MITAZAMO (NADHARIA) MBALIMBALI JUU YA SANAA ZA MAONYESHO
Kabla hatujaanza kujadili mitazamo hii ni vema tukajua kwanza dhana ya sanaa, kwamba tunaposema sanaa tunamaanisha nini.
Sanaa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifiwa, umbo ambalo mtu hulitumia kueleza hisi zinazomgusa kwa kutoa kielelezo au vielelezo vyenye dhana maalum. Kuna aina kuu tatu za sanaa. Kwanza ni sanaa ambazo uzuri wake hujitokeza katika umbo la kudumu, umbo ambalo linaweza kuhifadhiwa na uzuri wake kuonyeshwa wakati wowote. Hizi ni sanaa za uonyesho. Nazo ni kama vile uchoraji, uchongaji, ufinyanzi, kutarizi n.k. sanaa amabazo hututolea vitu kama vile picha, vinyago, nguo zilizotariziwa, vyungu n.k.
Aina ya pili ya sanaa ni sanaa za ghibu. Hizi ni sanaa ambazo uzuri wake haujitokezi kwenye umbo linaloonekana kwa macho au kushikika bali katika umbo linalogusa hisia. Mifano ni kama vile usahiri, uimbaji, upigaji muziki n.k. uzuri wa sanaa hizi umo katika kuzisikia.
Aina ya tatu ya sanaa ni sanaa za vitendo. Uzuri wa sanaa za aina hii umo katika umbo la vitendo, na ili kuupata uzuri huu yampasa mtu kutazama vitendo vikifanyika. Umbo hili linalazimisha kuwepo kwa mwanasanaa na mtazamaji wa sanaa mahali pamoja kwa wakati mmoja ama sivyo sanaa haikamiliki. Hali hii ndiyo iliyosababisha sanaa hizi za vitendo kuitwa sanaa za maonyesho, kwa sababu lazima wakati zinapotendeka awepo mtu wa kuonyeshwa, maana uzuri wake umo katika vitendo vyenyewe.
Kwa hiyo sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa nne ambazo ni:
i. Dhana inayotendeka
ii. Mtendaji
iii. Uwanja wa kutendea
iv. Watazamaji
Sasa baada ya kuagalia dhana ya sanaa za maonyesho, sasa tuangalie nadharia zinazojaribu kuelezea sanaa za maonyesho. Nadharia hizi zipo tatu ambazo ni:
1. Sanaa za maonyesho ni michezo ya kuigiza, ama ni michezo inayoonyeshwa kwenye jukwaa lenye pazia na mataa mengi ya jadi au ni michezo ya Shakespeare. Huu ni mtazamo mmoja wapo ambapo baadhi ya wataalamu wanaamini hiyo, kwamba sanaa za maonesho lazima zichezwe jukwaani, kuwepo na pazia na mataa mengi.
Tukizingatia nadharia hii huenda tukaamini kuwa sanaa za maonyesho ni tamthilia tu. Kitu ambacho kinaleta mashaka kidogo. Inafahamika kuwa tamthilia ni utanzu ulioletwa na wakoloni hapa Afrika Mashariki. Kwa hiyo, kuamini nadharia hii ni sawa na kusema kuwa hakuna sanaa za maonyesho zenye asili ya hapa Tanzania ama Afrika Mashariki. Au kwa upande mwingine ni sawa na kusema kuwa kabla ya mkoloni kutuletea tamthilia sisi tulikuwa hatuna sanaa za maonyesho zetu wenyewe. Wazo hili si kweli na ni wazo potofu. (Taz. Mhando &Balisidya 1976).
Kimsingi mtazamo huu unatokana na fasili ya sanaa za maonyesho inayodai kuwa sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa za mchezo, mchezaji, uwanja wa kuchezea na watazamaji. Ingawaje ufafanuzi huu ni sawa lakini hata hivyo mtazamo huu ni dhaifu kwani ulitokana na watu waliokuwa wakifafanua sanaa za maonyesho wakiegemea zaidi kwa zile za utamaduni wa kizungu. Ufafanuzi huu haukuzifikiria sanaa za maonyesho zenye ya utamaduni wa Kitanzania.
