Mwanakupona (Nana): Utenzi wa Mwanakupona

SURA YA KUMI NA MBILI
Kwa sababu utenzi huu wa Mwanakupona hubainisha vile ambavyo fasihi huwa katika jamii ya kimwinyi, yatubidi tuanze na maelezo ya jumla kuhusu fasihi ilivyo katika mfumo huo wa jamii. Maelezo hayo yatatusaidia katika kuupa utenzi huu uzito wa kiuchambuzi.
Fasihi Katika Mfumo wa Kimwinyi
Mfumo wa kimwinyi unabainishwa na mahusiano ya jamii ambayo ni ya kiutwana na ubwana, ambayo yamefikia hatua mpya ya juu zaidi, na tabaka tawala (la mamwinyi) hutawala njia zote za kiuchumi na za kitamaduni. Katika makala yake ya "Ushairi wa Kiswahili ni Nini(Lugha Yetu, 26 - uk. 12), M.M. Mulokozi amelielezea tabaka hali kama ifuatavyo:
Uozo na ubaradhuli wa maisha ya kiumwinyi, hasa wakati mfumo huu unapoanza kutetereka kutokana na nguvu za jamii na za uchumi, huwafanya mamwinyi, katika maisha yao ya kizembe na kifasiki, wapendelee sana mambo ya kuvutia macho na kuliwaza pua, kama vile mapambo aina aina, wanawake wazuri, nakshi, na marembo ya rangi za kuvutia katika makazi na malazi yao... marashi, manukato, udi na ubani na kadhalika.
Maisha ya namna hii aliyoyaeleza Mulokozi vilevile hujitokeza katika fasihi itokanayo na mfumo huu (na inayopata udhamini kutoka kwa tabaka tawala). Si katika Utenzi wa Mwanakupona tu, bali pia katika kazi zingine kama vile utenzi wa Al Inkishafi ulioandikwa na S.A.A. Nasir (Oxford, 1972). Katika Al Inkishafi, utaona maelezo yatolewayo kuhusu uzuri wa majengo na makazi ya masultani wa Pate, na pia ule wa wanawake ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuwaimbia wakubwa hao, kuipepea usiku kucha, pamoja na kuwatumikia. Beti za 43 hadi 57 za Al Inkishafi ni vielelezo vizuri vya mapambano yaabatanayo na ufasiki wa kimwinyi.
Kabla ya kuchunguza ni kwa vipi mambo yote hayo na mengineyo ya kimwinyi yamejitokeza katika Utenzi wa Mwanakupona yafaa kwanza tujikumbushe historia ya utenzi huu.
Historia fupi ya Utenzi wa Mwanakupona
Kama tuelezwavyo katika Utangulizi ulioandikwa na Ahamad Sheikh Mohamed Nabhany Mtamwini, Utenzi wa Mwanakupona ni utenzi maarufu sana ambao mwanzoni ulitungwa na mwanamke mmoja aliyeitwa Nana. Baada ya kutungwa hivyo ulisambazwa kwa njia ya masimulizi, huku ukizidishwa ama kupunguzwa jumla ya beti kufuatana na kumbukumbu za moyoni za wapokezi na wasambazaji.
Mtaalamu mmoja wa fasihi na lugha J.W.T. Allen alizifanyia utafiti nakala mbalimbali za utenzi huu akachagua nakala moja ambayo aliiona kuwa inaingiza mambo mbalimbali yajitokezayo katika nakala zote.
Nana ni jina la utani tu la Mwanakupona aliyeishi katika nusu ya kwanza ya karne ya kumi na tisa. Mume wa Mwanakupona alikuwa mtu maarufu katika historia ya Waswahili. Aliitwa Bwana Mataka, Shehe wa Siu. Huyu yasemekana kuwa alipigana vita vya msituni kwa muda wa miaka ishirini akipinga utawala wa Sultani wa Zanzibar, Seyyid Said.
