Lahaja Na Mitindo Katika Kamusi ya kiswahili Sanifu
Lahaja Na Mitindo Katika Kamusi ya kiswahili Sanifu
Utangulizi
Makala haya yamegawany wa katika sehemu mbili. Katika sehemu ya kwanza tutajaribu kutoa maelezo mafupi sana ya kinadharia kuhusu dhana zinazovipamba vipengele vya lahaja na mitindo katika lugha kwa ujumla. Katika kufanya hivyo tutajaribu pia kujadili umuhimu wa vipengele hivi katika utengenezaji wa kamusi kwa ujumla. Katika sehemu ya pili tutajaribu kujadili na kutoa tathmini ya namna vipengele vya lahaja na mitindo vinavyojitokeza katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu (tangu sasa K K S).
Lahaja
Wanaisimu wengi huelekea kukubali kwamba ni vigumu (na pengine haiwezekani) kuweka mipaka bayana baina ya lugha na lahaja; na kwamba kwa msingi huo si rahisi kutoa fasili ya lahaja inayokubalika kwa wanaisimu wote (ling. Anttila, 1972:289 - 292; Hudson, 1980: 21 -31; Akmajian, et al. 1984:286 - 298, kwa uchache). Kauli hii inathibitika zaidi tunapojaribu kuzichunguza fasili kadhaa zilizowahi kutolewa kuhusu dhana ya luhaja (taz. mifano) ifuatayo hapa chini).
Crystal katika kamusi yake ya A Dictionary of Linguistics and Phonetics (1985:92) anasema lahaja ni "mtindo bainifu wa lugha kieneo na kijamii unaobainishwa na seti maalumu ya maneno na miundo ya kisarufi" [tafsiri ni yangu]. Katika Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (TUKI, 1990:21) tunaambiwa kuwa lahaja ni "kitarafa cha lugha kinachobainika ama kijamii au kijiografia na kudhihirishwa na vipengee maalumu vya kisauti na kimuundo". Pei na Gaynor katika kamuisi yao ya Dictionary of Linguistics (1980:56) wanasema lahajani "namna maalumu ya lugha fulani inayotumiwa katika mahali au eneo fulani la kijiografia. yenye kuonyesha tofauti za kutosha, ikilinganishwa na ile [lugha] sanifu au ya kimaandishi. katika matamshi, miundo ya kisarufi na matumizi ya nahau kwa kiwango cha kuifanya namna hiyo ijibainishe kama kilu kinachoweza kusimama peke yake; lakini wakati huo huo isiweze knsigana mno na lahaja nyingine za lugha ihusikayo kwa kiwango cha kuifanya ibainishwe kama lugha tofauti" [tafsiri ni yangu].
Nayo kamusi ya Longman Dictionary of the English Language (1984:402) inasema lahaja ni" 1. mtindo bainifu wa lugha kieneo au kijamii... unaotofautiana na lugha sanifu; 2. yoyote mojawapo kati ya kundi la lugha zinazohusiana; 3. mtindo wa lugha unaotumiwa na kundi la watu wa shughuli moja". Tukizichunguza sana fasili hizi tutaona kwamha hakuna hata moja amhayo ni rupia kwa nyingine. Fasili zote zinasigana kwa kiwango fulani. jambo ambalo linathibitisha ugumu wa kuwepo kvva fasili moja mwafaka kwa wanaisimu wote. Lakini pamoja na msigano unaojitokeza katika fasili hizi kuna mambo mawili muhimu yanayojidhihirisha katika hali ya kufanana. Mambo hayo mawili ni mazingira ya kijiografia (au kieneo) na mazingira ya kijamii. Kutokana na sifa llizi mbili za lahaja, wanaisimu. na hasa wanaisimujamii, wamekuwa wakizigawa lahaja katika makundi makubwa mawili: lahaja za kijiografia na lahaja za kijamii. Katika mtazamo wa kijiografia lahaja ni mtindo maalumu wa lugha uliohainifu na unaotumiwa katika eneo fulani la kijiografia. Lahaja za kijamii ni mitindo maalumu wa lugha uliobainifu na unaotumiwa na tabaka fulani la kiuchumi-kijamii. k.m. makuli, wasomi. walala hoi. n.k. Aidha baadhi ya wanaisimu wamejaribu kupendekeza na kudai kuwa liko pia kundi la tatu la lahaja ambalo hupewajina la lahaja za kimbari. Mfano mmojawapo wa lahaja za namna hii ni ule mtindo wa Kiingereza uitwao "Yiddish English" - lahaja ambayo ina chimbuko la kihistoria (kutokana na Wayahudi wa zamani wa Ulaya Mashariki). Kwa kifupi lahaja za kimbari zina msingi wa kihistoria.
