Vipengele Vya Kimsamiati Katika Kamusi Ya Kiswahili Sanifu
Vipengele Vya Kimsamiati Katika Kamusi Ya Kiswahili Sanifu
Utangulizi
Baada ya muda wa zaidi ya miaka kumi ya kutumika kwa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, kwa kifupi KKS, kamusi hii inahitaji kudurusiwa, yaani kuhakikiwa na kusahihishwa ili ikidhi mahitaji ya watumiaji wake wa sasa. Aidha kuidurusu KKS ni muhimu sana kwani Kiswahili kinakua na kuenea haraka mno. Kuiboresha Kamusi ya Kiswahili Sanifu kwa kuingiza msamiati unaotumika sasa ni mchango maridhawa wa kuiboresha lugha yenyewe.
Dhana za msingi
Katika makala haya nitatoa fasili za dhana zihusuzo uwanja wa leksikografia, hususa tofauti na uhusiano uliopo baina ya msamiati, leksika na istilahi. Ingawa hatua hii si ya lazima sana. inasaidia kuelewa zaidi kiini cha mambo yanayozungumziwa. "Istilahi" ni maneno ya kitaaluma, kisayansi, kiufundi, n.k. Haya ni maneno yanayotumiwa katika fani fulani kama vile kemia. fizikia, isimu n.k.
"Msamiati" ni maneno ya lugha yanayotumiwa katika lugha ya kawaida. Msamiati wa kamusi ya kawaida kama KKS ni ule inaotumiwa katika mawasilianao ya kila siku. Leksika inahusu uhalisi wa lugha, na umilisi ujidhihirishao katika ujuzi wa msamiti mwingi. Akieleza uhusiano baina ya msamiati na leksika, J.Picoche anaandika : "Watu watakubaliana kuwa leksika nijumla ya maneno ambayo yamehifadhiwa na lugha kwa ajili ya wazungumzaji ilihali msamiati ni jumla ya maneno yatumiwayo na mzungumzaji ye yote yule katika uwanja wa matumizi halisi" (2). Inaonekana wazi kuwa mpaka baina ya dhana hizi si rahisi kuweka. Msamiati na leksika huingiliana kutokana na matumizi.
Maneno yaliyomo katika KKS yanaweza kutumiwa na mzungumzaji wa kawaida katika mazingira yasiyo rasmi, Hata hivyo, baadhi ya wahakiki wanaiona KKS kama inakosa upekee katika kazi za kileksikografia kwani kwa upande mmoja, KKS ni mpangilio wa maneno yasiyo na fasili za kutosha, na kwa upande mwingine si 'saiklopidia' itoayo maelezo ya ziada ingawa inatoa maelezo ya kuridhisha kuhusu historia, jiografia, n.k. Kamusi ya Kiswahili Sanifu ina makundi mawili muhimu ya msamiati yenye vikundi vidogo vidogo: -msamiati tenda ambao una matumizi mapana, na msamiati tendewa ambao hutumika mara chache. Katika KKS, kuna pia istilahi ambazo zimeingia katika msamiati wa kawaida kutokana na mazoea ya matumizi yanayothibitisha mahitaji ya msamiati huo. Kutokana na ujuzi wa Kiswahili tulionao na uchambuzi tulioufanya, msamiati wa KKS unatumiwa sana na Waswahili wengi, ingawa maneno mengi yanaonekana kama hayatumiki nje ya eneo la Dar es Salaam. Waswahili walio nje ya Afrika ya Mashariki wanapenda kuona kuwa maneno mengi yanayotumika kama Kiswahili katika mazingira yao yanaingizwa katika KKS.
Uchambuzi wa Vipengele vya Kimsamiati katika KKS
Vipengele vya kimsamiati vitachambuliwa kwa kuzingatia kigezo cha kiisimu na kisarufi, na kigezo cha matumizi.
Kigezo cha kiisimu na kisarufi
Kwa kawaida, katika kamusi ya lugha moja vigezo vya aina hii vinatolewa kwa jumla katikamaelezo kwa watumiaji ambao wanatarajiwa kuijua kwa kiasi kikubwa lugha ambayo wanaitafutia maana ya msamiati katika kamusi. Katika KKS, fonetiki haikutiliwa maanani. Ikumbukwe kuwa KKS inatumika duniani kote ambapo Kiswahili sanifu kinazungumzwa, kinafundishwa na kuandikwa: Afrika, Ulaya, Asia na Marekani. Kiswahili kina maneno mengi ambayo matamshi yake yanatatiza wanafunzi wa lugha hii. Kwa mfano, katika ukurasa wa 15 vidahizo barabara (A) na barabara (B) vina matamshi tofauti japokuwa tahajia yake ni moja. Tatizo jingine la matamshi katika Kiswahili ni uwekaji shadda katika neno. Kamusi haimwonyeshi mtumiaji mahali ambapo shadda huwekwa katika neno hususa katika maneno ya kuunganishwa au maneno marefu ya kukopa. Vinginevyo itakuwa kazi ngumu kutambua mahali paJipo na shida.