Mwanakupona alikuwa na watoto wawili, wote wa Bwana Mataka. Wa kwanza alikuwa mwanamumc aliyeitwa Muhammad bin Sheikh, na wa pili alikuwa binti aliyeitwa Mwana Hashima binti Sheikh. Huyu wa pili ndiye ambaye anahusika katika wasia utolewao kwenye Utenzi wa Mwanakupona, utenzi ambao ulitungwa na Mwanakupona alipokuwa anakaribia kufariki.
DHAMIRA KUU
Tutaanza kwa kuchambua vile ambavyo wasia utolewao juu ya wanawake na jukumu lao la kifamilia na kijamii lilivyoshikamana na misingi ya kimwinyi ambayo tuliitaja hapo awali.
Tulisema kuwa amali za kimwinyi husisitiza sana juu ya mapambano na uzuri wa juu juu. Katika Utenzi wa Mwanakupona msisitizo huo unajitokeza waziwazi. Tunauona katika "uzuri" ambao Mwanakupona anataka binti yake awe nao. Uozo wa mfumo wa kimwinyi husisitiza kuhusu mambo yanayovutia macho, na athari ya mkabala huu twaiona hata katika wasia utolewao. Tuangalie beti zifuatazo kama mifano ya dai hilo.
38. Na kowa na kiuisinga
na nyee zako kufunga
na asmini' kutunga
na firashini kutia
39. Nawe ipambe libasi
ukae kama arusi
maguu tia kugesi
na mikononi makoa
40. Na kidani na kifungo
sitoe katika shingo
mwili siwate mwingo
kwa marashi na dalia
41. Pete sikose zandani
hina sikome nyaani
wanda sitoe matoni
na nshini kuitia.
Katika kiwango hiki mwanamke anaonekana kuwa pambo tu, sawa na mapambo mengine mazuri mazuri. Kwa sababu ya athari hii basi, nafasi ya mwanamke katika jamii ya kimwinyi huwa ya chini na duni mno. Naye mwanamke hufanywa na mazingira haya aikubali nafasi hiyo duni. Ndiyo sababu twaambiwa kuwa watu wengi, hasa wanawake, walivutiwa mno na utenzi huu nao wakaamua kuuhifadhi "kwa moyo na wakawahifadhisha watoto wao wa kike" (Kitangulizi). Twaelezwa pia kuwa wengi wao hadi leo wanaujua utenzi huu kwa moyo.
Iko mifano mingi ya beti zinazodhihirisha nafasi duni aliyopcwa mwanamke katika janui na vile ambavyo mwenyewe kaikubali (zima kalazimika kuikubali). Tuangalie beti zifuatazo:
28. Keti naye kwa adabu
usimtie ghadhabu
akinena simjibu
jitahidi kunyamaa
31. Kilala siilcukuse
mwegemee umpapase
na upepo usikose
mtu wa kumpepea
34. Mnyoe mpalilize
sharafa umtengeze
na udi umfukize
bukurata wa ashia
35. Mtunde kama kijana
asiyojua kunena
kitu changalie sana
kifokacho na kuingic.
Zaidi ya kuwa uhusiano baina ya mume na mke ni sawa na ule wa bwana na mtwana, mume hapa yu bwege kabisa, na ubwege huu wa kimwinyi umesisitizwa kwa mume kulinganishwa na mtoto mdogo (kijana asiyejua kunena). Zaidi ya kuwa mke kaambiwa aketi na mumewe kwa adabu na hata akionewa asijibu, ubeti wa 36 nao unasisitiza nafasi hiyo duni ya mwanamke:
36. Mpumbaze apumbae
amriye sikatae
maovu kietayeye
Mngu atakulipia.
