MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA NA LUGHA YA TAIFA (KISWAHILI)

MAKOSA MBALIMBALI YANAYOJITOKEZA KATIKA LUGHA
Kutokana na taadhira hizi kuna aina mbalibali za makosa yanayojitokeza kwa watumiaji wa lugha. Makosa hayo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni makosa ya Kisarufi na makosa ya kimantiki. Katika kipengele hiki tutaangalia makosa hayo na namna ya kurekebisha.

MAKOSA YA KISARUFI
Kila lugha ina kanuni na taratibu ambazo hutawala katika matumizi ya lugha ili watu waweze kuelewana kanuni hizo zipo vunjwa au kukiukwa huweza kusababisha makosa kujitokeza na upotovu katika lugha. Makosa ya kisarufi yanaweza kugawanyika katika sehemu zifuatazo:- makosa ya kimsamiati, makosa ya kimuundo, makosa ya matamshi, kuongeza vitamkwa au viambishi, kuacha maneno, makosa ya tafsiri sisi.

MAKOSA YA KIMSAMIATI
Watumiaji wa lugha huchanganya masamiati wakati wa kuzungumza au kuandika. Watu hutumia msamiati usiolingana na msamiati usiolinga na maana iliyokusudia
Mfano:- Nona na nenepa
Wengi husema siku hizi umenona sana.
Badala ya kusema, Siku hizi umenenepa sana.
mazingira na mazingara
Watu husema Mazingara yameharibiwa sana siku hizi.
badala ya kusema Mazingira yameharibiwa sana siku hizi.
Ajali na ajili
Watu husema Amefariki wa ajili ya gari.
badala ya kusema Amefariki kwa ajali ya gari.
Wakilisha na wasilisha
Watu husema, Waziri wa fedha atawakilisha bajeti ya mwaka kesho.
Badala ya kusema Waziri wa fedha atawasilisha bajeti ya mwaka kesho.

MAKOSA YA KIMUUNDO
Kwa kawaida sentensi za kiswahili huanza na nomino ya mtenda au mtendwa.
Mfano:- mtoto mpole anacheza
Mzungumzaji asiye fuata kanuni husema Mpole mtoto anacheza.
Kalamu yangu imeibwa.
badala ya kusema kalamu yangu imeibiwa.

MAKOSA YA KIMATAMSHI
Watu wengi hushindwa kutamka baadhi ya sauti za kiswahili wakati mwingine huchanganya na kubadili sauti hizo Mfano Wakurya hutumia ’r’ badala ya ’l’
Nenda karare
badala ya kusema nenda kalale
Wandali hutumia ’s’ badala ya ’z’ na ’dh’ na ’th’
mfano selasini
badala ya thelathini
Sahabu
badala ya dhahabu
Samani
Badala ya zamani
Makosa haya mara nyingi yanatokana na athari ya lugha mama. Kwa kuwa lugha ya kiswahili ni lugha ya pili kwa wazungumzaji wengi. Hivyo lugha ya kwanza huwa na athari kubwa kwa mzungumzaji wa wa lugha ya pili.

KOSA LA KUONGEZA VITAMKWA
Baadhi ya wazungumzaji huongeza vitamkwa mahari pasipo hitajika na hivyo kuharibu lugha.
Mfano. Nendaga
badala ya nenda
Mashule
badala ya shule
Huwaga anapenda fujo
badala ya huwa anapenda fujo

KOSA LA KUACHA MANENO
Watumia lugha huweza kuacha maneno katika sentensi na bado wakafikiri wanatoa ujumbe uleule uliokusudiwa.
mfano, Watu husema Juma ameondoka kazini akiwa na maana kuwa Juma ameondoka kwenda kazini lakini sahihi ni kuwa Ametoka kazini.
Alfredi amerudi kazini akiwa na maana kuwa Afredi ametoka kazini.
Kwa mzungumzaji anatoa maana ambayo ni kinyume kabisa na ile maana aliyo kusudia kusema. Ambapo anakusudia kuuliza kama Alfredi amekwenda tena kazini.