Mitindo
Ikichukuliwa katika mtazamo mpana zaidi istilahi mitindo hujumuisha vipengele vingi ikiwa ni pamoja na lahaja sanifu, lahaja za kimaandishi, lahaja za kijiografia, lahaja za kihistoria, lahaja za kijamii, n.k. (ling. Crystal, 1985:292). Kwa madhumuni ya makala haya istilahi mitindo imetumiwa kwa maana ya mitindo kulingana na matumizi ikitatbutishwa na mitindo kulingana na watumiaji (ling. Hudson, 1980:48) au vinginevyo. Kwa maneno mengine tunaweza kusema istilahi mitindo, katika matumizi yetu ya sasa, ina maana ya kile ambacho baadhi ya wataalamu wamekiita rejesta; yaani matumizi ya lugha kulingana na muktadha. Binafsi napendelea zaidi kutumia istilahi ya mtindo muktadha badala ya rejesta. Hivyo kuanzia sasa nitakuwa nikitumia istilahi mtindo muktadha nitakapokuwa nikirejelea dhana hii.
Tumesema kwamba Mtindo muktudha, ambao ndio tutakaohusika nao katika majadiliano yetu, huhusu matumizi ya lugha kulingana na muktadha. Kwa lugha ya kawaida tunaweza kusema mtindo muktadha ni matumizi ya lugha kulingana na mazingira mbalimbali ya mahusiano ya kijamii, k.m. mazingira ya kidini, kisayansi, kisiasa, kibaharia, n.k. bila knjali tahaka la mtu; tofauti na mtindo wa lahaja ya kijamii ambao huegemea zaidi matabaka ya watu (k.m. wasumi, walala hoi, wafanyiwa kazi, n.k.) mtindo muktadha haukukitwa kwenye matabaka ya namna hiyo.
Lahaja na Mtindo Muktadha katika Kamusi
Je kuna haja yoyote ya kuingiza maneno ya kilahaja au ya kimtindo muktadha katika kamusi? lunaweza tu kupata jibu la swali hili kwa kujiuliza swalijingine: je. kamusi ni nini? Kwa lugha sahili kabisa tunaweza kusema kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno ya lugha (ambayo aghalabu hupangwa katika mtindo wa kialfabeti) yenye maelekezo kuhusu maana zake, tahajia zake na matamshi yake; au orodha ya maneno ya lugha rnoja na visawe vya maneno hayo katika lugha nyiungine. Tukizingatia fasili hiyo ya kamusi itatudhihirikia wazi kwamba kamusi haibagui lahaja wala mtindo muktadha. Ndiyo kusema kazi ya kamusi ni kueleza maneno yote (au baadhi tu ya maneno hayo) ya lugha kama yanavyotumika. Ama kwa hakika maelezo hayo yanashadidiwa na ukweli uliowahi kujitokeza katika baadhi ya lugha kama vile Kiingereza. Katika lugha ya Kiingereza tunao ushahidi unaoonyesha kwamba mapema kabisa mnamo mwaka 1671 Skinner katika kamusi yake ya Etymologicon Lingua Anglicana alifanyajitihada za makusudi kabisa kuingiza maneno ya kilahaja 1. Halikadhalika Coles naye katika kamusi yake ya An English Dictionary (1676) alifanya jitihada za makusudi za kuingiza maneno ya kilahaja. Katika kamusi hiyo Coles alikuwa akieleza au akitoa fasili za "maneno magumu" yaliyokuwa yakitumiwa katika nyanja mbalimbali za elimu/maarifa katika lahaja mbalimbali za Kiingereza2
1 Katika baadhi ya maandishi kamusi ya Coles (1676) ndiyo isemekanayo kuwa ya kwanza kuingiza maneno ya kilahaja (ling. Osselton, N.E., 1958; Landau S.I. 1984).2 Hapa yaelekea "maneno magumu" ina maana ya maneno ya nyanja maalumu kulingana na lahaja.
