UANDISHI WA HADITHI FUPI: MISINGI YA HADITHI FUPI ZA MAPOKEO NA ZA KUBUNI ZA KISASA
UANDISHI WA HADITHI FUPI: MISINGI YA HADITHI FUPI ZA MAPOKEO NA ZA KUBUNI ZA KISASA
SURA zilizotangulia zimejadili mambo mbalimbali kuhusu hadithi fupi za Kiswahili. Katika sura hii tutaangalia misingi na mbinu mbalimbali za uandishi wa hizo hadithi fupi. Misingi yake ya uandishi itazingatia aina mbili za hadithi fupi tulizozijadili hapo awali. Kwa vile hadithi za kingano huelekea kwenye masimulizi ya mapokeo katika maandishi, hapa tutajadili mambo ya msingi yanayohusu hadithi fupi ya kubuni kwanza.
Maana ya Kubuni
Suala la kueleza jinsi ya kubuni ni gumu. Haliwezi kuelezwa kwa urahisi. Ugumu wake unatokana ua ukweli, kama anavyosema S.A. Mohamed kwamba "jinsi hali ilivyo, hakuna maelezo yanayoweza kutolewa ambayo yatamfunga mtu katika lazima ya kufuata na kutekeleza kanuni za sheria kama vile mfuasi wa dini anayefuata nguzo zake. Kazi ya uandishi (wa hadithi fupi) ni mithili ya maskani wanayokutania waandishi mbalimbali, kila mmoja akiwa amepita njia yake. Njia zinakuwa nyingi, lakini mwisho ni mmoja."1
Aidha, kila mwandishi anayebuni maandishi anapata mawazo yake kutoka katika mazingira yake yaliyomlea na kumkuza ama kumfinyanga kwa kila hali. Mazingira hutawaliwa na nguvu za kiuchumi na za kihistoria zajamii ambazo hubadilika.
Tatizo kubwa la mtu anayetaka kuandika hadithi sio kuzua wazo tu bali ni kuwa na wazo linalohitajika kwa kipindi fulani na jamii inayomzunguka, ua hatimaye kuunda kazi ya kisanaa ya kubuni. Kinachoweza kufanyika mara nyingi kwa mtaalamu wa hadithi fupi ni kutoa maoni yake juu ya uandishi wa hadithi hizo na kuifanya kazi iwe ya sanaa (ki), lakini si kumfundisha mtu jinsi ya kuzua wazo na kutoa sheria na kanuni za uandishi wa aina hii kama nguzo katika Koran Tukufu au Biblia Takatifu. Mwanafasihi Victor Jones anaamini kuwa:
Mambo mawili muhimu yanaweza kuwajenga waandishi na kazi zao za sanaa. Kwanza ni kipawa chake mtu binafsi. Pili, ni uzoefu utokanao na maisha yake (...) kitu muhimu ni kukuza kipawa hicho, kwani hakuna kipawa Idnachoweza kukomaa na kufanya kazi chenyewe bila kuongozwa vilivyo ama kupewa mazoezi mazito ya daima katika uwanja wa kisanaa uliochaguliwa na kushughulikiwa.2
Maelezo hayo yana msingi mkubwa. Ni kweli kuwa hakuna sheria zilizowekwa ili zifuatwe na kuzingatiwa ili ziandikiwe hadithi fupi. Kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na taratibu za mabadiliko ya kijamii yanayokwenda sambamba na historia yake. Tena, pamoja ua kukubali kuwa uandishi wa hadithi fupi za kubuni kwahitaji kipawa, lazimajuhudi ifanywe kukuza kipawa hicho kwa kutumia mbinu mbalimbali. Maarifa mengi yatokanayo ua maisha ya mwandishi ni nguzo muhimu isaidiayo kukuza kipawa hicho cha mwandishi. Suala la kubuni, kipawa cha mwandishi na uzoefu wa jumla wa mwandishi ni mambo yanayohusiana sana katika kuiunda au kujenga hadithi fupi ya kubuni. Akielezea maana ya kubuni, M.S. Abdulla anasema:
Kuweza kuzua uwongo uliofanana na ukweli ni kutunga au kubuni. Kubuni ni kuumba kiumbe kwa fikra na mawazo kikawa kinashikika, bah ingawa kuumba huko ni kwa mawazo tu, kiumbe cha kubuni kina sifa zote za kiumbe cha kweli.3
Labda neno hili uongo linaleta picha isiyo nzuri juu ya suala zima la ubunaji wa hadithi. Dhana ya uongo hapa inachukuliwa kuwa ni jambo lisiloelezea ukweli unaolandana na tukio lililotokea moja kwa moja ua aliyetenda jambo hili. Hata hivyo kuna ukweli fulani juu yajambo lililotendeka au linaloweza kutendeka. Akitoa maoni yake juu ya maana ya kubuni na maana ya hadithi kwa ujumla naye M.L. Matteru anasema:
...ni kazi ya kubuni. Ni hadithi inayotungwa kufuatana na uwezo wa fanani kwa kuibusha mambo kutokana na mazingira yake. Yawezekana wahusika ua vituko visiwe vya kweli bali hata hivyo huwakilisha mambo mahsusi, watu n.k. katika nyakati na mahali mbalimbali.4
Maelezo ya madondoo yote mawili yanaelekea kukubaliana katika mtazamo wake. Wananadharia wote wawili wanakubaliana kuwa kuna kuzua kwa wazo ambalo laweza kuwa limetendeka au halijatendeka, lakini linawakilisha ukweli fulani juu ya maisha halisi ya jamii. Mtazamo ulioelezwa katika madondoo haya mawili, ambao unaelekea kuungwa mkono na wanataaluma wengine kama vile F.V. Nkwera5 ndio unaochukuliwa katika mjadala huu wetu hapa kuwa ni kubuni.
Katika suala zima la ubunaji, mwandishi anatumia mazingira yake na kuunda ulimwengu wa hadithi anayoitunga. Ulimwengu wa mwandishi una tabia mbalimbali, lakini muhimu ni kuwa ulimwengu wake unaweza kuwa ule anaoufahamu, au unaweza kuwa haufahamu kabisa. Anaweza kuwa na jambo la kufikirika mawazoni tu, au anaweza kuwa na jambo aliloliona.
Waandishi wa hadithi fupi pia wanaweza kuandika mambo yaliyotokea kweli, lakini huyafanya kuwa ni ya kubuni, na pengine huandika maneno: Hii ni hadithi ya kubuni, haimhusu mtu yeyote aliye hai au marehemu! Maandishi hayo yanawekwa na mwandishi kwa nia ya kujilinda endapo kutatokea mtu atakayelalamika kuwa ameandikwa pengine kinyume cha matakwa yake Wakati mwingine jambo hili linasaidia katika ngazi ndogo ya mahusiano kati ya mtu na mtu, lakini haiwezi kusaidia kujiokoa katika ngazi ya mwandishi na mtawala wake kama ilivyojadiliwa kirefu katika sura ya pili, endapo mwandishi huyo atakuwa ameligusa tabaka tawala visivyo, yaani ikiwa ataligusa kinyume na matakwa ya maono yak Mwandishi pia anaweza kuandika mambo aliyoyasikia na kuyafanya ameyabuni.