Sauti za [ ], [ ] na [ ] zisizo katika lugha za Kibantu ziandikwe kama zinapatikana kwa wakati mmoja katika neno moja. Kwa mfano ghaidhi, ghadhabu au thumni. Hili ni muhimu kwa kuwa baadhi ya Waswahili bado wanatawaliwa na lafudhi ya Kiarabu. Vile vile neno ambalo litaonekana kuwa geni sana kwa wazawa wa Kiswahili liandikwe kifonetiki. Nitatoa maoni kuhusu othografia, viambishi wingi, homografu, unyambuaji, n.k. Othografia katika KKS haikuweza kuamua maumbo ya msamiati wa kigeni. Kwa upande mmoja, ari ya kusanifisha inavutwa na ujenzi wa lugha moja, kwa upande mwingine, inapingwa na uzembe wa binadamu wenye sababu za kutobadilisha mazoea yajamii ya kawaida.
Msamiati mwingi uliokopwa kutoka Kiarabu na lugha za kigeni haujulikani kama umeshatoholewa na kuingia kweli katika Kiswahili. KKS unaupa msamiati huu tahajia totauti, k.m.: ihsani/ hisani; ikrahi/kirahi. Baadhi ya athari hizi zinatokana na lugha chasili ambayo inaendelea kulemea Kiswahili.
K.m. (uk. 50) edita /editori chakleti, chokoleti/chakuleti/ chakeleti, (uk 27) bulangeti/blangeti/blanketi. (uk. 20) choki/chaki (uk. 27)
Inafaa kufanya utafiti wa kitakwimu ili kuthibitisha vibadala vinayotumika sana na kupendekezwa kuwa ndio sanifu. Viambishi vya ngeli (umoja, wingi, hali ya kukuza na kudunisha) vimetumiwa kwa majina yote tenabila kujali uhusiano na unyambuaji isipokuwa vitenzi na nomino zenye wingi katika lugha chasili na rnsamiati mwingine Vidahizo havina budi kuanzia na mizizi, lakini ndani ya kila kidahizo, umbo la neno zima lipatikane na mpangilio wa kialfabeti uheshimishwe. Si vizuri kuingiza umbo la wingi wa neno kama kidahizo katika kamusi. Kama wingi huo umeundwa kinyume na utaratibu wa kawaida, lazima uandikwe katika mabano mbele ya umbo la umoja linalohusika. Kwa mfano, kwa nini, azmatnu (uk. 11) limeingizwa kama kidahizo cha wingi wa zimamu, na abidi (uk. 1) kama wingi wa abdi. Utaratibu unaofaa ungekuwa: zimamu (wingi wa azmamu), abidi (wingi wa abdi). Kuhusu nafasi ya viambishi ngeli katika kamusi, Jean na Claude Dubois wanasema:
"Kama wingi ni kuongeza kiambishi cha wingi kwenye kipashio cha maana, hali hii haiundi kidahizo kipya pekee [...]. Kidahizo cha kamusi ni kipashio cha kinadharia, kimefasiliwa kutoka maana ya neno zaidi kuliko kwa maana ya mofimu. Hili linathibitishwa wazi kwa kuwa leksikografia inajikita katika utendaji usemi, siyo katika umilisi wa lugha" (4).
Pengine, wingi wa neno homografu au neno lililonyambuliwa liingizwe kama kidahizo pekee kama kinabeba maana maalum. k.m.:
mori:
(1) ng'ombe jike
(2) hasira kali. (uk. 182)
Neno linaloonekana kuwa na uhusiano na jingine liingizwe na kufasiliwa chini ya kidahizo kimoja. Maneno yenye mofolojia inayokaribiana ki-homografia yatofautishwe lakini yaingizwe chini ya kitomeo kimoja. Kwa nini. neno kisura, (uk.125) lisipatikane chini ya kidahizo, sura, uk. 268. Vivyo hivyo kwa neno mkulima (uk.176) na kilimo (uk.117) yaingizwe chini ya neno lima uk.144). Inafaa maneno yanayohusiana yaandikwe na kurejewa kwenye maelezo ya pamoja. K.m:
kivumbi --> chini ya vumbi (uk. 314)
Kiunguja --> chini ya Unguja (uk. 302)
kitutu --> chini ya tutu (uk. 288).
