Abdilatif Abdallah: Sauti ya Dhiki




Abdilatif Abdallah: Sauti ya Dhiki


SURA YA KUMI
Inafaa tuelewe tangu mwanzo kuwa mashairi yaliyomo katika kitabu hiki yaliandikwa na mshairi wakati alipokuwa kifungoni huko Kenya tangu 1969 hadi 1972 baada ya "kupatikana na hatia ya kuchochea watu waipindue Serikali ya Kenya kwa kutumia silaha." Bila shaka wote tumekwishasoma maelezo yaliyotolewa katika dibaji ya Sauti ya Dhiki kuhusu kesi na kifungo bicho.
Kwa wasomaji waliokwishasoma mashairi ya akina Ho Chi Minh, Agostino Neto, na wengineo wa aina hiyo, watakubaliana nami kuwa Abdilatif si mpweke katika kuandika mashairi akiwa kifungoni. Tukiweza kusoma kazi ya Ho Chi Minh ya The Prison Diary ofHo Chi Minh na Neto ya Sacred Hope tutaweza kupanua mtazamo wetu kuhusu kitabu hiki cha Sautiya Dhiki.
Mbali na Sauti ya Dhiki, Abdilatif Abdalla aliandika pia Utenzi wa Maisha ya Adamu na Hawaa. Hiki kilikuwa kitabu chake cha mwanzo, nacho kilishughulikia kisa cha kuumbwa kwa mtu kama kilivyoelezwa katika misahafu.
Kinyume na Utenzi wa Maisha ya Adamu na Hawaa uliochimbuka kutokana na imani za kidini, diwani ya Sccuti ya Dhiki imechimbuka kutokana na maisha na hali halisi ya mazingira ya kisiasa, kitamaduni na kiuchumi. Imetokana na kifungo alichoadhibiwa mwandishi, kilichosababishwa na imani zake za kisiasa. Hali hii ndiyo iliyomsukuma kuyatoa mawazo yake; kudhihirisha hasira, imani na matumaini yake; jazba, na dhiki yake. Hiki ndicho kiini kikubwa cha dhamira kuu zinazojitokeza katika diwani hii ya Sauti ya Dhiki.
Katika sura hii tutajadili dhamira kuu za diwani hii, na mwishoni tutachambua fani ya baadhi ya mashairi.
DHAMIRA KUU
Ziko dhamira nyingi ambazo zimeibuka katika diwani hii. Baadhi yake ni hizi zifuatazo:
1. Vita baina ya haki au wema na dhuluma
2. Uzalendo
3. Umuhimu wa subira na kuyaelewa mazingira ya mapambano
4. Umuhimu wa kuwa na matumaini ya ushindi
5. Mjadalawanafsi.
Vita vya Haki au Wema na Dhuluma
Dhamira hii imefungamana na ile ya imani ya mwandishi kuhusu ukweli, nayo ni msingi wa dhamira zinginezo zinazoshughulikiwa katika diwani hii. Mashairi ya "Mnazi: Vuta N'kuvutc" (uk.17), "Mamaetu Afrika" (uk.36), "Usiniuwe" (uk.51), na "Kutendana" (uk.89), ni mifano tunayoweza kuitumia kuwa vielelezo vya dhamira ya vita baina ya dhuluma na haki.
Mshairi, katika shairi la "Mnazi: Vuta N'kuvute" katoa taswira ya mgawanyiko wa jamii kati ya matabaka ya watu wa juu na wa chini. Anaonyesha hasira zake kuhusu mambo yalivyo katika jamii yake ambayo ijapokuwa inajiita huru, uhuru wake ni wa bendera. Baada ya kutoka katika ukoloni mkongwe sasa jamil hiyo iko katika makucha ya ukoloni mamboleo. Serikali iliyokuwa inashikwa na watu weupe sasa imeshikwa na Waafrika, ila inaendeleza itikadi ile ile: kuwanyonya wananchi na kutumikia mfumo wa kibepari. Katika ngonjera hii fupi tunakutana na wahusika wawili: Alii na Badi. Hawa wanawakilisha matabaka makuu mawili yanayopingana katika jamii, kama inavyoonekana kwenye mabishano yao:
ALII
Sababu ya kukwambiya, ya kwamba ushuke tini
Ni kuwa nataka kweya, hukojuu mnazini,
Kwa ajili nami piya, nitunde nazi mwendani

N'shakwelew kwa nini

BADI
Hayo niya kulekesha, unambiyayo ndu yangu
Wataka niteremsha, juu ya mnazi wangu?