Mifano iliyotolewa hapo juu ni michache tu kati ya mifano mingi iliyopo inayoonyesha kwamba watungaji wa kamusi za Kiingereza walikuwa wakizingatia sana vipengele vya kilahaja. Ama kwa hakika kuanzia miaka ya 1650 na kuendelea tunaona kamusi nyingine za Kiingereza zikiibuka na zikiwa na maneno mengi ya kilahaja. Kwa upande wa mtindo muktadha hali ilikuwa hiyohiyo. Mmoja kati ya mifano maarufu ni ile faharasa ya S. Pegge: Alphabet of Kenticism (1735), na ile ya W. Pryce: Mineralogia Cornubiensis (1778) ambayo ina maneno yaliyokuwa yakitumika katika migodi ya bati ya Corn.3 Hii inadhihirisha kwamba kamusi hizo za zamani zitikuwa pia zikizingatia maswala ya mitindo muktadha.
3 Kwa lugha ya kileo tunaweza kusema maneno haya yalikuwa istilahi.
Je, kila Kamusi ilizingatia Vipengele hivi?
Ingawa tumesema kwamba kamusi za zamani za Kiingereza zilizingatia sana masuala ya lahaja na mitindo muktadha yafaa tutoe hadhari kwamba si kila kamusi ilifanya hivyo. Ama kwa hakika kuingizwa au kutoingizwa. kwa makusudi. kwa vipengele vya lahaja na mitindo muktadha kulitegemea madhumuni ya kamusi iliyohusika. Kwa mfano kamusi nyingi za Kiingereza za kabla ya karne ya kumi na saba hazikufanya jitihada za makusudi za kuviingiza vipengele vya lahaja na mitindo muktadha. Kuhusu suala hili Wakelin (1987) anasema kwamba wanaleksikografia wa zamani wa Kiingereza kama vile Levin (1570). Mulcaster (1582), Coote (1596). Cawdrey (1604). Bullokar (1616), n.k. hawakutanyajitihada zozote za makusudi za kuingiza maneno ya kilahaja katika kamusi zao (Burchfield. 1987: 156-177). Hii ni kwa sababu lengo lao kubwa lilikuwa ni kuelezea maana za "maneno magumu".
Kwa hakika si wanaleksikografia wa karne kabla ya kumi na saba tu ambao hawakulizingatia suala la lahaja. Hata wanaleksikografia wa baadaye pia waliliweka kando kidogo suala hili. Mfano mzuri hapa ni wa Johnson katika kamusi yake ya A Dictionary of the English Language (1755). Katika kamusi hii Johnson hatilii maanani masuala ya lahaja. Lakini Johnson anafanya hivyo kwa makusudi kabisa kutokana na haja ya wakati huo ambayo ilikuwa ni kufanya lugha iwe bora zaidi na iwe na mfumo na rnuundo usioyumba- yumba. kujenga matanishi ya aina moja yanayokubalika, n.k. Kwa ufupi nia yake ilikuwa imelenga zaidi katika usanifu wa lugha. Katika mpango wa kamusi ya Johnson neno "lahaja" halitajwi kabisa. Mpango wake unaeleza dhahiri kwamba kamusi hiyo iliegemea zaidi lugha ya maandishi ya wale waandishi marufu wa enzi hizo.
Lahaja na Mitindo Muktadha katika kamusi sanifu
Tumekwishasema hapo juu kwamba kuingizwa na kutoingizwa kwa lahaja na mitindo katika kamusi kunategemea sana nia na madhumuni ya kamusi inayohusika. Kwa kuwa uingizaji wa vipengele hivi katika kamusi unategemea nia na madhumuni ya kamusi hiyo haiwezekani kukawa na kamusi za aina moja. Lakini la msingi zaidi na ambalo linatuhusu hapa ni kwamba kamusi ambayo imelengwa katika usanifishaji wa lugha hujaribu, kadri iwezekanavyo, kuepuka mambo ambayo yamemili yaani yameegemea zaidi katika upande wa lahaja au yaliyomili zaidi katika mitindo muktadha. Hata hivyo hapa inabidi tutoe tahadhari kidogo. Yako maneno ambayo kwa hakika yanaweza kuwa na msingi wa kilahaja au kimtindo muktadha lakini yakawa yamekwishapenya katika lugha kwa kiasi cha kuyafanya yasiweze kuepukwa katika kamusi ambayo madhumuni yake ni kusanifisha lugha. Hata kamusi ya Johnson tuliyoitaja hapo juu haikufanikiwa kabisa katika kuepuka maneno yenye asili ya kilahaja au yale ya mtindo muktadha. La muhimu kuzingatia ni kwamba maneno ya namna hiyo huingizwa katika kamusi sanifu ya lugha kwa kuzingatia mambo mawili. Kwanza ni kuhakikisha kwamba maneno hayo ya kilahaja yamek wishajipenyeza katika lugha kwa kiwango cha kueleweka na kukubalika (na pengine kutumika katika lahaja nyingine). Pili, maneno hayo huingizwa katika kamusi sanifu inapokuwa yanavveza kueleza vizuri dhana mpya ambazo ama hazina kabisa maneno ya kuziwakilisha au maneno yanayoziwakilisha katika lahaja sanifu hayatoshelezi. Vinginevyo ni muhimu kuhakikisha kwamba maneno ya mitindo ambayo ni ya kilahaja yanaepukwa kadri iwezekanavyo katika zoezi la kutunga kamusi sanifu.
