Saadani A. Kandoro: Mashairi ya Saadani



Saadani A. Kandoro: Mashairi ya Saadani


SURA YA NNE
Na
E. Kezilahabi
Bwana Saadani Abdu Kandoro alizaliwa Kasingirima Street, Ujiji, Mkoa wa Kigoma tarehe 8 Desemba, 1926. Baada ya masomo ya Shule ya Primary Ujiji aliendelea na masomo yake Government School Iringa, Mwanahela School na Teachers Training School Bwiru.
Mwaka 1944, Bwana Kandoro aliingia katika Idara ya Kuweka Hazina Uyui Tabora. Katika miaka iliyofuata alishughulika sana kuanzisha Vyama Vya Ushirika na Ustawi wa Jamii ya Waafrika na hatimaye alikuwa Diwani wa kwanza katika Advisory Council ya Mji wa Tabora. Katika mwaka 1952 alikuwa Provincial Secretary wa Tanganyika African Association, Lake Province. Mwaka 1954, alikuwa miongoni mwa watu 17 walioanzisha Chama kitukufu cha TANU mjini Dar es Salaam.
Maneno haya tunayosoma karibu na picha yake kwenye jalada la kitabu yanatosha kuonyesha kuwa Bwana Kandoro ni mwanasiasa, na maandishi yake ambayo tunayajadili katika makala haya hayako mbali naukwelihuu.
Katika dibaji ya kitabu hiki Bwana Mnyampala anasema "ilikuwa vigumu kuweza kupambanua baina ya tungo za Sheikh Amri na mpwae huyu Sheikh Kandoro." Hii si kweli, maana mengi ya maandishi ya Amri Abedi yaliambatana sana na misingi ya dini wakati ya Kandoro yanamhusu hata mwanadamu katika jitihada ya kushindana na mazingira yake.
Katika muhtasari wetu wa Kiswahili imeandikwa kwamba baadhi ya mashairi yaliyomo katika kitabu hiki tunayaona katika Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri na tofauti hizi si ndogo. Nafikiri Kandoro angeweza kutunza majina yale yale na mahali ambapo ameongeza beti ingekuwa bora kama angeeleza hizo beti zimetoka wapi. Jambo hili ni muhimu sana maana linaweza kumpa shaka mhakiki. Kosa kama hili lilitendeka pia kwa baadhi ya maandishi ya Shaaban Robert.
Udhaifu mwingine wa Bwana Kandoro tunauona katika muundo wa mashairi yake. Huu si udhaifu wa Kandoro peke yake, ni udhaifu wa washairi wengi wa siku hizi. Karibu mashairi yote yaliyomo kitabuni ni ya mizani kumi na sita na mistari ni minne, yaani tarbia.Mashairi ya aina ya tathlitha, takhmisa na ukawafi hatuyaoni kabisa. Sifa hii anayo Shaaban Robert na inaonekana washairi wa siku hizi wameshindwa kuvaa taji lake. Wale ambao wamejaribu kulivaa naona limcwapwaya.
Katika dibaji hayati Mnyampala anatwambia: "Bwana Kandoro ni mshairi maarufu sana nchini Tanzania." Watunzi wenye fani ya Bwana Kandoro ni haba sana leo. Wenye fani sawa na yake walikuwa akina marehemu Sheikh Shaaban Robert na mjombae Sheikh Kaluta Amri Abedi n.k. Lakini mimi naona Kandoro bado anao udhaifu mwingine. Ukisoma kwa uangalifu baadhi ya mashairi yake utaona kwamba ameiga mno ushairi wa Muyaka. Kwa mfano shairi la "Usione Kwenda Mbele" (uk.32) halina tofauti sana na shairi la Muyaka liitwalo "Kurudi Nyuma si Kazi." Katika shairi la Kandoro liitwalo "Baada ya Dhiki Faraja" (uk.l29) tunasoma:
Baada ya dhiki faraja, Muyaka alifumbua
Uendepo ngezi maji, kwa safari ya mashu wa
Hapo ukumbuke mbiji, ya kutweka na kutuwa
Muyaka alifumbuwa, baada ya dhiki faraji.