Kama ikionekana kwamba uhusiano wa maneno hayo ni wa mbali sana, yaani maneno hayana uhusiano wa karibu na mizizi au ambayo hayabadiliki sana, basi yabakizwe kama vidahizo pekee.
K.m. mirathi --> rithi (uk. 242)
ulafi, ulaji --> la: (uk. 142)
mlo --> la: (uk. 142)
malisho --> la: (uk. 142).
Itakumbukwa kuwa ni ukweli usiopingika kuwa vidahizo huorodheshwa kialfabeti kufuatana na herufi zao za mwanzo. Katika lugha za kibantu, unyambuaji una nafasi kubwa sana. Kamusi hii ingeorodhesha msamiati wote ulio na uhusiano wa kiumbo fulani karibu na kidahizo cha msingi. KatikaKiswahili, msamiati mwingi unatokana na unyambuaji, utohozi na uunganishi utegemeao mizizi ya maneno. Mizizi hiyo iandikwe kwa herufi kubwa.
K.m.
- Gogota, king'ota
- Gongonala, kiGong'ota
- kiGogota, kiGotagota
- La, mLo, maLisho --> mLafi, (jina) KuLika, KuLiwa (kitenzi)
Tazama A. Lenselaer (1983)
maReheinu --> Rehema (uk. 282)
mSanii --> Sanaa. (uk. 323)
Kwa vyovyote iwavyo, si mtindo mzuri kutumia viambishi ngeli, viambishi vya wingi, n.k. katika upangaji msamiati katika kamusi. Vipengele hivyo vyote muhimu ni vya kisarufi : vinaonyesha jinsi ya kufanya kazi ya lugha, havina nafasi kubwa katika kamusi. Kadiri viambishi vinavyobadilika kufuatana na matumizi ya lugha, ndivyo vinavyoweza kumzubaisha mtunga kamusi. Kuhusu kategoria za kisarufi zinazopatikana katika KKS, ni wazi kuwa msamiati mwingi kama kawaida ni vitenzi, na majina, vivumishi vya msingi, n.k. Yako pia maneno yanayoainishwa kwa shida kabisa. Mengi ya maneno ya aina hii yameainishwa kama Viingizi na Vielezi.
K.m aisee ! (uk. 4)
abaa! (uk. 1)
cho! lo! cha (uk. 34)
do! la! (uk. 46)
la! (uk. 142)
lo! (145)
Msamiati huu umeingizwa kwa wingi katika KKS ingawa sina uhakika kuwa Waswahili wengi wanajua kuutumia vizuri. Kama sivyo, wanazoea kutumia msamiati mwingine ambao haukuhifadhiwa. Inashauriwa kwamba, upangaji wa maana za maneno katika kategoria zake ufuate utaratibu unaokubalika. Ni vema kuanza na majina, vifuate vitenzi, n.k.
2.2 Kigezo cha matumizi
Katika utangulizi wa KKS, msomaji anajulishwa kuwa msamiati wa kibaharia, kidini na kishairi umeashiriwa. Taarifa hii inamtatiza msomaji asiyetoka katika mazingira ya kibaharia na kidini : kwa nini hadhi hii isipewe maneno mengine? Je inawezekana kuwa watunzi wa KKS hawakufahamu nyanja nyingine zaidi ya hizi?. Kuashiria maneno haya kwa misimbo kumeathiri KKS kwa kuwa inaonekana kuwa mazingira yaliyofanyiwa utafiti sana ni Dar es Salaam (penye dini ya Kiislamu na Kikatoliki, biashara na shughuli za bandarini na baharini, mashairi kama nguzo ya upeo wa utamaduni na fasihi ya Waswahili). Ndiyo sababu umekusanywa msamiati wa kiundani:
hagali [kd] vazi la wanaume la kichwani (uk. 72)
chicha uchafu wa ngozi isiyotahiriwa (uk. 33)
audhubillahi : sehemu ya tamko la Waislam. (uk. 10)
Zaidi ya hayo yapo vile vile majina ya miezi ya Kiislam ambayo yako kwenye mstari mmoja kimatumizi na miezi ya Desemba, Novemba.