Lahaja katika KKS
Kwa bahati mbaya mpango uliotumiwa katika KKS hauonyeshi wazi ni maneno yapi ambayo ni ya kilahaja na yapi ambayo si ya kilahaja. Kutokana na hali kama hiyo haiwi rahisi kujua moja kwa moja ni neno lipi limetoka katika lahaja gani. Lakini hii haina maana kwamba hakuna maneno ya Idlahaja yanayojitokeza katika KKS; kwa hakika yako mengi sana. Swali la kujiuliza ni kwamba tutayakabili au kuyabainisha vipi maneno kama bayo?
Kwa madhumuni ya makala haya, na kwa kuwa hatutakuwa tunarejea kwenye labaja fulani maalumu, tutayagawa maneno yenye uelekeo wa namna hiyo katika makundi mawili- Kundi la kwanza ni yale maneno ambayo ingawa yanapatikana katika KKS lakini hayamo kabisa, au ni vigumu sana kuyakuta, katika matumizi ya lugha sanifu inayotumiwa na sehemu kubwa ya wasemaji wa Kiswahili. Mengi kati ya maneno haya yaelekea kuwa yale yenye asili ya Kiarabu ambayo" tunaweza kusema yalilazimishwa kuingia katika Kiswahili kisha yakashindwa kupata mashiko mahali pengi. Kundi la pili ni yale maneno ambayo katika eneo moja la Kiswahili hutamkwa namna tofauti au hupewa neno tofauti na eneo jingine.
Ili kuweza kupata picha kamili ya suala hili yafaa tutoe mifano michache. Tuchunguze mifano ifuatayo ambayo inahusu kundi la kwanza, (namba zilizomo katika mabanoupinde zinaooyesha ukurasa katika KKS ambako neno linalohusika hupatikana)
adawa =
|
uadui (2)
|
ujihi =
|
tembelea mtu aishiye mbali (4)
|
ajinabia =
|
-a kigeni, -gem (4)
|
alfeni =
|
elfu mbili (5)
|
arshi =
|
malipo kwa kuntoa mtu damu; dia; fidia (9)
|
arshi =
|
kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu, kiti cha enzi cha mfalme au mtawala (9)
|
ashara =
|
kumi (9)
|
aruba =
|
nne (9)
|
arubii =
|
haraka, upesi (9)
|
atibu =
|
toa makosa; laumu (10)
|
bahaimu =
|
mnyama mwenye. tabia za ovyoovyo; mpuuzi (12)
|
bahaluli =
|
mtu mpumbavu asiyetumia akili yake (12)
|
balighisha =
|
fikisha maneno au salamu (14)
|
balwa =
|
balaa, baa (14)
|
baraste =
|
barabara iliyotengenezwa vizuri (15)
|
bariziana =
|
kabiliana katika vita (16)
|
budhara =
|
uharibifu au upotevu wa mali kwa matumizi ya fujo (22)
|
fulifuli =
|
haraka sana; mbiombio (59)
|
fulusi =
|
fedha, pesa. seti, hela (59)
|
gahamu =
|
kataa kuendelea na jambo (64)
|
gashi =
|
msichana (65)
|
gawadi =
|
mtu anayemtongozea mtu mwingine; kuwadi (65)
|
ghaidhi =
|
hasira, ghadhabu (66)
|
ghashi =
|
udanganyifu, ulaghai (66)
|
hadhirina =
|
watu walichudhuria (72)
|
jalili =
|
enye kuheshimika (88)
|
hadhongo =
|
chai; chirimiri, hongo (95)
|
kadimisha =
|
peleka mbele; tanguliza (95)
|
maujudi =
|
enye kupatikana whati wote (156)
|
msalkheri =
|
tamko linaiotumiwa kumwamkia mtu agh. wakati wa jioni au usiku (187)
|
nusklua =
|
nakalu (218)
|
sabalkheri =
|
tamko la kumtaka mtu hali wakati wa asubuhi ..... (245)
|
sabatashara =
|
kumi na saba (245)
|
ubahaimu =
|
unyama; hali ya kuwa na tabia zilizo za ovyo (290)
|
wabaadu =
|
na baada ya haya (aghalabu.... katika barua) (315)
|
wahedi =
|
moja (316)
|
wahshi =
|
enye kutokuwa na maana; ovyo (316)
|
zeriba =
|
zizi au boma la ng 'ombe. (322)
|
zuumu =
|
kuwa na nia ya kufanya jambo
|