Uzoefu wa Mwandishi
Suala la uzoefu ni la muhimu pia katika uandishi wa hadithi fupi na hata uandishi kwa ujumla wa kazi nyingine za kisanaa au hata za kitaaluma. Uzoefu unampa nafasi mwandishi wa kuyajua mambo mengi kama msanii Alexander Prokofiev anavyosema wakati wa kujadili suala la kubuni ushairi:
Nimeishi mno na nimeona mengi. Yote hayo yanahitajika katika ushairi halisi. Ni pale unapokuwa na msiba, huzuni, ndipo unapoweza kujua maisha ni nini ... ni shida kwa mtunzi wa kazi za sanaa kuandika chochote ildwa hana matukio ya kutosha yaliyochotwa katika maisha.6
Maelezo hayo yanathibitisha kuwa kazi ya sanaa humtaka msanii kuwa na jicho kali la kupenya katika jamii yake ili aweze kubuni sanaa itakayosawiri maisha vile anavyoelewa wakati akitumia kalamu yake: kuhoji, kuhakiki, kusaili, kukejeli na mambo mengineyo. Matukio mbalimbali ambayo hutumiwa na mwandishi yanapatikana sehemu nyingi zilizo tofauti na katika hali mbalimbali.
Utafiti
Katika uandishi, utafiti ni jambo la msingi na ni la muhimu. Jambo hili linashirikisha mbinu mbalimbali za kumpa mwandishi uzoefu. Mwandishi anatakiwa afanye utafitijuu ya mambo mbalimbali katikajamii yake ili apate kujua kuwa yameandikiwa chochote au la! Na kama yameandikiwa, yameandikwa vipi na yeye anapoliandikia ataongeza jambo gani muhimu ambalo lilipaswa liandikiwe na hao waliotangulia na hawakuliandika vyema. Kutokana na jambo hilo, mwandishi hutakiwa kuanza ua utafiti na kusoma hadithi fupi zilizoandikwa (au kazi nyingine zilizoandikwa licha ya hadithi). Ni muhimu asome vitabu vingi vinavyohusu jambo hilo, au hata vile vya taaluma mbalimbali ili aweze kupanua mawazo yake ya kitaaluma. Ni vema atafute taarifa hizo kwenye maktaba, kwenye magazeti ama miswada mbalimbali ua nyaraka katika kumbukumbu zilizohifadhiwa za taifa.
Njia nyingine ya kufanya utafiti ni ile ya kuwafuata wataalamu wa mambo mbalimbali ambayo mwandishi angetaka kuyaandikia hadithi ama kitabu kwa ujumla. Kwa mfano kama mwandishi anataka kuandika kitabu juu ya mada ya kisayansi katika hadithi yake, itawajibika yeye kuwafuata wataalamu wanaohusika katika jambo hili ili apate uhakika na ukweli wa jinsi mambo yalivyo na halafu kuyaandikia hadithi. Mwandishi huyo akikutana ua wataalamu hao atakuwa na nafasi ya kuzungumza nao na kujadili masuala mbalimbali ya kimsingi juu ya mada ile anayotaka kuiandikia hadithi yake.
Habari zinaweza kupatikana matembezini pia. Kwa kawaida mwandishi hutembeatembea sehemu mbalimbali katika harakati zake za kujitafutia riziki kwa maisha yake. Binadamu anaweza kutembea sehemu mbalimbali, ndani na nje ya nchi. Kila pale anapofika, mwandishi anaweza kukutana na mambo ambayo anaweza kuyaandika katika kijitabu chake cha kumbukumbu anachotakiwa awe nacho kila afanyapo utafiti. Anaweza kukutana na mapenzi, anaweza kukutana na chuki, mashaka, misiba, wasiwasi ua furaha, matatizo au uonezi, wivu na ujinga, ndoa, n.k. Akishapata matukio hayo sasa anaweza kuandika hadithi yake.
Mawazo ua Fikra
Mara nyingi mwandishi anafikiri na kuwazajuu ya mambo mbalimbali, ya kijamii. Kila akiwaza huibua hisia na vionjo, yakazalishwa matamanio yatakay-oridhisha moyo wake yakitekelezwa vile anavyofikiri yeye ni sahihi. Kila akiwaza kwa upande mwingine kuna uzoefu fulani anaoupata kimaisha. Mawazo hayo anaweza hatimaye kuyatumia katika uandishi wake wa hadithi.
