UCHOTARA WA LUGHA YA KISWAHILI UNA MSINGI KATIKA CHIMBUKO NA ASILI
UCHOTARA WA LUGHA YA KISWAHILI UNA MSINGI KATIKA CHIMBUKO NA ASILI YAKE
Kwa Mukhtasari
WATAALAMU wa lugha wameandika kuhusu Kiswahili kama lugha ya taifa na lugha rasmi inayokadiriwa kutumiwa na watu wapatao zaidi ya milioni 60 duniani kote.
Tambua kuwa Kiswahili ni lugha kamili na wala si lugha chotara kwa maana ya mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na lugha ya Kibantu kama watu wengi wanavyodhani.
Hutumika katika nchi za Afrika Mashariki na Kati kama Tanzania, Kenya, Uganda na katika eneo la mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Vilevile katika nchi za Burundi, Rwanda, Msumbiji, Zambia, Comoro na Malawi. Kiswahili kinazungumzwa pia katika nchi za Uarabuni kama Dubai, Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Yemen na Dubai.
Kwa kipindi cha miaka zaidi ya miaka elfu moja, kumekuwa na mawasiliano kwa viwango tofauti katika nchi za Mashariki ya Kati, Uajemi, India, China, Ureno na Uingereza.
Nchi hizi zimechangia kwa kiwango kikubwa kwa kukopesha maneno mengi ya lugha zao katika lugha ya Kiswahili. Katika sehemu mbalimbali duniani, viko vyuo vinavyofundisha lugha hii. Pia viko vituo vingi vya utangazaji vya redio na runinga vinavyotumia Kiswahili.
Ukichunguza muundo wa maneno na miundo wa sentensi za Kiswahili utagundua kuwa Kiswahili kinafanana sana na lugha za Kibantu kuliko Kiarabu, Kiajemi na Kihindi.
Inasemekana kuwa idadi ya maneno ya mikopo kutoka lugha za kigeni katika lugha ya Kiswahili inaweza kulinganishwa na mikopo ya maneno katika lugha kongwe kama Kilatini,Kigiriki na Kifaransa ambazo zimechangia sana katika kuikuza lugha ya Kiingereza. Ni dhahiri kuwa ukopaji wa maneno katika lugha yoyote ile ni dalili ya kukua kwa lugha husika.
Nchini Tanzania na Kenya, Kiswahili ni lugha rasmi za mataifa haya.
Nchini Tanzania na Kenya, Kiswahili ni lugha rasmi za mataifa haya.
Kwa upande wa Kenya, Kiswahili ni somo la lazima linalofundishwa katika shule za msingi na sekondari. Pia kinatumika kufundishia nyingi za taaluma katika vyuo vikuu.
Nchini Tanzania, Kiswahili ni somo la lazima pia katika shule za sekondari hadi kidato cha nne na pia ni lugha ya kufundishia katika shule za msingi.
ASILI YA KISWAHILI
Yako maneno mawili ambayo tunayochanganya katika matumizi nayo ni, asili ya Kiswahili na chimbuko lake. Neno 'asili’ lina maana ya jinsi jambo lilivyoanza au lilivyotokea. Ama kwa neno 'chimbuko’, maana yake ni mahali kitu au jambo lilipoanza. Kwa hiyo asili na chimbuko yanatofautiana katika maana.
Zimewahi kutokea nadharia kadhaa kuhusu asili ya Kiswahili ambazo nitazieleza hapa. Kwanza ipo nadharia kuwa Kiswahili kimetokana na Kiarabu. Pili iko nadharia kuwa Kiswahili ni mchanganyiko wa Kiarabu na lugha za Kibantu zilizotumika katika upwa wa Afrika Mashariki.
Tatu, ni kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu iliyoathiriwa sana na Kiarabu hasa kimsamiati. Nne, Kiswahili kilitokana na mchanganyiko wa lugha kadhaa za Kibantu zilizokuwa katika upwa wa Afrika Mashariki.
Nadharia isemayo kuwa Kiswahili kilitokana na Kiarabu inaegemea sana wingi wa maneno yenye asili ya Kiarabu na pia dini ya Kiislamu.
Inadaiwa kwamba kwa kuwa Kiswahili kilianza pwani na kwa kuwa idadi kubwa ya wananchi wa pwani ni Waislamu na kwa kuwa Uislamu uliletwa na Waarabu, basi Kiswahili nacho kinashabihiana na Kiarabu.