Mistari miwili ya mwisho ya ubeti huu wa 36 inatuleta katika suala lingine lihusulo amali na maisha ya kimwinyi. Zaidi ya kuamua kuwa mwanamke amtumikie mwanamume, anaaswa asimbishie wala asimjibu ila amtii na amwogope, na unyonge huu unahalalishwa kwa vitisho vya dirii. Vitisho vya dini hufikia kilele katika mfumo wa kimwinyi, nayo dini hutumiwa kuwa taasisi kubwa ya kudumisha na kuhalalisha mgawanyiko wa jamii katika matabaka ya watu wa juu (mamwinyi) na ya wa chini (watwana); hutumiwa kuhalalisha unyonge si wa wanawake tu bali wa watu wote wa matabaka ya chini. Ubeti huo wa 36 unaonyesha vile ambavyo dini hapa inatumiwa kumgandamiza zaidi mwanamke ambaye anaaswa kuwa maovu yoyote yale atakayotendewa na mumewe asiyashughulikie kwani Mungu atamlipia. Beti za 24-27, zinasisitiza msimamo na mtazamo huu:
24. Naawe radhi mumeo
siku zote mkaao
siku mukhitariwao
awe radhi mekuwea
25. Na ufapo wewe mbee
radhi yake izengee
wende uitukuzie
ndipo upatapo ndia
26. Siku ufufuliwao
nadhari niya mumeo
taulizwa atakao
ndilo takalotendewa
27. Kipenda wende peponi
utakwenda dalhini
kinena wende motoni
huna budi utatiwa.
Misingi ya dini katika mfumo huo iliwekwa katika hali ambayo humdunisha mwanamke. Mwanamume kapewa hata madaraka ya kuamua siku ya ufufuo kuwa mkewe aende ahera ama motoni. Mwanamke basi, anapaswa afuate yote anayoamriwa na mumewe kwani yote hayo ni amri ya Mungu. Hapa tunazigundua dhahiri athari za kitabaka zilizojikita mizizi yake katika taasisi ya dini - athari ambazo zinanuia kumgandamiza mtu wa chini zaidi na zaidi.
Kutokana na mkabalatuuonao katika wasia utolewao katika Utenzi wa Mwanakupona kwa wanawake, tunaweza kusema kuwa utenzi huu umetudhihirishia vile ambavyo zaidi ya mwanamke kufanywa aonekane kuwa ni pambo, hapohapo maisha ya kimwinyi yanamfanya kuwa chombo cha kutimizia haja za mwanamume, na pia kuwa mtwana wa mwanamume.
Dhamira Zinginezo
Mambo yote hayo ambayo tumeyahusisha na mfumo wa kimwinyi yanatokana na wakati ambapo utenzi huu uliturigwa pamoja na mazingira ya kitamaduni, kiuchumi na kisiasa yaliyoongozwa na maadili ya kimwinyi. Ndio sababu hata kudunishwa kwa watu wa chini hakuishilii kwa wanawake tu bali kwa watu wote wa tabaka la kitwana. Kwa mfano katika beti za 15-19 mwanamke anaaswa awaheshimu "maqabaili":
15. Tena mwanangu idhili
mbee za maqabaili
uwaonapo mahali
angusa kuwainukiya
16. Wangiapo wenukiye
na moyo ufurahiye
kisa uwapeke mbeye
watakapokwenda ndiya
17. Ifanye mteshi teshi
kwa maneno yaso ghashi
wala sifanye ubishi
watu wakayatukiya.
Lakini, zaidi ya kuambiwa awaheshimu na kuwaabudu hao mamwinyi, anaaswa asifanye hivyo kwa watu wa chini, tena hata asiwakaribie, Haya tunayaona katika ubeti wa 20, kwa mfano:
20. Silangane na watumwa
ile mwida wa huduma
watakuvutia tama
labuda nimekwambiys.
Katika utenzi huu yanajitokeza pia maadili mengine. Mwanamke anaaswa kuwa maisha hayana maana, na kuwa mtu si kitu mbele ya muumba wake:
6. Mwanadamu si kitu
na ulimwengu si wetu
walau hakuna mtu
anibao atasaliya.
Kwa hiyo basi anaambiwa kuwa jambo la kwanza ashike dini:
12. La kwanda kamata dini
faradhi usiikhini
na suna ikimkini
ni wajibu kuitiya.
Pia utenzi huu unafunza kuhusu umuhimu wa usafi nyumbani kama tusomavyo katika ubeti wa 37 na wa 42 kwa mfano:
37. Mwanangu siwe mko'o
tenda kama uona'o
kupea na kuosha choo
sidharau mara moya.
42. Nyumba yako inadhifu
mumeo umsharifu
wakutanapo sufufu
msifu ukimweteya.
