KUCHUNGUZA DHAMIRA ZA KIJAMII NA KISIASA KATIKA RIWAYA YA SIRI ZA MAISHA
1.2 Usuli wa Tatizo la Utafiti
Riwaya ni moja kati ya tanzu za fasihi
andishi ya Kiswahili unaotumika kueleza visa na matukio kwa kutumia lugha ya
mjazo (Njogu na Chimerah, 1999). Utanzu huu hueleza visa na matukio kwa kina na
kwa undani zaidi kuliko aina nyingine yoyote ile ya fasihi andishi na hata
fasihi simulizi (Mulokozi, 1996). Asili na chimbuko la utanzu wa riwaya
unatajwa kuwa ni masimulizi ya ngano yaliyokuwa yakisimuliwa na bibi au babu
kwa wajukuu wake wakati wanaota moto usiku (Mlacha na Madumulla, 1991). Kuzuka
kwa maandishi, hususani katika karne ya 19 kulikoambatana na mapinduzi ya
viwanda, kulifanya masimulizi ya ngano kuandikwa na ndipo riwaya ilipoibuka.
Mapinduzi ya viwanda yalikuja na mambo mengi yakiwemo ya hali ngumu ya maisha,
uhaba wa ajira, umaskini, maradhi na ujinga, wizi, ubakaji na ufedhuli. Mambo
haya yalihitaji utanzu ambao unaweza kuyasawiri kina bila ya kuacha hata jambo
moja. Utanzu huo si mwingine bali ni riwaya kwani ndio utanzu wenye kubeba
mambo mengi kwa wakati mmoja.
Katika nchi ya Tanganyika na baadae
Tanzania utanzu wa riwaya katika maandishi ulijitokeza katika kipindi cha
ukoloni ambapo kazi mbalimbali za riwaya hususani za Shaaban Robert
ziliandikwa. Kazi hizo ni Utu Bora
Mkulima, Maisha Yangu na Baada ya
Miaka Hamsini, Kusadikika na Kufikirika. Kazi hizi za Shaaban Robert
ziliandikwa kwa ajili ya kusawiri hali ya maisha ilivyokuwa katika kipindi cha
ukoloni. Serikali ya kikoloni inasawiriwa kuwa ilikuwa ni serikali ya mabavu,
nyonyaji, kandamizi na isiyojali masilahi ya wananchi bali maslahi yake yenyewe
(Ambrose, 2014). Hata hivyo, Shaaban Robert alilazimika kutumia ustadi wa fani
ya hali ya juu katika kuwasilisha matukio na visa katika riwaya zake ili
asinaswe na rungu la mkoloni. Kwa mfano, katika riwaya zake za Kusadikika na Kufikirika ametumia mandhari ya nchi inayoelea angani ili kuonyesha
kuwa nchi anayoisawiri siyo hiyo inayotawaliwa na wakoloni bali ni nchi
inayowazika tu mawazoni.
Baada ya kupatikana kwa uhuru wa
Tanganyika mwaka 1961 waandishi mbalimbali wa riwaya walijitokeza na kuanza
kuandika riwaya tofautitofauti. Kazi hizo ni kama vile Kwaheri Iselamaganzi, ambayo ni riwaya ya Kihistoria kazi
iliyoandikwa na Katalambula. Baadaye katika miaka ya 1970 walijitokeza
waandishi wengi zaidi wa riwaya wakiongozwa na Euphrase Kezilahabi aliyeibuka
na riwaya maarufu ya Rosa Mistika (1971).
Kazi hii ya Kezilahabi ilifuatiwa na kazi nyingine za Kichwamaji, Gamba la Nyoka
na Dunia Uwanja wa Fujo. Kazi hizi
pia zilisawiri Azimio la Arusha pamoja na utekelezaji wake. Mwandishi mwingine
aliyeandika kazi zake mara baada ya kupatikana kwa uhuru ni Shafi Adam Shafi
aliyeandika riwaya za Kasri ya Mwinyi
Fuad, Kuli, Vuta N’kuvute na Haini
(Abdallah, 2014).
Riwaya ya Kiswahili hivi sasa imeota
mizizi katika jamii ya Watanzania kwa kusawiri masuala ya kijamii na kisiasa
yanayojitokeza katika maisha ya kila siku ya jamii (Wamitila, 2008). Riwaya ya
Kiswahili hivi sasa inasawiri masuala ya kijamii kama ndoa, elimu, afya,
malezi, burudani, uganga na ushirikina pamoja na uchawi (Mlacha na Madumula,
1991). Pia riwaya za Kiswahili zimekuwa zikisawiri masuala ya kisiasa kama
uongozi mbaya, dhuluma, nafasi ya mwanamke katika jamii, haki na usawa, ufisadi
na rushwa, uwajibikaji na uadilifu (Abdallah, 2014). Miongoni mwa kazi za
riwaya zinazoyasawiri mambo haya ni zile za Emmanuel Mbogo ikiwemo riwaya ya Siri za Maisha. Hata hivyo, mpaka
kufikia sasa hakuna utafiti wa kina ambao umefanywa katika kuchunguza dhamira
za kijamii na kisiasa katika riwaya za Emmanuel Mbogo. Utafiti huu utafanywa
ili kuziba pengo hili la utafiti kwa kuchunguza dhamira za kijamii na kisiasa
katika riwaya ya Siri za Maisha.