Madai haya hayana mashiko kwani Kiswahili ni lugha kamili iliyokopa maneno kutoka katika lugha za Kiarabu, Kiajemi, Kireno, Kihindi, Kijerumani na Kiingereza kutokana na mawasiliano ya karne nyingi kati ya wenyeji wa pwani na wafanyabiashara wa kigeni
Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa Kiswahili hasa wanaisimu wamegundua kuwa mabadiliko yalihusu msamiati tu na wala si maumbo ya maneno wala miundo ya tungo za Kiswahili.
Ikumbukwe pia kwamba uchunguzi ulikwishafanywa kwa kipindi kirefu na kubaini kwamba Kiswahili kilitumia maneno mengi kutoka katika lugha za Kibantu kwa kuwa wasemaji wengi wa Kiswahili ni Wabantu.
Jambo la msingi ni kuwa, kwa lugha kuwa na maneno mengi ya kukopa kutoka katika lugha nyingine haifanyi lugha hiyo ionekane imetokana na hiyo lugha ngeni.
Inabidi kuzingatia zaidi msingi wa lugha kwa upande wa fonolojia, mofolojia, semantiki na sintaksia ya lugha husika. Kimsingi, vigezo pekee vinavyoweza kutumika ili kuibainisha lugha ni vya kisimu kama vile fonolojia, mofolojia na sintaksia lakini msamiati si msingi wa pekee wa kuzingatia.
Nadharia ambazo zinazaweza kuwa ni msingi wa uhakika ni mbili. Moja ni ile isemayo kuwa Kiswahili kina asili ya Kibantu. Msingi wa pili ni kuwa Kiswahili ni lugha iliyotokana na lugha kadhaa za Kibantu katika eneo la Pwani ya Afrika Mashariki.
Kiisimu, Kiswahili ina utaratibu maalumu ambao ni herufi kama konsonanti na irabu ambapo huweza kuunda silabi kama 'ba’, 'ma’, 'ka’, 'la’; au konsonanti, konsonanti na irabu kama katika, 'gha’, 'mwa’, n.k.; au konsonanti, konsonanti, konsonati na irabu kama, 'mbwa’, 'ngwe’ n.k.
CHIMBUKO LA KISWAHILI
Ni vigumu kusema kwa uhakika mahali ambapo ni chimbuko la Kiswahili. Pengine tunaweza kusema kuwa Kiswahili kilianzia sehemu maalumu na kuenea hadi mahali fulani.
CHIMBUKO LA KISWAHILI
Ni vigumu kusema kwa uhakika mahali ambapo ni chimbuko la Kiswahili. Pengine tunaweza kusema kuwa Kiswahili kilianzia sehemu maalumu na kuenea hadi mahali fulani.
Inadaiwa kuwa chimbuko la Kiswahili liko katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya lakini madai haya hayajawahi kuthibitishwa kwa hoja zenye mashiko.
Ni wazi kuwa wanahistoria waliowahi kuandika kuwa mawasiliano na maelewano kati ya watu wa eneo fulani kwa kiasi fulani kulizuka lugha moja iliyoeleweka kwa watu wote katika eneo hilo. Mawasiliano ya aina hii yalizua lugha ambazo zilitofautiana kuanzia Kaskazini hadi Kusini mwa Pwani ya Afrika Mashariki ambazo zilijulikana kama lahaja za Kiswahili.
Kuanzia Kaskazini, kuna lahaja ya Chi-Miini ambayo huzungumzwa katika eneo la Barawa, Pwani ya Somalia. Kusini zaidi kulikuwa na lahaja za Kitukuu na Kibajuni katika eneo la Kusini mwa Somalia na Kaskazini mwa Kenya.
Kuanzia Kaskazini, kuna lahaja ya Chi-Miini ambayo huzungumzwa katika eneo la Barawa, Pwani ya Somalia. Kusini zaidi kulikuwa na lahaja za Kitukuu na Kibajuni katika eneo la Kusini mwa Somalia na Kaskazini mwa Kenya.
Nyingine ni Kisiu katika sehemu za Pate na pia kukawa na Kiamu huko Lamu, Kimvita kinasemwa katika sehemu za Mombasa, Kivumba na Kimtang’ata katika sehemu za Pwani ya Kaskazini mwa Tanzania, Kimakunduchi, Kihadimu, Kitumbatu katika sehemu za Unguja na Kipemba kinazungumzwa sana eneo la Pemba. Lahaja hizi zinafanana na lugha nyinginezo za Kibantu.
Lahaja hizi zinatofautiana kidogo na Kiswahili sanifu kwa sababu Kiswahili sanifu kina maneno mengi ya mkopo. Lahaja zote hizo ni lugha zinazojitegemea.