Wanistaajabisha, kuniamuru kwa changu

Una kishaa mwenzangu.

ALII
Sina kishaa sinani, akiliyangu kamili
Ni wewe usobaini, pale utipo ukweli
Mnazi ni tangu lini, ukawa ni yako mali?

Sinitendeefeeli
Mahojiano haya yanatoa picha ya tofauti za kitabaka arnbazo zipo katika jamii ya mwandishi. Ni wazi kuwa Badi ni kiwakilisho cha watu wa matabaka yaliyo na njia zote za uzalishaji mali, njia ambazo wamezichukua kwa mbinu za kidhalimu.
Upande wa pili wako akina Alii, masikini hohehahe ambao kwao uhuru umemaanisha kuendelea na umaskini wao. Akina Badi wameteka nyara uhuru uliopatikana, nao hawataki kuuachilia mnazi ili matunda yake yawafaidie walio wengi katika jamii. Mnazi hapa unawakilisha njia kuu za uchumi; na hapa upo mvutano wa kihasama baina ya matabaka mawili tuliyoyataja. Alii pia anawakilisha mawazo ya Abdilatif Abdalla katika shairi hili. Chama cha K.P.U. kilichopigwa marufuku huko Kenya, na ambacho Abdilatif alikuwa mmoja wa viongozi wake, kilinuia kuchukua madaraka ya kisiasa na kiuchumi Kenya, na ndiyo sabahu kilipigwa marufuku na viongozi wake wakahukumiwa kufungwa. Nia na madhumuni ya Chama hicho yanajitokeza katika maneno ya Alii (uk 21):
ALII
Kwa kuwa ni haki yangu, sitahayari kudai
Tatumiya nguvu zangu, madhali ningali hai
Nilipate fungu langu japo kwa ya ghali bei

Nawe hapo uwe hoi
Shairi la "Mamaetu Afrika" nalo ni mfano mzuri wa kielelezo cha vita baina ya haki na dhuluma. Vita hii imetolewa kwa njia ya kilio: kilio kinachosikitikia mambo yalivyokwenda mrama katika bara la Afrika.
Shairi hili linatuchukua katika safari ndefu ya mambo yaliyoisibu Afrika katika historia yake. Beti za 1 hadi 22 zinaonyesha madhambi ya ukoloni - vile ambavya. Afrika ilitawaliwa kwa mabavu, ikanyonywa na kunyanyaswa chini ya ukoloni. Masuaia ya utumwa (ubeti wa 7) na unyonyaji wa hivi sasa wa uchumi katika Afrika (Tazama beti za 9, 10, 11, na 12 na kadhalika) yamejadiliwa humu. Twaelezwa kuwa ni kutokana na kunyonywa kwa Afrika ndiyo sababu mataifa yaliyokuwa yametutawala yameendelea sana leo hii:
Mama tau si wanayo, kupelekwa ugenini
Lau kwamba si maliyo, kubwakurwa mikononi
Hivi leo Bara hiyo, iitwayo Ulayani
Ingekuwa haifani, na kupawa sifa Mama
Ndiyo yaliyowalisha, na kutengenezeya huko,
Miji wakasimamisha, kwa nguvu za mali yako,
Lililowatajirisha, nijwsho la mwili wako,
Damu ya wana wako, ndiyo kuwa hayo Mama.
Lakini dhuluma haiwezi kuendelea daima: lazima ina mwisho. Ubeti wa 22 waeleza haya:
Adui tukamshinda, ikawa sasa atoke
Tukamwamba toka nenda, na kumpiga mateke,
Alikuwa yu wadinda, hakutaka kwenda zake
Kwa nyingi tamaayakeya kukudhulumu Mama.
Shairi linaendelea kutueleza kuwa bado hata hivyo sehemu mbalimbali za Afrika zimo chini ya ukoloni. Hapohapo harakati zingali zikiendelea za kupinga dhuluma hiyo.