Wakati mwingine mawazo hujitokeza kwa mtindo wa njozi/ndoto. Na ndoto zinaangaliwa katika ngazi mbili: Kwanza, kama ndoto ameziota mwandishi mwenyewe. Ikiwa ndivyo, mwandishi ataeleza mambo yalivyomgusa. Ngazi ya pili m kama ndoto zimeotwa na mtu mwingine na mwandishi anasimuliwa. Katika hali hii, mwandishi anaeleza tukio hilo la njozi kama anavyofikiri lilivyomfikia yule mwotaji. Kitendo hiki kinaweza kuwa na athari mbili: mwandishi anaweza aeleze jambo kwa kutia chumvi sana, au anaweza kulieleza jambo akiwa amelipunguza nguvu sana.
Juu ya fikra, hizo kimsingi huwa mwanzoni tu. Mwandishi anafikiri juu ya jambo fulani na kisha hujenga matazamio fulani. Matazamio hayo yanaweza kuwa mema ama pia yanaweza kuwa mabaya. Fikra katika hali yake ya kawaida zinaweza kuzua furaha au hofu, kutegemeana na jinsi fikra hizo zinavyojengwa ua matukio mbalimbali yanayoweza kuzalisha hofu.
Kipawa cha Mwandishi
Baadhi ya wataalamu wamekuwa wakikataa kuwa hakuna kitu kiitwacho kipawa katika suala zima la uandishi. Wataalamu hao wenye kutazama mambo kiyakinifu aidha wanakubali kuwa mwanadamu anao uwezo mkubwa wa kuiga maisha ya jamii. Lakini pia hawasemi kuwa kila mwanadamu anao uwezo huo na ni kweli kuwa si binadamu wote wanaweza kuwa waigaji wakubwa wa maisha ya jamii. Wazo hili la pili la kuiga maisha ndilo wanalolishikilia kuwa ni zao la uandishi. Kwa hiyo wanahitimisha kwa usemi kuwa "kufikiri kuwa kuna kipawa kwa mwandishi ni kuleta fikra za kitabaka zisizo ua msingi."7
Yaelekea knwa tatizo hasa liko katika istilahi inayofaa kutumiwa katika kulieleza jambo hilo la kipawa kwa upande mmoja na uwezokwa mtazamo mwingine. Tatizo kubwa hapa ni la kimaelezo na wala si la kimantiki. Hali ilivyo, jambo lilelile moja huelezwa kwa kutumia maneno mawili ambayo kimsingi hutoa dhana moja Wakati shule moja huona kuwa mwanadamu ana uwezo wa kulga maisha, shule nyingine huona kitu hicho kuwa ni kipawa cha kuandika mambo ya kubuni. Madai kwamba kila mtu ana uwezo wa kuiga maisha kwa kuandika ni mapotofu, kwa sababu si kweli kuwa kila mtu anaweza kuiga maisha kwa kiwango kilekile kimoja. Ziko sababu nyingi zinazoweza kusababisha jambo hili: malezi na mazingira n.k.
Mtazamo wa mjadala huu ni kuwa mwandishi lazima awe na kipawa (uwezo) (kwa maana ya uwezo maalumu) (wa kiakili) na kutumia mbinu mbalimbali kuunganisha matukio mara kariha (hamu ya kuandika) ikisha mpanda. Dai kwamba kila mtu anaweza kuandika halina msingi, japokuwa andiko hili halipingi kabisa uwezekano wa mtu yeyote kuwa mwandishi baada ya kukikuza kipawa chake.
Kuna tofauti ya uwezo wa uandishi kati ya mtu na mtu, tofauti zitokanazo na kulelewa ama kukuzwa katika mazingira mbalimbali kama tulivyokwisha kudokeza hapo juu. Au tofauti nyingine zinaweza kutokana na koo mbalimbali: kwamba kila mwandishi anarithi kiasi fulani cha usanii kutoka kwa mababu zake. Na urithi huu kila mtu anao. Kila mtu anazaliwa na kiasi fulani cha akili anazoweza kuiga maisha.
