Usanifu Wa Vidahizo Vya Kamusi Ya Kiswahili
Usanifu Wa Vidahizo Vya Kamusi Ya Kiswahili
Utangulizi
Makala haya yanakusudia kujadili usanifu wa vidahizo vya Kamusi ya Kiswahili Sanifu (KKS). Ili kuweza kuikabili mada hii ipasavyo, itafaa kwanza kujadili kwa muhtasari suala la usanifishaji. Tunafanya hivyo kwa sababu mbili: Kwanza mada yenyewe ni juu ya usanifuwa vidahizo vya Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Pili, kwa kawaid a dhana ya Kamusi imehusishwa na vidahizo sanifu, ijapokuwa kwa fasiri inachukuliwa tu kuwa kitabu chenye orodha ya maneno yaliyopangwa kialfabeti pamoja na kategoria, maana, etimolojia, matamshi, n.k. ya kila neno. Baada ya kuelezea usanifishaji tutachambua suala la usanifu wa vidahizo vya Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Matarajio yetu ni kutoa mchango utakaohamasisha juhudi za kukuza na kuendeleza taaluma muhimu ya leksikografia. Hatimaye makala yatahitimishwa kwa kutaja mafanikio yaliyopatikana na matatizo yaliyokabiliwa yakiwapo.
Suala la Usanifishaji
Usanifishaji umejadiliwa na wanaisimu na wanalugha wengi wanaotajika (Allerton. 1982, Crystal. (ed.) 1980, Haas, (ed.) 1982. Kitsao, 1983, 1991, Lyons. 1977, Vachek, 1982. Zgusta 1971 miongoni mwa wengineo). Hivyo basi makala haya hayawajibiki kulishughulikia kwa undani suala hili bali kulirejelea kimapisi tu kwajinsi linavyokuwa daraja la kufikisha kwenye mahusiko hasa. Kusanifisha ni kuanzisha kifani au utaratibu unaonuiwa kusawazisha jambo. Ni kuweka kigezo kinachokubalika na kuzingatiwa kiujumla.
Usanifishaji wa lugha ni maratibu unaopuuza tofauti zote za lu gha zinazotokaua na lahaja na kuhusiana na jinsia. umri, hadhi ya kaz i, n.k. Lugha sanifu ni matokeo ya juhudi ya jamii kulazimisha lahaja moja kuwa lugha sanifu. Usanifishaji wa lugha ni uanzishaji wa aina fulani ya utaratibu jumuishi unaokuwa msingi wa maneno na miundo ambayo wengi wa waongeaji wa lugha husika wangeukubali na kuuchukulia kuwa horomo kwa kiasi kikubwa kutokana na jinsi usivyotia maanani tofauti ndogondogo zinazotokana na lahaja.
Usanifishaji hushughulikia lugha, ukizingatia hasa matamshi. tahajia semantiki na sarufi. Maneno hudhihirika katika tahajia au grafimu inapowakilishwa kimaandishi. Hivyo basi matamshi na tahajia huwa na uhusiano mkuruba kiasi kwamba makala haya yanazungumziu kipamoja.
Kuna lugha nyingi ulimwenguni, ambazo matamshi ya maneno hayaoani na maandishi yake. Hizi ni lugha zenye matamshi hijai, totau ti na hijai matamshi, ambapo hijai za neno hazioani na matamshi kwa upande mmoja. na hijai za neno kukubaliana na rnatamshi kwa upande mwingine. Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazodhihirika kihijai matamshi. Hii ina maana kwamba kwa jumla maneno au leksimu za Kiswahili hutamkwa jinsi zinavyoonekana kimaandishi. Kuna jambo moja tu la kuzingatia - matamshi ya Kiswahili hutiliwa mkazo kwenye silabi moja kabla ya ile ya mwisho. Hivyu basi tuna haki ya kusema kuwa suala la matamshi katika lugha ya Kiswahili si bina. Tatizo hasa ni kwenye hijai kama tutakavyoonyesha baadaye. Semantiki ni tawi kuu la isimu linaloshughulikia uchunguzi wa maana za maneno. Semantiki ina misingi yake katika suala la lugha kuwa imeasisiwa kimaana. Bila lugha kuasisiwa jinsi hiyo, hapangekuwa na mawasiliano miongoni m wa jamii ya waongeaji. Hii ndio sababu iliyofanya Kamati ya Lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki (1930) kukubaliana matumizi ya maneno au msamiati uliopo na mpya.