Tukiyachunguza sana maneno baya tunaona dhahiri kwamba ingawa yamo katika kamusi ya KKS hayaelekei kuwa sanifu kwa sababu mbili kubwa. Kwanza si maneno yanayojitokeza sana katika maandishi mengi ya Kiswahili sanifu; achilia mbali ukweli kwamba wasemaji wengi wa Kiswahili sanifu hawayajui. Pili, mengi kati ya maneno haya yanaelekea kuwa oa asili ya Kiarabu au lugba nyingine. Kutokana na hali hiyo ni dhahiri kwamba watumiaji wengi wa maneno haya ni wale ambao ama wana athari au wana msingi wa iugha ya Kiarabu. Kwa hakika haya ni maneno ambayo aghalabu yatakuwa yanatumiwa zaidi na watu wa pwani wenye sifa iliyotajwa hapo juu. Kwa yale maneno ambayo hayana asili ya Kiarabu au lugha nyingine mbali na Kiswahili huenda yametokana na lahaja.
Tulisema kwamba kundi la pili ni lile lenye maneno ambayo katika eneo moja la Kiswahili hutamkwa namna tofauri na eneo jingine. Chunguza mifano ifuatayo:
abunuwasi > banawasi > bunuwasi > kibanawasi [jina la mhusika mjanja katika hadithi za masimulizi] (1)ahadharu > ahdhari > akhdhari [rangi ya kijani] (3)angalau > angalao > ngaa > angaa > angao [neno litumikalo kuelezea lililokuwa afadhali; japokuwa. lau] (8)bajia > badia > bagia [aina ya chakula kama andazi dogo...] (13)biringani > biringanya > biringiani [aina ya mboga jamii ya nyanya mshumaa ...] (20)blangeti > blanketi > bulangeti > burangeti [guo zito la kujifunika ili kujihifadhi na baridi] (20)bradha > bruda [mtawa mwanamume asiyekuwa kasisi au padre] (22)chakleti > chakeleti > chakuleti > chokoleti [aina ya peremende rangi ya kunde ....] (28)charahani > cherehani [mashine ya kushonea] (30)dazani > darzani > dazenu > darzeni [jumla ya vitu kumi na mbili] (42)durusu > darisi > durusi [soma kitabu kwa mazingario; pitia tena yale uliyokwishasomeshwa] (49)ebu > hebu > hembu [tamko linalotumiwa kumwita mtu atazame ..] (50)edita > editori (mtayarishaji wa makala au maandishi....] (50)epa > hepa > kwepa [jiondoa, jitoa, jihadhari usipigwe na kitu] (51)faharasa > faharisi [orodha ya vichwa mambo yaliyomo...]fazaa > fadhaa [hangaiko la moyo; wasiwasi.................] (55)goligoli > golegole > goregore [ndege aliyefanana na ... : kobozi liliokaa...] (69)halwaridi > alwaridi > lawaridi > wardi [ua mojawapo linalonukia vizuri; uturi ulio...] (74)husudu > husudi [onea kijicho; penda mno. sifu] (83)ibra > ibura [kitu au tukio la ajabu....; mafundisho,....] (83)ilimu > elimu [mafunzo, masomo au ujuzi ..; maarifa,...] (85)jamati > jamatikhana > jamatikhane [jumba la mkusanyiko wa wafuasi wa Agha Khan....] (88)karne > karni > karini [muda wa miaka mia moja] (102)legalega > regarega [kosa kuwa imara] (143)lekeza > elekeza [onyesha, basa njia, kwa maelezo au michoro] (143)nwongo > mrongo [mtu mwenye tabia ya kutosema ukweli] (206)ngeu > ng 'eu [rangi nyekundu; damu; jeraha la kichwani..](214)paaza > paza > paraza [saga kitu kama vile mbegu za mahindi, ...] (224)pachipachi > patipati [katikati ya; sehemu iliyoko katikari ya ....] (224)purutangi > patangi > pwitangi [aina ya chombo kama puto kubwa ....] (237)rejea > regea [fika tena ulipokuwa umepaondoka] (241)sombera > sombea [jisogeza kwa kutumia miguu na mikono...] (264)wehua > ehua [fanya mtu kuwa mwehu] (318)ziaka > riaka [kitu maalumu kinachotengenezwa kwa ngozi ...] (322)