Kipawa cha mwandishi kinaweza kukuzwa ama kudumazwa kwa njia mbalimbali. Ukuzaji wa kipawa cha uandishi wa hadithi fupi hauna njia moja kama lilivyo suala zima la uandishi na ubunaji wake. Baadhi ya njia za ukuzaji wa vipawa zimefafanuliwa hapa chini.
Kipawa: Ukuzaji Wake
Mwandishi bingwa kabla hajafikia hatua hii anatakiwa ajifunze na awe hatimaye na uwezu mkubwa wa lugha. Uwezo wake katika lugha unatakiwa uzingatie ufasaha katika matumizi ya tamathali za userni, misemo, methali na pia ukamilifu wake katika sarufi.
Ili mwandishi aweze kuwa na uwezo huo lazima ajibidishe kujifunza kutoka kwa waandishi wengine pmbao ni wakongwe ama chipukizi. Mwandishi huyo anatakiwa asome miundo na mitindo mbalimbali katika lugha ya Kiswahili na hata katika lugha nyingine anazozijua: Kiingereza, Kifaransa n.k. Mwandishi anashauriwa kusoma kazi mbaya na nzuri ili aweze kuwa na nafasi ya kujifunza mambo yote: mazuri na mabaya!
Sifa za Mwandishi
Baada ya kujadili misingi ya mwanzo katika uandishi wa hadithi fupi za Kiswahili, sasa tuangalie misingi ya utendaji wake katika uandishi. Euphrase Kezilahabi anatoa maoni yake anapohitimisha makala yake juu ya uandishi wa riwaya na hadithi fupi hivi:
(Mwandishi) uwe mbanizi wa maneno. Kila sentensi isukume mbele (matukio?) ya hadithi. Usirudierudie maneno. Lugha yako iwe rahisi. Kumbuka kuonyesha ukweli fulani wa maisha ya binadamu. Maiuihari yako yawe unapofahamu. Mwanzowa hadithi uwe na mshindo. Wafahamu wahusika wako vizuri. Matendo yawiane na mawazo yao. Usiandike hadithi ya kusikitisha au kufurahisha tu toka mwanzo hadi mwisho. Huu si ukweli wa maisha. Wahusika wazungumze wao kwa wao na watende kama kwamba wanaishi. Usihubiri.8
Maoni hayo ni ya jumla kwa mtu yeyote anayeandika hadithi. Lakini labda hapa itatupasa tuangalie uandishi wa hadithi fupi katika makundi yale tuliyoanza nayo kujadili huko mwanzo katika sura iliyopita. Lengo letu hapa ni kuelezea mbinu zinazohitajika wakati wa kuandikwa kwa hadithi hizo ambazo E. Kezilahabi anapendekeza zizingatie mambo muhimu ahyoyataja.
Uandishi wa hadithi fupi tunaugawa katika makundi mawili, ambayo ni (a) uandishi bila kutumia madondoo ama vidokezo ua (b) uandishi unaotumia vidokezo ama madondoo.
Uandishi Bila Kutumia Madondoo/Vidokeso
Baadhi ya waandishi, hasa wale wenye uzoefu katika masuala ya uandishi wanatoa mawazo yao kichwani na kuyaandika moja kwa moja. Wengine huandika kwa kalamu ya wino, na baadhi wenye uwezo kifedha hutumia mashine ya kupiga chapa (typewriter).
Katika njia hii, mwandishi anajenga kila kitu akilini mwake ua anapoamua kuandika huwa anatoa habari zote kichwani mwake. Njia hii ina ugumu wake. Mwandishi anaweza kusimulia ama kuandika hadithi yake lakini ghafla anaweza kujikuta anachanganyikiwa na kukwama asijue anaendelea vipi. Pengine ni rahisi kuandika hivyo kwa hadithi fupi, lakini ni vigumu kila mara kufanya hivyo kwa kuandika riwaya, japokuwa ni jambo linalowezekana.