Rajabu (uk. 239)
Ramadhani (uk. 239) Dhiklaadi (uk. 45)
Dhilhaji
Ni vema msomaji aelekezwe kwenye majina ya miezi yanayotumika katika lugha ya kawaida ya kila siku. Msamiati mwingine uliupendelewa unaparikana vile vile kwa wingi.
K.m. uwanja wa bahari:
dau [A] chombo kama jahazi (uk. 42)
chenga [A] aina ya samaki. (uk. 32)
Hata hivyo, msamiati ulioandikwa katika KKS unajaribu kuzingira nyanja nyingi za matumizi katika Kiswahili. Hili nijambo zuri. Ipo haja katika kudurusu kamusi hii kuzingatia na kuongeza nyanja mpya pia kwa sababu kuna baadhi ya wachambuzi waonao kuwa KKS inawasaidia zaidi wanafunzi shuleni na kwamba wazungumzaji wa kawaida na wanataaluma hawakushughulikiwa. Ijapokuwa ni zoezi zuri kutenganisha nyanja ya matumizi ya msamiati, tutambue vilevile kwamba kimatumizi, kutegemea watumiaji, wakati na mahitaji, msamiati unaingiliana. Kwa mfano, msamiati wa kiuchumi, unaweza kutumika katika uwanja mwingine. Inapendekezwa kwamba maneno mapya yanayoeleza maendeleo ya kitaaluma na kimaendeleo yaliyofikiwa katika sehemu mbalimbali yachotwe na kuingizwa katika KKS kama vile:
Siasa / Ulinzi / Utawala / Historia / Sheria/, n.k.
K.m. unyonyaji (uk.303)
Farao (uk. 45)
demokrasi (uk. 43)
akida (uk. 4)
Bailojia / Kemia / Fizikia / Zoolojia / n.k.
K.m. aorta (uk.9) /ateri (uk. 10)
choki (uk.34) fefe (uk. 55) atomi/atomiki (uk. 10)
digrii (uk.45) gawa (uk. 65)
batamzinga (uk. 16) kangambili (uk. 99) bakteria (u. 13)
Jamii/Utamaduni/Biashara, Burudani / Vifaa /, n.k.
baleghe (uk. 14)
chibuku (uk. 33)
danguro (uk. 41)
deni (uk. 43)
dadu (uk. 39)
bondia (uk. 21)
gambusi (uk. 64)
dizeli. (uk. 47)
Baadhi ya msamiati katika KKS umekopwa bila sababu. Kiswahili au lahaja za Kiswahili zina maneno mengi ambayo yangeweza kutumi wa katika Kiswahili badala ya haya maneno ya mkopo. Ndiyo sababu. ukusanyaji wa data kumhusisha mzungumzaji akubalikaye kuwa "anasema Kiswahili bila ubaguzi na upendeleo wowote. "Isitoshe hayana budi kutolewa maneno yaelezayo kazi na maisha ya Waswahili kadri kanda yao inavyozidi kupanuka. Mbinu hii isaidie kama ilivyofanya katika maneno.
bunge (uk. 24) na ikulu (uk. 84) kutoka lugha za bara. Kwa kanuni hiyo, neno Mhariri (uk. 169) litumike badala ya edita au editori kutoka "editor" lisilonyambulika vizuri.
Usanifishaji na Usambaaji wa Kiswahili
Watumiaji wengi wa Kamusi walioulizwa wamependekeza kuwa KKS iitwe tu KK, kwa sababu, usanifu wa msamiati unaweza kupunguza idadi ya maneno yaliyomo katika lugha. Kusudi kila mtumiaji apate kufaidika na KK, neno la Kiswahili (Kingwana au lahaja kubwa) liingizwe sambamba na kibadala chake cha Kiswahili sanifu. Kama hakipo, Kiswahili hicho kifasiliwe, na yatolewe maelezo kuhusu mazingira ya matumizi au chimbuko la neno hilo.
k.m.:
ulimbo (ji) (uk. 300)
kabulimbo (kingwana, linatumika Rwanda, Burundi, Zaire)
Taz A. Lenselaer, 1983 : 171
Kabulimbo taz. uLimbo
Zahabu (Kingwana) taz : Dhahabu (5).