Mifano iliyotolewa hapojuu ni sehemu kidogo tu ya maneno mengi sana yanayojitokeza katika KKS. Uchunguzi wa makini wa mifano hii unadhihirisha matatizo kadhaa. Baadhi ya matatizo hayo ni kama ifuatavyo:
(a) katika maneno haya kuna namna mbalimbali za matamshi ya neno hilohilo moja. Je, ni yapi matamshi sahihi: Ni yapi matamshi sahihi: halwaridi au alwaridi au lawaridi au wardi? Je, tutamke chakleti au chakeleti au chakuleti au chokoleti? Bila shaka matamshi haya yote yanakubalika na ndiyo maana yakaingizwa katika kamusi hii. Kwa msingi huo tunaweza kusema matamshi haya yote ni sahihi, angalau kwa mtazamo wa kiisimu. Lakini, je, matamshi haya yote ni sanifu? Hapa ndipo tatizo linapojitokeza. Kwa mujibu wa kanuni za usanifishaji haiwezekani kuwa na namna mbalimbali za matamshi ya neno hilo hilo moja katika lahaja hiyo hiyo moja. Katika usanifishaji wa matamshi ya lugha inashauriwa kuwe na namna moja tu ya utamkaji wa neno. Iwapo itakuwa hapana budi kuwa namna mbili za utamkaji wa neno hilo hilo moja basi ihakikishwe kuwa namna hizo mbili zinakaribiana sana. Tukichukulia kuwa msingi huu wa kinadharia ni sahihi itadhihirika kwamba matamshi ya maneno mengi katika KKS hayakusanifishwa. Iwapo matamshi ya maneno hayo si sanifu lakini yanakubalika kuwa matamshi sahihi katika maeneo mbalimbali ya wazungumzaji wa Kiswahili ni dhahiri kwamba matamshi hayo ni ya kilahaja.
(b) data yetu inadhihirisha kuwa kuna maneno mengi katika KKS ambayo yana namna mbalimbali za kuandikwa. Hapa pia inabidi tujiulize. Ni yapi maandishi sahihi: ahadharu au ahdhari au akhdhari?; bajia au badia au bagia ?; biringani au biringanya au biringiani?; dazani au darzani au dazeni au darzeni?; edita au editori ?; fadhaa au fazaa?. n.k. Pengine hapa pia kwa kuzingatia namna zote hizi ambazo zimewahi kutumiwa na waandishi mbalimbali wa Kiswahili tunaweza kusema kuwa kila namna iliyojitokeza hapa ni sahihi kulingana na lahaja za waandishi mbalimbali. Lakini kama tulivyosema kuhusu kipengere cha matamshi tunaweza kusema pia kwamba tukitaka kusanifisha maandishi ya lugha basi itabidi tuwe na namna moja tu ya kuliandika neno. Ni kweli kwamba mara moja moja katika haadhi ya kamusi za lugha nyingine tunaweza kukuta maneno ambayo yana namna mbili tafauti za kuandikwa. Lakini ni kweli pia kwamba kamusi hizo huwa hazidai kwamba namna zote mbili ni sanifu. Tukizingatia kauli tuliyotoa kuhusu usanifishaji wa maandishi katika kamusi tunaweza kusema kuwa kuna maneno mengi katika KKS ambayo maandishi yake si sanifu, ni ya kilahaja.
(c) katika KKS kuna tatizo jingine linalojitokeza na ambalo linahusiana sana na maandishi. Tatizo hilo ni utohoaji wa maneno. Tunapoyachunguza maneno kadhaa yaliyotoholewa tunashindwa kupata misingi thahiti iliyotumiwa katika kutohoa maneno hayo. Mifano michache itayadhihirisha madai yetu. Kwa nini neno blanket liwe ama blangeti au blanketi au bulangeti au barangeti?; kwa nini neno dozen liwe ama dazani au darzani au dazeni au darzeni ?; na kwa nini neno editor liwe ama edita au editori, n.k.? Laiti kungekuwa na misingi thabiti na sanifu ya utohoaji tungekuwa na namna moja tu ya kutohoa neno.