Katika uandishi wa hadithi fupi kwa mbinu hii isiyotumia madondoo inafaa pia nako tuangalie makundi mawili ya aina ya hadithi zinazoweza kuandikwa na wasanii. Makundi hayo ya hadithi fupi yanatokana na aina mbili ya fasihi tulizozidokeza hapo awali, ambazo ni fasihi andishi na fasihi simulizi.
Uandishi wa hadithi za mapokeo unasemekana sio mgumu ukilinganisha na ule uandishi wa hadithi fupi za kisasa ambazo ni za kubuni. Kuna sababu mbalimbali zilizoelezwa, lakini ya msingi ambayo pia tumekwisha kuitaja mahali pengine hapo mwanzo ni kuwa hadithi hizo za mapokeo zimekuwa zikiishi katika jamii kwa njia za masimulizi, ua zimekuwa zikipokezwana kutoka kizazi hadi kizazi. Kutokana na kuwa katika jamii kimasimulizi, wakati mwingine dhamira zimebaki vilevile, ama kama zimebadilika, zimefanya hivyo kwa kiasi kidogo mno. Kitu kikubwa kilichobadilika sana katika hadithi hizo ni zile mbinu za masimulizi yake ili kukidhi haja ya mazingira ya kihistoria yaliyobadilika. Mabadiliko hayo yametokana na sababu kadhaa. Kwanza, kulingana na sayansi ya mabadiliko ya jamii, mazingira yaliyofanya usimuliaji wake uwe wa rahisi kwa hivi sasa yamefutika au yamebaki kwa kiasi kidogo sana. Pili, wale fanani waliojua mizungu ya usimulizi wamekuwa wakifa kama ilivyo kawaida na taratibu ya viumbe wote hai. Kutokana na sababu hizo, hadihti hizo japokuwa zimebaki katika jamii zimebeba athari mbalimbali. Au zimeongezajambo ambalo kwanza halikuwako, au zimepunguza kitu ambacho kwa sasa labda kimeletwa na mfumo mpya wa maisha ya kihistoria. Jambo hili aghalabu haliondoi ukweli kuwa waandishi wa hadithi hizo za kimapokeo wamepokea hadithi hizo na kuziandika, na wamefanya hivyo bila matatizo makubwa sana.
Uandishi wa hadithi za kubuni nao umekuwa ukifanywa bila kutumia madondoo kwa baadhi ya waandishi. Said Ahmed Mohamed, katika mazungumzo yake namijuu ya suala hilo alithibitisha kuwa mara nyingi katika uandishi wake wa hadithi fupi hatumii mbinu zile za kuandika madondoo kwanza, japokuwa anaifahamu na amepata kuitumia mbinu hiyo.
Mwandishi huyo alikiri kuwa uandishi wa namna hii wa kutotumia madondoo kwa hadithi za kubuni haujawa rahisi kwa watu wote, bali unahitaji mazoea ya hali yajuu. Hii ni kwa sababu waandishi wake wamelazimika kupanga mambo yote kwa kichwa na kuyatoa kwa kichwa hivyohivyo wakihusisha na hali halisi ya matukio katika ulimwengu wanaouishi.
Labda tuangalie mfano wa hadithi fupi ya asiii ya kimapokeo ua ambayo kama tuliyoiona hapa juu haitumii madondoo wakati wa uandishi wake. Hadithi yenyewe inaitwa "Jani Bichi na Jani Kavu".