Ubeti huu unatukumbusha mashairi mawili ya Muyaka "Baada ya Ohiki Faraji" na "Simba wa Maji". Vile vile shairi la Kandoro liitwalo "Kimya Kina Mambo Mbele" (uk. 133) linafanana sana na shairi la Muyaka liitwaio "Kimya" ingawa Kandoro kalitumia katika mazingira tofauti.
Baada ya kujadili kwa kifupi udhaifu wa Kandoro mshairi, na ingawa si kawaida kuanza na udhaifu, inafaa sasa tuone upande wake mzuri ambao nafikiri utachukua nafasi kubwa zaidi.
Mashairi yaliyomo kitabuni si ya mtu mmoja. Yamo pia mashairi ya Amri Abedi, Mathias Mnyampala, Abubakari Mohamedi Mikdadi, Maria Rajabu, Salehe Tambwe, na wengineo. Katika ufafanuzi wangu wa masbairi ya Kandoro nitatumia yale yaliyo yake, na yale ya wengine nitakuwa nayataja tu inapohitajika - naona vigumu kupima uwezo wa mtu kwa kutumia maandishi ya watu wengine.
Tabia ya Bwana Kandoro imeelezwa vizuri sana na Sheikh K. Amri Abedi katika Utenzi wa Saadani tuuonao mwanzoni mwa kitabu. Beti hizi tano zatukumbusha machache tu kuhusu tabia yake.
Wema wake kwa yakini
Umemvutia shani
Ingawa kiduniani
Hupendezi wote pia.
Kwa kuwayu muhsani
Hufikiwa na wageni
Wajuu hata wa chini
Hupenda kufikia.
Hujitia mashakani
Ili kuridhi wageni
Hujingiw hatarini
Ili kuwatumikia.
Kijana mwenye makini
Ana nguvu ya maoni
Ana busara kichwani
Mengi hum wongokea.
Mwamuzi wa hisani
Watu wamtumaini
Uzukapo ukindani
Nduguze humuendea.
Shairi lake la kwanza "Staharaki" (uk. 10) laeleza maana ya jina lake la ushairi. Anaeleza kwamba hataharaki kwa tendo - hana haraka katika kutenda jambo, haghadhabiki na hakasiriki upesi.
Ndiye mimi Saadani, muendapole wa mwendo
Abdu si la utani, jina langu la upendo
Kandoro wangu ubini, baba simuweki kando
Sitaharaki kwa tendo, msonijua jueni.
Msonijua jueni, staharaki kwa tendo
Tendo nikilibaini, silifanyii vishindo
Vishindo ulimbukeni, limbuko si wangu mwendo
Staharaki kwa tendo, msonijua jueni.
Staharaki starani, staha wangu mtindo
Staharaki tatmi, kupigwa hata kwa nyundo
Staharaki kutamani, moyo huupigafundo
Staharaki kwa tendo, msonijua jueni.
Mshairi ametumia mtindo mzuri wa kuandika maelezo kidogo ya mashairi yake. Jambo hili karibu ni lazima katika ushairi wa Kiswahili. Mashairi mengi ya Kiswahili, hasa yale ya tambo na malumbano, ni vigumu sana kueleweka kwa watu wasio'ua chanzo au asili ya kuandikwa kwa mashairi hayo. Lakini Bwana Kandoro ameeleza kidogo maana ya mashairi fulani fulani, asili ya kuandikwa, na pengine wakati au mwaka shairi hilo lilipoandikwa. Maelezo haya tunayapata katika kila mwanzo wa shairi. Maelezo yake si mengi sana kiasi cha kumtafunia msomaji. Yanatosha kuwekamsirigi unaohitajika.
Tuchunguze kidogo jinsi Kandoro anavyoanza mashairi yake. Mara fulani fulani Kandoro anaanza mashairi yake kwa kishindo. Tazama kwa mfano, mwanzo wa shairi liitwalo "Mnapowacha Madogo na Makubwa Mtawacha" (uk. 25):
Amkeni kumekucha, wakubwa hata wadogo,
Wadogo sikuwaacha, kwa kuogopa kinyongo,
Kinyongo sikukificha, kukificha ni wongo,
Mnapowacha madogo, na makubwa mtawacha.