Usanifu wa Vidahizo vya KKS
Vidahizo ni yale maneno yanayoingizwa na kuelezwa katika kamusi. Tatizo linalojidhihirisha katika vidahizo vya KKS ni tahajia.
Tahajia na Usanifishaji
Tahajia ni kaida zinazozingatiwa wakati maneno yakiwa katik a umbo la matamshi yanapowakilishwa kimaandishi. Kwa kawaida lug ha yoyote ile ina lahaja mbalimbali zinazotumiwa na wazungumzaji wake. Lugha ya Kiswahili, ina takribani lahaja kumi na sita. Lahaja zote hizi zina tofauti za kimatamshi. Usanifishaji wa Kiswahili ulifanywa il i kurahisisha ufundishaji wake pamoja na kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wazungumzaji wake. Kazi hii ilifanywa na Kamati ya Lugha ya Kiswahili ya Afrika Mashariki iliyoundwa 1930. Kabla ya h apo kulikuwa na Kongamano la Elimu (1925), ambalo liliteua lugha ya kutumiwa kama lugha ya mawasiliano katika shule nyingi iwezekanavyo kote Afrika Mashariki.
Madhumuni makuu ya kamati za lugha (Kiswahili) ya Afrika Mashariki yalikuwa kusanifisha Kiswahili na kuendeleza usanifishaji n a ukuzaji wa lugha hii. hasa kwa upande wa msamiati. Kuhusu hasa usanifishaji wa tahajia. kamati ilipendekeza kufanywe makubaliano ya pamoja ya kuwa na tahajia moja kwa maneno yenye tahajia zaidi ya moja.
Maneno ya lahaja
Lahaja ni lugha za eneo au jamii fulani ya wazungumzaji wa lugha moja inayojidhirisha katika maumbo au matamshi ya maneno pamoja na miundo maalumu ya kisarufi. Ugawikaji wa lugha kilahaja ni tukio la kawaida katika lugha yoyote ile yenye idadi kubwa ya wazungumzaji. hasa pakiwa na mipaka ya kijografia au ya kijamii inayotenganisha watu. Kwa mfano neno mchele lina tahajia tofauti kati ka lahaja za Kiswahili kama .ifuatavyo: 'mtee' (Kiamu), 'mtele' (Kimvita). 'mchele' (Kiunguja). Kwa kuwa Kiswahili sanifu kinatokana na lahaja ya Kiunguja tahajia ya kiunguja ndiyo sanifu, na 'mtee' na 'mtele ni tahajia za kutumika katika lahaja zinazohusika.
Usanifishaji katika kiwango cha tahajia huhitaji uteuzi wa tahajia moja itakayokuwa sanifu na nyingine kuwa za kilahaja na ambazo zitatumika katika muktadha wa Jahaja inayohusika. Uteuzi wa vidahizo vya KKS haukuzingatia usanifu wa msamiati, bali tahajia za lahaja mbalimbali za Kiswahili: 'aghalabu' na pia aghlabu', 'elimu' na 'ilimu' 'ihitilafu' na 'hitilafu', 'ikitisadi' na 'iktisadi'. 'zaituni'na 'zeituni', 'ziaka' na 'riaka', n.k. Kwa bahati mbaya. KKS haionekani kuwa na msimamo kuhusu haya kwani haionyeshi tahajia iliyo sanifu na ile isiyo sanifu na mazingira ambapo vibadala vilivyoingizwa hutumika. Kwa mfano, kati ya baasiri na bawasiri, lipi ni sanifu. Iwapo ulikuwapo umuhimu wa kuonyesha kibadala cha tahajia sanifu ni muhimu kuonyesha kibadala hicho hutumiwa na wazungumzaji gani. Vivyo hivyo kwa dada na dade, fadhaika na fazaika, mwida na muda n.k.
Kamusi ya lugha sanifu kama ilivyo KKS haikustahili kuingiza tahajia za kilahaja za maneno. Uingizaji wa vidahizo vikiwa katika tahajia tofuati waelekea kuwa umefanywa kwa lengo la kuikuza KKS iwe kub wa kwa kuingiza vidahizo vingi isivyostahili au kujaribu kuwaridhisha watunzi wa kamusi hii ambao ni waongeaji wa lahaja tofauti waliotaka tahajia za lahaja zao nazo ziingizwe katika KKS. Hali hii ndiyo iliyoifanya KKS iwe na vidahizo pamoja na vibadala vyake kama ifuatavyo 'asubuhi' sambamba na 'asubuhi', 'usubuhi', 'baleghe' sambamba na 'balehe'; 'chakleti' sambamba na 'chakeleti', 'chakuleti' , na 'chokoleti', na 'muale' sambamba na 'muali' sabini. sambamba n a 'sabiini'; 'ahsante', 'sambamba' na 'asante' n.k. Tofauti hizi za tahajia zinazotokana na tofauti za matamshi ya neno miongoni mwa wazungumzaji wa lugha hazikustahili kuonyeshwa kwani haiwezekani kuridhisha kila mmoja. Watunzi wa KKS walipaswa kusanifisha tahajia moja.