Wakati huohuo shairi linaonyesha uso mwingine wa vita hivyo baina ya haki na dhuluma. Harakati hizo zinajitokeza katika jitihada za wananchi za kupigana na ukoloni mamboleo. Humu kuna waasi ambao wametekwa na kufanywa kuwa vibaraka wa mabepari wa ulimwengu kama ubeti wa 33 usemavyo:-
Wanayo hao ni hawa, waletao machafuko
Adui amewanunuwa, kuikosa radhi yake
Watapata masumbuko kwa wayatendayo Mama
Mwito wa umoja wa wanaoonewa na kunyanyaswa unatolewa katikabeti za mwisho za shairi hili. Beti hizi pia zinaonyesha ushindi wa haki juu ya dhuluma; ushindi unaotokana na ati, moyo na uamuzi kuhusu umuhimu wa kuendelea na harakati za ukombczi na za ulinzi.
Sisi hatutakubali, kurudishwa utumwani
Kurudia idhilali, tuliyopawa zamani
Mama wala yako mali, kupelekwa ulayani
Hatarudi mkoloni, tuamini wetu Mama
Tutakulinda vilivyo, pasipo kurudi nyuma
Na vyote ulivyo navyo, vitabakiya salama
Vitabaki vivyo hivyo, kimoja hakitahama
Tutamtafuna nyama, atayekugusa Mama
Tu tayari damu yetu, kwa mikondo imwaike
Tutayari roho zetu, kwa maelfu zitoke
Tukuhami mamaetu, kila baya likwepuke
Hishimayo tuiweke, Afrika wetu Mama.
Mashairi mengi mengineyo, kwa mfano "Usiniuwe," "Kutendana," na kadhalika, yameshughulikia pia dhamira hii ya mvutano baina ya haki na dhuluma. Ni juu ya wanafunzi na waalimu kuyachunguza na kuyajadili kwa undani.
Uzalendo
Ni dhahiri kuwa tunaweza kugundua dhamira hii ya uzalendo katika shairi tulilokwishalichambua la "Mamaetu Afrika," kwani katika shairi hili mshairi anaonyesha dhuluma iliyoikumba Afrika wakati wa utumwa, ukoloni mkongwe, kisha ukoloni mamboleo. Kwa kuililia na Kuitetea Afrika na hata kuwa tayari kumwaga darnu "kwa mikondo," na kupoteza roho "kwa maelfu," mshairi kaonyesha uzalendo wake mkubwa.
Hata hivyo ingembidi mshairi aupe uzalendo wake uchambuzi zaidi kuliko kuishilia tu katika kiwango cha kulaumu vibaraka katika wakati tulio nao. Kuna umuhimu kwa mwandishi yeyote yule anayelishughu-likia tatizo la ukoloni mamboleo kulichunguza kwa mapana na marefu yake hasa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Suala hili pia limeshikamana mwili na roho na mfumo wa kibepari duniani, na ili lichambuliwe kwa undani mfumo huo wa kibepari hauna budi kuchunguzwa kwa kina pia.
Lazima hapa tukiri pia kuwa picha ya mama ambayo mwandishi kaitumia kuieleza Afrika ni picha ionyeshayo undani wa mapenzi ya mwandishi kwa bara hili, mapenzi ambayo yenyewe ni kielelezo dhahin cha uzalendo wake.
Umuhimu wa Subira na kuyaelewa Fika Mazingira ya Mapambano
Dhamira ya umuhimu wa kuwa na subira wakati wa mapambano inajitokeza katika mashairi mengi ya diwani hii. Mashairi ya "Tuza Moyo" (uk. 6), "Jipu" (uk. 7), "Yatakoma" (uk. 32), "Moyo Iwa na Subira" (uk. 48), "Leo Nsingekuwako" (uk. 63) na kadhalika, yanasisitiza kuhusu umuhimu huo wa subira.