JANI BICHI NA JANI KAVU
Msimulizi: Jalia Mohamed (Bi)
HAPO zamani za kale kulikuwa na majani mawili: Jani Kavu na Jani Bichi. Yote hayo yalikuwa yakiishi katika mgomba mmoja. Kila mara wakati wa maongezi yao, Jani Kavu lilionekana kuwa na busara wakati wote. Kimaisha, Jani Kavu pamoja na busara zote hizo lilikuwa limechoka kabisa. Wakati huohuo Jani Bichi liliishi kwa vitisho na matatizo mengi mbele ya Jani Kavu. Jani Bichi lilikuwa na kiburi, dharau na ujeuri. Haikupita siku bila kusikia masimango makali yakielekezwa kwa Jani Kavu kutoka kwake. Kwake, hofn ya kupoteza maisha mapema haikuwa akilini mwake. Wala hakuna hofu ya uzee kama ile ambayo Jani Kavu iliikabili.Siku moja, kama ilivyokuwa kawaida ya Jani Bichi, Jani Bichi lilimsimanga sana Jani Kavu. Ndipo Jani Kavu likasema kwa hasira hiyo: "Uwe na adabu! Kumbuka kuwa bila mimi wewe hungekuweko. Tena kumbuka kuwa siku moja utakuwa kama mimi! Wadogo lazima wawaheshimu wakubwa.9
Hadithi fupi kama hii si lazima iandikiwe madondoo kwa sababu kwa vyovyote vile haiwezi kumkanganya mwandishi wake, hata kama ni yule anayejifunza tu kuandika. Aidha, si vizuri kuhusisha urefu na mbinu za uandishi wake, kwani la msingi ni uzoefu tu. Labda hapa tuangalie mfano wa hadithi zile zinazotumia madondoo wakati wa uandishi wake. Hapa tutatumia mfano mmoja wa hadithi fupi ya kubuni na ambayo ni ya kisasa.
Matumizi ya Madondoo
Uandishi huu ni mzuri ua unaelekea kupendelewa na waandishi wengi. Utaratibu huu wa uandishi humfanya mwandishi aandike mfululizo wa matukio yake katika hadithi ua kujenga dhamira na ujumbe unaotakiwa kwa jamii bila matatizo makubwa. Mwandishi wa hadithi hizo anategemewa tayari anazo nyenzo muhimu za uandishi kama vile ujuzi wa Lugha, ujuzi juu ya matumizi ya mandhari na wahusika, ujuzi juu ya muundo na mitmdo na mengineyo.
Katika uandishi wa kutumia madondoo, mwandishi anaweza kwanza kuandika jina la hadithi, dhamira kuu, mandhari, wahusika, muundo ua mtiririko hadi mwisho. Si lazima mfululize uwe kama ilivyotajwa hapa lakini ni muhimu mambo hayo yote yawepo katika mpango kuanzia mwanzo wa hadithi yenyewe inavyoandaliwa. Tuangalie mfano wa hadithi iitwayo Nyota ya Chiku.10
Jina la Hadithi
|
: Nyota ya Chiku
|
Dhamira Kuu
|
: Uhuru maana yake nini?
|
: Mapenzi hutawaliwa na pesa : Uwezo kipesa/kimadaraka hununua utu, hakuna uhuru
| |
Msimamo:
|
Pesa na starehe hupotosha maisha na huleta ugumu kwa wazazi katika kutekeleza wajibu wao wa malezi kwa watoto wao
|
Wahusika Wakuu:
|
- Elena Chiku Ntale
|
- Enos Kapinga.
| |
Wasaidizi
|
- Che Ng'ombo
|
- Na wengineo watajitokeza katika hadithi
|
Tabia mbalimbali za wahusika:
(a) Elena Chiku Ntale
· Ni mzuri, anasumbua roho ya kila mvulana anayekutana naye
· Anapenda uhuru wa kujiamulia mambo yake ya mapenzi lakini hana uwezo, mazingira yamemzuia
· Wanaume wanamgeuza kuwa chombo cha starehe
· Kwa sababu ya dhiki anakuwa mtumwa wa fedha
· Ni rafiki ya Kapinga
(b) Enos Kapmga
· Mvulana/kijana mjeuri kabisa
· Hajui kusoma wala kuandika
· Ni tajiri, hajui kutunza mali
· Ana kiburi na majivuno
· Mnafiki
· Mgomvi
(c) Che Ng'ombo
· Pandikizi
· Msomi
· Mstaarabu
· Ana busara
· Anajali maisha na kanuni za jamii
· Mpinzani wa Kapinga
Mtiririko na Muundo/Mtindo
· Mtiririko wake utakuwa katika sehemu mbalimbali. Muundo utakuwa wa moja kwa moja, lakini mbinu za viona nyuma na viona mbele zitatumika hapa na pale.