1.3 Tatizo la Utafiti
Riwaya
ya Kiswahili imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika kusawiri maisha halisi ya
jamii ya Watanzania tangu katika kipindi cha ukoloni hadi sasa. Katika nchi ya
Tanzania zipo riwaya ambazo zimekuwa zikisawiri maisha yalivyokuwa katika
kipindi cha ukoloni, baada ya ukoloni; wakati wa uhuru na kuendelea mpaka
katika kipindi hiki cha utandawazi (Kalegeya, 2013). Watafiti kadhaa
wamejitokeza katika kutafiti riwaya ya Kiswahili katika dhamira na fani.
Miongoni mwao ni Mlacha (1987), Mlacha na Madumula (1991), Mlacha (1996), Njogu
na Chimerah (1999), Khamis (2007), Kalegeya (2013), Ambrose (2014) na Abdallah
(2014). Kati ya watafiti wote hawa hakuna hata mmoja ambaye amechunguza riwaya
ya Siri za Maisha katika kipengele
cha dhamira za kijamii na kisiasa. Utafiti huu unaofanywa hivi sasa lengo lake
ni kuchunguza dhamira za kijamii na kisiasa katika riwaya ya Siri za Maisha ya Emmanuel Mbogo.
1.4
Lengo Kuu la Utafiti
Lengo kuu la utafiti huu ni kuchunguza
dhamira za kijamii na kisiasa katika riwaya ya Siri za Maisha.
1.4.1
Malengo Mahususi
Utafiti huu una jumla ya malengo
mahususi matatu ambayo ni:
a) Kuchambua
dhamira za kijamii zinazojitokeza katika riwaya ya Siri za Maisha.
b) Kuchambua
dhamira za kisiasa zinazojitokeza katika riwaya ya Siri za Maisha.
c) Kuelezea
mbinu za kisanaa zinazowasilisha dhamira za kijamii na kisiasa katika riwaya ya
Siri za Maisha.
1.4.2
Maswali ya Utafiti
a) Ni
dhamira gani za kijamii zinazojitokeza katika riwaya ya Siri za Maisha?
b) Ni
dhamira gani za kisiasa zinazojitokeza katika riwaya ya Siri za Maisha?
c) Ni
mbinu zipi za kisanaa zilizotumika kuwasilisha dhamira za kijamii na kisiasa
katika riwaya ya Siri za Maisha.
1.5 Umuhimu wa Utafiti
Utafiti huu una umuhimu katika maeneo
mbalimbali ya kitaaluma, kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Kwa upande wa
taaluma, utafiti huu utakuwa ni rejeleo muhimu kwa wahadhiri, walimu na
wanafunzi wanaosoma na kujifunza taaluma za fasihi ya Kiswahili hususani riwaya
ya Kiswahili. Wahadhiri na walimu watautumia utafiti katika kuandaa maandalio
ya somo na kukuza utafiti zaidi katika uwanja wa riwaya ya Kiswahili. Wanafunzi
wa taaluma ya fasihi watautumia utafiti huu katika kujisomea na kuandaa
mapendekezo ya utafiti ambao wataufanya baadae.
Kwa upande wa siasa utafiti huu utaeleza
masuala mbalimbali ya kisiasa ambayo yatawanufaisha watunga sera na
watekelezaji wa sera mbalimbali za maendeleo katika nchi ya Tanzania. Kwa
upande wa masuala ya kijamii vile vile utafiti huu utaibua masuala mbalimbali
ya kijamii ambayo yatahitaji kufanyiwa kazi na wataalamu kutoka katika serikali
na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
Kwa upande wa kiutamaduni, utafiti huu
utajadili na kuweka bayana masuala mbalimbali ya kiutamaduni kuhusiana na
masuala ya ndoa na kufanikiwa katika maisha. Mambo haya yatawanufaisha wasomaji
wote watakaosoma utafiti huu katika maisha yao ya kila siku.
1.6 Mipaka ya Utafiti
Utafiti huu unafanywa kwa lengo la
kuchunguza dhamira za kijamii na kisiasa katika riwaya ya Siri za Maisha peke yake. Mwandishi Emmanuel Mbogo anazo riwaya
zaidi ya hii lakini kulingana na malengo ya utafiti huu ilionekana kuwa riwaya
hiyo moja inatosha. Utafiti huu ni wa kifasihi na umetumia nadharia na mikabala
ya kifasihi katika uchambuzi wake.
1.7 Mpangilio wa Utafiti
Utafiti
huu una jumla sura tano ambapo sura ya kwanza inahusu utangulizi na usuli wa
tatizo la utafiti, sura ya pili inahusu mapitio ya kazi tangulizi na mkabala wa
kinadharia na sura ya tatu inahusu mbinu za utafiti. Sura ya nne inahusu
uwasilishaji, uchambuzi na mjadala wa data za utafiti na sura ya tano ni
muhtasari, hitimisho na mapendekezo.
>>>>>>>>>>INAENDELEA>>>>>>>>