Baadhi ya wahakiki wa utenzi huu wamesema kuwa beti tulizokwishazitaja zinazomuasa mwanamke ajirembe na kujipamba zinasisitiza kuhusu umuhimu wa usafi wa mwili zaidi ya kujipamba tu. Ili kuweza kutoa tafsiri ya beti hizo labda itambidi msomaji binafsi aamue mwenyewe. Ila ni wazi kwamba usafi uliotajwa pamoja na urembo na kujipamba kunakosisitizwa katika beti hizo - vyote hivi vimeeiekezwa katika kumpendezana kumfurahisha mwanamume kuliko kuwa na manufaa kwa mwanamke mwenyewe.
Sasa tuuchambue utenzi huu kwa kuulinganisha na kuulinganua na baadhi ya kazi za fasihi ya Kiswahili ambazo zimeshughulikia pia masuala sawa na haya ya utenzi huu. Tumetaja utenzi wa Al Inkishafi kama mfano wa kazi ambazo japokuwa haziambatani na wasia kwa wanawake tu bali kwa watu wote, hapohapo unaonyesha athari za baadhi ya amali za maisha ya jamii nzima. Suala la msisitizo kuhusu mapambano na pia nafasi ya dini katika jamii ndilo hasa tulilolihusisha na yaelezwayo katika Utenzi wa Mwanakupona.
Kazi ambayo inafanana sana na Utenzi wa Mwanakupona ni ile ya Shaaban Robert ya Utenzi wa Hati ipatikanayo katika kitabu chake cha Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini (Thomas Nelson, 1966). Katika Utenzi wa Hati ni mzazi pia ndiye katunga ili kumuasa binti yake kuhusu maisha na wajibu wake katika jamii. Tofauti hapa ni kwamba, mawazo kuhusu mwanamke katika Utenzi wa Hati ni ya kimaendeleo zaidi na yamepevuka zaidi kuliko yale ya Utenzi wa Mwanakupona.
Japokuwa kupo kushabihiana katika baadhi ya mawazo ya tenzi zote mbili kwa mfano katika wasia kuhusu umuhimu wa kushika dini - lakini sehemu nyingi za tenzi hizi zinatofautiana sana na hata kupingana. Kwa mfano, tulionajinsi beti za 15, 16, 17 na 20 zinazomuasa binti wa Mwanakupona asiwapende na kuwaheshimu watu wa tabaka la chini. Shaaban Robert anamuasa bintiye tofauti kabisa na mawazo hayo. Kwa mfano katika beti za 65 na 66 za Utenzi wa Hati Shaaban Robert anaasa:
65. Kupenda watukufu,
Kwa kumiliki sarafu,
Na fukara kukashifu,
Hatiyasema vibaya.
66. Penda wenye cheo,
Na wanyonge uwe nao,
Hayo ndiyo mapokeo,
Mema mtu kutumia.
Tenzi zote mbili zinamuasa mwanamke kuhusu umuhimu wa kuchunguza na kuyaelewa mambo (angalia ubeti wa 19 wa Utenzi wa Mwanakupona), na pia kuhusu umuhimu wa urafiki mwema na tabia nzuri. Lakini katika Mwanakupona sifa hizo zimeelekezwa zaidi katika nafasi duni ya chini aliyo nayo mwanamke katika jamii. Katika Utenzi wa Hati sifa hizo zimejikita katika ukombozi wa mwanamke ambaye ametakiwa atoke jikoni na kitandani, ashiriki katika mambo ya kujielimisha-hata anaambiwa kuwa ni jukumu lake kujifunza namna ya kujitegemea. Angalia ubeti wa 76 kwa mfano:
76. Tena kujitegemea
Ni ngao ya ukiwa
Siku ya kubakia
Peke yako hufaa.
Kinyume na mwanamke huyu wa Utenzi wa Hati, yule wa Utenzi wa Mwanakupona hapewi wasia wa kujikomboa bali anaaswa kuwa aendelee kuikumbatia nafasi yake duni na ya chini kabisa katika jamii-nafasi ya kutumiwa kama chombo na pambo, na pia kutumwa kama mtwana.