Tutazame mfano mwingine kutoka shairi liitwalo "Kigeugeu" (uk.22):
Kigeugeu geuka, kupinduka ni ulema
Ni uleme kupinduka, geuka ziso hekima
Kila mara kugeuka, ni kuharibu heshima
Kigeugeu si chema, kila mara kugeuka.
Katika shairi lake jingine liitwalo "Shujaa Haogopi Kitu Kilicho Halali Yake" (uk. 66) tunaona mwanzo huu.
Nisemayo muyashike, hii nishmri letu
A kuitae mwitike, tuendeshe mambo yetu
Shujaa na kitu chake, hadhulumiwi na mtu
Shujaa hahofu kitu, kilicho halaliyake
Vilevile tunapata mfano mwingine katika shairi la "Mkamia Kifo Nani?" (uk. 54).
Wasomaji kutaneni, pimeni inavyosema
Yatieni akilini, kwa busara na hekima
Tumekaa duniani, mambo mengi tunasema
Kufa mtu ni lazima, mkamia kifo nani?
Mifano hii inatosha kueleza jinsi Kandoro anavyoanza inashairi yake kwa kishindo. Tunasikia sauti yenye nguvu, sauti ya mtu mzima akizungumza, sauti ya mtu anayejua anachokizungumzia. Mwanzo kama huu husaidia kuamsha ari ya msomaji ya kutaka kuendelea.
Dhamira Kuu
Sasa tuone mawazo yake makuu yanayojitokeza katika kitabu uki. Mawazo haya nitayajadili katika mafungu matano:
1. Mawaidha yanayoambatana na misingi ya dini
2. Uvumilivu katika maisha
3. Uhusiano wake na Amri Abedi, na wenyeji wa Mafia
4. Ukoloni
5. Baada ya Uhuru
Misingi ya Dini
Katika Mashairi ya Saadani tunaona mashairi fulani fulani ambayo yanaambatana sana na misingi ya dini. Katika shairi liitwalo "Ihsani" (uk. 30) mshairi mwenyewe anatupa kwanza maelezo haya: "Shairi hili linajieleza lenyewe jinsi ya kuwafanyia ihsani viumbe na ubora wa kutenda ihsani, yaani wema. Inaeleweka katika mafunzo ya dini mbalimbali kwamba ukiwa mtenda mema japo uwatendeao wakulipe nuksani, yaani ubaya, mbele ya Mungu utalipwa wema wako."
Japo fakiri niwa, usikini na fukara
Na ubaya kufanyiwa, na kunionya ishara
Na matendo kulipiwa, ya faida na hasara
Isani kitu bora, mtenda na mtendewa.
Wazo hili kidogo sikubaiani nalo maana lina sehemu ndogo sana katika ulimwengu wa leo, ulimwengu wa kuoneana kisiasa, kiuchumi na kadhalika. Nashangaa kuona Bwana Abdu Kandoro akileta tena wazo la kupigwa shavu na kutega shavu la pili kwa tegcmeo la kulipwa na Mungu baadaye. Wazo hili linarudiwa tena katika shairi liitwalo "Binadamu Tenda Wema" (uk.18).
Katika shairi liitwalo "Moyo Maovu Sifate" (uk. 31) tunamsikia rnshairi akiuonya moyo wake:
Moyo wanambia kata, kitu cha watu sikate
Moyo wanambia vuta, kitu cha watu sivute
Moyo wanambia ita, usomjua simwile
Maovu moyo sifate, utanitia matata.