Katika "Tuza Moyo" (uk. 6) mshairi anaeleza juu ya ulazinia wa kukoma kwa dhiki na dhuluma, mradi tu wanaoonewa wawe na subira:
Akhi tuliza mtima, uwate kusononeka
Hakuna lisilokoma, siku 'kifika' tatoka
Kusubiri ni lazima, na kumuomba Rabbuka

Wasiya wako 'meshika
Hali hii ya kusubiri inajitokeza pia katika shair; ia "Jipu" linalosisitiza juu ya ulazima wa jipu kuiva na kutoboka. Hapa jipu limetumiwa kipicha tu kuwakilisha hali za maisha katika jamii ya mshairi wetu, hali ambazo zina mikinzano mingi ya kitabaka ambayo hatimaye lazima itaiva' na kulipuka. Ujumbe huu unaonekana pia katika shairi la "Yatakoma" ambalo latueleza kuwa iko siku inakuja ambapo mtima wa mshairi utatuwa atakapokuwa mbali na dhiki aliyo nayo. "Wasiwasi Enda Zako" nalo laendeleza ujumbe wa mashairi hayo tuliyoyataja. Linaufokea na kuukemea wasiwasi alio nao mtunzi, linajaribu kumpa moyo mshairi aendelee kuikabili hali mbaya aliyo nayo- Shairi la "Moyo Iwa na Subira" linasisitiza ujumbe kuwa jipu lazima kwanza liive ndipo litaweza kutumbuliwa. Ni dhahiri kwamba imani ya mshairi juu ya umuhimu wa kuwa na uvumilivu wa kungojea jipu liive ndipo litumbuiiwe, imejikita katika tahadhari inayotokana na kumbukumbu za yaliyompata alipojaribu kulitumbua jipu kabla halijaiva; jaribio ambalo lilimfanya yeye na wenzake wakamatwe na kut'ungwa. Hili nalo limemfanya aamue kubadili mwendo, kama atuambiavyo katika shairi la "Telezi" (uk.24):
6. Japo hivyo zilikuwa, ndiya hazipitiki
Baii mimi haamuwa, kwenendajapo kwa dhiki,
Kumbe vile nitakuwa, ni mfano wa samaki
Ni mfano wa samaki, kuiendeya ndowana
7. Zikanibwaga telezi, sikujuwa kuzendeya
Ningekwenda kwa henezi, yasingenifika haya
Lakini tena siwezi, mwendo huo kutumiya
Sitawata kutembeya, ila tabadili mwendo.
Beti hizi pamoja na zinginezo za mashairi yahusuyo subira hapohapo zinasisitiza umuhimu wa kuyaelewa fika mazingira ya harakati za ukombozi. Kitendo cha kulisubiri jipu hadi liive kinamaanisha kuwa anayelisubiri lazima wakati huo huo awe anayatalii mazingira na kuendelea na harakati zitakazoivisha jipu hilo. Kutalii huku pamoja na uzoefu aupatao mshairi ndio unaomfanya abadili mbinu zake za namna ya kuendeleza harakati dhidi ya adui.
Umuhimu wa Kuwa na Matumaini ya Ushindi
Mshairi asemapo kuwa hataacha kutembea ila atabadili mwendo, hapohapo anaonyesha tumaini na nia ya kuendelea na harakati. Mashairi ya "Tuza Moyo" (uk. 67), "Jipu" (uk. 7), "Siwati" (uk. 9), 'Mamba" (uk. 10). "Yatakoma" (uk. 28), "Mamaetu Afrika" (uk. 48), "Kokoiko" (uk. 64), "Zindukani" (uk. 69), "Nsharudi" (uk. 11), n.k. ni nufaro michache tu ya mashairi mengi yanayoonyesha tumaini la ushindi kalika mapambano. Katika mashairi yote haya upo wito pia wa kuendelea na harakati ili kuzifanya ndoto za matumaini ya ushindi ziwe kweli. Mshairi anashauri kuwa matumaini ya ushindi yasiwafanye watu walioko katika harakati kufikiri kuwa mapambano ni rahisi. Anaanza katika shairi la "Wasafiri Tuamkeni" (uk. 67):
Bado safari ni ndefu, wasafiri tusichoke
Na tusiwe wadhaifu, twendeni hadi tufike
Tusafiri bila hofu, wenye nazo ziwatoke
Huu ndiwo mwanzo wake, siwo mwisho wa safari
Twendeni tukifahamu, kila mtu akumbuke
Safari yetu ni ngumu, si rahisi ndiya yake
Kuna mbia yenye sumu, tunzani tusidunguke
Huu ndiwo mwawo wake, siwo inwisho wa safari.