(d) tatizo jingine linalojitokeza ni kule kuweko kwa matumizi badilifu ya sauti [l] na [r]. Kwa mfano kuna maneno kama: goligoli > golegole > goregore, bulangeti > burangeti; regarega > legalega. Ingawa ni kweli kwamba katika lugha nyingi za Kibantu kuna matumizi badilifu ya sauti [l] na [r] si kweli kwamba kila tutakapokuta mazingira ambamo sauti moja hutokea basi sauti nyingine pia huweza kutumiwa badala yake. Kwa mfano neno kilimo haliwezi kuwa *kirimo wala harufu haliwi *halufu. Kwa hiyo katika lugha sanifu kuna haja ya kuwa makini zaidi katika matumizi ya sauti hizi mbili. Kwa maoni yetu matumizi ya sauti [l] na [r] yanayojitokeza katika maneno hayo hapo juu yametokana na kuchukua matamshi ya neno hilo hilo moja katika lahaja mbalimbali na kuyaingiza katika KKS bila ya kuyasanifisha.
Ama kwa hakika kuna mambo mengi sana tunayoweza kusema kutokana na data tuliyonayo. Lakini tukiyaingilia hayo tutakuwa tunatoka nje ya mawanda ambamo tumepewa kuogelea. Tunachoweza kusema hapa ni kwamba kwa kuangalia mifano michache tuliyoiona ni dhahiri kwamba KKS ina maneno mengi yaliyotokana na lahaja nyingine za Kiswahili. Ingawa maneno haya ya kilahaja yanaitajirisha kamusi hii lakini yameingizwa kiholela bila kuzingatia kanuni za usanifishaji zitakikanazo ili kuifanya kamusi iwe kamusi sanifu.
Mtindo Muktadha katika KKS
Mtindo muktadha ni kipengee kimojawapo kati ya vipengee vilivyo vigumu kushughulikia katika kamusi sanifu ya lugha ya kawaida. Hii ni kwa sababu si rahisi kupata vigezo makini sana vya kutumia katika kuamua ni maneno ya mtindo muktadha upi yanastahili kuingizwa na ya mtindo muktadha upi hayastahili kuingizwa katika kamusi ya namna hiyo. Je, tuingize maneno ya kidini, kibaharia, kiteknolojia, kisayansi au yapi? Na kama tutaamua ni maneno ya mtindo muktadha upi yaingizwe, je tutumie vigezo gani katika kuamua ni kwa kiwango gani maneno hayo yaingizwe?
Uchunguzi kidogo tu wa maneno ya kimtindo muktadha yaliyoingizwa katika KKS utadhihirisha kwamba takribani robotatu ya maneno hayo ni maneno ya kidini, yakifuatiwa kwa kiasi tulani na maneno ya kibaharia. Tukizingatia mazingira ambamo Kiswahili kilianzia na kuinukia hatutashangaa kuona hali kama hii ikijitokeza katika kamusi hii. Lakini tukizingatia pia kwamba mawanda ya Kiswahili yamepanuka sana siku hizi iko haja ya kujiuliza kama kweli hatuna haja ya kuupa mtazamo tofauti kidogo utaratibu wa kukiingiza kipengele hiki katika kamusi kama hii. Kwa mfano tunaweza kujiuliza kama kweli maneno ya kidini yana umuhimu mkubwa zaidi kuliko yale ya kiuchumi, kisayansi au kiteknolojia; au kama maneno ya kidini yaliyomo katika KKS yamejipenyeza zaidi katika lugha ya kawaida kuliko maneno ya mitindo miktadha mingine.
Aidha tukiyachunguza, kwa makini maneno ya kipengele hiki yaliyoingizwa katika KKS tutatambua kuwa hakuna vigezo makini vilivyotumiwa katika kuchagua ni maneno yapi yaingizwe na maneno yapi yasiingizwe. Je, yawezekana kwamba maneno yameingizwa kwa kufuata kutokea kwake mara nyingi katika matumizi ya lugha ya kawaida? Uchunguzi kidogo wa maneno haya utathibitisha kwamba hii si kweli. Mfano mzuri hapa ni majina kama Muhamad na Yesu, majina ambayo yanasikika sana katika lugha ya kila siku katika wasemaji wa Kiswahili walio wengi. La kushangaza ni kwamba maneno haya hayamo katika KKS! Sababu ni nini? Je, inawezekana kwamba hayakuingizwa kwa sababu ni majina matakatifu? Lakini hiyo haiwezi kuwa kweli kwani majina hayo hayawezi kuwa matakatifu zaidi.kuzidi Allah (1) au Mungu (199), majina ambayo yamo katika KKS. Mfano mwingine unahusu uingizaji wa majina ya malaika. Je, ni kigezo gani kilichotumika kuingiza majiaa ya malaika Israfili (au Sirafili), Ibilisi na Munkari na kuacha kuingiza majina ya Ziraili (au Israeli) na Jibrili (au Gabrieli) ? Isitoshe, katika baadhi ya dini za wasemaji wa Kiswahili kunatambuliwa majina mengine ya malaika kama vile Rafaeli na Mikaeli; majina haya nayo hayamo katika KKS. Swali linaendelea: kigezo ni nini?