MAKOSA YA TAFSIRI SISISI
Tafsiri sisisi ni tafsiri ya neno kwa neno. Tafsiri hii inapofanywa huleta matatizo ya kisarufi katika lugha
mfano. Kimbizwa hospitali She runed to hospital
badala ya kusema amepelekwa hospitali
At the end of the day
Mwisho wa siku.
Badala ya kusema hatimaye.

MAKOSA YA KIMANTIKI
Mantiki ni utaratibu mzuri wa kufikiri. Makosa ya kimantiki ni yale yanayoonesha kukosekana kwa utaratibu wa fikra. Nimakosa yanatokana na upotovu wa mawazo ya mzungumzaji
Mfano watu wengi husikika wakiema hivi: Usimwage kuku kwenye mchele mwingi
Badala ya usimwage mchele kwenye kuku wengi
Nyumba imeingia nyoka  Badala ya kusema Nyoka ameingia ndani ya nyumba
Chai imeingia nzi Badala ya kusema Nzi ameingia kwenye chai.

MSWAHILI
Kutokana na mtazamo hiyo na dhana na maendeleo ya lugha ya kiswahili, inaonekana wazi kuwa ni vigumu kumpata mswahili ambaye ni mmiliki wa lugha hii ya kiswahili. Inaonesha dhahili kuwa mswahili anaweza kutazamwa kwa namna tofauti kama zifuatazo;-
i).  Mswahili anaweza kuwa ni mtu mahuruti yaani ni mtu chotara ambaye ni lazima awe ametokana mwingiliano wa pande mbili ambao ni wabantu na watu wanaonasibishwa na Waarabu
ii). Mswahili anaweza kuwa ni mtu wa mjini aliyeacha dini, utamaduni, mila na desturi zake za asili na kukimbilia dini, utamaduni, mila na desturi kutoka mataifa mengine kutoka uarabuni na nchi za kimagharibi
iii). Mswahili anaweza kuwa ni mtu ambaye anazungumza vizuri lugha ya kiswahili kwa kufuata taratibu zote za kiisimu na utamaduni wa lugha ya kiswahili
iv). Mswahili anaweza kuwa ni mkazi wa ya Afrika Mashariki hususani paeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki.
v). Mswahili anaweza kuwa ni mtu anayeishi katika maeneo ya kawaida ya mjini (uswahilini)
vi). Mswahili anaweza kuwa ni mtu ambaye ni mwafrika asili, anayepatikana katika nchi za Kenya na Tanzania
v). Mswahili ni mtu mwenye maumbile na ya kiafrika, ikimaanisha kuwa ni mtu wa miraba minne. 

VITABU VYA REJEA
Chiraghdin S. na Mnyapala M. (1977) Historia ya Kiswahili, Oxford University Press Nairobi
Nkwera, F.M.V, (1978), Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo, THP, Dar es salaam.
Massamba na wenzake (1999) Sarufi Miundo ya Kiswahili  Sanifu (SAMIKISA), TUKI, Dar es salaam
Khamis, A.A, 2003 Uchambuzi Halisi wa Matumizi ya Kiswahili Asilia, Zanzibar. SUZA Press
Msokile M (1992) Historia na Matumizi ya Kiswahili EPD Kibaha
TUMI ( ) Kiswahili Sekondari,
Broomfield (1930) Sarufi ya Kiswahili, London, The sheldon press
Habwe J. na Karanja P. (2004), Misingi ya Sarufi ya Kiswahili, Nairobi phonex Publishers LTD
Mwansoko HJM na Tumbo. (1996) Matumizi ya kiswahili Bungeni, TUKI, Dar es salaam
BAKITA, (2004), Makala ya siku ya Kiswahili Kiswahili na Utandawazi, Dar es salaamu
TUKI, (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la pili, Oxford university press, Nairobi

Powered by Blogger.