Mjadala wa Nafsi
Kama inavyoonekana, mashairi mengi ya Abdilatif Abdalla ni ya kimjadala, tena mjadala wenyewe wa kinafsi uchunguzao hali aliyo nayo katika ngome imuumizayo. Mengi ya mashairi tuliyotaja chini ya dhamira ya matumaini ya ushindi yanaingia katika dhamira hii ya mjadala wa nafsi. Angalia kwa mfano mashairi ya "Tuza Moyo," "Siwati," "Telezi," "Yatakoma," "Moyo Iwa na Imani," na kadhalika. Haya yanaungana na mengineyo ambayo yanamwonyesha mshairi akijihoji nafsi yake kuhusu mambo yaliyomfika. Yanaungana pia na mashairi machache ya mapenzi kwa mkewe na kwa rafiki zake, kwa mfano: "Nakukumbuka" (uk. 11), "Lilokuudhi ni Lipi"? (uk. 15), na "Sikakawane na Kimya" (uk. 65), ambayo yanaonyesha kuwa mwanaharakati ni mtu pia aliye na hisi za mapenzi kwa rafiki na wapenzi wake. Haya pia yaonyesha hali ya upweke aliokuwa nao mshairi alipokuwa gerezani.
Kwa kifupi, tunaweza kusema kuwa katika dhamira kuu tulizozijadili tunagundua si sauti ya dhiki tu bali hapohapo ipo sauti ya ujasiri na yenye imani na matumaini makubwa juu ya haki. Ni sauti ya kisiasa ambayo inawakilisha sauti za wanyonge wote ambao leo hii wanapigana na mfumo wa kikoloni mamboleo, mfumo wa ubepari ambao nao unafanya kila mbinu kuwanyonya na kuwagandamiza. Ni sauti ya mwito kwa hao kuungana, kuliivisha jipu, na kulitumbua.
MATUMIZI YA VIPENGELE VYA FANI
Upana wa miundo na mitindo aliyoitumia Abdilatif katika diwani hii umeonyesha ufundi mkubwa wa mshairi huyu. Hapa yapo mashairi ya utatu (tathlitha), na ya unne (tarbia). Ya utatu ni yale ambayo yana mistari mitatu tu katika kila ubeti, kwa mfano yale ya "Mamba" (uk. 10), "Nakukumbuka" (uk. 11), "Yatakoma" (uk. 28), na kadhalika. Haya yanatofautiana na yale ya unne ambayo yamejazana katika diwani hii.
Kimvita ndiyo lahaja aliyoitumia mwandishi katika diwani hii. Lahaja hii ni mojawapo ya zile kuu za Kiswahili zinazozungumzwa Mombasa. Lahaja hii imefanya mashairi mengi humu yaonekane kuwa ni magumu kwa baadhi ya wasomaji ambao hawakuizoea. Ila wakati huohuo imeyafanya mashairi yawe tajiri sana kimsamiati, hasa pale ambapo mshairi kataka wazo lake lielezeke kwa kifupi na linate akilini kwa msomaji. Na aghalabu, ufundi wa namna hiyo umajitokeza hasa pale mshairi alipotumia muundo wa tathlitha akaandika mashairi mafupi mafupi. Pale ambapo mashairi ni marefu na mshairi anaeleza mawazo mapana, muundo wa tarbia umetumika.
Ushairi ni utanzu wa fasihi unaotumia mpangilio wa lugha ya mkato, ya kipicha, na iliyopangwa kwa njia iletayo mapigo mahsusi kufuatana na maudhui yahusikayo. Lugha ya picha ni mojawapo ya nyenzo za kifani alizozitumia Abdilatif katika diwani hii ili kuufanya ushairi wake uwe hai zaidi. Ni mbinu mojawapo aliyoitumia katika karibu kila shairi humu kunasa hisia za msomaji huku akiwapangia mawazo na matukio yaliyofaulu kuumba taswira kamili katika bongo zao. Tuangalie kwa kifupi tu kuhusu matumizi ya taswira katikaSautiya Dhiki.
Kwa jumla mashairi yote yamehusishwa na picha na ishara kuu ya ngome ambayo inajitokeza awali kabisa kwenye dondoo kutoka katika shairi la Muyaka bin Haji (uk. v):
Ngome intuumiza
Naswi tu mumo ngomeni.