Si vizuri kuliondoa neno litumikalo tu katika mazingira yasiyo ya Uswahili wa asili; lazima Uswahili wa leo upate hadhi na nafasi katika KK. Jambo hili litaelewesha sababu za tofauti za kifonetiki na kiothografia za Kiswahili na kuzipunguza vile vile.
k.m. idhara taz izara (uk.84)
kwa nini, tusichukue
Dhambi (uk. 44) taz zambi
Cheka (uk. 31) taz. Ceka
Dhahabu (uk. 43) taz zahabu
thelathini (uk. 281) taz salasini.
Kama matamshi haya yaelekeayo kuwa ya Kibantu zaidi hayaleti mkinzano wa kimaana na kifonolojia katika matumizi ya kawaida ya lugha hakuna sababu yo yote ya kutoandika msamiati huu. Hili haliwezi kupotosha malezi na matumizi ya lugha katika shughuli mbalimbali kutokana na kuwa hata leo kila mahali wanafundisha aina fulani ya Kiswahili. Kila neno linalozoewa lazima liandikwe. Kingwana kinafundishwa huko Mashariki mwa Zaire. Inapendekezwa kuwa msamiati wa Kibantu utumike kwa sabahu sio siri kuwa kasumba na athari za Kiarabu katika Kiswahili zinawafanya watumiaji "kuogopa" kutumia maneno ya Kiswahili ya asili ya Kibantu,
K.m bwerere (uk. 26)
munyu. (uk. 139)
Yaongezwe pia maneno, yaliyosahauliwa na yale yaliyofichwa kwa vile leksika ni jumla isiyofungika, bali huundwa na maneno yasiyohesabiwa. Mwanaleksi- kografia hakutaka kuyaficha maneno hayo, ila hakuyakumbuka tu. Catach (1971:25) anaeleza kuwa
"msamiati uliosahaulika ni msamiati uliotumiwa katikafasili na mifano ya maneno yaanzayo kwa herufi X, lakini msamiati huu haukupangwa kialefabeti katika kamusi".
Pengine. msamiati huu unatumiwa kwa ajili ya kuifanya kamusi iwe kubwa. Msamiati uliofichwa ni ule ulioandikwa katika kamusi mahali ambapo hautazamiwi kupatikana.
K.m.
"protokali" (uk. 86)
kama fasili ya 2 ya kidahizo
"itifaki"
Maneno hadhira, mageuzi, data, ukimwi, mtwale, hayati, hisabati. mgenzi, ukimwi na mengine mengi yanatumika sana lakini hayakuingizwa katika KKS.Msamiati wa maendeleo na matukio mapya yaliyofikiwa yaelezwe (dhana mpya za kiulimwengu). Maneno yanayoundwa katika mazingira na matumizi ya kila siku katika vyombo vya habari k.v BBC, Sauti ya Amerika, Sauti ya Ujerumani, n.k., ufugaji, kazi za kilimo, ufundishaji. utamaduni na taaluma mbalimbali yachunguzwe. Msamiati wa kitamathali (picha, michoro,...) unapotumika mara nyingi, unaweza kuchukuliwa kama vidahizo. Kamusi zilizohifadhiwa katika kompyuta ni rahisi kusahihishwa na kuongezewa msamiati mpya.
Mapendekezo ya jumla yatokanayo na mapendekezo hayo
Dhima ya kamusi yo yote katika jamii ni kutunza. Inatoa maagizo ya kufuata. Mwanaleksikografia anaelekeza, bila kusita, matumizi yanayotatiza. Matumizi yasiyoidhinishwa yanaondolewa katika kamusi. Vipengele vya kimsamiati vilivyoelezwa hapo juu vinaweza kujaziwa na maoni haya: Kuna vidahizo vinavyotolewa fasili zinazotatanisha; visawe visivyojulikana, au visivyofasiliwa
K.m.
mtamba, ji mfarika uk. 193
mbaro ji hutumika katika msemo:
Tia - ni : kamata (uk. 158)
mtamanifu ji wa- mtu mwenye tabia ya kutamanitamani (uk. 193).