Kwa kuwa tofauti za kilahaja zinatokana na matamshi tu, kusanifu tahajia kusingeathiri mawasiliano kama Allerton (op. cit. 59) anavyosisitiza. Kwanza kabisa, nyingi ya tofauti tuzisikiazo kati ya waongeaji hazina misingi na hutokana tu na hali za kifisiolojia za watu binafsi. Tofauti kama vile thamani ya sauti. kiwango cha unazali, kwa mfano, hutumiwa kutambulisha mwongeaji siyo yale anayosema. Tofauti nyingine huwa kiushi ndogo za kilafudhi kutoka kwenye kaida za kifonemiki ambazo kwake msikilizaji anaweza kujirekebishia. Tofauti za kifonetiki ambazo kweli ni muhimu kwa mtengenezaji wa alfabeti ni zile zinazoathiri idadi ya ubainishi wa kifonemiki ambazo huhusiana na maneno hasa, hivyo basi akatumia kila moja ya fonimu zake. Thamani sahihi ya kifonetiki anayoipa fonimu zake (au, vizuri zaidi, alofoni zake) katika kila mmoja ya miktadha mingi ya kutukia kwake ina umuhimu kidogo tu.
Kushindwa kusanifisha Kiswahili kwa kuzingatia mapendekezo ya usanifishaji yaliyoasisiwa katika miaka ya 1930 ndiko kulikosababisha kuzuka aina ya lugha iliyomfanya mjumbe mmoja wa Idara ya Elimu y a Kenya alalamike kama ifuatavyo katika memoranda yake:
Tumesanifisha Kiswahili na kutika utaratibu huo Kiswahili kimekuja kuonekana kuwa lugha mpya. Ambapo bila shaka, sote tuko tayari kukiri kuwa Kiswahili, kama lugha nyingine yoyoce hakina budi kukua na kupanuka katika umbo, ndumo na msamiati, kutokana na athari ya staarabu za jamii hamizi, lakini kwa hakika ukuaji ni lazima utokane na moyo wa Waswahili, siyo kubandikwa kwao kutoka nje. Lakini hivyo hasa ndivyo ambavyo tumejaribu, na bado tumajaribu kuganya, matokeo yakiwa kwamba tumo katika ile hali isokubalika, ya kuchekesha - ya kuwafundisha Waswahili lugha yao wenyewe kupitia vyombo vya vitabu ambavyo vingi si vya Kiswahili katika umbo au yaliyomo, na ambavyo lugha yake inafanana kidogo sana na lugha ongezi. Labda tuna pupa ya kutufanya tusione ukweli hwamba Waswahili wenyewe hawana tu uwezo wu kurekebisha lugha yao kulingana na mahitaji ya kisusa bali pia wanafanya hivyo kwa kasi inayostaajabisha. (Whiteley, 1959:85).
Maoni haya yalizusha hoja kadhaa zilizoyapa umuhimu wa kuyafanya yajadiliwe kwa muda wa miaka ishirini iliyotuatia kwani yanaunga mkono madai kwamba usanifishaji haukueleweka na kutumiwa kwa utaratibu ufaao.
