KUCHUNGUZA DHAMIRA ZA KIJAMII NA KISIASA KATIKA RIWAYA YA SIRI ZA MAISHA
SURA YA KWANZA
1.0 UTANGULIZI
1.1 Utangulizi
Hii ndio sura ya kwanza katika utafiti
huu ambayo inazungumzia juu ya vipengele mbalimbali vya kiutangulizi katika
utafiti wa kitaaluma kama huu. Utafiti huu unahusu kuchunguza dhamira za
kijamii na kisiasa katika riwaya ya Siri
za Maisha. Siri za Maisha ni
riwaya iliyoandikwa na Emmanuel Mbogo katika mwaka wa 2010 na kuchapishwa na
kampuni ya E & D Vision Publishing. Riwaya hii ina jumla ya sura saba huku
kila sura ikiwa na lengo kuu moja linalozungukiwa. Sura ya kwanza inamhusu
mhusika Pama akitafakari kuhusu mustakabali wa maisha yake na ya familia
kutokana na ukata wa fedha unaomkabili. Sura ya pili inahusu safari ya
Melkizedeki na Pama kwa kutumia chombo cha ajabu kinachoitwa mashua-anga. Hii
ilikuwa ni safari ya kwenda mahali patulivu ili Pama na Melkizedeki waweze
kuandika kitabu kitakachoitwa Siri za
Maisha. Sura ya tatu inahusu uandishi wa kitabu ambapo sasa tayari Pama
amekwishapatiwa kalamu na Melkizedeki akiwa upande wa pili kumuongoza.
Pia, sura ya nne inahusu namna ya
kujenga programu kwa kufuta programu tasa katika akili za wahusika kama Joni.
Sura ya tano inahusu makatazo ya mambo mbalimbali ambayo mtu anatakiwa kuyaacha
ili aweze kufanikiwa katika maisha. Miongoni mwa mambo hayo ni ulevi, woga na
hofu, kukata tamaa, uvivu na uzembe. Sura ya sita inahusu kifo cha Pama. Sura
ya saba inahusu namna ya kuandaa malengo na mipango katika maisha.
Baada ya muhtasari huo wa riwaya, sura
hii ya kwanza imeelezea vipengele vya kiutangulizi katika tasinifu. Vipengele
hivyo ni pamoja na usuli wa tatizo la utafiti, tatizo la utafiti, lengo kuu la
utafiti, malengo mahususi ya utafiti na maswali ya utafiti. Vipengele vingine
ni umuhimu wa utafiti, mipaka ya utafiti na mpangilio wa tasinifu.
>>>>>>INAENDELEA>>>>>>>>>>>>