Uvumilivu Katika Maisha
Uvumilivu na kufanya kazi kwa bidii ni wazo mojawapo kubwa ambalo linaweza kujadiliwa pekee. Kwa kifupi tunaweza kusema kwamba Mashairi ya Saadani ni kitabu kinachoonyesha jitihada ya Bwana Abdu Kandoro katika kujiendeleza mwenyewe, matatizo aliyoyapata, na hatimaye kufanikiwa kwake. Tunamwona yeye na rafikiye, Tambwe, wakikazana wapate kujisukuma mbele katika maisha. Kwa upande wa Bwana Kandoro, amefanikiwa sana katika maisha. Amepata kuwa · mkuu wa wilaya, na hakuna kufanikiwa kuliko kutenda jambo ambalo umma unalitambua. Katika "Naisubiri Subira" (uk. 61) tunamsikia akisema:
Mpaka kubahatisha, ndipo upate bahati
Bahati yafurahisha, mbeleya watu umati
Aipatae hutisha, akawekwa katikati
Mtu hapati bahati, mpaka kubahatisha
Bahati kuimarisha, yataka umadhubuti
Mpaka umejichosha, kazi yako kudhibiti
Kazi yako imarisha, usiiwachie kati
Mtu hapati bahati, mpaka kubahatisha
Bwana Kandoro anapoanza kuona matunda ya kufanikiwa kwake maishani anasema katika 'Usiku Ukikomaa Karibu Kupambazuka' (uk.77):
Kipigo ukapigika, mfano wa kulemaa
Ndipo juto hukuftka, wakati wa kuchumaa
Na kupona kutafika, usiondoe tamaa
Usiku ukikomaa, karibu kupambazuka.
Amri Abeid na Weayejt wa Mafia
Uhusiano uliopo kati ya Kandoro na Amri Abedi umechukua pia sehemu kubwa kitabuni, nao umezungumziwa si katika kitabu hiki tu bali pia katika baadhi ya mashairi yaliyopo katika kitabu cha Amri Abedi cha Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri. Hapa tunaweza tu kufupisha mazungumzo haya kwa kutumia maneno ya Mathias Mnyampala yaliyomo katika Jarida la Kiswahili Toleo 35/1 Machi. 1965.
Mgogoro ule ulioanza wakati wa kuoana kwao yeye na mkwewe, Shami ulizuka tena. Fitina hiyo siwezi kuieleza hapa bali kila mmoja anaweza kuona na kusoma mashairi yaliyomo katika kitabu cha Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri.Kisa na mkasa vimeelezwa humo. Bwana Saadan Abdu Kandoro alijitahidi sana kupatanisha ugomvi huo. Juhudi hiyo ilifaulu kidogo tu na mwaka 1951 Sheikh Amri Abedi alimtaliki Bi Shami Binti Sudi baada ya mgogoro mkubwa sana.
Kati ya mashairi yanayoweza kugusa sana msomaji ni lile la "Mola Muweke Peponi Mjomba Wangu Kaluta" (uk.50), shairi juu ya kilio cha Bwana Kandoro kuhusu kifo cha Amri Abedi.
Makiwa yamenipata, imenishika huzuni
Meno ninajikeketa, nimeku wa msibani
Kandoro na ata-ata, la kushika silioni
Mola muweke peponi, mjomba wangu Kaluta.
Njiani ninapopita, mawazo tele moyoni
Msiba niliopata, kifo cha mwanachuoni
Kifo cha Sheikh Kaluta, kimemkaba yakini
Mola muweke peponi, mjombo wangu Kaluta
Jjapo tutamfata, kifo hakina fulani
Sikitiko ni kujuta, tulobaki mashakani
Maisha mwenye kufua, mwenye nguvu ni Manani
Mola muweke peponi, mjomba wangu Kaluta.
Ukoloni
Kuanzia ukurasa wa 124 hadi 164, tunaona mashairi ya kisiasa. Mashairi ya kisiasa yanachukua sehemu kubwa kitabuni kuliko mashairi ya aina nyingine. Bwana Abdu Kandoro - kama tulivyosema hapo awali - ni mmoja katika watu kumi na saba walioanzisha chama cha TANU mwaka 1954. Ni mmoja kati ya watu waliokazania sana uhuru wa Tanganyika miaka ile ya ukoloni. Bwana Kandoro alipigania uhuru kwa njia mbili: kimatendo na kimaandishi. Katika mashairi yake haya sehemu zote mbili tunaziona. Tunamwona anasafiri kwenda Mwanza kwenye mkutano wa kisiasa. Kwa upande wa maandishi Bwana Kandoro lazima apewe sifa kubwa sana kwa ujasiri aliokuwa nao - ujasiri wa kuandika mashairi yaliyokashifu serikali ya mkoloni wakati (mkoloni) akiwa bado nchini akitawala. Watu wachache sana walionyesha ujasiri huu wa kumpinga mkoloni. Washairi waliotaka kujipendekeza kwa wazungu, au walifanya hivyo kwa woga - wakiogopa utawala wa mkoloni! Lakini Bwana Kandoro ni kinyume cha waandishi kama hao. Sikiliza kwa mfano, sauti yake ya hasira katika shairi la "Kwetu Ni Kwao Kwa Nini? (uk. 139).