Kasoro zilizomo katika KKS kwa upande wa msamiati si nyingi. Icakuwa bora zaidi kwa kukusanya maneno muhimu yanayopatikana katika matumizi ya Kiswahili kote ulimwenguni, machache yakiwa hayajulikani katika mwambao. Kuibana Kamusi ya Kiswahili Sanifu kama "kitabu cha maneno na maana yake (...) katika shughuli rasmi" hakushawishi watumiaji wa Kamusi ya Kiswahili. "Uamuzi unaambatana sana na masiala ya gharama, natasi, n.k. ambayo, kwa hakika, hayahusiani na lugha moja kwa moja, bali ni ya muhimu" (KKS vii). Huu ni ukweli tusioweza kuukiuka japo itachukua muda mretu. Ili kufanikisha yote yaliyoelezwa katika makala hii inapendekezwa knwa: (1) Kamusi ndogo ndogo za kila mahali au shughuli iandikwe (2) kwanza kuingizwa katika kamusi ya Kiswahili msamiati wa lahaja muhimu (ili kila atakaye taka kupata neno lenye hadhi katika kanda yake, alipate, lielezewe pale linapotoka, au/na linapotumika). (3) Kamati ya kusanifu Kiswahi iundwe. Kwa kuwa shughuli hizi zitahitaji fedha. UNESCO iombwe kuwa mdhamini na agharamie kazi hii.
Tanbihi
(1) Rey, A., 1970, Initiation á linguistique, la lexicologie, Ed. Kilincksieck, Paris, (utangulizi). "Le lexique est forme de beaucoup d'ensembles dans lesqueles il faut distinguer les niveaux de langue divers : langue litteraire. langue ecritc, controlee ou commune..."(2) Picoche, J. 1977 Precis de lexicologie francaise... uk. 44 "on conviendra d'appeler lexique l'ensemble des mots qu'une langue met a la disposition des locuteurs et vocabulaire, l'ensemble des mots utilises par un locuteur donne dans les circuonstances donnees"(3) Rey, A. (Kitabu kile) uk. 103 "La separation des mots est un fait non universel parce que les Grecs ne les separaient pas dans l'ecriture, ils parlaient pourtant des mots [...] critere d'unite indecomposable de la pensee. critere autre que graphique".(4) Jean et Claude Dubois, 1971, Introduction a la lexicographie: le dictionnaire, Larousse, Paris, 1971 uk. 61 "Si le pluriel est seulement l'addition a la definition semantique du composant de pluralite, il ne constitue pas une entree distincte [...]. L'entree du dictionnaire est donc une unite theorique, plutot definie a partir de la notion de mot qu'a partir de celle de morpheme. Bt ceci sejustifie par le fait que la lexicographie s'elabore a partir du modele de performance, des realisations du discours et non, a partir du modele de competence. de la langue".(5)
- Lenselaer, A. 1983, Dictionnaire swahili-francais, Paris, Karthala- Heylen, W. 1985, Kamusi, Vocabulaire, Francais-Kiswahili, Kiswahili-Francais, Ed. Saint Paul. Lubumbashi - Zaire. uk. 193.
MAREJEO
BELLE-ISLE, J. Gerard. 1979. Dictionnaire general (anglais-francais) Beauchemin: dunon.
CAHIL, W.F. 1972. Kamusi ya kwanza, Kiswahili-Kiingereza. Nelson.
CATACH, N.et al. 1971. Orthographe et lexicographie, Paris: Didier.
DUBOIS Jean et Claude. 1971. Introduction a la lexicographie le dictionnaire. Paris: Larousse.
DUCTOR Oswald et al. Les mots du discours: le scns comun.
GALISSON. R. 1979. Lexicologie et enseignement des langues. Paris: Ed. Hachette.
GALISSON. R. 1978 Recherches de lexicologie descriptive: la banalisation lexicale. Contribution et recherches sur les langues techniques. Paris: Fernan Nathan.
GUIRAUD, Pierre. 1964. L'etymologie. Paris: P.U.F., q.s.j.
HANSE, Joseph. 1971. Dictioinnaire des difficultes grammaticales et lexicologiques, Ed. CNES.
HEYLEN, W. 1985, Kamusi. Vocabulaire, Francais-Kiswahili, Kiswahili-Francais, Ed. Saint Paul, Lubumbashi - Zaire. uk. 193.
JOHNSON. F. 1980. Kamusi va Kiswahili. Nairobi: OUP.
LENSELAER, A. 1983. Dictionnaire Swahili-Francais Paris: Ed. Karthala.
PICOCHE, J. 1977. Precis de lexicologie francaise: l'etude et I'enseignement du vocabulaire. Paris: Fernan Nathan.
REY, Alain. 1970. Initiation a la linguistique, la lexicologie. Paris: Ed. Kilincksieck.
REY, Alain. 1979. La tenuinologie, Noms Notions, Paris: P.U.F. q.s.j.
RUKIRAMAKUBA, E. 1989. Etude Socieolinguistique du covabulaire politique dans le Rwanda Revolutionnaire et Independent 1957-1987, Memoire de Licence, Rehengeri, U.N.R.