Leksimu Unganishi
Dhana ya 'leksimu' hapa inatumiwa kama inavyoeleweka na wanaisimu, ikirejelea kisehemu kidogo bainishi katika utaratibu wa kisemantiki wa lugha fulani. Inachukuliwa kulingana na madhumuni yake ya awali, yaani kupunguza utata wa dhana ya neno, ambayo ilihusiana na viwango vya kiorthografia/kifonolojia, kisarufi na kileksika, na kubuni dhana mwafaka zaidi kwa matumizi katika muktadha wa kujadili msamiati wa lugha. Hivyo basi leksimu inapendelewa kwa kufaa kwake katika kusimamia seti za miundo ya ki.sarun inayodhihirika kama vile kwa uradidi wa 'piga' -> 'pigapiga', maneno ambatano k.m. 'mwanadamu' na 'ngombedume', pamoja na viambatani kama vile katika 'yoyote'. 'vivihivi', n.k. Hivi ni kusema kwamba leksimu ni visehemu maneno vinavyotamkwa kama neno mojamoja lakini ambavyo huorodheshwa kama kwamba ni visehemu huru katika kamusi kama Lyons (1977:534-5) anavyofafanua: "Leksimu unganishi ni neno ambalo shina lake huundwa kwa kuunganisha mashina2 mawili au zaidi (na au bila marekebisho ya kimofolojia)" ufafanuzi huu unakuwa muhimu hasa kwa sababu ubainishi unaweza kufanywa katika lugha maalumu. kati ya miundo-maneno na miunganisho za miundo maneno.
Katika Kiswahili, uwakilishi wa miunganisho kama vile 'pigapiga' na 'ng'ombedume' kama vidahizo katika kamusi si bina. Yanayotuhumu ni madhihiriko kama vile 'yeyote', 'vivihivi'. 'mmojammoja', 'mbalimbali'. 'kutekote', n.k. Kigezo kikuu cha kubainishia leksimu katika Kiswahili ni kile cha msisitizo. Kwa jumla, kila leksimu katika Kiswahili huwa na msisitizo mmoja wa kimsingi, mahali pake pakiwa silabi moja kabla ya ile ya mwisho. Msisitizo kwenye silahi ya pili katika 'barabara'. tofauti na msisitizo wa kawaida katika 'harabara' ni muhimu kwa madhumuni tu ya kubainisha maana. Kwa kutia maanani kwamba mifano ya uradidi pamoja na miunganisho kama vile 'kiamshakinywa' na 'kiguu-na-njia' huchukuliwa kuwa leksimu moja hata kama huunganishwa kwa vistari katika lugha maandishi, na kwa kuona kuwa leksimu katika Kiswahili zina misisitizo wazi kwenye silabi moja kabla ya mwisho, tunapendekeza kwamba miundo kama vile mmojammoja'. 'yeyote'. 'vivihivi'. 'tofautitofauti', n.k. ambayo msisitizo mmoja ni leksimu moja na yafaa kuainishwa na kuwakilishwa hivyo.
Maneno Mkopo
Kwa mujibu wa Crystal (1980) maneno ya mkopo "ni faridi ya kiisimu. (kwa kawaida faridi ya kileksika) ambayo imekuja kutumiwa katika lugha au lahaja. mhali na kule kwenye asili yake". Maneno mkopo yanaweza knchukuliwa na lugha pokezi bila mofimu zake ngeni kubadilishwa au angalau kurekebishwa kidogo. Hali namna hii inaweza kutolewa mfano wa 'hwana' (mkopo katika kamusi ya CHAMBERS TWENTIETH CENTURY DICTIONARY. kutokana na Kiswahili) na propaganda kutokana na Kiingereza katika KKS).
Lakini wakati mwingine, sehemu ya neno, hasa likiwa unganishi, hupisha mofimu. au, hasa katika Kiswahili, fonimu nyenza ya lugha pokezi. Katika Kiswahili, leksimu hukopwa kifonetiki (jinsi zinavyosikika kimatamshi) au kifonemiki,( namna zinavyodhihirika kimaandishi) katika lugha kopeshaji. Hivi ni kusema kwamba ukopaji hufanywa kama leksimu katika lugha kopeshaji hudhihirika kitahajia matamshi au kimatamshi tahajia. Leksimu inayopokewa kifonetiki katika Kiswahili kama lugha kopaji ni kama vile 'ajenda', 'baiskeli', 'namba', 'edita'. 'pensheni'. na 'taksi', kama zinavyopatikana katika KKS. Kamusi hii haikustahili iingize pia tahajia vibadala kwa leksimu zilezile: 'agenda', 'baiskili', 'nambari', 'editori', 'pencheni'. 'teksi'. Uingizaji wa vibadala vya tahajia ya maneno ya mkopo unapotosha dhana ya kusanifisha lugha.
'Agenda' na 'pencheni' kama vibadala vya 'ajenda' na 'pensheni', hata kama dhana ya usanifishaji ingepuuzwa au hata kama maneno haya yangewakilishwa kifonemiki bila shaka ni kosa kutojua. Ukweli ni kwamba, herufi inayoshikwa na jicho kama g kwa upande wa'agenda' au kusikika sikioni kama ch kwenye 'pension' si g wala ch kifonetiki. Kwa mfano neno 'geography' hukopwa kama 'jografia'.siyo kama 'gografia'.