Tenzi mbili hizi tulizozichunguza zinatudhihirishia ukweli kwamba mwandishi na mturigaji wa kazi ya fasihi, sawa na fasihi yenyewe, ni zao la mazingira maalum kwa wakati maalumu. Tofauti za mifumo ya jamii na mwamko wa kisiasa kwa jumla katika jamii, aghalabu huleta tofauti pia baina ya waandishi wa mifumo itofautianayo. Mwanakupona alizaliwa na kulelewa na jamii ya mfumo wa kimwinyi, na jamii hii ndiyo iliyozaa na kulea mtazamo wa kilimwengu wa kimwinyi tuuonao katika wasia autoao. Shaaban Robert alizaliwa na kukulia katika mfumo wa kibepari chini ya ukoloni, mfumo ambao umepevuka zaidi ya ule wa kimwinyi. Katika mfumo huu wafanyakazi hudai haki zao kwa njia dhahiri, na hata wanawake hudai haki zao kwa kuunda vyama vyao - na nafasi yao katika jamii si jikoni na kitandani tu bali twawaona katika harakati za kupigania uhuru katika nyanja za elimu, sayansi na kadhalika; sambamba au hata juu zaidi ya wanaume. Haya yote aliyaona, aliyasoma na aliyasikia Shaaban Robert, na si ajabu kuona kuwa mkabala wake kuhusu nafasi ya mwanamke katika jamii ni wa kimaendeleo zaidi ya ule wa Mwanakupona.
MATUMIZI YA VIPENGELE VYA FANI
Yako machache sana tuwezayo kusema kuhusu fani katika utenzi huu. Labda hili linatokana na ukweli kuwa wasia utolewao umetolewa kwa njia ya moja kwa moja bila matumizi mengi ya picha ama tamathali za semi.
Kwa jumla utenzi huu umefuata muundo wa kimapokeo wa tenzi za Kiswahili. Sawa na ule wa Shaaban Robert wa Utenzi wa Hati,utenzi huu unaanza kwa kumwita mhusika mkuu, binti yake, halafu unaeleza kwa njia ya dibaji kuhusu madhumuni ya mwandishi au mturigaji, halafu maudhui kuhusu dini na Mungu yanajitpkeza, na baada ya hapo maudhui yenyewe yanatolewa kwa kirefu kabla ya utenzi kufungwa kwa mambo ya sala, Mungu na dini. Huu ni muundo uliozoweleka katika tenzi za kimapokeo zaKiswahili.
Utenzi huu una "urahisi" wa kifani anibao hata hivyo haimaanishi kuwa unapwaya. Katika "urahisi" huo kuna faida ya kueleweka kwa maudhui ya utenzi huu bila shida kubwa kwa msomaji, japokuwa kwa baadhi ya wasomaji msamiati mwingi wa lahaja itumiwayo humu ni mgeni na mgumu kwao.
Maswali
1. Eleza historia fupi ya Utenzi wa Mwanakupona. Je kuna umuhimu gani wa kuielewa historia hiyo?
2. Eleza uhusiano uliopo baina ya fasihi na jamii ya kimwinyi. Ni kwa vipi uhusiano huo umetokeza katika Utenzi wa Mwanakupona?
3. Yachambue kwa undani maudhui ya Utenv wa Mwanakupona. Upe uchambuzi wako uzitpo kwa kuyalinganisha maudhui hayo na ya kazi nyirigine au zingine za fasihi ya Kiswahili ambayo au ambazo zime-yashughulikia pia masuala yajitokezayo katika utenzi huu.
4. "Katika wasia utolewao na Mwanakupona tunagundua jela na silasila za maisha ya mwanamke zaidi ya uhuru na utu wake." Ijadili kauli hii kwa kuitolea mifano dhahiri kutoka katika Utenzi wa Mwanakupona. Katika jibu lako ihusishe kauli hiyo pia na baadhi ya mashairi yaliyomo katika kitabu cha Shaaban Robert cha Ashiki KitabuHiki.
5. Je tunaweza kusema nini kuhusu fani katika Utenzi wa Mwanakupona?
Powered by Blogger.