Dosari kubwa katika ufafanuzi huu imo katika neno mchezo (play). Neno hili lina maana duni likilinganishwa na hali na umuhimu wa sanaa za maonyesho zenye asili ya Kitanzania/Kiafrika. Tukichukua kwa mfano unyago, jando, kusalia mizimu, au masimulizi ya hadithi, ambayo ni mifano ya sanaa za maonyesho zenye asili ya Kitanzania, tunakuta zile sifa zote nne zipo. Isipokuwa tunajua kuwa shughuli zote hizi siyo mchezo na umuhimu wao hauruhusu hata kidogo kuingiza neno mchezo. Shughuli hizi zina maana muhimu ambayo inahusu maisha ya binadamu katika jamii yake. Ni shughuli zinazobeba wazo maalum lenye lengo la kujenga utu wa mwanajamii. Basi vipi tuseme shughuli hizi zina sifa ya mchezo? Wenzetu wazungu wanaridhika na neno hili kwa sababu sanaa za maonyesho za utamaduni wao mara nyingi zinafanywa kwa masihara tu. Sanaa za maonyesho zao zaidi ni kwa madhumuni ya kujiburudisha au pengine kutafuta kipato. Lakini kila aina ya sanaa za maonyesho ya Kitanzania ina dhana fulani ndani yake, kwa mfano dhana kuhusu maana ya maisha, kuhusu utekelezaji wa madaraka ya kiutu uzima, kuhusu ushujaa, mafunzo ya historia ya jamii n.k.
Kwa hiyo basi sanaa za maonyesho za Kiafrika ni dhana zilizo kwenye umbo linalotendeka na siyo mchezo. Kutokana na utamaduni wa Kiafrika tunaweza kusema kuwa: sanaa za maonyesho ni dhana inayotendeka. Na ili dhana hii itendeke anahitajika mtu wa kuitenda (mtendaji). Mtendaji huyu huhutaji uwanja wa kutendea hiyo dhana na wakati akiitenda wanakuwapo watazamaji.
2. Sanaa za maonyesho ni vichekeso au ni maigizo yanayochekesha.
Wazo hili linatokana na historia ya sanaa za Maonyesho hapa Tanzania. Wakati mkoloni alipotuletea sanaa ya Maonyesho ya kikwao sisi tulishiriki katika tamthilia za Shakespeare kama washiriki au watazamaji tu. Kwani tamthilia hizi hazikuwa na maana yoyote kwetu kutokana na kuwa zilibeba na ziliongelea utamaduni wa kizungu. Tulifurahishwa na vile vitendo vilivyofanywa kwenye jukwaa katika tamthilia hizi na hivyo vitendo hivi vilituchekesha tu. Basi jambo kubwa kwa Mwafrika ikawa ni vile vichekesho na hivyo kudhani kuwa jambo muhimu katika tamthilia ni kule kuchekesha kwake.
3. Sanaa za maonyesho ni maigizo.
Wazo hili limetokana na tafsiri mbovu ya neno play ambalo limetafsiriwa kuwa mchezo wa kuigiza. Inawezekana aliyetafsiri neno hili alifuata nadharia za zamani sana za drama, ambapo ilidhaniwa kuwa uigizaji (imitation) ndio kiini cha drama. Hata hivyo nadharia hii ilitupiliwa mbali kwa vile haikudhihirisha kiini hasa cha drama. Tafsiri hii ndiyo imeleta matatizo hapa Tanzania katika kufahamu sanaa za maonyesho. Wengi wamepotoshwa na wazo kuwa uigizaji ndio kiini cha sanaa za maonyesho kama vile neno michezo ya kuigiza linavyoonyesha. Hivyo, hata katika kutazama sanaa za maonyesho za asili wengi wamekuwa wakitazama iwapo kuna uigizaji. Na hapa wengi wanakwama kwani katika unyago, jando, kusalia miungu n.k hakuna uigizaji bali wanaoshiriki wanashika nafasi fulanifulani. Hivyo ni bora kutumia neno tamthilia pale tunaporejelea neno plays.
Kwa ujumla kuwepo kwa mitazamo hii huweza kuwa kumesababishwa na mambo yafuatayo:
Wakoloni kutokutambua ama kwa makusudi ama kwa kutokuelewa kuwa tulikuwa na sanaa za maonyesho za kwetu, hivyo akatuletea drama kama vile anatuletea sanaa mpya ambayo aina yake haikuwepo hapa kwetu. Hivyo, mkazo wa sanaa za maonyesho ulitiliwa katika drama tu.
Mkoloni alitumia mbinu mbalimbali za kufuta vitendo vyote ambavyo hasa ndiyo sanaa zetu za maonyesho. Mfano alitumia dini ya Kikiristo kupiga vita vitendo kama vile unyago, jando, kusalia mizimu n.k ambavyo viliitwa vya kishenzi.
Tafsiri mbovu zinazofuata nadharia zilizopitwa na wakati kama ilivyoelezwa hapo awali.
Kwa hiyo, tukisema sanaa za maonyesho, tunarejelea vitendo maalum vyenye sifa zilizotajwa na kujadiliwa hapo awali. Hata hivyo tutambue kuwa sifa hizi ingawaje ziko sawa lakini kimsingi zinatofautiana katika uzito wake baina ya jamii moja na nyingine. Hatutazamii sanaa za maonyesho za Kihindi kuwa sawa kabisa na zile za Kijapani au za Kiafrika. Ingawa zote ni sanaa za maonyesho zina misingi tofauti kutokana na tofauti za utamaduni wa jamii husika.