KKS haiwezi kutetea editori kama kibadala cha edita kwani hii inamaanisha kwamba ni mkopo kutokana na 'editory' ambayo haipatikani katika lugha kopeshaji. Ni kweli Kiswahili kimepokea 'nambari' kwa matumizi ya kila siku kiasi kwamba neno hili halihisiki kutokubalika. Lakini halina msingi wa kiisimu. Si 'numbery' bali 'number' katika lugha kopeshaji. Uwakilishi wa moja kwa moja wa ukopaji kifonetiki ungekaribisha maneno mageni kama vile 'fenomena', 'kafeteria'. 'logo' 'parafanelia'. n.k. Hivi ndivyo ambavyo Kiswahili kimekopa maneno kama vile 'penalti', 'digrii', 'bucha' na 'buchari'.
Mbali na utohozi wa moja kwa moja wa faridi za kileksia kama zilivyojadiliwa hapojuu, uwakilishi kifonetiki wa manenomkopo unaweza kufafanuliwa ili kusahilisha matamshi katika lugha pokeaji. Ukopaji wa istilahi za taaluma umekuwa na msingi imara wa kutegemea, uliojengwa na leksimu tangulizi kama vile katika 'filosofia', na biolojia hata ijapokuwa maneno haya huenda yalikopwa kimajaribio hapo awali. Matokeo ni kwamba hivi leo tuko huru kuwa na 'bibliografia', 'leksikografia'. 'orthografia', n.k. katika kundi moja; 'methodolojia', 'etimolojia', n.k. katika jingine. Utaratibu unaoonekana kuzingatiwa ni kuwa fonimu /phy/ na /gy/ za lugha kopeshaji zirekebishwe na kukaribishwa kama /fia/ na /jia/ katika lugha pokeaji.
Kuhusiana na /ry/, /cs/, /x/ na /sis/ kama vile kalika 'history'. 'physics', 'syntax', na 'hypothesis', kama vile katika 'historia', 'fizikia', 'sintaksia', na 'haipothesia'. Katika muktadha wa ruwaza hizi leksimu 'kemia' badala ya 'kemistria' (kutokana na 'chemistry'), na paradigmatiki na semantiki badala ya 'paradigmatikia' na 'semantikia') (kutoakana na 'paradigmatics' na 'semantics' zaweza kusemekana kuwa ziliteleza. Huenda waliozisanifu walizichukua hivyo ili kusahilisha matamshi kwa kujaribu kuzipunguza urefu.
Hitimisho
Makala haya yamejadili haja ya kutazama upya usanifu wa vidahizo vya KKS. Katika mjadala huu tumeunyesha upungufu wa KKS katika kikishughulikia Kiswahili sanifu. Kamusi imeshindwa kuorodhesha masaniati sanifu. Kuwa hivyo ipo haja ya wanaoidurusu KKS kuvipembua vidahizo vilivyomo na kuorodhesha vile tu vilivyo katika tahajia inayokubalika. Leksikografia, haiwezi kujitenga na usanifishaji wa lugha, Kwa hivyo inahitaji kutekelezwa kwa uvumilivu, kujitolea na ujuzi japokuwa ni kazi ngumu na yenye kuchosha. Mwanaleksikogratia hana budi kutamhua kuwa kamusi ni rejeo muhimu amhalo watumiaji wa lugha huirejelea ili kupata majibu ya maswali mengi yanayoihusu lugha.
Upungufu mwingine wa KKS ni kukosekana kwa minyambuliko na maneno ya kawaida kama vile 'nyama' na 'kama' ya 'masharti' k.m. 'kama utakuja, sema'. Kasoro zilizo katika KKS zinahitaji kufanyiwa utafiti. Ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika KKS inafaa wanaleksikografia kufanya juhudi ya dhati ya kuyabaini matatizo yaliyomo na kuyasahihisha ipasavyo kwa kuzingatia nadharia za isimu na kanuni za utungaji wa kamusi.