Tunachojaribu kusema hapa ni kwamba utaratibu uliotumiwa katika kushughulikia kipengele cha mtindo muktadha katika KKS haukukitwa kwenye vigezo tbabiti, na hivyo kukifanya kipengele hiki kuwa na sura iliyokaa kombo.
Pamoja na vigezo vingine vinavyoweza kutumiwa katika kushughulikia kipengele hiki katika kamusi ya namna hii kuna vigezo muhimu viwili ambavyo vinapaswa kuzingatiwa. Kwanza maneno ya kimtindo muktadba ambayo yameelemea zaidi katika taaluma maalumu yafaa yasiingizwe katika kamusi ya namna hii. Kwa msingi huo maneno kama adaa (2), allahuma (6), altare (6). istiskaa (86), katekista(103), pengine yasingestahili kuingizwa katika KKS. Pili, kama tulivyodokeza hapo awali maneno ya kimtindo muktadba yanayostahili kuingizwa katika kamusi kama KKS shurti kwanza yawe yamekwishajipenyeza katika lugha ya kawaida kwa kiwango cha kuyafanya yaonekane ya kawaida na yenye kukubalika katika matumizi yasiyo ya kitaalamu. Kwa mfano, ingawa maneno kama Ramadhani, maulidi, kusilimu, kuhiji, msikiti, mfungo mosi, Krismasi, Pasaka, Kwarezima, ubatizo, kanisa, Muhamad, Yesu na Mungu ni maneno ya mtindo muktadha wa dini yanastahili kuingizwa katika KKS, kwa sababu takribani watumiaji wote wa Kiswahili wanayajua na wameyazoea.
Hitimisho
Makala haya yamejaribu kushughulikia mambo mawili muhimu kuhusu vipengele vya lahaja na mitindo katika kamusi. Kwanza tumejaribu kutoa maelezo mafupi ya kinadharia kuhusu uingizaji wa vipengele hivi katika kamusi na hasa kamusi sanifu ya lugha yoyote ile. Pili, tumejaribu kuonyesha jinsi gani vipengele hivi viwili vimeshughulikiwa katika KKS. Katika kuchunguza mamna vipengele hivi vilivyoshughulikiwa katika KKS tumeona matatizo kadhaa yakijitokeza. Kutokana na matatizo hayo tukahitimisha kuwa maneno ya kilahaja na mitindo yaimeingizwa katika KKS bila kuzingatia utaratibu wa usanifishaji wa lugha. Tumejaribu pia kuonyesha jinsi gani matatizo hayo yaliyojitokeza yangeweza kuepukwa. Ni matarajio yetu kwamba mchaago wetu utaweza kusaidia kidogo katika zoezi la kuiduruso kamusi ya KKS.
MAREJEO
Akmajian, A. et. al 1984. Linguistics: An Introduction to Language and Comunication: Second Edition. Massachusetts: MIT Press.
Anttila, R. 1972. An Inroduction to Historical and Comparative Linguistics. New York: Macmillan Publishing Co., Inc.
Bwenge, C.M.T. 1992. "Uteuzi wa Msamiati na Uingizaji wa Vidahizo katika Kamusi Ukarii wa KKS." Makala yasiyochapishwa.
Crystal, D. 1985. A Dictionary of Linguistics and Phonetics.
Homby. A. (Ed.) 1974. Oxford Advanced Leamers Dictionary of Current English. Oxford: Oxford University Press.
Hudson, R.A. 1980. Sociolinguistics. Cambridge: Cambridge University Press.
Pei, Mario A. and Frank Gaynor 1975. Dictionary of Linguistics. Littlefield, Adams & Co.
TUKI. 1981. Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi, Dar es Salaam: OUP.
Wakelin. Martyn F. 1987. "The Treatment of Dialect in English Dictionories" in Burchfield, R. (Ed.) Studies in Lexicogrophy. Clarendon.