Sehemu ya Kwanza
· Elena Chiku Ntale ni mzuri, hataki kufanya kazi kwa wazazi wake wala hataki kufuata sheria
· Ana mgogoro na wazazi wake, anaamua kukimbilia mjini.
Sehemu ya Pili:
· Kapinga anakutana na Elena Chiku Ntale mjini, anazungumza ua kumshawishi aishi naye kihuni· Mara ya kwanza anakataa (ndivyo wasichana walivyo) lakini hatimaye anakubali kufanya hivyo kwa sababu hana chakula.· Maisha yao ni ya matatizo· Vita kila wakati, anamjeruhi vibaya na kutaka kumzika mzima
Sehemu ya Tatu
· Che Ng'ombo anamwokoa
· Anamsaidia kurudi nyumbani kwao Litembo
· Mwisho, hakuna uhuru usio na mpaka
Mtindo: Pamoja na mambo mengineyo, mambo yanayohusu lugha, matumizi ya nafsi ya kwanza, pili na tatu mchanganyiko zitatumika.
Mandhari.
Mazingira: Mandhari zitskuwa za aina mbih: Kijijini na mijni.Wakati: Sehemu kubwa itatumia muda. uliopita. Lakini kutakuwa pia na muda uliopo na ujao katika nafasi maalumu za hadithi hii.
Baada ya kutengeneza vidokezo kama hivyo, rnwandishi sasa anaweza kuandika hadithi yake. Hadithi hii inaweza kuchukua umbo ambalo atalitaka mwandishi wake kwa kuzingatia mpango uliokwisha andikwa hapo juu Hadithi hii iko katika Diwani ya Hadithi ya kitabu hiki katika sehemu yake ya pili.
Aidha, mbinu zote, ya madondoo na isiyo ya madondoo, zinatumika kuandika hadithi ua wasanii. Ni suala la uamuzi wa msanii kuwa atumie madondoo ama asitumie madondoo
Mwisho, ni vyema kusisitiza bapa kuwa wakati msanii anapoandika kazi yake awe na lengo maalumu kwa hadhira aliyonayo akilini mwake anayoiandikia. Ajue wazi kuwa anataka kusema iambo fulani, na atalisema vipi, atatumia mbinu zipi kulisema jarnbo iake baada ya kushikwa na ghamidha na kariha!
Maelezo
1. S.A. Mohamed, "Ubunaji na Uandishi wa Biwaya," (Makala), 1976.
2. V. Jones, Creative Writing, Penguin Books, London: 1975.
3. M.S. Abdulla, "Kuandika Hadithi za Kubuni," katika Uandishi wa Tanzania, EALB, Dar es Salaam, 1974.
4. M.L. Matteru, "Hadithi na Riwaya," katika Zinduko, Chama cha Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: 1974.
5. F.V. Nkwera, Sarufi na Fasihi: Sekondari na Vyuo, TPH, Dar es Salaam: 1978
6. A. Prokofiev, Soviet Literature, Progress Publishers, Moscow, 1975.
7. Haya ni mawazo ya wanataaluma wengi wenye mtazamo wa Ki-Marx.
8. E. Kezilahabi, "Utunzi wa Riwaya ua Hadithi Fupi," (Makala), 1978.
9. Hadithi hii niliipata wakati nilipokuwa nikifundisha katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Iringa mwaka 1974. Msichana aliyenipa hadithi hiyo ni Jalia Mohamed, mwenyeji wa Kilimanjaro, ambaye kwa mwaka huo alikuwa kidato cha kwanza. Namshukuru popote alipo.
10. Hadithi hii nimeibuni kwa madhumuni ya mjadala wa mbinu za uandishi wa hadithi fupi.