndio uelezao ufundi wa Kezilahabi. Mashairi mengi katika Kichomi yametumia mbinu ya taswira Ui kutolea maudhui yake. Kwa mfano taswira ya nzige wagugunao, na walao bila kushiba imetumiwa kueleza uhalisi wa hali ya ukoloni mamboleo (uk. 7071) Ni juu ya kila msomaji kuichambua mbinu hii kwa undani ili afaulu kuelewa ujumbe na falsafa ya mashairi kwa undani pia.
Maswali
1. Chambua dhamira ya ujenzi wa jamii mpya ilivyoshughulikiwa na mshairi wa Kichomi.
2. Ni kwa vipi dhamira ya uzalendo imejitokeza katika Kichomi?
3. Chambua utatuzi wa matatizo uliopendekezwa na mshairi katika Kichomi.
4. Eleza maana ya taswira halafu ujadili matumizi ya taswira katika diwani ya Kichomi.
5. Jadili hoja isemayo kuwa vina na mizani siyo uti wala roho ya ushairi wa Kiswahili kwani katika Kichomi kanuni hizi hazikufuatwa na bado mashairi ya diwani hii ni mazuri sana.