Magumashi -2

Yake hayaeleweki, ndivyo huwa magumashi,
Kwa jambo haaminiki, hagaukosa uzushi,
Ahadi haziwekeki, hugeuka matapishi,
Huyu kweli magumashi, yake hayaeleweki !

Ya kwake hayapangiki, hata akiwa mshashi,
Ni mwingi wa urafiki, hujivuta kwa nakshi,
Ila hathaminiki, kwa tabia ya mzishi,
Huyu kweli magumashi, yake hayaeleweki !

Kubipu yake ashiki, apate kukushawishi,
Akiwa nacho mnafiki, hugeuka washiwashi,
Huku nje hasifiki, ila ndani ni mwandishi,
Huyu kweli magumashi, yake hayaeleweki !

Hukuitia steki, hadi kwenda kwake bushi,
Ukifika taharuki, hutauona moshi,
Sababu atahakiki, ana udhuru mpishi,
Huyu kweli magumashi, yake hayaeleweki !

Wengine ni mamluki, aidha na matoashi,
Na usipotaharuki, kukopa kwao hakwishi,
Deni likiwa lukuki, wakubwa mno wazishi,
Huyu kweli magumashi, yake hayaeleweki !

Ndoto zao za malaki, wenye nacho kuwapushi,
Mabinti na wataliki, kwenda kwao hawaishi,
Huota ndoto shiriki, kuja kujenga aushi,
Huyu kweli magumashi, yake hayaeleweki !

Waliogota visiki, mabinti wenye marashi,
Wenzetu huwaafiki, na kuwapamba nakshi,
Hazina wanaomiliki, hawaati kushawishi,
Huyu kweli magumashi, yake hayaeleweki !

Wasemayo yana haki, na wala sio wazushi,
Huwafika ya kindaki, wasitamani kuishi,
Nao hawa mamluki, bado wavuta hashishi,
Huyu kweli magumashi, yake hayaeleweki !

Powered by Blogger.