Maelezo
1. Neno hili linatumika Kenya kwa maana ya tahajia.
2 Yaonekana Lyons anatumia dhana ya shina kwa maana maalumu kurejelea neno kama linavyoeleweka kikawaida. Ingawaje katika Kiswahili, dhana hii hutumiwa bila utata kurejelea msingi au mzizi wa neno unaoweza kuongezwa viambishi. Kimatumizi 'yeyote' hudhihirika kama ye yote, 'vivihivi' kama 'vivi hivi' 'mmojamoja', kama 'mmoja mmoja', 'mbali mbali', kama 'mbalimbali', na 'kote kote' kama 'kotekote'. Kwa jumla miunganisho hii haipatikani katika kamusi (za Kiswahili).
MAREJEO
Allerton, D.J. 1982 "Orthography and dialect". katika Haas, W. (ed.)
Antilia, R. 1972. An Introduction to Historical and Comparative Linguistics New York: MacMillan Publishing Co., Inc.
Broomfield, G.W. "The Development of the Swahili Language," in AFRICA Vol. 3.1930.
Cartford, J.L. 1966. ALinguistic Theory of Translation London: O.U.P.
Cary, E.A. & Jumplet, R.W (eds.) 1950. Quality in Translation. London: Pergamon Press Ltd.. The International Federation of Translators.
Crystal, D (ed.) 1980 A First Dictionary of Linguistics and Phonetics. London: Andre Deutsch Ltd.
Fullas, H. "Problems of Terminology". in Whiteley, W.H. 1971. Language Use and Social change. London: OUP.
Gower, R.H. "Swahili Borrowings From English" katika Africa Vol. 22, 1952.
Gurr, A." Literary Translation, Impure But Anticolonial". in Gorman, T. (ed.) Journal of Language Association of Eastern africa Vol.2. University of Nairobi, Nairobi 1971.
Guenthner, F. & Guenther 1978 M. Meaning and Translation: (eds.) Philosophical and Linguistic Approaches. London: Duckworth & Co. Ltd.
Haas, W. (ed.). 1982 Standard Languages: Spoken and Written. Manchester: Manchester University Press.
Hyder, M. "Swahili in a Technical Age", in Africa Contemporary Monographs, No. 4 East African Publishing House. 1966.
Johnson, F. 1939. A Standard Swahili-English Dictionary. Nairobi O.U.P. Kirkpatrick, E.M. (ed.) 1983. Chambers 20th Century Dictionary Great Britain: W & R Chambers Ltd.
Kitsao, J. Ukubalifu wa msamiati/ Istilahi. Mifano kutoka Kenya. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Chuo Kikuu.
Kitsao, J. Usainfitshaji wa Istilahi za Kiswahili. DSM: TUKI. 1989
Kitsao, J. Standardisation of Kiswahili: A Review with Special Reference to Othography: makala yaliyowasilishwa katika 22nd Annual Conference on African Linguistics (ACAL) Chuo Kikuu cha Nairobi, Nairobi, Kenya. 1991.
Krapf, J.L. 1882. A Dictionary of the Swaluli Language. London.
Lyons, J. 1977. Semantics 2 London, NewYork: Cambridge University Press.
Madan, A.C. 1894. English-Swahili-Dictionary. London.
Madan, A.C. Swahili-English Dictionary. London.
Nida, E.A. 1961. Bible Translation. London: United Bible Society. Towards a Science of translating. Printed in Netherlands. 1975
Exploring Semantic Features. Munchen: Fink.
Pyles, P. & Algeo, J. 1993. The Origin and Development of the English Language. Fourth Edition. Harcourt Bracc Juvanovich College Publishers.
Snoxall, R.A 1958 A Concise English-Swahili Dictionary. Nairobi, DSM:OUP.
Steere, E.1870 A Handbook of the Swahili Language as Spoken at Zanzibar London.
TUKI Lugha ya Kiswahili. UDSM. 1990.
TUKI Usanifishaji wa Istilahi za Kiswahili UDSM. 1990
TUKI Kamusi Sanifu va Biolojia. Fizikia na Kemia. UDSM. 1990
Ullmann, S.1951. Word and their use. London: Muller, Series, Man and Society,
United Bible Sucieties. 1952. The Holy Bible in kiswahili. Union Version.
Vachek, J. English Orthography, in Haas, (ed.) ambayo imerejelewa.
Wajiyewardene, G.E.T. 1959. SWAHILI CONCEPTS OF HEALTH AND DISEASES. Kampala: E.A. Insitute of Social Research. Makerere College.
Whiteley, W. 1969. SWAHILI: The Rise of a national Language. London: Methuen & Co. Ltd.
Zgusta. L. 1971. MANUAL OF LEXICOGRAPHY Paris: Mouton.