Mtu kuuliza nini, kitu hiki cha nini?
Kitu hiki ni cha nani, na hiki kitu cha nini?
Nacho kinailwa nim, ni cha nani na kwa nmi?
Kwetu ni kwao kwa nini, na kwao kwetu kwa nini?
Na kwa nini cha nani, na chake kwa njia gani?
Jawybu liweyakini, lisiwe purukshani?
Kwa nini sababu gani, kwao ni kwetu kwa nini?
Kwetu ni kwao kwa nim, na kwao kwetu kwa nini?
Kwa nini kwao kwa nini, kuwe kwetu ni kwa nini?
Na kwetu pia kwa nini, kuitwa kwao kwa nini?
Kwa nini ina yakini, kwetu ni kwao kwa nini?
Kwetu ni kwao kwa nini, na kwao kwetu kwa nini?
Mtu kwao kuthamini, ijapokuwa jiweni,
Pia alale mtini, na baraza liwe chini
Nile matunda porini, kuitwa kwenu kwa nini?
Kwetu ni kwao kwa nini, na kwao kwetu kwa nini?
Wakati Sheikh Amri Abedi alipokuwa kule Missionary College Rubwa, Pakistan, Bwana Kandoro alimuandikia shairi la "Siafu Wamekazana" ili kumjulisha maendeleo ya wananchi katika kupigania Uhuru. Ni shairi la kiwango cha juu sana, lakini hapa nitadondoa beti mbili tu:
Nyoka amegutuka, ndani ya shimo katuna
Tena amekasirika, hasira zenye kununa
Nyoka anababaika, shimoni kwa kujikuna
Siafu wamekazana, nyoka amekasirika.
Shimoni ataondoka, hilo nataja kwajina
Nyoka anajuwa fika, siafu wakiungana
Nguvu zinaongezeka, shimoni watagombana
Siafu wamekazana, nyoka amekasirika.
Baada ya Uhuru
Jambo la mwisho ambalo nitagusia ni mashairi yake yaliyoandikw, baada ya uhuru. Katika mashairi haya tunamwona Kandoro huko Mafia akiwa mkuu wa wilaya hiyo, na jinsi anavyoshirikiana na watu na kuwahimiza wafanye kazi kwa bidii. Mhakiki wa kitabu hiki anasema:
Washairi wengine nyoyo zao huguswa zaidi na vitu kama uzuri wa umbile la dunia, mabonde, milima, ndege n.k. Wengine huguswa zaidi na fikira za upeo mbali mbali kama vile mwenendo mwema, imani kwa Mungu, ubaya na wema katika maisha n.k. Bwana Kandoro anaguswa zaidi na watu wenzi wake, sahiba zake, na hata wapinzani wake.
Mashairi aliyoandika baada ya uhuru yanatufikisha kwenye upeo wa maisha yake. Kwa kumalizia tunaweza kusema kwamba Bwana Kandoro ameweka msingi mzuri sana kwa washairi wa Tanzania - nchi ambayo inajali zaidi watu kuliko uzuri wa milima na mabonde wanamoishi.
Maswali
1. Ijadili dhamira ya uzalendo ijitokezavyo katika Mashairi ya Saadani.
2. Tumia shairi la "Siafu Wamekazana" ujadili matumizi ya taswira katika kujenga dhamira ya shairi hili.
3. Chagua dhamira kuu tatu zijitokezazo katika Mashairi ya Saadani ujadili kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mwandishi katika kuziibua dhamirahizo.
4. "Katika Mashain ya Saadani tunagundua mshairi ambaye yu mwanasiasa tangu mwanzo hadi mwisho." Jadili.
Powered by Blogger.