JIPIME-MTIHANI
MAELEKEZO:
- Karatasi hii ina sehemu A, B, C, D
- Jibu maswali saba 7 kwa kuchagua swali (1) kutoka kila sehemu isipokuwa B jibu maswali (2).
- Zingatia mpango mzuri wa kazi na mwandiko unaosomeka.
- Fuata maelekezo na maagizo kwa kila swali.
SEHEMU A: UFAHAMU NA UFUPISHO
Soma habari ifuatayo kisha jibu maswali yote.
(Nyumbani kwa mama Suzi: Wakati Mama Suzi anafua nguo anasikia mbisho wa hodi).
(kutoka nje) Hodi, hodi wenye nyumba!
MAMA SUZI : Nyumba yako hii shoga (Anainuka kuonana na mgeni. Anaingia mama Joti)
MAMA JOTI: Vipi una safari?
MAMA SUZI: Safari?
MAMA JOTI: Ee naona unafua
MAMA SUZI: (Huku anampa kiti) Shoga naye. Mtu hafai mpaka awe na safari? Umaridadi tu (wanacheka).
MAMA JOTI: Haya mwenzangu za tangu jana?
MAMA SUZI: Mh unadhani mimi nina cha kusema? Nina mfikiria Suzi wangu. Msiba wa Fausta umenitia woga.
MAMA JOTI: Siyo wewe tu. Hebu niambie toto la mtu lile, lilivyokuwa limeenea vile. Si mashavu hayo, si macho, si ------ mh! mh! Mungu amuweke pema mtoto Fausta!
MAMA SUZI: Mtoto kesha vile mpaka anageuka kizuka! Nilitaka kukimbia ati, pale nilipotupa macho kwenye jeneza. Mtu si mtu, kizuka si kizuka!
MAMA JOTI: Cha kushangaza ni pale tunapoambiwa eti kafa kwa kukanyaga nyaya.
MAMA SUZI: Kukanyaga nyaya? Mbona wengine wanasema kafa kwa ukimwi?
MAMA JOTI: Wewe nawe unakuwa nyuma nyuma kama koti? Mtu aliyekufa kwa kukanyaga nyaya maana yake kafa kwa ukimwi.
MAMA SUZI: Kiswahili cha siku hizi ni kigumu! (Anastuka) shoga unanisahaulisha kazi yangu. Anaendelea kufua) Lakini shoga watu wanatafuta maana ya marehemu. Kitoto kama kile; kife kwa ukimwi! Ungeingilia kona gani?
MAMA JOTI: Wewe unamwona Fausta alikuwa mdogo? Ukubwa siku hizi siyo kuvunja ungo au ulikuwa unadanganywa na utakatifu wa usoni? Shoga, mtakatifu wa kwenye mwanga si lazima awe mtakatifu gizani.
MAMA SUZI: Aa bwna mie siamini. Labda ungesema yalimkuta hayo kwa kuchangia wembe, kuchoma sindano isiyochemshwa au kuongezewa damu yenye virusi vya UKIMWI. Lakini jinsi ninavyoijua familia ile, Fausta asingeweza ama kufanya au kufanyiwa mambo haya. Kwanza Fausta alikuwa na afya njena sana katika uhai wake.
MAMA JOTI: Chanzo cha kifo cha Fausta ni zinaa. (Kwa ukali kidogo). Shoga mbona unakuwa mgumu kama mpingo?
MAMA SUZI: Fausta alikuwa mtoto sana mtoto wa darasa la tano mambo hayo asingeyajua.
MAMA JOTI: Mwenzangu kwa nini tubishane? Haya…..
Taji vaa wewe umeshinda. (Anaingia Suzi akiwa amevalia sare ya shule)
SUZI: Shikamoo mama
MAMA SUZI: Marahaba Suzi. Pole na shule
SUZI: Ahsante mama (Anaingia ndani)
MAMA SUZI: Kile kitoto vile kilivyokuwa si kama hicho changu?
MASWALI
(a) Andika kichwa cha habari uliyoisoma
(b) Kwa mujibu wa mwandishi ukimwi unaambukizwaje?
© Kulingana na habari hii eleza mtazamo potofu uliojikita katika Jamii kuhusu maambukizi ya ukimwi.
(d) Mwandishi anazungumza nini kuhusu unyanyapaa?
(e) Unajifunza nini kupitia habari?
2. Fupisha habari hii maneno yasiyozidi 30.
SEHEMU B: MATUMIZI YA SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA
Jibu maswali mawili
3. Eleza maana ya dhana zifuatazo
(a) Fonolojia
(b) Mofolojia
© Sintaksia
(d) Semantiksia
(e) Fonimu
4. Jadili mambo mbalimbali yanayodhoofisha lahaja.
5. Eleza kwa ufasaha hatua anazopitia mwanadamu kujifunza lugha ya kwanza.
6. Taja dhima za mofimu za maneno yafuatayo
(a) Tumesomea
(b) Hakiliki
SEHEMU C: UTUNGAJI
7. Andika Insha isiyozidi maneno 250 kuhusu ukimwi.
SEHEMU D: MAENDELEO YA KISWAHILI
8. Kwa kutumia ushahidi wa kiisimu thibitisha kuwa Kiswahili ni kibantu.
9. Fafanua hatua zilizochukuliwa na wakoloni wa kijerumani katika kukuza na kueneza Kiswahili nchini Tanzania.
SEHEMU E: FASIHI
10. (a) Nini tofauti ya Fasihi na sanaa
(b) Usanaa wa fasihi unatokana na nini?