Ngome ni ishara ya ukandamizaji, na dhiki yote inayojadiliwa katika SautiyaDhiki imejikita katika taswira hii kuu ya ngome.
Tumeshaona jinsi ambavyo shairi la "Mnazi: Vuta N'kuvute" linavyotuchorca picha ya mtu aliye juu ya mnazi na ya aliye chini. Na taswira hii imetakiwa iwakilishe mvutano kati ya wanyonge walio chini na wanyonyaji walio juu ambao wameshikilia kuwa "nazi" ni zao.
Shairi la "Mamba" (uk. 10) nalo linatutolea picha inayombeza adui:
Kuna mamba, mtoni metakabari
Yuwaamha, kwamba taishi dahari
Taswira ya mamba aliyekakawana na maji ya mto akidai ni yake, na kwamba ataishi daima dumu, inatukumbusha Badi wa "Mnazi: Vuta N'kuvute." Ni ishara ya udhalimu na unyonyaji si katika nchi ya Kenya tu ambako kina "Badi" na "mamba" wanadhulumu umma wa akina Alii, bali ni kiwakilisho kikuu cha wote wale waundao tabaka nyonyaji na dhalimu katika nchi zilizoko chini ya mfumo wa ubepari, uendelezao ubeberu na ukoloni mamboleo.
Katika shairi la "Usiniuwe!" (uk. 51) tunapata picha ya kiumbe dhaifu - mtoto mchanga tumboni - anayelalamika na kudai haki yake ya uhai. Baadhi ya wahakiki wa Abdilatif Abdalla wamelichukulia shairi hili katika kiwango cha mimba ya kawaida tuijuayo na kitendo dhalimu cha kuitoa. Hata hivyo wengine wameipa taswira hii upana wa maana na kusema kuwa mimba hapa inawakilisha kwanza jela ambamo Abdilatif alikuwa kafungwa; na pili jela kuu ambayo ni ya mfumo wa jamii wa kibepari unaojaribu kuwagandamiza akina Alii, na wanyonge wengine.
Picha ya jipu linalozidi kuiva kila uchao tulishaiona katika shairi la "Jipu." Hii inawakilisha hali za kitabaka katika jamii, na jinsi ambavyo hizi zimo katika kukua na kuiva. Ni sawa na volkano ichemkayo ndani kwa ndani na ambayo batimaye hulipuka.
Tunaweza kugundua taswira nyingi nyinginezo katika diwani hii, ambazo zimcongezea uzito wa maudhui yaliyomo kwenye mashairi ya Sauti ya Dhiki. Nyingi za taswira hizo zimeambatana na matumizi mengine ya ishara. Ni juu ya wanafunzi na walimu kuzichambua wenyewe ili kuyapa majadiliano yao ya mashairi haya uzito unaostahili.
Maswali
1. Hiyo sauti ya dhiki inajitokezaje katika diwani ya Sauti ya Dhiki?
2. Zijadili kwa kifupi dhamira kuu za Sauti ya Dhiki.
3. Je, picha iibukayo katika shairi la "Jipu" ni taswira gani? Taswira hiyo ina uhusiano gani na dhamira kuu za diwani hii ya Sauti ya Dhiki?
4. "Kichomi akipatacho mwaodishi wa Kichomi, E. Kezilahabi kinashabihiana sana na sauti ya dhiki aitoayo mwandishi wa Sauti yaDhiki." Ijadili kauli hii kwa kuitolea mifano dhahiri.
5. "Fasihi hupata uhai wake kutokaoa NA hali halisi za jamii, kama vile za uchumi, siasa, na utamaduni kwa jumla." Ni kwa vipi twaweza kuihusisha Swtiya Dhiki na tamko hilo?
6. "Matumizi ya taswira katika diwani ya Sauti ya Dhiki yameambatana na yale ya ishara." Jadili.
7. Kwa kutumia mifano dhahiri, ijadili kauli kuwa upana wa miundo na mitindo aliyoitumia Abdilatif katika diwani ya Sauti ya Dhikiumeonyesha ufundi mkubwa wa mshairi huyu katika kueneza ujumbe wakewakisasa.
Powered by Blogger.